杏MAP导航

Tafuta

Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Tatu ya Kwaresima Mwaka C: “Nimeyaona mateso ya watu wangu huko Misri nami nimesikia kilio chao, maana nimeyajua maumivu yao nami nimeshuka ili niwaokoe…” Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya Tatu ya Kwaresima Mwaka C: “Nimeyaona mateso ya watu wangu huko Misri nami nimesikia kilio chao, maana nimeyajua maumivu yao nami nimeshuka ili niwaokoe…”  

Tafakari Dominika ya Tatu Kwaresima Mwaka C: Utakatifu, Toba Na Wongofu

Liturujia ya Neno la Mungua Dominika ya tatu ya Kwaresima inatutafakarisha juu ya: “Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na neema." Yeye ni Baba yetu mwema, mwenye upendo na huruma isiyo na mipaka. Licha ya sisi wanadamu kukosa uaminifu kwa Agano ambalo alifanya kwanza na taifa lake teule la Israeli, na baadaye amefanya nasi sote taifa lake jipya kwa njia ya Mwanaye Yesu Kristo, bado Mungu anatupenda na kutuhurumia. Utakatifu, Toba na Wongofu!

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., - Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi. Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 3 ya Kipindi cha Kwaresima, mwaka C wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika ya tatu ya Kwaresima inatutafakarisha juu ya, “Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na neema” Mwenyezi Mungu ni Baba yetu mwema, mwenye upendo na huruma isiyo na mipaka. Licha ya sisi wanadamu kukosa uaminifu kwa Agano ambalo alifanya kwanza na taifa lake teule la Israeli, na baadaye amefanya nasi sote taifa lake jipya kwa njia ya Mwanaye Yesu Kristo, bado Mungu anatupenda na kutuhurumia. Mwenyezi Mungu anatarajia tuzae matunda mema, tuwe mwanga na baraka kwa mataifa mengine. Licha ya kushindwa kwetu bado anatupa nafasi ya pili, nafasi ya kuanza upya katika mahusiano yetu naye na mahusiano kati yetu sisi kwa sisi. Mwenyezi Mungu hapendi hata mmoja wetu apotee na anatujumuisha sote katika mpango wake wa tangu milele, mpango wa ukombozi. Katika Dominika ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima, tumshukuru Mungu ambaye kwa upendo na huruma alimtuma kwetu mwanaye wa pekee, Bwana wetu Yesu Kristo, ili kutuletea sisi watu wa mataifa yote ukombozi wa milele, na kututoa katika utumwa wa dhambi na mauti. Katika kipindi hiki cha Kwaresima kwa namna ya pekee tunaalikwa kupokea mwaliko wa kuanza maisha mapya. Kwa njia ya neema na baraka nyingi tunazopokea kutoka kwa Mungu, tumwombe Mungu atusadie tuweze kuzaa matunda.

Musa Mtumishi wa Mungu alibahatika kuwa mbele ya Mungu
Musa Mtumishi wa Mungu alibahatika kuwa mbele ya Mungu

Somo la 1: Ni kutoka katika Kitabu cha Kutoka 3:1-8a, 13-15. Somo la kwanza tulilolisikia, Mwenyezi Mungu anamtokea Musa (Ufunuo; theophany) katika mlima Horebu, mlima wa Bwana. Kijiti kinachowaka moto bila kuteketea (Kut 3:2-3) ni ishara ya uwepo wa Mungu, Mungu mwenye nguvu, Mungu wa milele, hana mwanzo, hana mwisho (God’s eternal nature and sustaining power). Shauku ya Musa kugeuka ili aone maono hayo makubwa ni ishara ya kuwa wazi, na utayari wake wa kutaka kuelewa na kupokea ufunuo wa Mungu (openness to divine revelation). Kisha Bwana anamwita Musa kwa jina, ishara ya wito binafsi (personal vocation), na anajitambulisha kwa Musa kama, “Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka na Mungu wa Yakobo” akisisitiza mwendelezo wa uaminifu katika ahadi na Maagano aliyofanya na Baba zake. Mungu mwenye huruma anatamka kwa Musa kwamba, “Nimeyaona mateso ya watu wangu huko Misri nami nimesikia kilio chao, maana nimeyajua maumivu yao nami nimeshuka ili niwaokoe…” Mungu anaguswa na mateso na maumivu ya taifa lake teule, anaguswa na kilio chao. Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma anamtuma Musa, anakwenda kuanzisha safari ya ukombozi ya watu wake kutoka utumwani Misri ambapo walikaa utumwani na kuteseka kwa takribani miaka 430 (God’s compassion and Mission). Kisha kwa mkono wa Musa, Mungu anaanzisha safari ya ukombozi kwa watu wake kutoka utumwani Misri, kuelekea nchi ya Ahadi, nchi ijaayo maziwa na asali.

