杏MAP导航

Tafuta

Matumaini ni fadhila ya Kimungu inayomwezesha mwamini kutamani heri ya Ufalme wa mbinguni na uzima wa milele, kwa kutumainia ahadi za Kristo na kutegemea, siyo nguvu zao, bali msaada wa neema ya Roho Mtakatifu. Matumaini ni fadhila ya Kimungu inayomwezesha mwamini kutamani heri ya Ufalme wa mbinguni na uzima wa milele, kwa kutumainia ahadi za Kristo na kutegemea, siyo nguvu zao, bali msaada wa neema ya Roho Mtakatifu.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Kwanza ya Kwaresima Mwaka C: Tumaini Kwa Mungu

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025 unanogeshwa na kauli mbiu “Tutembee kwa pamoja katika matumaini.” Kwaresima ni kipindi cha imani na matumaini; toba na wongofu wa ndani, ili kukumbatia na kuambata huruma na upendo wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa mtu mmoja mmoja na kama Jumuiya ya waamini. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya hija ya imani na matumaini, kama ilivyokuwa kwa Waisraeli.

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., - Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi. Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 1 ya Kwaresma, Mwaka C wa Kanisa. Kwa kuadhimisha Jumatano ya Majivu, Kanisa linaanza kipindi kingine katika kalenda ya mwaka wa kanisa, kipindi cha Kwaresima. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025 unanogeshwa na kauli mbiu “Tutembee kwa pamoja katika matumaini.” Kwaresima ni kipindi cha imani na matumaini; toba na wongofu wa ndani, ili kukumbatia na kuambata huruma na upendo wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa mtu mmoja mmoja na kama Jumuiya ya waamini. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya hija ya imani na matumaini, kama ilivyokuwa kwa Waisraeli, waliotembea Jangwani kwa muda wa miaka arobaini, wakapata fursa ya toba na wongofu wa ndani. Hii ni safari ya pamoja kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, kwa kutoka katika ubinafsi wao na hivyo kujielekeza katika ujenzi wa umoja kwa kujitambua kwamba, wao wote wamekuwa ni wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Rej. Gal 3:26-28, mwaliko wa kuweka nia ya kuweza kufikia lengo kwa kusikilizana katika upendo na uvumilivu. Liturujia na Neno la Mungu Dominika ya kwanza ya Kwaresima inatualika, “kumtumainia Mungu” Maisha yetu yote yanamtegemea Mungu Baba yetu, anayetupenda, anayejua mahitaji yetu ya roho na ya mwili, anayetusamehe na kutuhurumia makosa yetu, anayetupa nafasi kila mara ya kuzifaidi ahadi zake kwetu. Amemtuma Mwanaye wa pekee, ili kuuangamiza utawala wa Shetani na kusimika kati yetu utawala wa Mungu. Ndugu wapendwa, tunapoanza safari yetu ya siku arobaini, tutafakari safari yetu ya maisha ya hapa duniani. Tupo jangwani kuelekea katika nchi yetu ya ahadi yaani mbinguni. Kama wana wa Israeli walivyojaribiwa kwa sababu ya changamoto walizokutana nazo za njaa na kiu sisi pia tutegemee katika safari yetu ya maisha tutajaribiwa. Yesu ameshinda vishawishi akituonesha nasi pia kuwa, sala, kufunga, na kumtumainia Mungu, vinatusaidia kushinda majaribu ya mwovu Shetani.

Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu na utakatifu wa maisha
Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu na utakatifu wa maisha   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Katika Dominika ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima, tumshukuru Mungu ambaye daima ni mwema na mwaminifu kwa ahadi alizoahidi kwetu (Kum 26:4-10). Tumtumainie yeye ili tushinde katika majaribu, taabu, magumu na vishawishi vya mwovu Shetani (Lk 4:1-13, Mt 4:4, Zab 91:1-2, 10-15) na tutambue thamani ya sadaka ya Kristo, ambayo kwayo amefanya Agano jipya na la milele kati yetu sisi na Mungu (Rom 10:8-13). Maana ya Kwaresima: Kwaresima imetokana na Neno la Kiingereza cha zamani (Old English) “Lencten” yaani “Spring season.” Ni kipindi ambacho mimea huanza kuchipua tena baada ya kusinyaa kutokana na baridi na barafu kali, ikiwa ni ishara tena ya matumaini, mwanzo mpya, maisha mapya, furaha na uhai. Katika muktadha wa Wakristo, Kwaresma yatokana na neno la Kilatini “Quadragesima”, yaani siku 40, ambapo ni muda wa kufunga na kufanya toba, kusali na kufanya matendo ya huruma, kama maandalizi ya maadhimisho ya fumbo kuu la Pasaka yaani, mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kutoka kwenye maana ya kwanza “lencten” au Spring season, Kwaresma kwetu ni muda ambapo kila mmoja anapata nafasi ya kuanza tena upya. Ni muda wa kukusanya tena nguvu rohoni za kuweza kusonga mbele katika safari yetu ya kueleka mbiguni. Baba Mtakatifu anatualika, “Tusafiri pamoja katika matumaini” sisi kama mahujaji wa matumaini hapa duniani kuelekea mbinguni. Tunaalikwa pia kusimama imara katika Imani (1 Kor 16:13), ujumbe unaotuongoza kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika kipindi hiki cha kwaresima. Mwisho, katika siku hizi zote, tunaalikwa kusali, kufunga na kufanya matendo ya huruma.

Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani
Kwaresima ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani   (Vatican Media)

Kwaresima ni kipindi cha kuimarisha na kuboresha imani, matumaini na mapendo kwa: kufunga na kusali; kwa kufanya toba na malipizi ya dhambi; kwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa; Kwa kusoma, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji.Lengo ni kujitakasa na kuambata utakatifu wa maisha, ili hatimaye, kushiriki furaha ya Kristo Mfufuka wakati wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana, huku wakiwa wamepyaishwa kwa neema ya Roho Mtakatifu. Waamini watambue kwamba wanaitwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwa watu wanaowazunguka na wale wote ambao Mwenyezi Mungu anawajalia fursa ya kukutana nao katika hija ya maisha yao, ili waweze kujaliwa mwanga na furaha ya Injili katika maisha yao. Mateso na kifo cha Kristo Msalabani, kiwe ni kikolezo cha toba na wongofu wa ndani kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anayesema: “Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.” Gal 1: 22-24. Waamini wajitahidi kuwa na kumbukumbu hai ya kukutana na Kristo Yesu katika maisha na utume wao. Ni wakati wa kuuvua utu wa kale na kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Kipindi cha Kwaresima kinasimikwa katika nguzo kuu nne: yaani; Sala, Kufunga, Neno la Mungu na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji.

Kwaresima ni hija ya Ubatizo, Sala, Kufunga na matendo adili na matakatifu
Kwaresima ni hija ya Ubatizo, Sala, Kufunga na matendo adili na matakatifu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Somo la Kwanza ni kutoka Kitabu cha Kumbukumbu la Torati 26:4-10. Somo la kwanza tulilolisikia, ni kutoka katika Kitabu cha Kumbukumbu la Torati. Wayahudi walikua na utamaduni na ibada ya kutoa malimbuko, yaani uzao wa kwanza wa Wanyama na mazao kwa ajili ya Mungu. Walifanya hivyo kama shukrani yao kwa Mungu, aliyewatoa utumwani, akatembea nao kwa miaka arobaini, akawatia nguvu katika nyakati ngumu za majaribu, na mwisho akawaingiza katika nchi ya ahadi ambapo walikaa kwa amani na utulivu. Hivyo walipaswa kuleta malimbuko yao mbele ya altare na kuhani aliyapokea na kuyaweka chini ya altare ya Bwana. Kisha watu walipaswa kusujudu mbele za Bwana na kusikiliza kwa makini historia namna Mungu alivyowatendea mambo makuu. Walikumbushwa mambo makubwa matatu. Kwanza, Mungu alivyomwita Abrahamu kutoka Mesopotamia hadi Kanaani, nchi aliyompa Bwana. Pili, walikumbuka namna Mungu alivyowatoa utumwani Misri kwa mkono wake wenye nguvu. Tatu, walikumbuka ahadi ya Mungu ya kuwapa nchi ya ahadi na baadaye namna Mungu kwa mkono wake alivyowapa nchi hiyo kuwa mali yao. Ibada hii ilifanyika kila mwaka ambapo walikumbuka na kuhaisha tena Agano ambalo walifanya na Mungu, ambalo kwalo walipata utimilifu wa ahadi za Mungu. Walimshukuru Mungu kwa zawadi ya ardhi yenye rutuba (gift of the Land), ukarimu wa Mungu (God’s providence), na zawadi ya ukombozi (Liberation). Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mambo manne ya kujifunza. Kwanza: Kwaresima inatukumbusha juu ya ukombozi wetu kutoka utumwa wa dhambi (New Exodus). Taifa la Israeli walikumbuka kila mara historia yao, walikumbuka namna Mwenyezi Mungu, Baba yao mwema na mwenye huruma alivyowatoa utumwani misri, na kuwapeleka katika nchi ya ahadi, alivyowatoa katika kifo na kuwapa uhai tena. Wakiyakumbuka hayo wanakumbuka pia Agano walilofanya na Mungu na kuweka ahadi ya kuanza tena upya, wanaiungama Imani yao kwa Mungu.

Kwaresima ni pindi cha sala, toba na wongofu wa ndani
Kwaresima ni pindi cha sala, toba na wongofu wa ndani   (Vatican Media)

Katika kipindi hiki cha Kwaresima, ni muda kila mmoja anapata nafasi ya kutafakari juu ya thamani ya wokovu wetu. Tunatafakari juu ya mapendo makuu ya Mungu, ambaye kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa mwanaye, ametutoa sisi sote kutoka katika utumwa wa dhambi. Nasi kwa njia ya ubatizo, tunakuwa hai tena kiroho, tunakuwa huru kutoka katika utumwa wa dhambi. Ni muda wa kuweka nia ya dhati ya kuacha dhambi, na vilema vyote, na mazoea mabaya ambavyo vinatufanya kufa kiroho. Pili: Mwenyezi Mungu ameweka Agano Jipya na la milele kati yetu sisi naye (New and Eternal Covenant). Katika siku ya kutoa malimbuko, taifa la Israeli walipata nafasi ya kukumbuka Agano walilofanya na Mungu. Kwa Agano hilo, wakawa watu wa Mungu na Mungu akawa Baba yao. Mwenyezi Mungu amefanya Agano jipya na la milele kwa njia ya Mwanaye mpendwa Yesu Kristo. Mwenyezi Mungu ametupenda hivi hata akamtoa mwanaye wa pekee ili kila amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele. Yesu amefanya Agano jipya na la milele kati yetu sisi na Mungu, kwa hilo sisi sote tunakuwa uzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu na watu wa milki ya Mungu (1Pet 2:9-10). Kila mmoja wetu akumbuke Agano alilofanya na Mungu, kwanza kabisa katika ubatizo wetu, tukawa watoto wa Mungu na watoto wa Mama Kanisa mtakatifu. Tumefanywa kuwa warithi wa ahadi za Mungu pamoja na Kristo. Kwaresima inatupa nafasi ya kuendelea kukiri imani yetu kwa Mungu, kuweka ahadi ya kuendelea kuwa waaminifu katika ubatizo wetu na maagano mengine tuliyofanya na Mungu kila mmoja kwa hali yake, ili tupate neema ya kufika mbinguni ilipo nchi yetu ya ahadi. Ndugu mpendwa sana, muda ni sasa, bado sijachelewa, bado hujachelewa. Mungu anayetupenda anatupa kila siku nafasi ya kuanza upya ili tusipotee bali tuupate uzima wa milele ambalo ndio lengo msingi la Mungu kutuumba sisi.

Kwaresima ni kipindi cha kujibidiisha kukutana na Kristo Yesu
Kwaresima ni kipindi cha kujibidiisha kukutana na Kristo Yesu

Tatu: Mwenyezi Mungu anatuimarisha kwa chakula cha mbinguni katika safari yetu hapa duniani (New Manna in the gift of the Eucharist). Walipomtolea Mungu dhabihu kila mara katika sikukuu ya majuma, Wayahudi walikumbuka jinsi Mungu mkarimu alivyowalisha na kuwashibisha kwa manna walipokuwa katika safari yao ngumu na yenye majaribu ya kuelekea nchi ya ahadi. Manna kwetu ni Ishara ya Ekaristi Takatifu, sadaka ya shukrani kwa Mungu kwa zawadi ya ukombozi. Kwaresima inatupa nafasi ya kutafakari ukarimu wa Mungu ambaye katika safari yetu ya maisha ya hapa duniani, alituachia chakula, yaani mwili wake na Damu yake Takatifu. Kama vile wana wa Israeli walivyohitaji nguvu ili waweze kusafiri kuelekea nchi ya ahadi, ndivyo nasi, tusafiripo katika ulimwengu huu ambapo kuna changamoto mbalimbali, majaribu mbalimbali tunahitaji nguvu rohoni. Nguvu hiyo tunaipata katika Ekaristi Takatifu, uwepo wa Mungu mwenyewe katika maumbo ya mkate na divai. Tukumbuke wajibu wetu wa kupokea Ekaristi Takatifu katika hali ya neema ili ituimarishe daima na kututia nguvu. Pia tunaye Yesu katika safari yetu, hatutembei peke yetu. Kila mmoja apate muda binafsi wa kukaa karibu zaidi na Yesu, lakini pia tutembee naye katika njia yake ya msalaba ili nasi kila mmoja wetu apate nguvu na ujasiri wa kutembea katika njia yake ya msalaba. Yesu yupo nasi, hatuna hofu na mashaka.

Kishawishi cha uchu wa mali na madaraka
Kishawishi cha uchu wa mali na madaraka   (AFP or licensors)

Nne: Mwenyezi Mungu anatuahidi nchi ya ahadi, ambapo yeye anatawala milele na milele (A new Promised Land). Wayahudi walipomtolea Mungu dhabihu walikumbuka Mungu alivyotimiza ahadi yake, alivyowapatia nchi ya ahadi, nchi ijaayo maziwa na asali. Ni Mungu mwaminifu, anayetimiza ahadi zake kwa watu wake. Kwaresima ni muda wa kutafakari wema na ukarimu wa Mungu katika maisha yetu ya kila siku. Kumshukuru kwa neema na baraka anazotujalia kila siku katika maisha yetu. Kumshukuru kwa uaminifu wake kwetu, kwa kutujibu sala na maombi yetu, kwa kutimiza kwetu ahadi zake kwa wakati wake. Tunamshukuru zaidi kwa kuwa alituahidia zawadi ya ukombozi na kweli wakati utimilifu wa nyakati ulipotimia akamleta kwetu mkombozi. Kwaresma kumbe inatukumbusha kila siku kuwa, uraia wetu sisi ni mbinguni, maisha ya hapa duniani ni ya kupita na kamwe tusiwekeze hapa, bali tuwekeze katika uzima wa roho zetu ili tufike mbinguni. Somo la Injili: Ni Injili ya Luka 4:1-13. Somo la Injili Takatifu kutoka katika Injili ya Luka, latueleza kuwa, mara baada ya Yesu kubatizwa, Roho Mtakatifu alimwongoza kwa muda wa siku arobaini kwenda nyikani ambapo alifunga. Mwinjili Luka anatueleza kuwa, “Yesu aliongozwa na Roho Mtakatifu” akisisitiza, utume wa Yesu utaongozwa na Roho Mtakatifu, aliyeshuka na kukaa juu yake katika Ubatizo wake pale Mtoni Yordani. “Kurudi kutoka Yordani” mwijili Luka anatueleza kuwa Yordani ilikua ni ishara ya mwanzo mpya, au ishara ya mabadiliko, kuanza upya pia katika kujaribiwa. Kisha Yesu anaongozwa na Roho kwenda jangwani. Jangwani ni sehemu ya kujaribiwa, tukirudi nyuma kutazama namna wana wa Israeli kwa miaka yao arobaini walivyojaribiwa kule jangwani (Exodus 34:28). Yesu mwana wa Mungu, anakua mtii kwa Baba na anashinda majaribu yote.

