Tafakari Neno la Mungu Dominika ya Kwanza Kwaresima Mwaka C: Vishawishi Jangwani
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Mpendwa msikilizaji na msomaji wetu, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu kutoka Studio za Radio Vatican. Maisha ni safari… katika safari hiyo mchakamchaka ni mkubwa ukibeba mambo mengi mema na mabaya kimwili, kijamii na kiroho hivi upo uwezekano wa kuchoka na kujisahau. Katika mazingira hayo Mama Kanisa ametuzawadia kipindi cha Kwaresima ili “kupunguza mwendo” na “kupumua” ili kujipatia tena nguvu mpya safari iweze kuendelea. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025 unanogeshwa na kauli mbiu “Tutembee kwa pamoja katika matumaini.” Kwaresima ni kipindi cha imani na matumaini; toba na wongofu wa ndani, ili kukumbatia na kuambata huruma na upendo wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa mtu mmoja mmoja na kama Jumuiya ya waamini. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya hija ya imani na matumaini, kama ilivyokuwa kwa Waisraeli, waliotembea Jangwani kwa muda wa miaka arobaini, wakapata fursa ya toba na wongofu wa ndani. Hii ni safari ya pamoja kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, kwa kutoka katika ubinafsi wao na hivyo kujielekeza katika ujenzi wa umoja kwa kujitambua kwamba, wao wote wamekuwa ni wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Rej. Gal 3:26-28, mwaliko wa kuweka nia ya kuweza kufikia lengo kwa kusikilizana katika upendo na uvumilivu. Jangwa ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza kutoka katika undani wa mtu mwenyewe, yaani dhamiri nyofu. Hii ni chemchemi ya majibu ya Mungu katika sala. Ni mahali pa majaribu na kishwawishi kikubwa! Kumbe, jangwa, katika Biblia, ni mahala ambapo mtu anajitambua kuwa “ni nani” mbele ya watu na mbele ya Mungu. Kwaresima ni muda uliokubalika wa kuingia katika jangwa la maisha ya kiroho, yaani upweke, ili kusikiliza kile kinachotoka moyoni, ili hatimaye kukutana na ukweli wa maisha.
Masomo ya Dominika ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka C wa Kanisa yanaangazia kadhia muhimu za maisha ya Kikristo katika kipindi hiki cha Kwaresima. Hii ni pamoja na majaribu ya Yesu jangwani, na ushindi wake dhidi ya Shetani. Katika muktadha huu, kuna muunganiko mkubwa kati ya injili ya Mathayo 20:18 na masomo ya dominika hii: Yesu anatangaza wazi kuhusu mateso, kifo na ufufuo wake. Hii inatoa mwanga kwa kipindi cha Kwaresima, ambapo Wakristo wanajiandaa kiroho kwa kufunga, kujinyima na kuishi maisha ya toba ili kushiriki katika mateso ya Kristo. Ingawa Shetani alijaribu kumshawishi Yesu kwa kumtaka akubali fahari na nguvu za ulimwengu huu, Yesu alijibu kwa maneno ya maandiko, akithibitisha kuwa Mungu ndiye wa kwanza na wa pekee wa kumtumikia. Kwaresima ni majira ya kukua kama