杏MAP导航

Tafuta

“… Na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea” (Kut 3:2b) “… Na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea” (Kut 3:2b) 

Tafakari Dominika ya Tatu Kwaresima Mwaka C wa Kanisa: Muda Wa Toba Na Wongofu!

Kujifunza kutenda mema ni sheria na kanuni ya toba na wongofu wa ndani. Waamini wajitahidi kukimbia dhambi na nafasi zake kwa kujifunza kutenda mema yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya mtu! Mama Kanisa anawaalika waamini kutumia kikamilifu rasilimali muda uliowekwa mbele yao ili waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa haki, huruma, upendo na mshikamano; mambo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Rasilimali Muda!

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Mpendwa msikilizaji na msomaji wa Vatican News Karibu katika tafakari ya Neno la Mungu. Dominika iliyopita tulisimuliwa namna Kristo alivyong’aa juu ya mlima, tukaomba neema ya kuwapandisha wengi juu ya mlima wa Mungu na kubaki mlimani ili kushiriki utukufu wake. Mama Kanisa anawaalika watoto wake kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu katika kipindi hiki cha Kwaresima. Watakatifu ambao kimsingi ni wadhambi waliotubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu ni watu waliotenda dhambi lakini daima walikimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanaondokana na tabia ya kuishi katika dhambi za mazoea. Waamini wajifunze kutenda mema na kwamba, huuu ni mchakato wa kila siku katika maisha ya waamini kama ilivyo kwa watoto wadogo. Kujifunza kutenda mema ni sheria na kanuni ya toba na wongofu wa ndani, safari ndefu katika maisha. Waamini wajitahidi kukimbia dhambi na nafasi zake kwa kujifunza kutenda mema si tu kwa maneno, bali maneno yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya mtu! Mama Kanisa anawaalika waamini kutumia kikamilifu rasilimali muda uliowekwa mbele yao ili waweze kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa haki, huruma, upendo na mshikamano; mambo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu na utakatifu wa maisha
Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu na utakatifu wa maisha   (© Mirek Krajewski)

Leo tungali bado juu ya mlima wa Mungu anayetufikia kwa njia ya Musa mtumishi wake kwenye sura ya kijiti kinachowaka bila kuungua… Ile lilikuwa ni aina ya “Ufunuo” yaani “Epifania ya” Mwenyezi Mungu akijipambanua kwa mwanadamu kama Mungu “aliyepo” si tu mbinguni bali kati ya watu (Emmanuel), Mungu anayesikia vilio vya watu wake na kuyaona mateso na mahangaiko yao, na sasa ameshuka ili kuwaokoa… kijiti kinachowaka bila kuteketea ni dhamiri njema na hai, mahali pa ndani kabisa pa mwanadamu anapokutana na Mwenyezi Mungu na hapo kwa kawaida hapaathiliwi na dhambi, ingekuwa Kanisani basi ni pa takatifu pa patakatifu… mahali hapo ni nchi takatifu sana ambapo “Mimi niko ambaye niko” anasema nasi ndani kabisa ya mtima wetu… ni mahali pa ukamilifu, mahali wito wetu unaanzia, chemchemi ya utumishi wetu… ni mahali ambapo nguvu iwakayo na kuangaza ya Mungu huonekana. Katika Injili hii, Yesu anatoa mfano wa mti wa tini usiozaa matunda, akisema kuwa kama hautaonyesha matunda, utakatwa. Huu ni wito kwa waamini kutubu, kuongoka na hatimaye na kuzaa matunda kwa kutenda mema, kwani neema ya Mungu inahitajika kwa wokovu wetu.

Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani
Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani   (Vatican Media)

UFAFANUZI: Heshima, kuabudu na hofu ya Musa vinajidhihirisha mbele ya “Uwepo” mtakatifu…  hali ya kichaka kuwaka bila kuteketea ni ishara ya utakatifu wa Mungu usioisha wala kufifia, utakatifu utishao na kuvutia, unaoogofya lakini unafariji, unaalika na kutuma, unaasa na kukumbatia, na hapo, pamoja na Musa, tunaelekezwa kuvua viatu yaani kuvua utu wa zamani wa dhambi na kuvaa utu mpya, utakatifu wa ndani… kutoka hapo tunaelekea Misri kwa kazi maalumu, kuwakomboa walio utumwani mwa dhambi, wanaoonewa na Ibilisi, ili kuwaongoza nchi ya ahadi ifurikayo maziwa na asali, ndio uhuru wa watoto wa Mungu. Pia kijiti kile kilichowaka bila kuteketea ni ishara ya ubikira wa Maria, Mama na papo hapo Bikira daima… usafi wa moyo, weupe wa roho, upevu wa akili, adabu njema na utakatifu. Mazingira ya wito wa Musa yatuhamasishe sisi pia kuitikia wito wetu wa kuwa watakatifu. Katika somo la Injili (Lk 13:1-9) kuna watu waliuawa na Pilato na wengine kuangukiwa na mnara, watu wanapomsimulia Yesu visa hivi Yeye anasema sio kwamba hao walikuwa na dhambi kuliko wengine, maana yake yeyote yule anaweza kupata changamoto aidha sababu ya dhambi au kama sehemu ya maisha, ndivyo asili ilivyo. Lililo muhimu sio kunyoosheana vidole na kujadili mapungufu na matatizo ya wagalilaya au wasiloamu (akina mimi tulio wakosefu) bali kujitathmini binafsi na kufanya toba, msimu huu wa Kwaresima utusaidie kukutana na Mungu katika utakatifu wake kwenye sura ya kijiti kinachowaka bila kuteketea.

