Siku ya Wanawake Duniani,Machi 8:Thalitha Kum na vita dhidi ya biashara haramu ya binadamu!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Siku ya Wanawake duniani ilianzishwa rasimi na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 1977, ili kuadhimishwa kila ifikapo tarehe 8 Machi ya kila mwaka, siku ambayo inaakisi umuhimu wa kupambania haki za wanawake na ukombozi wa wanawake. Kaulimbiu ya mwaka huu 2025 iliyochaguliwa na Umoja wa Mataifa, inataka hatua zichukuliwe ambazo zinaweza kufungua haki sawa, uwezo na fursa kwa wote na mustakabali wa wanawake ambapo hakuna anayeachwa nyuma. Jambo la msingi katika maono haya ni kuwezesha kizazi kijacho: vijana, hasa wanawake wachanga na wasichana balubalu kuwa kama vichocheo vya mabadiliko ya kudumu. Vile vile mwaka huu 2025, Jumuiya ya kimataifa inaadhimisha kumbukumbu ya miaka thelathini ya Mkutano wa Nne wa Dunia wa Wanawake na kupitishwa kwa Azimio la Beijing na Jukwaa la Utekelezaji kunako mwaka 1995.
Mabalozi wa Talitha Kum:wito wa kuchukua hatua
Ni katika fursa hiyo na Mwaka wa Jubilei, ambapo Mabalozi Vijana na vijana wa Matumaini wa Mtandao wa Kimataifa wahamasishaji wa Siku ya Maombo Ulimwengini na Tafakari dhidi ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu tarehe 6 Machi 2025 walizindua Wito mpya wa haraka wa kuchukua hatua kukabiliana na janga la kimataifa la biashara haramu ya binadamu. "Tumechagua tarehe hii ya mfano kwa ajili ya kujitolea kwetu katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu, kutokana na ukweli wa kutisha kwamba asilimia 70 ya waathirika wa biashara hiyo ni wanawake na wasichana, kulingana na Umoja wa Mataifa. Mwaka huu 2025, tunajiunga na kampeni ya kimataifa: #AccelerateAction, inayoakisi mada ya sasa ya mgogoro unaodai hatua za pamoja na za haraka. Kwa Wito huo wa "Kuchukua Hatua," tunapyaisha ahadi yetu ya pamoja na Mabalozi Vijana ili kukuza sauti za waathiriwa, walionusurika, wahamiaji na wakimbizi,” alisema Sr Abby Avelino, Mratibu wa Siku ya Kimataifa ya Sala na Uhamasishaji dhidi ya Biashara haramu wa Binadamu na Mtandao wa Kimataifa wa Talitha Kum, unaoongozwa na Watawa Ulimwenguni kote.
Wito kwa serikali,taasisi na watu binafsi wa imani na asili zote
Katika hati, iliyoandaliwa mnamo tarehe 8 Februari 2025, mwishoni mwa toleo la 11 la Siku ya Sala na Tafakari dhidi ya Biashara Haramu ya Binadamu inawaalika vijana kutoka ulimwenguni kote kujiunga na sababu na kuchukua hatua madhubuti ya kukomesha uhalifu huu dhidi ya ubinadamu. Inatoa wito kwa serikali, taasisi na watu binafsi wa imani na asili zote kufanya maamuzi ambayo yanapambana kwa uthabiti na biashara haramu ya binadamu. Maandishi hayo, yaliyoandikwa na wanaharakati vijana, walionusurika na wataalamu, ambayo yanasisitiza kwamba biashara haramu ya binadamu inawakilisha aina ya utumwa mamboleo, ambayo inawanyima watu hadhi na haki zao za kimsingi. "Usafirishaji haramu wa binadamu ni uhalifu usioonekana ambao unazidisha mateso ya wanadamu. Kwa hili, lazima tuunganishe nguvu ili kuongeza uelewa katika jamii zilizo hatarini na kuacha biashara haramu,” lilisisitiza kundi la kimataifa la mabalozi wa matumaini waliokusanyika mjini Roma. Hati hiyo inapendekeza hatua madhubuti, ikiwa ni pamoja na: sala na huduma kwa waathirika na wale wanaowasindikiza; mikakati ya ukarabati na ujumuishaji upya kwa waathirika; elimu na ufahamu juu ya jambo hilo, kupitia mbinu za ubunifu na za jumla; uundaji wa nafasi halisi na kidijitali kwa usasishaji na usaidizi unaoendelea.
Siku ya sala na tafakari ilianzishwa na Papa Francisko 2025
Siku ya Sala na Tafakari dhidi ya Usafirishaji haramu wa binadamu ilianzishwa na Baba Mtakatifu Francisko mwaka 2015 ili kuongeza ufahamu kote ulimwenguni kuhusu hali halisi ya usafirishaji haramu wa binadamu na kukuza hatua za pamoja. Mpango huo unahamasishwa na wakuu wa Mashirika yakitawa UISG na pamoja na Umoja wa Mama wakuu wa mashirika (USG na kukabidhiwa kwa uratibu wa Harakati ya Kimataifa ya Talitha Kum ambao ni mtandao wa watawa waliojitolea katika vita dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu ulimwenguni kote. Maandishi kamili wito huo yanapatikana katika lugha 4 (Kiingereza, Kiitaliano, Kifaransa, Kihispania).