Tafakari Dominika ya Kwanza Kwaresima Mwaka C: Vishawishi na Majaribu Katika Maisha
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima, mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa. Ni kwaresima ya kipekee kabisa kwa sababu iko ndani ya Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025 unanogeshwa na kauli mbiu “Tutembee kwa pamoja katika matumaini.” Kwaresima ni kipindi cha imani na matumaini; toba na wongofu wa ndani, ili kukumbatia na kuambata huruma na upendo wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa mtu mmoja mmoja na kama Jumuiya ya waamini. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya hija ya imani na matumaini, kama ilivyokuwa kwa Waisraeli, waliotembea Jangwani kwa muda wa miaka arobaini, wakapata fursa ya toba na wongofu wa ndani. Hii ni safari ya pamoja kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, kwa kutoka katika ubinafsi wao na hivyo kujielekeza katika ujenzi wa umoja kwa kujitambua kwamba, wao wote wamekuwa ni wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Rej. Gal 3:26-28, mwaliko wa kuweka nia ya kuweza kufikia lengo kwa kusikilizana katika upendo na uvumilivu. Na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC katika ujumbe wao wanatuhimiza hivi; “Simameni Imara katika Imani.” Ni kipindi cha toba, na Mwenyezi Mungu katika maneno ya wimbo wa mwanzo anatoa ahadi hii kwa kila anayefanya toba ya kweli; “Ataniita nami nitamwitikia; nitamwokoa na kumtukuza; kwa siku nyingi nitamshibisha” (Zab. 91:15-16). Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi, utujalie tuzidi kuifahamu siri ya Kristu na kupata manufaa yake katika mwenendo wetu mwema kwa mfungo wa Kwaresima wa kila mwaka.”
Somo la kwanza ni la kitabu cha Kumbukumbu la Torati (Kumb. 26:4-10). Sehemu hii ya somo hili inahusu maelekezo ya Musa kwa waisraeli ya namna walivyopaswa kumtolea Mungu sadaka ya shukrani baada ya kuingia nchi ya ahadi, Kaanani. Hivyo anawakumbusha mpango wa Mungu wa kumkomboa mwanadamu tangu kumwita na kumteua Ibrahimu kuwa baba wa mataifa yote mpaka walipotoka utumwani Misri na kuingia katika nchi ya Kaanani. Itakumbukwa kuwa Mungu alimpa Ibrahimu ahadi mbili: ardhi ya Kaanani kuwa mali yake na uzao wake (Mwa 15:18-21), na mrithi wa uzao wake mwenyewe, Isaka baba ya Esau na Yakobo (Mwa 17: 15), baba ya makabila 12 ya Israeli.Kutokana na wivu, watoto wa Yakobo walimuuza ndugu yao Yosefu, kwa wafanyabiashara waliokuwa wanaelekea Misri nao wakamuuza huko. Kwa mkono wa Mungu, Yosefu akawa kiongozi mashuhuri, baada ya kutafrisi ndoto ya Farao ya kuwa kutakuwa na shibe miaka 7 na njaa miaka 7, hivyo yeye akateuliwa kukusanya chakula katika miaka 7 ya shibe. Wakati wa miaka 7 ya njaa ulipowadia, Yakobo na familia yake walifika Misri kutafuta chakula. Farao kwa heshima ya Yosefu aliwapa ardhi ili wapate kuishi huko. Ni katika ardhi hii Yakobo alifariki huko katika uzee wake. Baada ya Farao asiyemjua Yosefu kuchukua madaraka na baada ya kifo cha Yosefu, Wamisri waliwageuka Waisraeli, wakawafanya watumwa wao, wakawatumikisha kwa kazi ngumu na kuwatesa sana. Nao walipomlilia Mungu, alisikia sala zao, akawakomboa kwa mkono wa Musa na kuwaongoza mpaka nchi ya ahadi kwa miujiza mingi aliyoifanya mbele ya Farao na watu wake, akiwapiga kwa mapigo saba, la mwisho likiwa ni kuwaua wazaliwa wa kwanza wote wa Wamisri, akiwamo mtoto wa Farao. Mungu aliwafungulia Waisraeli Bahari ya Shamu, ikawa njia kavu nao wakavuka, lakini majeshi ya Farao na magari yao akayateketeza kwa maji. Kwa sababu ya kukosa imani kwa Mungu wao, iliwachukua miaka 40 kwao kutangatanga jangwani kabla ya kufika nchi ya ahadi. Baadae, kwa uwezo wa Mungu wakiongozwa na Yoshua walipigana vita vingi na kuwashinda watu walioishi katika ardhi ya Kaanani, wakawafukuza na kuikalia ardhi yao. Hivi ndivyo Mungu alivyotimiza ahadi aliyomwapia Ibrahamu: “Nitawapa uzao wako ardhi hii iwe yao” (Mwa 15:18).
