Tafakari Dominika ya 8 Mwaka C wa Kanisa: Kibanzi na Boriti: Kujikosoa!
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., - Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 8 ya mwaka C wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika inatualika, “kuwa tayari kufundishwa na Kristo Yesu ili ndani mwetu yatoke matunda mema” Ili tuweze kuishi vyema ukristo wetu, na kuzaa matunda mema na yanayodumu, hatuna budi kukubali kuongozwa na kufundishwa na Kristo Mwalimu wetu. Katika somo la kwanza (Ybs 27:4-7) latueleza kuwa, hali ya mtu ya ndani inatambulikana kwa nje kwa njia ya maneno na matendo yake, hivi kwamba, yamtokayo ndiyo yaliyoujaza moyo wake. Mungu akiwa ndani mwetu, tutasema na kutenda daima yaliyo mema na yenye kumpendeza. Katika somo la Injili Takatifu (Lk 6:39-45), Yesu anatufundisha kuwa, mwalimu apaswa kutoa mfano mwema kwa wale anaowaongoza. Asiyekubali kufundishwa na kufanana na Mwalimu wake, huyo atawapoteza wengine. Sisi tunaongozwa na Kristo, kila mmoja apaswa kuishi kadiri ya mafundisho ya Kristo Mwalimu wetu ili aweze kuzaa matunda. Katika somo la pili, (1 Kor 15:54-58), Mtume Paulo anawaasa Wakorintho kuwa maisha haya ya duniani ni ya kupita tu. Mwili huu tulio nao utakufa na kuoza, lakini kwa kuwa tunamwamini Yesu, tuna hakika ya uzima wa milele. Anatusihi sote kuwa imara, kutotikisika na kuzitenda kwa uaminifu kazi za Bwana wetu Yesu Kristo Mwalimu wetu, kwa hizo tutapata tuzo ya uzima wa milele. Katika Dominika ya leo, tumshukuru Mungu (Zab 92:1-2, 12-15) ambaye alikuja kukaa kati yetu ili atufundishe njia iendayo kwa Baba. Tuombe neema yake, ili tuweze kuyashika mafundisho yake na kwa njia ya maneno na matendo yetu tuweze kuleta uponyaji wa kiroho na kimwili kwa wengine (Shangilio, Mt 4:23.)
Somo la Kwanza Ni Kitabu cha Yoshua bin Sira 27:4-7. Somo la kwanza tulilolisikia, ni kutoka katika kitabu cha Yoshua bin Sira. Kitabu hiki cha Yoshua bin Sira (Ecclesiaticus) kiliandikwa mnamo karne ya 2 B.C, na kilitumika sana katika Liturujia na mafundisho kwa wakatekumeni. Kadiri ya Utangulizi wa kitabu hiki (prologue), Yoshua bin Sira alikua ni mwandishi msomi (learned scribe), mnyenyekevu na mwenye bidii aliyeishi huko Yerusalemu. Kitabu kilikua na lengo la kuwakumbusha Wayahudi juu ya Imani yao. Ni kipindi ambapo utamaduni wa Kigiriki (Hellenistic culture) ulianza kuenea kwa kasi ambao ulikua kinyume kabisa na utamaduni na Imani ya Kiyahudi. Kwa sababu hiyo waliibuka watu wengi ambao walikua na falsafa mbalimbali. Katika somo hili la kwanza Yoshua bin Sira anatuonya kutokumsifia au kumuunga mkono mtu yeyote kabla ya kumsikiliza. Mwandishi atueleza kuwa, hali ya mtu ya ndani inatambulikana kwa nje, kwa njia ya maneno na matendo yake. Kumbe bila kuwa na hekima ya kimungu ni rahisi kupotoka na kuwapotosha pia wengine kwa njia ya maneno na matendo yetu ambayo yanadhihirisha wingi wa yaliyo ndani mwetu. Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mambo manne ya kujifunza. Kwanza: Tathmini binafsi ni muhimu katika maisha yetu (Self-reflection). Katika somo hili mwandishi anatumia mfano wa chekecheke vile inavyochuja na kutoa mbegu safi na kisha kuacha juu makapi. Anatualika kufanya tathmini ya ndani kabla ya kunena kwa kuwa maneno yetu yanaeleza kwa kina jinsi mioyo yetu ilivyo. Ndugu wapendwa, tunapokosa Hekima ya kimungu, hatupati nafasi ya kukaa kimya na kujitathmini kila mmoja ndani kabisa ya moyo wake. Ninapokosa hekima ya Kimungu sina nafasi ya kusema na moyo wangu, nikatambua makosa na udhaifu wangu. Matokeo yake moyo wangu utajazwa na sifa, majivuno, wivu, roho mbaya, ubinafsi, ulafi na mambo mengine mengi yaliyo kinyume na amri za Mungu. Maneno yangu yataeleza yaliyoujaza moyo wangu, na hivyo kuwa chanzo cha ugomvi na makwazo kwa wengine na kushindwa kuwaongoza kwa njia ya maisha yangu waone tunu za kimungu ndani mwangu. Kila mmoja ajitahidi kuwa na ukimya wa ndani, kuzungumza na Mungu ili atufundishe yale yanayotupasa kuwaza, kusema na kutenda.
