Nigeria.Mseminari aliyekuwa ametekwa nyara mwanzoni mwa machi kauawa na kuachiliwa huru Padre
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Huzuni nchini Nigeria kutokana na taarifa za kifo cha Andrew Peter, mseminari mwenye umri wa miaka ishirini, mmoja aliyeuawa na watekaji nyara wake, baada ya kuchukuliwa kwa nguvu na watu wenye silaha mnamo tarehe 3 Machi 2025 katika Jimbo la Edo, kusini mwa Nigeria. Kijana huyo alitekwa nyara pamoja na Padre Philip Ekweli, ambaye aliachiliwa huru tarehe 13 Machi 2025. Habari hizo ziliripotiwa katika taarifa kwa vyombo vya habari kutoka Jimbo Katoliki la Auchi, iliyoripotiwa na shirika la Habari za Kimisionari FIDES. Padre na mwanasemina huyo walitekwa nyara wakati wa shambulizi dhidi ya Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro huko Iviukhua-Agenebode, Etsako Kaunti ya Mashariki. Watu wawili hao walikuwa wamepelekwa kwenye misitu ya karibu.
Jimbo linabainisha kuwa watu wamo hatarini mitaani,mashambani na majumbani
Jimbo hilo pamoja na kushukuru kwa maombi na msaada wa kimaadili uliopokelwa, inatoa wito kwa mamlaka na vikosi vya usalama kulinda jamii mahalia dhidi ya utekaji nyara unaoendelea katika Jimbo la Edo, ambalo limekuwa kimbilio salama kwa watekaji nyara, ambao wanaweza kufanya kazi bila kuadhibiwa, wakati idadi ya watu wanahisi kutokuwa na msaada na kutelekezwa. “Watu wamo hatarini, mitaani, mashambani mwao na hata majumbani mwao,” inasema taarifa ya Jimbo hilo ambayo inataka hatua zaidi za kuwaokoa waliotekwa nyara, ili kuepuka na kuacha juhudi zote za uokoaji mikononi mwa jamaa na marafiki wa waliotekwa nyara pekee yao. Taarifa hiyo pia inakumbusha kwamba “katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, mapadre wake sita katika jimbo hilo wametekwa nyara, kuteswa na kuachiwa, watatu walishambuliwa lakini wakafanikiwa kutoroka na mmoja, Padre Christopher Odia, aliyeuawa kikatili; na sasa mseminari Andrew Peter pia ameuawa. Taarifa ya jimbo inatoa sala ya mwisho ni kwa ajili ya wote waliouawa na watekaji nyara ili kwa rehema za Mungu wapumzike kwa amani."
Utekaji nyara unafanyika mara kwa mara na ukosefu wa usalama katika maeneo mengi
Shirika la Kipapa la Msada wa Kanisa Hitaji (ACS), katika taarifa kwa vyombo vya habari kutoka sehemu yake ya Italia, pia linakumbuka jinsi mauaji ya kijana Andrew Peter yalivyotokea siku chache baada ya kutekwa nyara, katika siku ya Jumatano ya Majivu, ya Padre Sylvester Okechukwu, wa Jimbo la Kafanchan, katika serikali ya kaskazini-kati la Kaduna. Pia alikuwa ametekwa nyara siku moja kabla. Kwa mujibu wa shirika hili, (ACS)l inabainisha kuwa Nigeria inakabiliwa na ukosefu mkubwa wa usalama katika maeneo mengi. Utekaji nyara hufanyika mara kwa mara, hasa na magenge ya wahalifu yanayotafuta faida, katika muktadha wa ukosefu wa utulivu ambao unashuhudia operesheni ya vikundi vya itikadi kali kama vile Boko Haram na Iswap, tawi la Afrika Magharibi linalojiita Dola la Kiislamu (IS), na ambalo limeshuhudia mashambulizi mengi ya wachungaji wanaohamahama dhidi ya wakulima wasio na makazi.