binadamu, kuishi maana halisi ya maisha, kuimarisha mahusiano na Mungu na wenzetu, kugeukia mbali na dhambi… ni msimu mahsusi kabisa wa kuongeza kitu cha ziada kwenye ratiba za kila siku… ni kipindi chema cha toba, mfungo na sadaka kwa wahitaji tukijiandaa kwa “tukio la Kristo!” Katika kipindi hiki, Wakristo wanaitwa kufuata mfano wa Yesu katika kujiweka kando, kuteseka, na kujitolea kwa ajili ya wokovu wa dunia. Kama ilivyo kwa Yesu alivyokutana na majaribu na kushinda, vivyo hivyo, katika kipindi hiki cha Kwaresima, Wakristo wanaitwa kupigana vita dhidi ya dhambi na majaribu ya ulimwengu. Madhumuni ya kipindi cha Kwaresima ni kujitahidi kufuata nyayo za Kristo, kujivua ubinafsi na kuwa na moyo wa kujitolea kwa wengine, huku tukikumbuka mateso ya Kristo kwa ajili yetu. Majira ya Kwaresima yanatuelekeza Getsemane kwa Kristo Mteseka, tumuone barazani mbele ya Pilato, tutembee naye kwenye vituo vya njia ya Msalaba, tukeshe naye mlimani Kalvari na tupumzike pamoja naye bustanini ndani ya kaburi lile jipya, halafu tunafufuka naye kisha haoo mbinguni pamoja naye… tunapotafakari tendo hilo kuu la Mwana mpendwa wa Baba tuone uchungu namna maisha yetu yanavyousaliti upendo huo, tujikumbushe maana ya maisha yetu na lengo la kuumbwa kwetu kisha tujipige vifuani tukisema “Ee Mungu utuhurumie sisi ni wenye dhambi” (Lk 18:13b)… tusiruhusu msimu wa Kwaresima upite bure, tuonje moyoni mwetu hitaji la kutubu na kuongoka.
UFAFANUZI: Mtakatifu Paulo, Mtume katika Somo la Pili (Rum 10:8-13) anatuambia “Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako na katika moyo wako” … Neno lenye pumzi ya Mungu, mwanga katika njia yetu, neno lenye kutupatia ufunuo wa kimungu, latuwezesha kumfikia Mungu na kuyajua mapenzi yake… tukiwa mwanzoni mwa msimu wa Kwaresima sharti tuongozwe na Neno la Bwana na hivi kupigana vita vya roho msimu huu wa Kwaresima na katika safari nzima ya maisha. Neno la Mungu linatusaidia kuelewa vema fundisho la Mwalimu wetu Mkuu Kristo katika Injili ya leo (Lk 4:1-13), kwamba maisha na majaribu/vishawishi ni chanda na pete… tazama, mwanadamu ana maelekeo ya kujiona mnyonge na mdhaifu wa daima asiyejiwezea kabisa akutanapo na majaribu makubwamakubwa ya maisha. Kristo kwa kushinda majaribu yake jangwani anatupa moyo na hamasa kwamba inawezekana kujaribiwa na kushinda kwa msaada wa Mungu. Jubilei ya Matumaini inaadhimishwa katika muktadha wa safari ya kiroho inayochochewa na wito wa kutafuta maisha bora na kwa ajili ya kuleta wokovu kwa watu wote. Ni mwaka wa kutafakari juu ya furaha na matumaini tunayopata kutoka kwa Kristo, hata wakati wa majaribu na shida. Katika muktadha wa Injili ya Matayo 20:18, ambapo Yesu anasema waziwazi kwamba atateswa na kuuawa, lakini pia atafufuka, matumaini ya Kikristo yana maana kuwa kifo hakushindi, bali ni mlango wa uzima wa milele.
