Tafakari Dominika ya Tatu Ya Kwaresima Mwaka C: Toba Na Wongofu Wa Ndani
Na Padre Pascha Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, katika Dominika ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima, mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, siku ya kumi na tisa ya kujitakatifuza kama Mungu kwa kinywa cha Nabii Ezekieli anavyosisitiza katika wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya dominika hii anavyosema; “Nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtatakasika na uchafu wenu wote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, asema Bwana” (Ez. 36:25). Huu ni utakaso wa kiroho unaopatikana kwa kufunga na kusali. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya Koleta anasali na kuomba hivi; “Ee Mungu, wewe ndiwe asili ya rehema zote na mema yote. Umeonyesha kuwa dawa ya dhambi ni kufunga, kusali na kuwapa maskini. Utusikilize kwa wema sisi tunaokiri unyonge wetu, ili tunaponyenyekea moyoni, utuinue daima kwa huruma yako.” Ni katika muktadha huu, masomo ya dominika hii yanatuelekeza kutubu dhambi ili tuokolewe. Na toba ya kweli ni kumwelekea Mungu ambaye ndiye mwenye uwezo wa kutuokoa kama anavyotuasa mzaburi (Zab. 25: 15-16); “Macho yangu humwelekea Bwana daima, naye atanitoa miguu yangu katika wavu. Uniangalie na kunifadhili, maana, mimi ni mkiwa na mteswa.” Madhara ya kukaza shingo na kutokutubu ni kuangamia milele.
Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha; ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya, yanayovunjilia mbali ubinafsi ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya mang’amuzi ya huruma inayowakirimia furaha, hata kama maisha yao bado yanasheheni matatizo na changamoto mbalimbali, ili kuondokana na utamaduni wa huzuni, utupu na upweke unaopelekea msongo wa mawazo kwa watu wengi! Huruma ya Mungu inajidhihirisha kwa namna ya pekee, katika maadhimisho ya Sakramenti za Uponyaji yaani: Sakramenti ya Upatanisho na Mpako wa wagonjwa. Baba Mtakatifu anapenda kutoa mkazo wa pekee katika Sakramenti ya Upatanisho inayowaonjesha waamini huruma, upendo na msamaha wa dhambi; mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kumwilisha upendo wa Mungu katika maisha.
Somo la kwanza ni la Kitabu cha Kutoka (Kut 3:1-8, 13-15). Katika somo hili Mungu anamwita na kumtuma Musa arudi Misri kuwakomboa watu wake akimwambia hivi; “Nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nimesikia kilio chao, nami nimeshuka ili niwaokoe, niwapandishe kutoka nchi ile niliyowaahidia baba zao”. Musa anaitwa akichunga kondoo wa mkwe wake Yethro, kuhani wa Midiani. Hivyo anapaswa kufanya safari ile ile aliyoifanya kutoka Misri mpaka mlima Horebu kupitia jangwani alipotoroka akiikimbia hasira ya Farao. Safari hii ataifanya tena akiwaongoza wana wa Israeli kutoka Misri mpaka mlima wa Bwana. Kuitwa kwa Musa akiwa mlimani ni ishara kuwa anayemuita ni Mungu, na kijiti kiwakacho moto, hakiteketei ni ishara ya upendo na huruma ya Mungu iliyo ya milele. Musa anaomba kujua jina la Mungu. Mungu anamwambia; “Mimi Niko ambaye Niko”. Huu ni ufunuo wa kuwa Mungu ni Yule Yule, Jana, Leo na hata milele. Mungu anamtaka Musa “kuvua viatu kwa sababu mahali aliposimama ni nchi takatifu”. Hii ni alama ya toba na kusamehewa dhambi alizotenda akiwa Misri. Musa alipaswa kuacha chuki na hasira aliyokuwa nayo juu ya watu wa Misri. Ni mwaliko wetu sote wa kuvua kwa nguvu rohoni mwetu yale yote yanavunja urafiki wetu na Mungu. Mungu anatualika tusafishe roho zetu kwa kufanya toba ya kweli. Ni katika muktadha huu, mzaburi katika wimbo wa katikati anasema hivi; “Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu, vilihimidi jina lake takatifu. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, wala usizisahau fadhili zake zote. Akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote, aukomboa uhai wako na kaburi, akutia taji ya fadhili na rehema. Bwana ndiye afanyaye mambo ya haki, na hukumu kwa wote wanaoonewa. Alimjulisha Musa njia zake, wana wa Israeli matendo yake. Bwana amejaa huruma na neema, haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili. Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, kadiri ileile rehema zake ni kuu kwa wamchao” (Zab. 103: 1-4, 6-8, 11). Nasi tukifanya toba ya kweli na kumrudia Mungu Baba yetu kwa moyo wa unyenyekevu na majuto, Yeye ni mwingi wa rehema atatusamehe na kutusafisha na uovu wetu wote.
