Tafakari Dominika ya Pili Kwaresima Mwaka C: Kung'ara Kwa Sura ya Yesu: Torati na Unabii
Na Padre Pascha Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya pili ya kwaresima, mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, siku ya kumi na mbili ya kipindi cha majiundo ya kiroho. Masomo ya Dominika hii yanatuongoza kuutambua ukuu wa Yesu Kristo, mwana wa Mungu katika tukio la kugeuka kwake sura mlimani Tabor, na kuudhihirisha Umungu wake. Musa na Eliya ni watu muhimu sana katika historia ya Wayahudi. Musa ndiye anayewakilisha Torati, yaani sheria na taratibu zinazoongoza maisha yote ya Wayahudi. Eliya yeye anawakilisha Manabii. Zaidi ya hapo kuweka pamoja Musa na Eliya, yaani Torati na Manabii, katika lugha ya kibiblia maana yake ni ufunuo wa Maandiko Matakatifu. Torati na Manabii ni neno lililotumika kumaanisha Maandiko Matakatifu katika Agano la Kale. Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unasema hivi; “Moyo wangu umekuambia, Bwana, uso wako nitautafuta, usinifiche uso wako” (Zab. 27:8-9). Yesu Kristo, Mwana pekee wa Mungu, amekuja kutuonesha ukuu wa Mungu, kutufunulia wema, upendo na huruma yake. Ndiyo maana Mungu Mwenyewe anatutaka tumsikilize Yeye. Ni katika tumaini hili Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, umetuamuru tumsikie Mwanao wa pekee. Upende kutulisha neno lako ndani yetu. Nasi tukiisha takata, tufurahi kuuona utukufu wako”. Yesu ni ufunuo wa utukufu, wema, upendo, na huruma ya Mungu kwetu sisi wanadamu. Naye anatuhimiza kuwa tukitaka kuuona utukufu, wema, upendo na huruma ya Mungu kupitia Yeye, lazima tuwaonee huruma na kuwasaidia ndugu zetu wahitaji, tukitembea nao kwa pamoja kama mahujaji wa matumaini kama anavyosisitiza Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wa Kwaresima kwa mwaka 2025, na kumwilisha ndani mwetu utamaduni wa kuwatendea matendo ya huruma. Mababa Askofu Katoliki Tanzania, TEC wakilitambua hili, katika ujumbe wao wa Kwaresima 2025 wanasema hivi; Vitu vinavyotuwezesha kusimama imara katika imani ambavyo ni dira na mwongozo wa maisha yetu ya kikristo ni matendo ya huruma ya kiroho: Kuwaelimisha wajinga, kuwashauri wenye mashaka, kuwaonya wakosefu, kuwavumilia wasumbufu, kuwasamehe wanaotukosea, kuwafariji wenye huzuni na kuwaombea wazima na wafu. Kisha tumwilishe ndani mwetu matendo ya huruma ya kimwili: kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu, kuwavika walio uchi, kuwakaribisha wageni, kuwahudumia wagonjwa, kuwatembelea wafungwa, na kuwazika wafu.
Somo la kwanza ni la Kitabu cha Mwanzo (Mwa 15:5-12,17-18). Somo hili linahusu Agano kati ya Mungu na Ibrahamu baba wa imani. Alama na ishara ya Agano hili ni moto, alama wazi ya uwepo wa Mungu, uliopita juu ya nyama alizoziandaa Ibrahamu. Nayo Imani ya Ibarahimu kwa Mungu inajidhihirisha kwa jinsi alivyoweka matumaini yake yote kwake tangu siku alipoitwa na kuitika, hata katika majaribu alibaki mwaminifu kwa Mungu. Itakumbukwa kuwa Ibrahimu aliitwa na Mungu akiwa na miaka 75, ili aiache nchi yake, mali zake na jamaa zake aende mpaka nchi asiyoifahamu. Ibrahamu kwa Imani alitii sauti ya Mungu “akaenda kama Bwana alivyomwamuru” (Mwa 12:4), akafika Kaanani, Mungu akamwahidi kumpa nchi na ardhi hiyo kuwa mali yake, yeye na uzao wake (Mwa 15:18), utakaotoka katika viuno vyake (Mwa 15:4), licha ya uzee wake na utasa wa mkewe Sarah. Ni katika muktadha huu, Mungu alifunga Agano na Ibrahimu kama ilivyokuwa desturi ya watu wa wakati huo – walichinja mnyama/mmoja au zaidi na kumpasua katikati vipande viwili na kuviweka kwa kutazamana. Katikati ya vipande hivi viwili, waliacha njia ya kupita kwa wadau wa agano wakati wa kula kiapo, ishara kwamba, yeyote atakayeenda kinyume na kiapo cha Agano hilo, adhabu yake ni kifo. Kwa kufuata utamaduni huu, Ibrahamu alichinja mwana ndama wa miaka 3, mbuzi mke wa miaka 3, na kondoo dume wa miaka 3, akawapasua katikati vipande viwili viwili na kuvipanga kuelekeana kama ilivyokuwa desturi. Tunasoma hivi; “Ikawa, jua lilipokuchwa, giza likaingia, tazama, tanuru ya moshi na mwenge unaowaka ulipita kati ya vile vipande vya nyama. Siku ile Bwana akafanya Agano na Ibrahimu, akasema; uzao wako nimewapa nchi hii, kutoka mto wa Misri mpaka huo mto mkubwa, mto Efrati.”