Mahujaji wa Imani, Matumaini na Mapendo kwa Mungu na Jirani
Mahujaji wa Imani, Matumaini na Mapendo kwa Mungu na Jirani   (Vatican Media)

Katika muktadha wa Jubilei ya Matumaini, tafakari hii inatufundisha kuwa matumaini ya Kikristo yanatufundisha kumtumikia Mungu kwa maisha ya matunda ya toba na kujitolea kwa wema. Matumaini haya hayana maana kama hatujaishi kulingana na mapenzi ya Mungu. Kama mti wa tini unavyohitaji kuzaa matunda ili uonyeshe maisha, vivyo hivyo sisi, kama Wakristo, tunapaswa kuonyesha matunda ya toba, huduma kwa wengine, na uaminifu kwa Mungu. Jubilei ya Matumaini inatufundisha kuwa tukiishi kulingana na mapenzi ya Mungu, tunaweza kuwa na matumaini ya uzima wa milele. Tufanye kitubio Kwaresima hii, toba haiji wakati tunapolia machozi bali hufika kilele chake sekunde ile tunapofaulu kutubu na kumwongokea Mungu. Tusifanane na Pilato ambaye katika ukatili wake anawaua watu na kama haitoshi anachanganya damu zao na sadaka zao, au Injinia aliyejenga mnara Siloamu ukaangukia watu 18… Pengine hapa na pale tumekuwa na tabia za Pilato, hatujamshikia mtu upanga lakini tunaua kwa mitazamo, maneno, kutotoa ushirikiano, ushauri mbaya, uvivu na choyo, kutokuguswa na shida za wenzetu, na kuona kero wanapotukaribia…

Mahujaji wa matumaini ni cheche za mabadilio na wongofu wa ndani
Mahujaji wa matumaini ni cheche za mabadilio na wongofu wa ndani   (Vatican Media)

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wa Kwaresima 2025, anatukumbusha kuhusu wito wa toba na wongofu wa ndani. Kama vile Yesu anavyozungumzia juu ya mti wa tini, tunahamasishwa kutafuta mabadiliko ya kweli katika maisha yetu, kuzaa matunda ya imani na kujitolea. Kwaresima ni muda wa kujitafakari na kufanya mabadiliko ya kiroho ili tuweze kushiriki katika utukufu wa ufufuo wa Kristo. Hii ni Kwaresima, tuyaache hayo tukapate kumwona Mungu kwenye sura ya kijiti kile… tumejitahidi sana mpaka sasa, somo II (1Kor 10:1-6, 10-12) linatuhamasisha tujiangalie tusianguke katika yale mema tuliyoyasimamia. Haitoshi kuadhimisha sakramenti pekee bali ni budi kuitikia kila siku wito wa Kristo kwa ufunuo halisi wa kimungu alivyoutoa kwa Musa mtumishi wake. Mungu wetu ni Bwana mwenye kutuvumilia sababu anatupenda na daima anatupatia nafasi ya pili kama unenavyo mfano wa leo wa mtini usiozaa… mtini ule unapewa nafasi nyingine kwa kumwagiliwa, kupaliliwa, kutiliwa samadi kusudi uzae matunda yake, maana yake ni misaada ya neema kutoka kwa Mungu, kutoka kwa wenzetu na karama tunazojaliwa kila siku na Roho wa Bwana, sakramenti, sala na baraka za Kanisa… basi na tuitumie vema nafasi hiyo ili matendo yetu mema yakawe ni mtini wenye kuzaa daima. Dominika ya Tatu ya Kwaresima inatufundisha kuhusu umuhimu wa toba na kuzaa matunda ya imani, matumaini na mapendo. Katika kipindi hiki cha Kwaresima, tunaitwa kujiandaa kwa neema ya Mungu, tukikumbuka kuwa maisha yetu yanahitaji mabadiliko ya kiroho ili tuwe na sehemu katika furaha ya ufufuo wa Kristo. Jubilei ya Matumaini inatufundisha kuwa, kwa imani na toba, tunaweza kufikia matumaini ya wokovu na maisha ya milele.

Liturujia Kwaresima D3
21 Machi 2025, 14:23