Kabla ya kuingia katika nchi ya ahadi, Mungu aliwapa maagizo matatu. Kila mzaliwa wa kwanza wa binadamu na wa wanyama ni mali Yake (Kut 13:1, 11-14; 22:29; Hes 18:16) - watoto watatumikia hekaluni na wanyama watatolewe kama dhabihu hekaluni. Lakini mzaliwa wa kwanza wa punda atakombolewa kwa mwanakondoo, na ambaye hakutaka kumkomboa alipaswa kumvunja shingo. Na pia mzaliwa wa kwanza wa wanadamu anaweza kukombolewa kwa kutoa sadaka ya mwanakondoo au njiwa 2 (Kut. 13:13). Mazao ya kwanza kutoka shambani ni mali ya Bwana (Kut 22:29-30). Ilikuwa ni katika ibada ya kutolea yale waliyoamriwa na Mungu, Waisraeli walirudia ahadi ya Imani kwa Mungu. Hivi ndivyo somo la kwanza linavyotueleza jinsi waisraeli walivyokiri upendo wa Mungu kwao na kumtolea dhabihu za shukrani. Somo hili linatukumbusha hali yetu ya utumwa na mateso yatokanayo na dhambi na kwamba ni Mungu tu ndiye awezaye kutukomboa kwa mkono wake kwa njia ya Kristo Yesu aliye njia, ukweli na uzima. Kwa ubatizo tulivuka bahari ya Shamu, tulivuka dimbwi la utumwa wa dhambi. Kristo kama Musa mpya anatuongoza katika jangwa la dunia hii akitupeleka katika nchi ya ahadi – mbinguni. Kila mara hata sisi tunaasi njiani na kurudia maisha ya kale, utumwa wa dhambi. Kwaresima ni kipindi cha kujitafakari na kumrudia Mungu. Ni safari ya pamoja kama anavyosisitiza Baba Mtakatifu Francis katika ujumbe wa Kwaresima wa mwaka huu 2025 akisema; “Tutembee kwa Pamoja kwenye Matumaini”. Kama Waisraeli walivyotembea kwa pamoja kuelekea nchi ya ahadi nasi tutembee kwa pamoja bila kumuacha yeyote yule katika hali ya kuteseka peke yake tunapoelekea Mbinguni kwa Mungu Baba.
Ni katika muktadha huu Mzaburi katika wimbo wa katikati anasema hivi; “Ee Bwana, uwe pamoja nami katika taabu zangu. Aketiye mahali pa siri pa Aliye juu, atakaa katika uvuli wake Mwenyezi. Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini. Mabaya hayatakupata wewe, wala tauni haitaikaribia hema yako. Kwa kuwa atakuagizia Malaika zake, wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuchukua, usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Utawakanyaga simba na nyoka, mwana- simba na joka utawaseta kwa miguu. Kwa kuwa amekaza kunipenda, nitamwokoa na kumweka palipo juu, kwa kuwa amenijua jina langu. Ataniita nami nitamwitikia; nitakuwa pamoja naye taabuni, nitamwokoa na kumtukuza” (Zab. 91:12, 10-15). Somo la pili ni la waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 10:8-13). Somo hili linatueleza jinsi Mungu wakati wa Agano la Kale, alivyowafunulia watu mapenzi yake kwa njia na hali tofauti tofauti. Lakini katika Agano Jipya, Yuko kati yetu kwa njia ya Yesu Kristo aliyekufa na kufufuka, naye anayemwamini ataokoka. Hivyo kumkiri Yesu kwa kinywa ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni kuwa Mungu alimfufua katika wafu, ni njia sahihi ya kupata wokovu. “Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena; Kila amwaminiye hatatahayarika kamwe”. Kumbe kipindi hiki cha kwaresima tuweke matumaini yetu kwa Yesu Kristo, Bwana na mwokozi wa maisha yetu, tukifanya toba ya kweli kwake aliyetukomboa kwa mateso, kifo na ufufuko wake, Yeye atatuokoa na hatari zote na kifo. Ni katika tumaini hili Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Kwaresima 2025, akimnukuu Mtume Paulo anakihoji kifo akisema; “Kuko wapi Ewe mauti kushinda kwako? Uko wapi Ewe mauti uchungu wako?” …Lakini ashukuriwe Mungu, Yeye atupaye ushindi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo (1Kor. 15:55-56). Kifo kimeshindwa na Upendo wa Mungu. Nasi tuna uhakika kuwa hakuna cho chote kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu” (Rm 8:37-38).
