杏MAP导航

Tafuta

Tukio la kung’ara kwa Yesu linasindikizwa na uwepo wa Musa na Eliya waliokuwa wanazungumza na Kristo Yesu, kielelezo cha utimilifu wa Sheria na Unabii katika Maandiko Matakatifu Tukio la kung’ara kwa Yesu linasindikizwa na uwepo wa Musa na Eliya waliokuwa wanazungumza na Kristo Yesu, kielelezo cha utimilifu wa Sheria na Unabii katika Maandiko Matakatifu  

Tafakari Dominika Ya Pili Kwaresima Mwaka C wa Kanisa: Utimilifu Wa Torati na Unabii

Tukio la kung’ara kwa Yesu linasindikizwa na uwepo wa Musa na Eliya waliokuwa wanazungumza na Kristo Yesu, kielelezo cha utimilifu wa Sheria na Unabii katika Maandiko Matakatifu Mwanga angavu uliokuwa kiini cha tukio hili ni kielelezo cha mwanga unaopaswa kuangaza akili na mioyo ya Mitume wa Yesu ili waweze kumfahamu Bwana wao. Ni mwanga unaoangaza Fumbo la maisha ya Yesu na hivyo, kufunua maisha na utume wake wote hapa duniani.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka C wa Kanisa inasimulia jinsi ambavyo Kristo Yesu alivyowachukua Mitume wake watatu yaani: Petro, Yakobo na Yohane wakajitenga na hapo akang’ara sura mbele, kiasi cha kuwafunulia ukuu, utukufu na utakatifu wake ambao walipaswa kuupokea kwa njia ya imani, mahubiri pamoja na miujiza mbalimbali aliyotenda katika maisha yake. Tukio la kung’ara kwa Yesu linasindikizwa na uwepo wa Musa na Eliya waliokuwa wanazungumza na Kristo Yesu, kielelezo cha utimilifu wa Sheria na Unabii katika Maandiko Matakatifu Mwanga angavu uliokuwa kiini cha tukio hili ni kielelezo cha mwanga unaopaswa kuangaza akili na mioyo ya Mitume wa Yesu ili waweze kumfahamu Bwana wao. Ni mwanga unaoangaza Fumbo la maisha ya Yesu na hivyo, kufunua maisha na utume wake wote! “… hivyo simameni imara katika Bwana, mkiwa na matumaini zaidi” (Filp 3:17-4:1) Mpendwa msikilizaji na msomaji wetu, Karibu katika tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican, tafakari ya leo nitaanza na mfano wa marafiki wawili, Kijana mdogo alimuuliza rafiki yake, ‘Hivi ni wa nini ninyi watu wanene ni watu wa amani sana’ akamjibu ‘Ni vile hatuwezi wala kukimbia wala kupigana’… lilikuwa jibu la mtu anayetambua uwezo na udhaifu wake na hivi afanye nini. Mt Paulo anatualika tuwe watu tunaojitambua wenyewe na lengo la kuwepo kwetu duniani, kujua wenyeji wetu halisi si hapa bali ni mbinguni na hivi kusimama imara katika imani. Kama daima anavyowatafakarisha waamini wake Mhashamu Askofu mstaafu wa jimbo la Sumbawanga nchini Tanzania Askofu Damian Kyaruzi, akisisitiza maneno ya mtume Paulo “tusimame imara katika imani, anaendelea, kusisitika kusimama imara katika: wito, malezi na matumaini nk.

Uwepo wa Musa na Eliya ni Utimilifu wa Sheria na Unabii
Uwepo wa Musa na Eliya ni Utimilifu wa Sheria na Unabii   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kamusi ya Kiswahili inaeleza neno “imara” kama hali ya kuwa na uthabiti, madhubuti isiyotetereka wala kuyumbishwa… wito wetu leo ni kuwa madhubuti kiroho (kiimani), kiakili, kihisia, kimwili na halafu kijamii. Uimara tunaofundishwa kuusimamia unaonekana katika somo I (Mwz 15:5-12, 17-18) kwamba tuwe waaminifu kwa Agano letu na Mungu… Namna Mungu alivyotendeana na waisraeli, kupitia Musa, mababu na manabii, kabla ya Kristo ndilo Agano la Kale… Namna Mungu anavyotendeana na watu wote, kupitia Kristo ndilo Agano Jipya… mwanzoni Mungu aliweka Agano na Adamu na Eva (Mwz 2:4-17) halafu na Nuhu baada ya gharika (Mwz 9:17) ikashindikana sababu mwanadamu daima si mwaminifu, ndipo akaweka tena Agano.

