Tafakari Dominika ya 8 Mwaka C wa Kanisa: Jifunzeni Kutoka Kwa Yesu
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji katika Liturujia ya Neno la Mungu, leo ikiwa ni Dominika ya Nane ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa. Maneno na matendo adili na matakatifu ni ushuhuda wa Mkristo. Kwa mateso, kifo na ufufuko wake, Kristo Yesu amewaandalia waja wake maisha na uzima wa milele. Kipofu ni mtu anayehitaji msaada. Hawezi katika hali yake kumwongoza mwingine anayehitaji msaada. Kumbe kwanza anahitaji apate kiongozi, yeye afuate nyayo za kiongozi na ndipo anapoweza kumshika mkono kipofu mwingine amuongoze. Mfano huu unawaelekea kwanza mitume, watakaochukua nafasi ya kutangulia mbele ya wafuasi, lakini pia unawaelekea wafuasi wote wa Kriso kwamba wamweke daima mbele yao Kristo kama kiongozi na mwalimu na wote pamoja wafuate nyayo zake ili wasiingie shimoni. Katika safari hiyo ya kumfuasa Kristo, mfano wa pili unawaalika wafuasi kuchukuliana. Lipo hitaji la kurekebishana pale mmoja anapokosea na huu ni wajibu wa msingi. Kristo anataka yule anayechukua wajibu wa kumrekebisha mwingine amrekebishe akijua kuwa na yeye anayo mapungufu yake na inawezekana yakawa makubwa kuliko ya yule anayerekebishwa. Si mfano unaozuia maonyo au kukosoana. Ni mfano unaozuia kuwahukumu wengine, kujisafisha kwa njia ya kuwachafua wengine, kuwa wa kwanza kuyaona makosa ya wengine ilhali makosa yetu tunayafumbia macho. Mfano wa tatu, sambamba na miwili iliyotangulia, unalenga kuonesha utu wa ndani na utu wa nje wa mtu. Matendo ya mtu daima ni matokeo ya undani alionao katika utu wake, kutoka katika hazina njema ya utu wa ndani hufuata matendo mema na kutoka katika hazina mbaya ya utu wa ndani hufuata matendo mabaya.
“Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema” (Lk 6:39-45). Siku moja Abba Paphnutius alipotea njia akajikuta kwenye kijiji kimoja na kuona wanakijiji wakitenda dhambi waziwazi, alisimama, akafumba macho na kuanza kusali na kujuta dhambi zake mwenyewe. Malaika akamtokea na upanga mkononi na kumwambia “Wanaohukumu wenzao huangamia kwa upanga huu, lakini wewe kwa vile hujahukumu mtu ila umejinyenyekeza na kusali juu ya dhambi zako mwenyewe jina lako limeandikwa katika kitabu cha uzima.” Maneno ya vinywa vyetu, matendo yetu, wepesi au uzito wa utendaji wetu na mapato ya chochote tunachofanya hudhihirisha namna tulivyo ndani ya akili na mioyo yetu… akili njema na moyo mweupe hudhihirika kwa matendo ya nje na kinyume chake. Leo Kristo anatamani tuondoe macho yetu nje yetu na kujitazama wenyewe tukijitafakari bila kujionea aibu au kujihurumia kusudi tujitambue na tujirekebishe. Hatuna budi kujihoji sana iwapo macho yetu yanaona au tu vipofu sisi… iwapo yamezibwa na kibanzi au na boriti… iwapo tu miti mizuri izaayo matunda mema au la, kwamba wenzetu wategemee kuvuna tini nzuri na zabibu safi au wajiandae kukutana na miiba na mbigili zenye kuumiza… kujichunguza huku kutusaidie kukua tukijigeuza kutoka ndani kuwa wazuri zaidi na hivi kuzaa matunda yastahiliyo uzima wa milele.
Ufafanuzi: Mabadiliko ya kiroho yaani toba na wongofu wa ndani huanza na tafakari na taamuli za mara kwa mara kujihusu wenyewe, hili linadai unyenyekevu sababu maelekeo ya mwanadamu ni kumtazama zaidi na kumjadili mwingine. Ukali wa maneno na wa matendo kuhusu jirani: nyumbani, shambani, ofisini, kwenye biashara… Kristo hasemi tusionyane hapana, haitatusaidia… “Mmoja anaweza kunyamaza kimya, lakini kama anahukumu moyoni mwake basi huyo anapiga mayowe makubwa zaidi” (Abba Poimen)… Kristo ana maana hii kwamba tunapojichunguza wenyewe mahali pa kwanza na kujirekebisha ndipo tunakuwa na nguvu na moyo wa kuwarekebisha na kuwafundisha ndugu zetu na hayo mawili yanatufanya kuwa bora zaidi… tutafute kuponya kuliko kuhukumu, anayehukumu wengine hajijui mwenyewe sababu mtu anayejitambua vema huwa haoni makosa ya wengine… Mpende mkosaji, lichukie kosa lake… usilipende kosa sababu ya aliyelifanya, usimchukie mtu kwa alichokitenda, ni jirani yako huyo… dhambi yake ni adui wa jirani yako. Hakuna mdhambi ‘kwa asili’ ila amekuwa hivyo kwa sababu hii au ile… dhambi yake ikiisha kuondolewa kinachobaki kwa mdhambi huyu ni kile tu alichokiumba Mungu, nacho chastahili kupendwa! Pamoja na fundisho hili, Kristo anatufundisha pia ufuasi ulio bora, kwamba mwanafunzi ahitimu vizuri afanane na mwalimu wake. Hili ni jambo jema sana, kumfuasa ili kufanana na Kristo mwalimu wetu, tumtumie kwa furaha na unyenyekevu kwa ufanisi wote. Tujifunze kumsikia na kumsikiliza tukijifunza kutoka kwake ili tusiwe viongozi vipofu tukiwangoza wenzetu kutumbukia mashimoni.
Somo la Kwanza (YbS 27:4-7) linatupeleka kwenye meza ya majadiliano... katika kujadili tunapata suluhu ya tofauti zetu sababu kila mtu ni wa pekee, amejaliwa fikra, muono, mtazamo, tabia na malezi tofauti na mwingine. Hata hivyo tunaunganishwa na jambo moja, UTU… kwa ajili ya utu tofauti zetu zinajadilika na maridhiano kufikiwa. Hili huondoa manung’uniko, lawama na kuleta amani na kuridhika... Wenzetu walio katika vita ya silaha muda huu Mwenyezi Mungu awasaidie ili roho ya majadiliano na makubaliano ifikiwe kwa ajili ya utu. Sote tunatamani ukamilifu, hata hivyo kuishi mashauri ya Injili ni jambo gumu kiubinadamu. Mtakatifu Paulo katika Somo la Pili (1Kor 15:54-58) anatupa moyo akitukumbusha kujiimarisha katika uvumilivu, kutokutikisika na kutenda daima kazi ya Bwana na taabu yetu haitakuwa bure. Changamoto zipo ikiwamo kifo hata hivyo Mungu anatujalia kushinda katika Bwana wetu Yesu Kristo, jambo muhimu ni kuitengeneza vema mioyo yetu sababu “mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema…”