“Lile neno li karibu nawe” … jaribu la kwanza la Kristo lilihusu ‘mlo’, naye Kristo licha ya njaa aliyokuwa nayo anajibu kwamba neno la Mungu ni muhimu zaidi “Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu” (Mt 4:4). Njaa ya neno la Mungu iwe kubwa zaidi kuliko ya chakula cha kawaida, tulitafute, tulisome, tuliishi. Limo katika Biblia, Mapokeo yake, mafundisho ya Mama Kanisa na kwa mifano ya maisha ya watakatifu... Katika hilo tunapata kujua lililo sahihi na lenye kumpendeza Bwana. “Lile neno li karibu nawe”… jaribu la pili la Kristo lilihusu ‘kumsujudia’ Ibilisi aliye baba wa uongo. Ni neno la Mungu lililomwezesha Kristo kumuondoa Ibilisi ‘mchezoni’ akisema ‘imeandikwa msujudie Bwana Mungu wako, umuabudu Yeye peke yake’ … huenda maisha yetu hayajampa Mungu heshima ipasayo, hapa na pale tumekuwa na mambo yetu tunayoyaabudu, labda ni watu, vitu, kazi, maeneo, fedha… ‘lile neno li karibu nawe’ nalo lakukumbusha leo ya kuwa ni Mungu pekee ndiye wa kuabudiwa. Matumaini ni nguvu inayotuongoza katika maisha yetu ya kila siku, kama ilivyo kwa Yesu mwenyewe aliyejua mateso yaliyokuwa mbele yake lakini aliendelea kwa imani. Katika kipindi cha Kwaresima, tujiulize: Je, tunaweza kuvumilia mateso yetu kwa matumaini ya Kristo? Huu ni muda wa kuimarisha imani yetu kwa Mungu, na kufanya kazi za huruma kwa ajili ya wengine. “Lile neno li karibu nawe”… jaribu la tatu la Kristo lilihusu ‘matumizi’ mabaya ya uwezo na karama za kimungu, kwamba Kristo ni mwanasarakasi wa kujirusha toka juu ya minara… ni neno la Mungu lililomthibitisha Kristo akajibu kwa upole wa kifasaha ‘imenenwa, usimjaribu Bwana Mungu wako’… inawezekana tumemjaribu Mungu kwa namna nyingi, Neno la Mungu Kwaresima hii lituguse, liturudishe kusudi tupatanishwe na Mungu katika Yesu Kristo Bwana wetu.
Mazoezi ya kiroho ya Kwaresima (kusali, kufunga na matendo ya huruma) ni mwiba kwa Ibilisi na malaika wake, anatuzuia kwa kila hali tuyapuuzie hivi tutegemee majaribu mengi zaidi wakati huu. Kristo alijaribiwa, sisi pia… Majaribu yajapo tusijikunyate, tuyafurahie, sababu imani yetu inapojaribiwa huzaa uvumilivu, uvumilivu hupelekea ukomavu, ukomavu unatupelekea ukamilifu na ukamilifu unatustahilishia taji ya uzima wa milele… “Lile neno li karibu nawe”… kwa njia ya neno, amesema Mt Paulo kwenye somo II (Rum 10:8-13), tunafaulu kumkiri Kristo kwa vinywa vyetu ya kuwa ni Bwana, na kuamini mioyoni mwetu ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu na hivi kuokoka. Basi tuamini kwa moyo ili tuipate haki, na kwa kinywa ili tuupate wokovu, hatutahayarika…. kwa njia ya neno la Mungu tunajipatia mioyo ya shukrani anavyoagiza Musa katika somo I (Kum 26:4-10). Tumtolee Mungu shukrani, sio tu ya mavuno mapya, bali ya mioyo yetu tukimrudishia Yeye sifa na utukufu katika kila jambo tunalofaulu kulifanya katika maisha yetu. Tutakiane Kwaresima ya baraka, tujivike hamu ya kufanya vizuri… si jambo jema kusherehekea Pasaka kama ratiba tu, tukio hilo litukute na hali njema kusudi litupatie athari chanya kiroho na kimwili… ‘lile neno lililo karibu nasi…’ lituongoze vema ili siku yetu ikifika tuimbe kwa furaha “alleluia” ya milele. Jubilei ya Matumaini katika muktadha wa Kwaresima inatufundisha kuwa, ingawa tunakutana na majaribu na changamoto, tunapaswa kuwa na matumaini kwa sababu Kristo alishinda kifo na alituambia kuwa katika yeye, tunapata uzima wa milele. Katika kipindi hiki, tunaitwa kujitolea kwa Mungu na kwa wema wa watu wengine, na kushiriki matumaini haya kwa njia ya huduma na imani. Tumaini hili linajenga matumaini kwa ajili ya wokovu wa dunia nzima, na linatuongoza kuelekea Pasaka, ambapo tunasherehekea ushindi wa Kristo dhidi ya kifo na dhambi.