Somo la pili ni la Waraka wa Kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 10:1-6, 10-12). Katika somo hili, Mtume Paulo anatutahadharisha tusirudi katika dhambi baada ya kukombolewa kwa Damu Azizi ya Yesu Kristo na kuondolewa dhambi zetu kwa njia ya sakramenti ya ubatizo na kushibishwa kwa Ekaristi Takatifu chakula chetu cha kiroho kama Waisraeli waliookolewa toka utumwani Misri na wakalishwa kwa manna jangwani, ili tusije tukaangamia na kufa kama waisraeli walivyopotea na kufa jangwani sababu ya dhambi zao. Mtume Paulo anasisitiza kuwa, habari zao ziliandikwa ili sisi tuzifahamu tusije nasi tukaingia katika shida na taabu kama wao. Basi tuchukue tahadhari ili tusirudi katika utumwa wa dhambi maana dhambi inaleta mateso, mahangaiko na mwisho wake ni kifo na kuangamia milele. Msisitizo ni huu; “Anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke” (1Kor. 10:12). Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk 13:1-9). Katika sehemu hii ya Injili, Yesu anatoa maonyo makali ya madhara ya kukaza shingo, kuwa na mioyo migumu, kuikomalia dhambi na kukataa kutubu na kuungama – matokeo yake ni kuangamia milele. Yesu alitoa maonyo na fundisho hili baada ya watu walijikinai na kujiona kuwa wao ni watakatifu, hawana dhambi walipompasha habari za Wagalilaya ambao Pilato alitoa amri wauawe na damu yao kuchanganywa na dhabihu zao walizokuwa wanamtolea Mungu Hekaluni, na za watu wengine kumi na wanne, walioangukiwa na mnara huko Siloamu wakafa. Yesu anawaambia kuwa hakuna binadamu yeyote aliyemkamilifu. Sote mbele za Mungu tu wadhambi. Hivyo tusipotubu tutaangamia milele. Kufa au kuendelea kuishi, kuugua au kutokuugua, kupata majanga au mafanikio sio ishara ya utakatifu. Kuendelea kuishi ni mapango tu wa Mungu wa kumpa mwanadamu muda na nafasi ya kutubu makosa yake ili asife katika dhambi, akaangamia milele.
Ili kufafanua ukweli huu, Yesu anatoa mfano wa mtini uliopandwa katika shamba la mizabibu. Mwenye shamba alipoona hauzai matunda kwa miaka mitatu, alitaka kuukata. Lakini mtunza shamba akamuomba asiukate ili aweze kuupalilia na kuutilia samadi, nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo aukate. Ni mwaliko kwetu kujipatanisha na Mungu kwa kuziungama dhambi zetu katika Sakramenti ya Kitubio. Tukumbuke kuwa; “tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu. Lakini tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe na kutusafisha toka kwenye udhalimu wote…” (1Yn. 1:8-10). Usipoziona dhambi zako ujue kabisa umezizoea na kuzifanya sehemu ya maisha yako ndiyo maana huzioni. Ndiyo maana waswahili wasemavyo; “Mtu hawezi kunusa harufu yake mwenyewe”. Lakini pia yawezekana kuwa mizani yako ya kimaadili imekengeuka kwa kiburi kwa maendeleo na mafanikio uliyonayo na hivyo kujiona huna dhambi. Mzaburi anatutahadharisha na hali hii akisema; “Dhambi huongea na mtu mwovu, ndani kabisa moyoni mwake; wala jambo la kumcha Mungu halimo kabisa kwake. Kwa vile anajiona kuwa maarufu hufikiri kuwa uovu wake hautagunduliwa na kulaaniwa. Kila asemacho ni uovu na uongo; ameacha kutumia hekima na kutenda mema. Alalapo huwaza kutenda maovu, wala haepukani na lolote lililo baya” (Zab.36:1-4).