Mungu ameyaona mateso ya watu wake ameshuka kuwaokoa
Mungu ameyaona mateso ya watu wake ameshuka kuwaokoa   (AFP or licensors)

Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mambo manne ya kujifunza. Kwanza: Mungu mwenye Huruma anaona mahangaiko ya watu wake, anashuka kuwakomboa (God’s compassion and deliverance). Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na Neema kwa watu wake. Anaona na kuguswa na shida na mahangaiko ya taifa lake waliopo utumwani Misri. Anapomtokea Musa anamwambia, “Nimeyaona mateso ya watu wangu huko Misri nami nimesikia kilio chao, maana nimeyajua maumivu yao nami nimeshuka ili niwaokoe…” (Kut. 3:7-8.) Ndugu mpendwa sana, Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na neema aliona na kuguswa na kilio chetu sisi watu wake, tuliokuwa katika utumwa wa dhambi na mauti. Akamtuma Mwanaye wa pekee, Bwana wetu Yesu Kristo, akashuka na kukaa kati yetu ili atuletee ukombozi wa milele (Yn 1:14). Kwa njia yake sisi sote tumefanywa kuwa huru, na tumeshirikishwa ahadi ya uzima wa milele pamoja na Kristo. Nasi sote kila mara tunapopanda katika mlima wa Bwana, tunapokuja kukutana naye katika Neno lake na katika Sakramenti, anashuka na kukaa nasi. Anatuambia kwa sauti yake ya upole, “Nimeona mateso na mahangaiko yako mwanangu mpendwa, nimesikia kilio chako, nimeyajua maumivu yako, nami nimeshuka ili nikuokoe” Ni maneno ya faraja, ni maneno yanayoamsha matumaini na kutupa nguvu mpya ya kusimama tena tukiwa na Imani na matumaini thabiti, kwamba Mungu atafanya kitu katika hali zetu mbalimbali ambazo kila mmoja wetu anapitia kwa wakati wake. Ninakuombea ndugu mpendwa, Mungu mwenye huruma na neema akafanye kitu kwa ajili ya maombi yako mbalimbali, kwa ajili yako, kwa ajili ya familia yako, kwa ajili ya wito wako, kwa ajili ya kazi yako, kwa ajili ya watoto wako, masomo yako, kwa ajili ya utume wako wa kila siku, kwa ajili ya biashara yako nk.

Mambo msingi: Utakatifu, toba na wongofu wa ndani
Mambo msingi: Utakatifu, toba na wongofu wa ndani   (Vatican Media)

Pili: Mungu aliye Mtakatifu anatualika sote kumwendea katika utakatifu (God’s invitation to holiness.) Musa anapokutana na Mungu katika mlima Horebu Mungu anamwamuru asikikaribie kijiti kinachowaka moto. Anamwamuru avue viatu vyake maana mahali pale ni mahali patakatifu. Kuvua viatu ni ishara ya heshima mbele ya Mungu aliye mtakatifu sana (reverence in the presence of divine holiness). Ndugu wapendwa, Mwenyezi Mungu aliye Mtakatifu sana anatualika sisi sote kuwa watakatifu (Law 20:26, 1 Pet 1:15-16). Hatuwezi kumwendea Mungu aliye mtakatifu kama sisi pia hatujibidiishi katika kuutafuta Utakatifu. Kipindi cha Kwaresima ni kipindi ambacho kila mmoja wetu anapata nafasi ya kujitathimini na kuboresha mahusiano yake ya ndani kabisa kati yake na Mungu. Tunaalikwa kufanya toba ya kweli, kuacha dhambi na kukumbatia neema ya kuanza maisha mapya ndani ya Kristo mfufuka. Musa anaambiwa na Mungu anaamriwa na Mungu, “Kuvua viatu” ishara ya heshima na ibada kwa Mungu aliye Mtakatifu. Katika kipindi hiki cha Kwaresima tunaalikwa sote kuvua viatu vyetu, maana yake kuondoa vikwazo vyote ndani ya nyoyo zetu ambavyo vinatuzuia kwa namna moja au nyingine katika kumtumikia Mungu katika Utakatifu na haki. Huenda nyakati fulani, majivuno, chuki, starehe na anasa, roho ya visasi na wivu, kukata tamaa na kuwakatisha wengine tamaa, kulipiza visasi na kuwa chanzo cha maumivu kwa wengine vinanifanya kuwa mbali kabisa na Mungu. Hivi huenda ni viatu ambayo vinatuzuia kumwendea Mungu katika hali ya Utakatifu. Tunapata nafasi kila mara ya kuvua hivyo viatu na kumwendea Mungu katika utakatifu.