Mungu kwa upendo na huruma yake alijishusha na kufanya Agano na Ibrahimu, na kumfanya kuwa Baba wa imani, ambaye kutoka kwake taifa teule la Israeli lilizaliwa kwa maandalizi ya kumpokea Mkombozi Yesu Kristo. Hivyo kutoka katika viuno vya Ibrahimu, alizaliwa Isaka - Ahadi ya Mungu (Mw. 21:1-6). Kutoka viuno vya Isaka walizaliwa – Esau na Yakobo (Mw. 25:26-27). Na kutoka viuno vya Yakobo, walizaliwa watoto 12 wa kiume, ndiyo makabila 12 ya Israeli (Mw. 27:1-37:1). Hawa wote walikuwa ni wazao wa Ibrahimu kadiri ya mwili. Kutoka kwa ukoo wa uzao wa Ibrahimu amezaliwa Yesu Kristo (Mt. 1:1-17), na kutokana na Yesu Kristo, taifa takatifu na la milele - Kanisa - limezaliwa. Sisi sote ndio taifa jipya la Mungu na kwa sababu hiyo tuna haki ya kumwita Ibrahimu, Baba yetu wa Imani. Ni katika muktadha huu mzaburi katika wimbo wa katikati anasema hivi; “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, nimhofu nani? Ee Bwana, usikie, kwa sauti yangu ninalia, unifadhili, unijibu. Moyo wangu umekuambia, Bwana, uso wako nitautafuta, usinifiche uso wako, usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira. Umekuwa msaada wangu, usinitupe, wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu. Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana, katika nchi ya walio hai. Umngoje Bwana, uwe hodari, upige moyo konde, naam, umngoje Bwana (Zab. 27:1, 7-9, 13-14). Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi (Filp 317-4:1). Katika somo hili Mtume Paulo anawaonya Wafilipi wajihadhari na wale wanaotaka kuwashurutisha washike torati ya Wayahudi ili wawe Wakristo, wafuate mfano wake aliyeweka tumaini lake kwa Yesu Kristo peke yake, atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake.