Kristo Yesu ni kielelezo cha Agano Jipya na la Milele
Kristo Yesu ni kielelezo cha Agano Jipya na la Milele   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

UFAFANUZI: KristoYesu anadhihirisha utukufu wake kwa wafuasi wake, akionyesha kwamba ugumu wa msalaba unaofuata utakuwa na lengo la kufikisha utukufu wa Mungu. Hii ni ishara ya matumaini kwa wafuasi wake, licha ya changamoto na mateso wanayoweza kukutana nayo. Katika muktadha wa Kwaresima, tunapata wito wa kumfuata Yesu, kujiandaa kwa mateso yake, lakini pia kushiriki katika utukufu wake. Agano na Ibrahim kadiri ya somo Ia I, baadaye akaliratibisha kwa mkono wa Musa huko Sinai (Kut 20, Kumb 5), likarudiwa tena kwa Mfalme Daudi (2Sam 7, Zab 89) na kufikia kilele katika damu ya Kristo Yesu iliyo Agano jipya na la milele (Mt 26:28, Mk 14: 24, Lk 22:20, 1Kor 11:25). Basi tusimame imara tukishika daima Agano letu la ubatizo kwa kumkataa shetani, mambo na fahari zake zote na kumsadiki Mungu mmoja na wa milele. Tunahitaji kusimama imara katika Bwana ili tufanikiwe kupanda mlima wa Bwana na kung’ara pamoja naye kama tunavyosimuliwa katika somo la Injili (Lk 9:28b-36), hii ni saa ya mlimani… Mlima ni mahali pa kukutana na Mungu, ni dakika ile ambapo mwanadamu mwenye hali ya kufa anakutana na Mungu anayeishi milele, juu ya mlima Mungu anakutana na watu wake katika Kristo aliye daraja kati ya mbingu na dunia. Matukio yote muhimu yametendeka juu ya mlima. Safina ya Nuhu ilitua juu ya mlima Ararati (Mwz 8:4), Ibrahim alikuwa tayari kumtoa sadaka Isaka juu ya mlima Moriah (Mwz 22), mlima huu huitwa mlima Sayuni mji wa Yerusalemu ukikaa juu yake… Mungu alinena na Musa juu ya mlima Horeb, akampa amri mlimani Sinai, baadaye alifia juu ya mlima Pisgah.. Kristo amesulibiwa juu ya mlima Kalvari… Nabii Isaya anashangilia akisema “Na katika mlima huu Bwana wa majeshi atawafanyia mataifa karamu ya vitu vinono” (25:6)…

Mlimani ni mahali pa kukutana na Mungu
Mlimani ni mahali pa kukutana na Mungu   (ANSA)

Juu ya mlima ni mahali pa ukweli, upendo, amani na ufunuo wa kimungu. Mlima ni udumifu wa roho, utulivu, ukimya na fikara. Mungu anasema nasi kwa sauti mororo ya utulivu tuwapo juu ya mlima (1Fal 19:12b) tena mlima ni ishara ya kuwa macho, kukesha na Kristo… na huko juu ya mlima ndiko nyumba ya Bwana itakakosimikwa, kutoka huko juu itakuja sheria nasi tutajifunza njia zake na kutembea katika mapito yake (Mika 4:1-2) … hii ni saa ya mlimani! Leo Bwana anang’ara juu ya kilele cha mlima Tabor, ni tukio muhimu sababu mosi linakamilisha utukufu wa siku ya ubatizo wake mtoni Yordani na kudhihirisha ukamilifu wa maisha ya mbinguni… pili, kama ilivyokuwa kwa Petro, Yakobo na Yohane sisi pia tunaonjeshwa faraja na raha ya kipasaka na hivi “kusimama imara katika Bwana” wakati wa majaribu… tatu, kwa uwepo wa mababu wa zamani, ni dhahiri kuwa Torati (Musa) na manabii wote (Eliya) vinajipatia ukamilifu wake katika Kristo, Agano la Kale linajivuta ili Agano Jipya litamalaki ndani ya Yesu Masiha…  Uwepo wa Musa na Eliya, watakatifu wa zamani, unathibitisha fundisho la Kristo mwenyewe kwamba ‘Mungu wetu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai’ (Mt 22:32b)… na hii ni saa ya mlimani! Katika ufufuo wa Kristo, tunaona mwisho wa mateso na mwanzo wa maisha mapya. Hii ni nguvu ya matumaini inayoangaza katika maisha ya kila mmoja wetu. Hata katika kipindi cha Kwaresima, ambapo tunatafakari juu ya kifo cha Kristo, tunamwazia pia jinsi alivyoshinda kifo na kuleta uzima kwa wote wanaoamini. Pamoja na uzuri na utukufu wa mlimani, ipo pia milima mibaya na hiyo Yohane Mbatizaji alisema hatuna namna ila wakati tunajaza mabonde ni lazima kuisawazisha pia milima ya namna hii (Lk 3:5). Kipindi hiki cha Kwaresima kitusaidie kuliishi neno la leo “… hivyo simameni imara katika Bwana, wapenzi wangu” (Filp 4:1) tukivaa uthubutu wa kusawazisha milima hiyo mioyoni yetu, yaani tabia na mazoea yasiyofaa.