Tukumbuke kuwa kutenda dhambi ni kumkataa Mungu, na kumkataa Mungu ni kupoteza neema ya utakaso. Ni kitubio peke yake kinachoweza kuturudishia neema hii ya utakaso, yaani uwepo wa Mungu ndani yetu. Lakini pia kitubio kinatusaidia kurudisha urafiki wetu kwa wengine na kupatana na waliotukosea kwa sababu tunapoungama dhambi zetu tunajikubali kuwa tu wakosefu, tu wadhaifu hivyo tunahitaji kuomba msamaha na kupatana na wale tuliokosana nao. Tukumbuke daima kuwa Mungu anatusamehe dhambi zetu katika sakramenti ya kitubio kupitia makuhani aliowachagua na kuwaweka kuwa wapatanishi wetu naye. Kama ilivyo katika maisha ya kawaida, ili aliyekosa asamehewe anapaswa kukiri kosa lake na kuomba msamaha kwa kusema; “nimekosa naomba msamaha” na aliyekosa anahitaji kusikia; “nimekusamehe”. Ndivyo ilivyo katika sakramenti ya kitubio tunahitaji kusikia; “Umesamehewa dhambi zako nenda na amani.” Maneno “nami kwa mamlaka niliyopewa na Kanisa nakuondolea dhambi zako” au “Nenda na amani dhambi zako zimeondolewa”, yanatupatia uhakika wa kile tulichokipata na haya maneno hayawezi kutamkwa na yeyote yule isipokuwa na Padre anayefanya hivyo katika nafsi ya Kristo. Hivyo tunahitaji kuungama kwa Padre ili tupate hakikisho la msamaha wetu kwa kusikia maneno haya. Na tukumbuke kuwa Sakramenti hii iliweka na Yesu mwenyewe; “Wowote mtakaowaondolea dhambi wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi wamefungiwa” (Yn 20:23). Lakini pia tunapoungama kwa Padre, licha ya malipizi tunayopewa kwa afya ya roho zetu, tunapata pia ushauri wa namna ya kupambana na vishawishi vilivyotuangusha dhambini visitushinde tena.
Mwisho tukumbuke kuwa upatanisho wetu na Mungu unahitaji upatanisho wetu na ndugu zetu. Ili tusamehewe na Mungu, tunahitaji kuwasamehe ndugu zetu waliotukosea. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana utujalie kwa ajili ya sadaka hizi, tujitahidi kuwasamehe jirani zetu, maadam tunakuomba utusamehe sisi dhambi zetu wenyewe”. Na habari mbaya ni hii, baada ya kifo hakuna tena nafasi ya kutubu, wakati uliokubalika ndiyo sasa. Basi tufanye hima tujipatanishe na Mungu kabla ya kifo. Tufanye toba ya kweli tungali hai, ili tuweze kuionja furaha ya mbinguni tukingali bado duniani kama mama Kanisa anapohitimisha maadhimisho ya dominika hii, anavyosali katika sala baada ya Konumio akisema; “Tumepokea amana ya fumbo la mbinguni. Nasi tumeshiba mkate wa mbinguni tukingali bado hapa duniani. Tunakuomba kwa unyenyekevu, ee Bwana, hayo tuliyopokea katika fumbo tuyatimize kwa matendo.” Tumsifu Yesu Kristo!