Injili ni kama ilivyoandikwa na Luka (Lk 9:28-36). Sehemu hii ya Injili inatupa simulizi la kugeuka sura Bwana wetu Yesu Kristo mlimani Tabor. Tukio hili lilitokea wakati Yesu ameenda kusali pamoja na wanafunzi wake watatu – Petro, Yohane na Yakobo. Ni katika kusali, sura yake iligeuka, na mavazi yake yakawa meupe, yakimeta-meta, Musa na Elia wakatokea wakiwa katika utukufu, wakanena naye habari za kifo chake na baadae wanatoweka. Kisha sauti ikatoka katika wingu ikisema; “Huyu ni mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye.” Lakini kwa nini Yesu aliwachukua wanafunzi watatu tu na sio wote? Kwa nini aligeuka sura mbele yao? Uwepo wa Musa na Eliya na baadae kutoweka maana yake ni nini? Kwanza kabisa tukio hili lilitokea baada ya Petro kukiri kuwa Yesu ni “Mwana wa Mungu na Masiha,” na baada ya Yesu kusema kuwa imempasa kupata mateso mengi, kukataliwa na wakuu wa makuhani na wazee na waandishi, kuuawa kifo cha msalaba na kufufuka siku ya tatu. Tamko hili lilikuwa kikwazo cha mitume, wengine wakarudi nyuma na kukatokea majibizano kati ya Petro na Yesu. Petro akisema haiwezekani mambo haya kutokea, naye Yesu akamkemea na kumwambia; “Rudi nyuma yangu shetani wewe maana unawaza ya binadamu sio ya Mungu” (Mt. 16:22). Katika hali hii Mababa wa Kanisa wanatufundisha kuwa Yesu aliwachukua wanafunzi hawa watatu akawaimarishe kwa kuwaonesha utukufu atakaoupata baada ya mateso na kifo chake ili wakati wa majaribu wasitetereke bali wawaimarishe wenzao waweze kudumu katika imani, matumaini na mapendo. Imani kwa Petro, Baba Mtakatifu wa kwanza ili aweze kushuhudia Umungu wa Kristo bila mashaka. Ndivyo anavyoshuhudia mwenyewe akisema; “Hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu wa watu tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo, bali tuliona wenyewe ukuu wake” (2Pt.1:16ff). Matumaini kwa Yakobo mtume wa kwanza kuteswa na kufa shahidi kwa ajili ya Kristo na Mapendo kwa Yohane aliyemkabidhiwa kwa Mama yetu Bikira Maria naye kukabidhiwa kwake. Lakini pia idadi yao watatu ni ili kushuhudia kuwa tukio hili ni la kweli kwani kwa mila na desturi za Wayahudi, ushahidi wowote wa jambo kubwa na zito ili uweze kukubalika ilibidi utolewe na wanaume wawili na kuendelea (ushahidi wa wanawake na watoto haukuwa halali).
Kutokea kwa Musa na Eliya na kutoweka kwao ni ishara ya kuanza kutimia kwa yaliyoandikwa na kutabiriwa katika Agano la Kale. Musa akiwakilisha Torati/Sheria, na Eliya akiwakilisha manabii. Torati na manabii kwa pamoja zinajenga msingi wa utabiri wa ujio wa masiha Yesu Kristo. Bila ufunuo huu wa torati na manabii, Yesu Kristo angekuwa fumbo lisiloweza kufumbulika. Ndiyo maana baada ya ufufuko wake ili kuwafanya wanafunzi wa Emmaus waelewe maana ya Fumbo la mateso, kifo na ufufuko wake, aliwafunulia maandiko kuanzia Musa na manabii akiwaeleza mambo yaliyomhusu yeye mwenyewe (Lk 24:27). Hawa wawili kutoweka ni ishara kwamba, wakati wa kuwasiliana na Mungu kwa njia yao umekwisha, sasa kuwasiliana na Mungu ni kwa njia ya Mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo (Ebr. 1:1-4). Wingu jeupe ni uthibitisho wa uwepo wa Mungu na kuwa sauti iliyosema; “Huyu ni mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye” ni sauti yake Mungu. Hii ni kwa sababu katika Agano la Kale wingu lilikuwa ishara ya uwepo wa Mungu na mlima ni mahali patakatifu pa kukuta na Mungu. Mitume walipoonja utukufu wa Yesu alipogeuka sura na kung’aa, walifurahi sana, hata kutamani kuendelea kukaa huko. Sisi tunauonja utukufu huu katika Sakramenti ya kitubio. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba sadaka hii ifute dhambi zetu na kuwatakasa waamini wako mwili na roho, wapate kuadhimisha sikukuu ya Paska”. Kumbe kuingia katika maisha ya utukufu mbinguni, lazima tupambane kuacha dhambi, ambayo sio kazi rahisi bali ni ya kuteseka kama utangulizi wa dominika hii unavyosema; “Yeye aliwaambia mapema wafuasi wake kwamba atauawa; na pale katika mlima mtakatifu aliwaonyesha utukufu wake, akaonyesha kwamba kama ilivyoandikwa katika Torati na Manabii, atapata utukufu wa ufufuko kwa kuteswa”. Kwa namna hii tunaanza kuyaonja ya mbinguni tungali bado duniani kama Mama Kanisa anavyosali katika sala baada ya Komunio anapohitimisha maadhimisho ya dominika hii akisali; “Ee Bwana, baada ya kupokea mafumbo yako matakatifu, tunataka kukushukuru, kwa maana ingawa tuko bado hapa duniani watushirikisha ya mbinguni." Na hili ndilo tumaini letu.