Waamini wanaalikwa kuwa ni mahujaji wa matumaini
Waamini wanaalikwa kuwa ni mahujaji wa matumaini

Katika maadhimisho ya mwaka wa Jubilei ya Matumaini, tafakari ya Dominika hii ina uhusiano mkubwa. Tunakumbushwa kwamba, kama Yesu alivyodhihirisha utukufu wake katika Mlima, hivyo ndivyo sisi tunavyohitaji kuwa na matumaini yanayotufanya kuvumilia changamoto na majaribu ya maisha kwa imani na matumaini kwa uzima wa milele. Jubilei ya Matumaini ni mwaliko kwa Wakristo kuwa na matumaini, licha ya magumu, kwa kuzingatia kuwa Kristo alishinda kifo na dhambi. Ni katika muktadha wa ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa kipindi cha Kwaresima kwa 2025, tunahamasishwa kutafakari kuhusu wito wetu wa kumfuata Yesu kwa toba na kujinyima. Kama alivyoshinda majaribu ya ulimwengu na akadhihirisha utukufu wake, vivyo hivyo tunatakiwa kushinda majaribu ya dhambi na dunia hii ili tuwe na sehemu katika utukufu wa ufufuo wa Kristo. Tufanye nini basi? tutamani kuungana na Petro ili kujenga vibanda na kukesha na Yesu mlimani… lakini wenzetu wengi zaidi wangali bado chini ya mlima, bondeni sio kuzuri, huwa tunamuomba Mama Maria atuombee sisi wana wa Eva tulio ugenini, bondeni huku kwenye machozi… bonde kubwa liliwatenga Lazaro, Ibrahim na tajiri aliyeteseka (Lk 16:26), ni bondeni baharini walifia nguruwe wengi waliopagawa na pepo (Mt 8:32)… bondeni chini ya mlima Mitume tisa waliobaki wanahangaika bila mafanikio kumsaidia mtoto mwenye pepo wa kifafa (Lk 9:37kk)… tusiogope, twendeni zetu bondeni tukawachukue wenzetu tuje nao juu ili nao wauone utukufu wa Kristo Yesu, wawaone Musa na Eliya, wamsikie Baba katika wingu jeupe, wamjue na kumsikiliza Mwana mpendwa wa Baba na halafu, wajenge vibanda vitatu na kukesha na Kristo kwa milele. Dominika ya Pili ya Kwaresima ni mwaliko wa kutafakari kuhusu utukufu wa Mungu, kuishi kwa matumaini, na kujiandaa kushiriki katika maisha mapya ya Kristo. Katika kipindi hiki cha Kwaresima, tunaitwa kupiga hatua za kiroho kuelekea utukufu wa Mungu, tukichukulia mfano wa Yesu katika toba, maombi, na kujiweka mbali na mambo ya dunia. Tumwombe Mungu mwema ajalie mioyo yetu iwe ni milima inayong’ara kwa utukufu wa Kristo sasa na siku zote, Amina.

Liturujia Kwaresima D 2
14 Machi 2025, 15:36