Pili: Nyakati za changamoto zinatufanya tuwe imara, ili tuwaimarishe wengine (challenges make us strong and strengthen others). Mwandishi anatupa mfano wa pili kuhusu tanuru ya moto na vyombo vya mfinyanzi. Mfinyanzi huweka vyombo vyake ndani ya tanuru ili viwe imara lakini pia kumsaidia kutambua chombo ambacho pia ni dhaifu bado. Kumbe bila kuvipitisha vyombo vyake kwenye tanuru mfinyanzi hawezi kutambua uthabiti na uimara wa vyombo vyake. Ndugu wapendwa, mara kadhaa mimi na wewe tunapita katika majaribu mbambali katika maisha yetu. Tunapokua katika changamoto na majaribu ndio wakati wa kupimwa uthabiti wa Imani yetu ambayo yasadifu pia tabia yetu ya ndani. Kuna nyakati Mungu anatuacha tupite katika changamoto na magumu ili atuimarishe, tuwe imara katika mitazamo yetu, tuwe imara katika Imani, matumaini na mapendo, lakini pia kuwa fadhila ya uvumilivu katika kuwaza, kusema na kutenda kwetu. Ustahimilivu wetu unakua darasa kwa wengine, unawaimarisha pia wale ambao tunawaongoza, katika familia zetu, katika jumuiya zetu, makazini kwetu, nk. Tatu: Tukikubali kuongozwa na Mungu tutazaa matunda mema (fruitfulness of the tree depends on the care of its keeper). Mwandishi anatufundisha kuwa matunda ya mti huonesha ulimaji wake. Kumbe, mti huu ili uweze kuzaa matunda unahitaji utunzaji wa muda mrefu. Mungu wetu anatutunza na kutupa kila tunachohitaji ili tuweze kuzaa matunda mazuri. Na anatarajia tutoe matunda mema na mazuri kwa kuwa hakuna tulichohitaji ili tuweze kuzaa matunda ambacho Mungu hajatupatia. Ndugu wapendwa, Mungu mwenye rehema nyingi ametupa kila neema na baraka tunazohitaji katika maisha yetu sisi kama watoto wake. Hayo yote ametupa ili tuweze kuishi maisha mema, maisha mazuri na yenye kumpendeza. Mara kwa mara tunashindwa kuzaa matunda kwa kuwa hatutengenezi ndani mwetu mazingira na kuweza kustawisha mbegu inayopandwa ndani mwetu ili tuweze kuzaa matunda mengi. Tuombe neema ya Mungu ili yale yote tunayopokea kutoka kwa Kristo, Neno lake ambalo linapandwa ndani mwetu, sakramenti mbambali tunazopokea, vitusaidie katika kukua na kuzaa matunda kila mmoja kwa nafasi yake. Pia vitusaidie katika majiundo yetu ya ndani ili yatakayotoka ndani mwetu yasadifu kweli ukristo wetu.