Vi vyema kujiaminisha kwa maongozi ya Roho Mtakatifu
Vi vyema kujiaminisha kwa maongozi ya Roho Mtakatifu   (ANSA)

Katika somo hili la Injili dominika ya leo tuna mafundisho manne ya kujifunza. Kwanza: Tunahitaji muda kujitenga, kuomba nguvu ya Roho Mtakatifu ili tuweze kufunga vyema (Personal encounter with God). Katika somo la Injili tumeona, Bwana wetu Yesu Kristo kabla ya kuanza rasmi utume wake, alikwenda jangwani kufunga na kusali. Na katika utumewe wake pia kila mara kabla ya kufanya jambo lolote Bwana wetu Yesu Kristo alisali alitundisha nasi sote hitaji la kuwa karibu na Mungu kwa njia ya sala. Kwaresima inatukumbusha wajibu wetu wa kuwa karibu na Mungu kwa njia ya sala. Ni muda kila mmoja anakumbushwa kuwa, njia pekee tunaweza kujenga urafiki na mafungamano na Yesu kwanza kabisa ni kwa njia ya sala. Tuaalikwa kujitenga na kusema na Mungu, juu ya mahitaji yetu mbalimbali ya roho na ya mwili. Tunaalikwa pia kuweka lengo, kuwa na nia maalumu muda huu ambapo tunapata nafasi ya kuwa karibu zaidi na Mungu. Muda huu wa siku arobaini ni mfano wa maisha yetu yote, kwamba hakuna namna tunaweza kuishi pasi na kutegemea nguvu ya Mungu. Tumwombe Roho Mtakatifu atuongoze kwa siku zote hizi arobaini, yaani siku zote za maisha yetu, atupe utulivu wa ndani ili kila mmoja ajizamishe kabisa katika sala na ili mfungo wetu huu uwe na manufaa ya kiroho kwetu sisi na kwa wale wote tunaowakumbuka katika sala zetu. Kila mmoja ajiulize, nipo karibu kiasi gani na Mungu? Mahusiano yangu na Mungu yapoje? Je ninamkumbuka Mungu pale tu ninapokutana na changamoto na magumu au ninamkumbuka Mungu wakati wote?

Kkwaresima ni kipindi cha Sala, Neno, Kufunga na Kusali
Kkwaresima ni kipindi cha Sala, Neno, Kufunga na Kusali   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Pili: Katika safari yetu ya maisha hapa duniani, tunakutana kila mara na vishawishi (trials and temptations). Bwana wetu Yesu Kristo akiwa jangwani, baada ya kufunga na kusali kwa muda wa siku arobaini mchana na usiku, alijaribiwa na Ibilisi. Lakini kwa kuwa alikuwa ameungana na Mungu, alimtumainia Mungu, Bwana wetu Yesu Kristo alivishinda vishawishi vyote vya ibilisi. Taifa la Israeli walijaribiwa na mara kadhaa walishindwa katika majaribu wakiwa katika safari yao jangwani kwa kuwa mara kwa mara walipoteza imani na matumaini yao kwa Mungu wao. Kumbe, imani thabiti inatufanya kushinda katika majaribu. Bwana wetu alijaribiwa, yeye ni Mungu, ni si hivyo tu, alikua katika kusali. Hii inatufundisha nasi kwamba katika maisha yetu ya kila siku tutajaribiwa. Kushinda kwetu katika majaribu kunategema ni kwa jinsi gani sisi tumeungana na Mungu wetu. Tunaposali zaidi ndivyo hivyo shetani anafanya jitihada ya kutaka kutuangusha. Nguvu ya sala ni kubwa kuliko hila za mwovu shetani. Tunaalikwa kuwa na imani thabiti kwa Mungu, kuungana naye kabisa ili akae ndani mwetu nasi tukae ndani mwake, na hivyo atatusaidia daima kushinda katika vishawishi. Tatu: Namna tunavyojaribiwa na jinsi tutakavyoshinda vishawishi. Bwana wetu Yesu Kristo alijaribiwa na Ibilisi katika mambo matatu. Nasi katika maisha yetu tunakutana na majaribu haya haya kutoka kwa mwovu shetani. Yesu kwa kuwa alimtegemea Mungu, alishinda katika vishawishi vyote. Kwanza: Njaa (Physical tempotations) Lk 4:3-4. Yesu akiwa katika kufunga, aliona njaa kwa kuwa kwa muda wa siku arobaini mchana na usiku alifunga na kusali. Ibilisi akijua hakika kuwa Yesu aliona njaa, basi anataka kumjaribu. Yesu alishinda jaribu hilo akitambua kuwa uhai wetu hautegemei tu chakula cha mwilini bali twamtegemea Mungu. Sisi nasi mara kadhaa shetani anatumia udhaifu, shida, matizo na changamoto zetu kutuangusha. Mara kadhaa tunapita katika dhiki nyingi, mateso, njaa, kiu, umaskini, dharau, manyanyaso, dhuluma upweke, haya yote yanatupa kishawishi cha kutafuta majibu ya haraka hata kwa njia ambazo hazimpendezi Mungu. Tutashinda ikiwa tutatambua kuwa njaa na kiu yetu itatulizwa na Mungu peke yake. Njaa yetu iwe daima kutimiza mapenzi ya Mungu. Njaa yetu iwe katika kumtafuta Mungu, kuishi na Mungu na tufe tukiwa na Mungu.

Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu na utakatifu wa maisha
Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu na utakatifu wa maisha   (Vatican Media)

Pili: Nguvu na mamlaka (Earthly power) Lk 4:5-8. Katika jaribu la pili, Shetani alimpandisha Kristo Yesu juu akamwonesha milki zote za ulimwengu. Anamwahidi kumpa Yesu milki zote ikiwa atamsujudia. Yesu anashinda jaribu hili akijua kuwa anayepaswa kuabudiwa ni Mungu peke yake. Tamaa ya nguvu, uchu wa mali na madaraka, sifa, utukufu na heshima vinaweza kutufanya tukamwacha Mungu. Tamaa ya haraka ya kupata utajiri na mali yaweza kutufanya tunakwacha Mungu wetu na kutafuta njia nyingine zisizo za kimungu. Mara kadhaa hekaheka za kidunia zinaweza kutufanya tukaona Mungu hana nafasi katika maisha yetu ya kila siku. Tukaona pengine kazi zetu, vyeo, utajiri, sifa, madaraka ndivyo vitu vya msingi katika maisha na hivyo tukavipa nafasi ya kwanza. Tunapaswa kutambua kuwa, vitu vyote tulivyo navyo ni mali ya Mungu hata sisi wenyewe. Hakuna kitu kinaweza kuchukua nafasi ya Mungu katika maisha yetu. Tufanye yote hali tukijua kua Mungu ana nafasi ya kwanza na ni yeye tu apaswa kuabudiwa na kutukuzwa, sio mali, sio vyeo wala utajiri wala madaraka.Tatu: Imani (Testing God) Lk 4:9-12. Mwisho Ibilisi anamjaribu Yesu Imani. Anampeleka Yesu mpaka kwenye kinara cha hekalu na kumwambia, “Ikiwa wewe ni mwana wa Mungu basi jitupe chini kwa maana imeandikwa, atakupelekea Malaika wake wakulinde…” Yesu alishinda kwa kumwambia Ibilisi kuwa haipaswi kumjaribu Mungu. Ndugu Wapendwa, katika maisha yetu kuna nyakati tuna wasiwasi juu ya uwepo wa Mungu kati yetu. Tuna wasiwasi juu ya nguvu ya Mungu inayotenda kazi ndani mwetu. Tuna wasiwasi juu ya uwepo halisi wa Yesu katikati yetu, katika sakramenti ya Ekaristi Takatifu na sakramenti nyingine, katika Neno lake takatifu, na pengine tunahitaji miujiza zaidi ili tuweze kuamini. Shetani anamtaka Yesu amjaribu Mungu. Mara kadhaa anatushawishi na sisi kumjaribu Mungu wetu. Tunaalikwa kuwa na Imani thabiti kwa Mungu wetu. Mungu anayetupenda, Baba yetu mwema, yupo katikati yetu, anatujua kila mmoja mpaka ndani kabisa ya mioyo yetu, anafahamu changamoto zetu na magumu mbalimbali, kufanikiwa na kushindwa kwetu, kuanguka na kuinuka kwetu, yeye anajua yote. Mwachie Yesu atawale. Mwachie Mungu atende kazi ndani mwako kwa wakati wake. Simama imara katika Imani.