Mahali hapa ni patakatifu
Mahali hapa ni patakatifu   (Vatican Media)

Tatu: Mwenyezi Mungu anatuita sote kufanya mabadiliko binafsi (call to personal transformation). Mungu mwenye huruma, anamwita kila mmoja kwa jina na anampa wajibu, kwa ajili ya wokovu wake na wokovu wa wengine. Musa aliitwa na Mungu kwa jina, kutoka katika kazi yake ya kawaida kabisa, kazi ya kuchunga kondoo na akapewa kazi ya kwenda kuwatoa wana wa Israeli utumwani Misri. Anaitwa katika ukawaida wake na anapewa wajibu mkubwa usio wa kawaida, wajibu wa kuwaongoza taifa la Mungu kuziendea ahadi zake. Ndugu wapendwa, kipindi cha Kwaresima ni muda kila mmoja wetu anapata nafasi ya kutafakari pia juu ya wito wake. Ni muda wa kutafakari namna Mungu kwa upendo, wema huruma na neema zake anavyotushirikisha kila mmoja kadiri ya wito wake katika kazi ya ukombozi kwa wengine. Ni muda wa kutafakari jinsi gani nimekua mwaminifu katika kuitikia wito wa Mungu na kuishi kadiri ya mapenzi yake matakaifu. Musa aliacha maisha yake ya zamani baada ya kuitwa na Mungu, na akaanza maisha mapya yaliyoendana na wito wake mpya. Kwaresima inatukumbusha kuwa tumeitwa sote kutoka katika maisha yetu ya zamani, maisha ya dhambi na kukabidhiwa wajibu mpya katika ubatizo wetu, yaani kuishi kadiri ya wito wetu kama watoto wa Mungu na watoto wa kanisa. Nne: Tunaalikwa kuwa na matumaini kwa Mungu (Trusting in God’s name). Baada ya Mwenyezi Mungu kumtuma Musa kwenda kuwapa ujumbe wa matumaini wana wa Israeli, Musa anamwambia Mungu, “Tazama nitakapofika kwa wana wa Israeli na kuwaambia, Mungu wa Baba zenu amenituma kwenu, nao wakaniuliza jina lake nani, niwaambii nini?” Mungu akamwambia Musa,“Mimi nipo ambaye nipo.” Ndugu wapendwa, Mungu wa milele ndiyo jina lake, Nipo ambaye nipo. Hana Mwanzo, hana mwisho, utukufu ni wake na enzi pia, nyakati zote ni zake na karne zote milele na milele. Ni Mungu asiyebadilika, tangu milele hata milele. Kulifahamu jina la Mungu inatukumbusha sisi waamini kwamba yeye ni wa milele, ni mwaminifu, ana nguvu na uweza juu ya maisha na hali zetu zote, na kwamba yupo daima katikati yetu wakati wote. Katika hali zote, tumtambue kama Bwana na Mungu wetu, tutambue nguvu na uweza utokao kwake, yeye ni mwaminifu, wanadamu waweza kubadilika, nyakati zabadilika, Mungu wetu habadiliki, ni wa milele. Tumtafute yeye aishiye milele, ili nasi tuishi na kutawala naye milele yote.

Mwenyezi Mungu anamkirimia mwanadamu fursa ya toba na wongofu wa ndani
Mwenyezi Mungu anamkirimia mwanadamu fursa ya toba na wongofu wa ndani   (AFP or licensors)