Nne: Tukiongozwa na Mungu tutaweza kutofautisha walimu wa kweli na wale wadanganyifu (discerning between true and false teachers). Mwandishi anatuasa kuwa makini katika kusikiliza kabla ya kukubaliana na mtu au kumwuunga mkono katika jambo lake lolote. Tusiwe warahisi kuchotwa na maneno matamu ya watu kabla ya kuwasikiliza vyema na kulinganisha wanachosema na wanachofanya. Ndugu wapendwa, tunaishi katika nyakati zilizogubikwa na wimbi la manabii na walimu wengi ambao kila mmoja anakuja na falsafa zake, mawazo na mitazamo yake ili kuwapata wafuasi na kisha kurajirika. Mambo haya yalikua tangu zamani ndio sababu tunaona maandishi mbalimbali yakituonya juu ya uwepo wa walimu na manabii wengi wa uwongo. Bila kuomba hekima ya kimungu, hatuwezi sisi wenyewe kutambua hila za wale wanaotupotosha na kutupeleka kwenye njia isiyo sawa na ya kimungu. Pia sisi wenyewe kwa maneno yetu twaweza kuwa chanzo cha kuwapotosha wengine, kuwakwaza na kuwatoa katika njia njema ya uchaji kwa Mungu. Kama wazazi twaweza kwa maneno yetu kuwa sababu ya kupotea kwa watoto wetu, sababu ya kuvurugika kwa familia zetu, na mahusiano mema kati yetu sisi kwa sisi. Tuombe neema ya kuwa walimu wema kwa njia ya ushuhuda wa maisha yetu ya kila siku.
Somo la Injili: Ni Injili ya Luka 6:39-45. Somo la Injili Takatifu ni kutoka katika Injili ya Luka, bado ni sehemu ya hotuba yake akiwa bado nyikani (inayoanzia sura ya 6:17-49) na leo ni kuanzia aya ya 39-45. Katika sehemu hii ya Injili takatifu Yesu anatumia mifano iliyoeleweka kuelezea mambo makubwa matatu. Kwanza anaelezea kuhusu upofu, kwamba hakuna yeyote aliye kipofu anaweza kumwongoza kipofu mwenzake. Anatukumbusha daima kujifunza kutoka kwake ili tuweze nasi kuwa viongozi wazuri kwa wengine. Pili anatuonya juu ya unafiki, kutokuwa wepesi wa kuwahukumu wengine ilihali na sisi hatujitathmini ndani mwetu. Tatu anatutaka daima tujaze katika hazina yetu yaani mioyo yetu yale yaliyo mema ili kutoka humo yatoke daima yaliyo mema na yale yanayompendeza Mungu. Tutajaza mioyo yetu hazina njema ikiwa tutaungana kabisa na Yesu na kukubali kufundishwa naye. Katika somo hili la Injili dominika ya 8 Ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa tuna mafundisho matano ya kukazia. Kwanza: Tunapokuwa vipofu kwa sababu mbalimbali hatuwezi kuwaongoza wengine (spiritual blindness) Lk 6:39. Yesu anatumia mfano wa kwanza wa kipofu ambaye kwa vyovyote hawezi kumwongoza kipofu mwenzake. Katika tamaduni za wayahudi, upofu (blindness) ulimaanisha “ujinga” hasa katika muktadha wa mambo ya kiroho (spiritual blindness). Katika sehemu hii ya Injili upofu huu Yesu aliongea hasa juu ya mafarisayo ambao walifundisha watu ila wao hawakutaka kuelewa njia za Mungu wala kuyapokea mafundisho ya Kristo. Wakawapoteza watu. Shimoni (pit) ilikua ni ishara ya kuangamia au kuharibiwa (ruin/destruction). Ndugu wapendwa, katika maisha yetu ya kila siku sisi pia tunakua na upofu nyakati mbalimbali. Upofu wa kiroho, unatufanya kushindwa kutambua nafasi ya Mungu katika maisha yetu, kuwaza kuwa tunaweza kufanya mambo yote pasi na Mungu. Upofu huu unatufanya kushindwa kuona wema na uzuri wa Mungu ndani mwetu na ndani ya wengine na hivyo tunakosa hekima yake ndani mwetu inayotusaidia kuchagua mambo yenye kufaa kwa ajili ya wokovu wetu na wokovu wa wengine. Tunashindwa kuwaongoza wengine kumjua Mungu, kumpenda na kumtumikia kwa uchaji.
Pili: Tunapaswa kutamani na kujitahidi kila wakati kufanana na Kristo Mwalimu wetu (the goal of the disciple is to become like a Master) Lk 6:40. Yesu anatufundisha kuwa tunapaswa daima kukubali kufundishwa naye ili tufanane naye Mwalimu wetu. “Kuhitimu” (katartismenos) lilimaanisha kukamilishwa au aliyepewa vifaa vyote (fully equipped). Kumbe Yesu anatufundisha kuwa lengo la kuwa mfuasi wake ni kujitahidi kufanana naye. Ndugu wapendwa, sisi kila mmoja wetu ni mfuasi wa Yesu. Kwa ubatizo na kwa miito mingine mbalimbali, kila mmoja ni mfuasi wa Kristo. Ili tuweze kufanana na Kristo mwalimu wetu hatuna budi kuwa tayari kufundishwa naye, kukaa miguuni pake na kumsikiliza. Mafarisayo na waandishi hawakua tayari kukaa chini na kumsikiliza Yesu na matokeo yake waliwapotosha watu. Vivyo hivyo nasi pia tusipokua na muda wa kukaa miguuni pa Kristo Yesu na kumsikiliza hatutaweza kuyaelewa mafundisho yake ambayo kimsingi yanatufanya kufanana naye. Mara nyingi tunavutwa na mambo mengi. Huenda tumekua na muda mwingi kwa ajili ya mambo yetu na kusahau kumpa Yesu muda wetu, kukaa karibu naye, kujenga urafiki naye ili tufanane naye. Tujitahidi pia kupokea sakramenti za kanisa, ili Yesu daima akae ndani mwetu, na ufalme wake ukue ndani mwetu.
Tatu: Tunapaswa kujitathimi ndani mwetu na siyo kuwahukumu wengine (Self introspection before judging others) Lk 6:41-42. Yesu anatumia mfano kuelezea juu ya unafiki ambao ulikua ndani ya Mafarisayo na mara kadhaa umo pia ndani mwangu mimi na wewe. “Boriti” (plank/ karphos) ni kipande kikubwa sana cha mbao, kinaweza kuwa pia kigogo au nguzo, au mbao yoyote pana. “Kibanzi” (speck/dokos) ni kichembe kidogo sana cha mbao, kama mchanga au vumbi ambao ni ngumu sana kukiona. Katika mfano huu Yesu anatufundisha kuwa kwa hali ya kawaida kama huwezi/ siwezi kuona boriti (udhaifu mkubwa ndani yangu) au nguzo iliyosimama mbele ya macho yangu, siwezi kuona vumbi (udhaifu hata mdogo kabisa wa wengine) lililo ndani ya jicho la jirani yangu. Ndugu mpendwa, Yesu anatufundisha kwamba kila mmoja apaswa kujitazama kabisa ndani mwake ili aweze kutambua udhaifu ulipo ndani mwetu kabla yakuanza kuwahukumu na kuwanyooshea watu wengine vidole kwa sababu pengine ya udhaifu wao pia. Maisha yasiyo na tathmini sio maisha ya Kuishi. Hatupaswi kuwa wepesi kuwalaumu na kuwahukumu wengine kutokana na udhaifu wao, bali tunapaswa kuwaombea ili waweze kutambua pia udhaifu wao na kuweza kubadilika. Tuombe neema ya kuona pia mema na mazuri katika nafasi ya kwanza yaliyo ndani ya wenzetu. Mara nyingi tunatazama pengine yale madhaifu tu na kusahau kwamba yapo mengi na mazuri pia yaliyo ndani ya wenzetu. Licha ya kuwa na tathmini binafsi tunapaswa pia kumruhusu Mungu azitathmini njia zetu, mawazo na fikra zetu. Tukimpa Mungu nafasi ataweza kutufundisha na kutukumbusha udhaifu wetu na kuona hitaji la mabadiliko. Pia turuhusu kukosoloewa pia na wenzetu, wao waweza kuona udhaifu fulani ndani mwetu ambao hata sisi wenyewe hatuwezi kuuona. Tuwe wapole pale wenzetu wanapotufanyia pia tathmini na tuyafanyie kazi yale mazuri na yale madhaifu yatusaidie kujirekebisha, kukua na kukomaa zaidi.
Nne: Tukikubali kuongozwa na Kristo daima tutazaa matunda (united with Christ, we will always bare good fruits) Lk 6:43-44. Yesu anatufundisha kuwa hakuna mti mzuri (kalon dendron) uzaao matunda mabaya (sapron kadron) wala mti mbaya (sapron dendron) uzaao matunda mazuri (kalon kapron). Kila mti hutambulika kwa matunda yake, mti mbaya matunda mabaya hali kadhalika mti mzuri matunda mazuri. Matunda hapa yamaanisha mawazo yetu, matendo na mitazamo yetu inayoonesha hali yetu ya ndani. Ndugu mpendwa, kila aliyeungana na Kristo anatarajiwa kuzaa matunda mema kwa kuwa Kristo aliye mzabibu wa kweli anaturutubisha sisi tulio matawi yake ili tuzae matunda (Yn 15:4-5). Matunda mema tunayopaswa kuzaa ni yale anayotuambia Mtume Paulo katika Waraka wake kwa Wagalatia sura ya 5:22. Upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, Fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Tuombe neema ya kuungana daima ya Yesu mwalimu wetu ili tuweze kujulikana kwa matunda yetu. Ndani mwetu yasitoke matunda mabaya wala watu wasitegemee kuona yaliyo nje ya ukristo wetu ndani mwetu. Tano: Mabadiliko ya kweli huanzia ndani kabisa mwa mtu (true transformation comes from within) Lk 6:45. Mwisho kabisa Yesu anatufundisha kuwa mabadiliko ya kweli huanzia ndani kabisa ya moyo wa mtu, hali kadhalika upotofu huanzia ndani ya moyo wa mtu. Maana ni katika moyo ilipo hazina yetu. Ndugu mpendwa, kumbe sote tunapaswa kulinda sana mioyo yetu kwani ndipo mawazo na matendo yetu yote huchipukia. Moyo ulio tayari kubadilika utatoa matokeo yake nje hali kadhali na moyo mgumu utatoa matunda yake nje. Tuijaze mioyo yetu kwa mambo mema, kwa fadhila za kimungu na hizo zitatuongoza kutoa kutoka katika hazina yetu yale yaliyo mema na yenye kumpendeza Mungu. Nini kimeujaza moyo wangu? Nini kimeujaza moyo wako? Yesu akae ndani mwetu daima ili aijaze mioyo yetu.
Somo la pili: Ni Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo 1 Kor 15:54-58. Katika somo la pili, (1 Kor 15:54-58), Mtume Paulo anawaasa Wakorintho kuwa maisha haya ya duniani ni ya kupita tu. Mwili huu tulio nao utakufa na kuoza, lakini kwa kuwa tunamwamini Yesu, tuna hakika ya uzima wa milele. Anatusihi sote kuwa imara, kutotikisika na kuzitenda kwa uaminifu kazi za Bwana wetu Yesu Kristo Mwalimu wetu, kwa hizo tutapata tuzo ya uzima wa milele. Kumbe katika maisha yetu ya hapa duniani, tukijua kabisa kuwa ni ya kupita na kwamba ni maandalizi ya maisha mapya ya utukufu, daima tutakua tayari kufundishwa na Yesu katika nafasi ya kwanza. Pili tutakua tayari kujifanyia tathmini na tatu tutakuwa wazi kupokea mafundisho na marekebisho kutoka kwa wengine ili daima mioyo yetu ijazwe na fadhila za kimungu na mwisho tupate tuzo ya maisha mapya ya umilele pamoja na Kristo. Hitimisho: Katika Dominika ya leo, tumshukuru Mungu (Zab 92:1-2, 12-15) ambaye alikuja kukaa kati yetu ili atufundishe njia iendayo kwa Baba. Tuombe neema yake, ili tuweze kuyashika mafundisho yake na kwa njia ya maneno na matendo yetu tuweze kuleta uponyaji wa kiroho na kimwili kwa wengine (Shangilio, Mt 4:23.)