Jangwani ni mahali pa mapambano ya maisha, sala na kufunga
Jangwani ni mahali pa mapambano ya maisha, sala na kufunga

Nne: Ibilisi mwishoni alimwacha Yesu, akaenda zake. Akitukuta imara atatuacha ataenda zake (devil’s departure). Baada ya Yesu kushinda katika majaribu yote, Ibilisi aliondoka akaenda zake. Aya hii yatuonesha tu kuondoka kwa muda kwa Ibilisi kutoka kwa Yesu. Bado katika utume wake na kazi ya ukombozi kwa ujumla, Yesu atakutana bado na majaribu, na kubwa zaidi akiwa Bustanini Gethsemane (Luke 22:39-46). Ibilisi alimjaribu Yesu mara zote Yesu alipoonekana dhaifu.Katika sehemu hii ya Injili ya Dominika ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka C, tunaambiwa, “Yesu aliona njaa” kwa kuwa Yesu alikua mtu kweli kama sisi. Hivyo kibinadamu aliona njaa na alikua dhaifu. Hali kadhalika akiwa Gethsemane ibilisi atakuja tena kumjaribu, katika mahangaiko yake kabla ya mateso. Kumbe tuwapo dhaifu, ndipo ibilisi anapata nguvu ya kutujaribu zaidi na zaidi. Yesu alimtumainia Mungu na hivyo alishinda katika majaribu yote. Ninakuombea ndugu mpendwa, ili uendelee kuwa imara zaidi na zaidi. Tambua kuwa unapolala kiroho ndipo shetani anashinda. Unapokuwa mbali na Mungu ndipo shetani anakuwa karibu nawe. Licha ya hayo yote, tumtumanie Yesu. Yeye alishinda, atatupa nasi nguvu za kushinda. Shetani atakwenda zake.Somo la pili: Ni Waraka wa Mtume Paulo Rom 10:8-13. Katika somo la pili, (Rom 10:8-13), Mtume Paulo anatufundisha kuwa, Mungu yupo kati yetu katika Yesu Kristo aliyekufa na kufufuka. Hivyo ili tufaidi, ahadi hii kubwa ya ukombozi, kwanza, kila mmoja apaswa kuamini moyoni nguvu na uweza wa Mungu aliyemfufua Yesu kutoka wafu. Pili, ikiwa tuna Imani thabiti kwa Yesu, hatutatayarika kamwe, tuna Imani kuwa tutashinda awapo karibu nasi. Tatu, ujumbe wa injili ya Kristo upo karibu na kila mmoja wetu na ni kwa ajili ya wote, Wayahudi hali kadhalika na Wayunani. Yesu atusaidie ili tumtumaini yeye aliye chanzo cha uzima wetu kwa njia ya Kristo Bwana wetu.   Hitimisho: Katika Dominika ya leo, tumshukuru Mungu ambaye daima ni mwema na mwaminifu kwa ahadi alizoahidi kwetu (Kum 26:4-10). Tumtumainie yeye ili tushinde katika majaribu, taabu, magumu na vishawishi vya mwovu shetani (Lk 4:1-13, Mt 4:4, Zab 91:1-2, 10-15) na tutambue thamani ya sadaka ya Kristo Yesu, ambayo kwayo amefanya Agano Jipya na la milele kati yetu sisi na Mwenyezi Mungu (Rom 10:8-13).

Mahubiri Kwaresima
08 Machi 2025, 15:20