Somo la Injili: Ni Injili ya Luka13:1-9. Somo la Injili Takatifu kutoka katika Injili ya Luka 13:1-9, ni sehemu ya mafundisho ya Yesu akiwa katika safari yake kuelekea Yerusalemu (9:51-19:27). Katika sehemu hii Bwana wetu Yesu Kristo anatoa mafundisho mawili mawili. Sehemu ya kwanza, 13:1-5 Yesu anafundisha juu ya hitaji la kufanya toba. Anajibu swali la watu waliodhani kuwa kuna uhusiano kati ya mateso na dhambi na hukumu ya Mungu, wakirejea matukio fulani yaliyotokea katika historia. Walidhani pengine mateso na kifo vilitokana na dhambi mtu alizotenda au walizotenda pia wazazi wake. Yesu anafafanua kuwa, wasiokua tayari kutubu na kubadilika, wataangamia.  Sehemu ya pili, 13:6-9 Yesu anatoa mfano wa Mtini, ambao licha ya kupewa kila matunzo ulishindwa kuzaa matunda. Mwenye shamba anataka kuukata lakini mtunzaji wa shamba anaomwomba mwenye shamba aupe tena nafasi ya mwisho ili kama usipozaa basi ndipo auangamize. Mfano huu wamwonesha Mungu mwenye huruma, ambaye licha ya kutupa kila kitu tunachohitaji ili tuzae matunda bado nyakati fulani tunashindwa kuzaa matunda. Licha ya hayo, yeye ni Baba mwenye huruma, bado anatupa nafasi nyingine tena. Katika somo hili la Injili dominika ya leo tuna mafundisho mawili ya kujifunza. Kwanza: Ulazima tathmini binafsi na toba ya kweli (inner self-examination and the urgency of repentance). Katika kipindi cha Yesu, na katika Mtazamo wa Agano la Kale, ilifahamika kwamba kulikua na uhusiano kati ya mateso ambayo mtu alipitia na dhambi. Watu walifikiri mateso na kifo vilitokana na dhambi na udhaifu wa watu husikia. Yesu anafundisha kuwa, bila kufanya tathmini ya ndani kila mmoja nafsini mwake, basi tutaangamia na kupatilizwa kwa sababu ya dhambi na udhaifu wetu. Ndugu wapendwa, kipindi cha Kwaresima ni kipindi cha neema, kipindi ambacho kila mmoja wetu anaalikwa kufanya tathmini ya ndani kabisa ya moyo wake. Nabii Yoeli anatuambia na mwaliko wa kurarua mioyo yetu wala sio mavazi yetu, yaani kwenda ndani kabisa ya mioyo yetu na kufanya mabadiliko ya kudumu, badala ya kutazama tu mambo ya nje. Yesu anatuonya kutokua wepesi katika kutazama na kuwahukumu wengine. watu hawa walifikiri pengine wale wagalilaya ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao walikua na dhambi kuliko wagalilaya wengine wote. Hawakua na muda wa kutazama ndani ya nafsi zao bali waliona udhaifu uliokua ndani ya hawa watu waliouwawa na Pilato. Mara kadhaa tunaacha kujitathmini sisi na tunakua tayari kuwahukumu na kuwafanyia tathmini wengine. Tumwombe Mungu atuguse kila mmoja ndani kabisa ya mioyo yetu, atupe neema ya kutambua udhaifu wetu na kuwa tayari kubadilika ili tuishi na kuupata uzima wa milele. Tuwasaidie wengine pia kujitathmini na kuweka sawa mahusiano yao na Mungu na mahusiano kati yao na wengine. 

Lengo ni kuzaa matunda ya: Utakatifu, toba na wongofu wa ndani
Lengo ni kuzaa matunda ya: Utakatifu, toba na wongofu wa ndani   (AFP or licensors)

Pili: Uhalisia wa maisha yetu watukumbusha hitaji la neema ya Mungu (we are equally in need of God’s grace). Matukio mbalimbali yanayotokea katika maisha yetu yanatukumbusha kuwa hakuna mwenye uhakika wa maisha ya uhai wake. Anayejua hatma ya maisha yetu ni Mungu peke yake. Watu walioangukiwa na mnara huko Siloamu ukawaua, watukumbusha kuwa muda na wakati wowote Mwenyezi Mungu anaweza kutuita na hapo tutajongea katika kiti chake cha hukumu. Nasi pia matukio mbalimbali yanayotokea kwenye maisha yetu yanatukumbusha kuwa uhai wetu ni mali ya Mungu na muda na wakati wowote atataka Hesabu ya maisha yetu ya hapa duniani. Tunahitaji neema ya Mungu ili itusadie daima kuwa tayari, kujiandaa kila mara kiroho ili muda na wakati ambao hakuna hata mmoja wetu anayefahamu, Mungu atakapotuita atukute katika hali ya neema nasi tumlaki katika ufalme wake wa Mbinguni. Tatu: Mungu mwenye Huruma, anatuvumilia, anatupa nafasi ya pili ili tuzae matunda (God’s mercy and patience). Katika mfano wa pili, Yesu anaelezea juu ya mtu aliyekuwa na mtini. Lakini mtini huu haukuzaa matunda. Alipotaka kuukata, yule mtunza bustani akaomba upewe tena muda, usipozaa ndipo ukatwe. Mtini ni mfano wa taifa la Israeli, mtu mwenye shamba ndiye Mwenyezi Mungu. Mtunza shamba aliyeomba mtini upewe nafasi ya pili, ni Bwana wetu Yesu Kristo, anayezuia hukumu ya mwenye shamba juu ya mtini ambao ulishindwa kuzaa matunda na kutupatia nafasi nyingine tena ya kufanya mabadiliko makubwa.

Waamini watumie fursa mbalimbali kutubu na kumwongokea Mungu
Waamini watumie fursa mbalimbali kutubu na kumwongokea Mungu   (Vatican Media)

Ndugu Wapendwa, mimi na wewe tu mzabibu wa Bwana. Anataka tuzae matunda mema, matunda mazuri ya roho, yaani upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi (Gal 5:22-23). Ametukirimia kila neema na baraka za mbinguni, ambazo kwa hizo tunaweza kuzaa matunda, yaani kuishi maisha yanayompendeza Mungu kadiri ya amri na mapenzi yake. Mara kadhaa kwa sababu ya udhaifu wetu wa kibinadamu, tunashindwa kuzaa matunda kadiri ya neema na baraka ambazo Mungu ametupa. Licha ya kushindwa kwetu, bado Mungu anatupa nafasi ya pili kwa njia ya Mwanaye mpendwa Yesu Kristo ambaye daima anatuombea kwa Mungu kama mpatanishi na kuhani wetu mkuu anayetufaa sana. Tukifikiri kama Mungu angekua anatuadhibu kila mara tunapotenda dhambi, ni nani angesimama? Mungu anatupa nafasi ya kufanya toba na kuanza tena upya na kisha tunaendelea kufurahia neema na baraka nyingi kutoka kwake. Hivyo ndugu zangu Wapendwa, Kwaresma hii iwe nami muda wangu wa kuzaa matunda. Maisha yangu ya kila siku yaendane na Ukristo wangu. Neema na baraka za Mungu ninazopokea kila siku katika maisha yangu zinisaidie kukua kiroho, kurekebisha udhaifu wangu, na kuanza maisha mapya ndani ya Kristo mfufuka. Mabadiliko ni swala la dharura, hakuna muda wa kusubiri kwa kuwa Mwenyezi Mungu kila mara anatupa nafasi nyingine.

Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo
Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo   (Vatican Media)

Somo la pili: Ni Kutoka Katika Waraka wa Mtume Paulo 1 Kor 10:1-6, 10-12. Katika Somo la pili, Mtume Paulo anafundisha kuwa, tunapaswa kutumia vyema neema na baraka za Mungu ili zitupatie wokovu. Anatoa mfano wa taifa la Israel, ambalo licha ya kuwa waliokolewa utumwani Misri, wakapata kila neema na baraka ili wafike nchi ya ahadi, bado kuna wengine walipotea. Sisi pia tumepata kila neema na baraka tunazohitaji ili tufike mbinguni, Neno la Mungu, Sakramenti za kanisa zinanisaidiaje kujiandaa kuupata uzima wa milele? Naweza kuwa nazo zote hizi ila bila utayari wangu hazitanisaidia kitu. Mtume Paulo, anatufundisha kwamba maisha ya nyuma yapaswa kuwa fundisho kwetu. Anawaandikia wakorintho ili waone na kujifunza kutoka katika maisha ya mababu zao. Kwaresma itukumbushe kuwa makosa na kushindwa ni daima kwetu. Licha ya hayo, hatupaswi kubaki katika udhaifu kwa kuwa Mungu anatupa nafasi ya kuanza tena upya. Mwisho, Mtume Paulo anatukumbusha daima kutojiamini kupita kiasi na kusahau kuingia ndani kabisa ya mioyo yetu na kujifanyia tathmini ya mahusiano yetu na Mungu. Tusijione tumesimama na kujitosheleza kiimani. Hitimisho: Katika Dominika ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka C wa Kanisa, tumshukuru Mungu ambaye kwa upendo na huruma alimtuma kwetu mwanaye wa pekee, Bwana wetu Yesu Kristo, ili kutuletea sisi watu wa mataifa yote ukombozi wa milele, na kututoa katika utumwa wa dhambi na mauti. Katika kipindi hiki cha Kwaresma kwa namna ya pekee tunaalikwa kupokea mwaliko wa kuanza maisha mapya. Kwa njia ya neema na baraka nyingi tunazopokea kutoka kwa Mungu, tumwombe Mungu atusadie tuweze kuzaa matunda.

Kwaresima D 3
22 Machi 2025, 09:23