Injili ni kama ilivyoandikwa na Luka (Lk. 4:1-13). Nayo inahusu majaribu ya Yesu aliyoyapata baada ya kufunga kwa muda wa siku arobaini, yaani mda wa kutosha, usiku na mchana, huko jangwani akidumu katika kusali. Katika mazingira hayo ya upweke na kuona njaa, shetani anamjaribu kwa majaribu matatu. Jaribu la kwanza ni hitaji la kimwili – kufanya muujiza wa kubadili jiwe kuwa mkate. Jaribu la pili ni la tamaa ya mali, mamlaka na madaraka – Ibilisi anaahidi kumpa Yesu enzi na fahari kama atamshujudia Yeye badala ya Mungu. Na jaribu la tatu ni la kumjaribu Mungu – Ibilisi anamwambia Yesu aujaribu uaminifu wa Mungu kwa kujitupa chini ili amtumie Malaika wamuokoe. Katika majaribu haya yote, shetani alitumia nukuu za Maandiko Matakatifu yanayothibitisha na kuidhinisha kila jaribu. Yesu naye ananukuu Maandiko Matakatifu kumjibu shetani: “Mtu hataishi kwa mkate tu” (Kumb 8:3); “Usimjaribu Bwana Mungu wako” (Kumb 6:16); “Msujudie Bwana Mungu wako na umtumikie Yeye peke yake” (Kumb 6:13). Ujumbe msingi hapa ni huu, tujijengee utamaduni wa kulisoma, kulitafakari na kuliishi Neno la Mungu maana ndiyo silaha madhubuti ya kupambana na kumuangamiza shetani. Tukifanya hivyo tutamshinda shetani na hila zake na kuingia katika furaha ya milele. Mama Kanisa anapotuwekea simulizi la majaribu ya Yesu mwanzoni mwa kipindi hiki cha Kwaresima ni kutuonyesha kuwa tunaingia katika mapambano dhidi ya mwovu, na mapambano haya yanaanzia ndani ya nafsi zetu, ndani kabisa mwa mioyo yetu. Tupambane na majaribu ya kutafuta mamlaka, kupenda vitu kuliko kumpenda Mungu. Tusitafute mamlaka, ufahari, na nguvu kwa kila namna hata kwa nguvu za giza na mauaji ya watu wengine.
Tukumbuke daima kuwa katika maisha yetu Shetani daima anatujaribu, na anatuacha tu kwa muda. Ndivyo alivyofanya kwa Yesu kama Injili inavyosema; “Basi alipomaliza kila jaribu, ibilisi akamwacha, akaenda zake kwa muda” (Lk 4:13). Nasi tuwe tayari kila wakati na kila mda kupambana na vishawishi vya mwovu shetani katika maisha yetu ya kila siku. Tusiogope maana silaha za kumwangamiza shetani na vishawishi vyake tunazo nazo ni bora kabisa. Sala ya utangulizi wa Dominika hii ya kwanza ya Kwaresima inaziweka wazi ikisema; “Yeye alifunga chakula siku arobaini, akaonyesha ubora wa namna hiyo ya kufanya kitubio. Amewaepusha watu wote na hila za nyoka wa kale na kutufundisha kushinda chachu ya uovu.” Kumbe, sala na mafungo ni silaha za kumuangamiza ibilisi. Tutambue kuwa; “Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu” (Mt. 4:4). Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala baada ya Komunio anahitimisha maadhimisho ya dominika hii akisali hivi; “Ee Bwana, sisi tumekula mkate wa mbinguni unaolisha imani, unaoleta tumaini, na kuzidisha mapendo. Tunakuomba utuwezeshe kumtamani Yeye aliye Mkate hai wa kweli, tuweze kuishi kwa kila neno litokalo katika kinywa chako”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo.