Nchi Takatifu:Njia ya Msalaba,wanafunzi wa shule Katoliki za Yerusalemu,kwa ajili ya amani na Papa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
“Mungu, Baba yetu uliye mbinguni, kwako tunainua maombi yetu kwa kila mgonjwa, hasa Papa Francisko,” ndiyo maandishi juu ya alama zilizobebwa na watoto wa Shule za Kikatoliki za Yerusalemu wakati wa Njia ya Msalaba iliyofanyika Ijumaa tarehe 14 Machi 2025 katika mitaa ya Mji Mtakatifu. Hayo yalielezwa na Dietrich Bäumer, Mkuu wa Shule ya Schmidt, kwa Shirika la Habari za Kimisionari Fides. Katika taarifa yake anabainisha kuwa kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Mahujaji wa Matumaini” iliyobeba mada ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwaka huu wa Jubilei ya miaka 2025 takriban wavulana na wasichana 700 waliotembea tena mitaa ya mji mkongwe wa Yerusalemu ambao Yesu alitembea akielekea Golgotha, pia wakiombea afya ya Askofu wa Roma.
Mkuu wa Shule ya Schimidt alisisitiza kuwa Njia ya Msalaba ya shule za Kikatoliki za Yerusalemu, ambayo hufanyika kila mwaka wakati wa Kwaresima, iliongozwa na Padre Francesco Patton, Msimamimizi wa Nchi Takatifu na Padre Ibrahim Faltas, Makamu Msimamizi wa Nchi Takatifu na Mkurugenzi wa shule ya Wafransiskani ya Nchi Takatifu. Padre Ibrahimu alikumbuka mwanzoni mwa kuanza Njia ya Msalaba(ambayo ilianza hata mwaka huu katika Kanisa cha Mijeredi cha Wafransiskani kwenye njia ya Uchungu) kwamba mamombi yangefanyika kwa ajili ya uponyaji wa Papa Francisko na Padre Ayman Bathish, waliojeruhiwa vibaya katika ajali siku zilizokuwa zimepita.
Mamia elfu ya Wanafunzi wengi wa shule walikuwa wametayarisha ishara kwa ajili ya Njia ya Msalaba zenye neno muhimu la Mwaka Mtakatifu: “Tumaini” katika lugha tofauti na maombi ya uponyaji wa wagonjwa wote, hasa Papa Francisko. Walimu na wazazi wa wanafunzi kutoka shule 13 za Kikristo huko Yerusalemu Mashariki pia walishiriki katika maandamano hayo yaliyopita katika Jiji la Kale la Jerusalemu. Vituo kuanzia cha 8-14, kulingana na mila na utamaduni, viliishia katika Kanisa la Wafransiskani la Mtakatifun Salvatore, karibu na Mlango Mpya. Hitimisho liliwekwa alama tena mwaka huu kwa baraka za mwisho na masalia ya Msalaba yaliyotolewa na Padre Francesco Patton Msimamizi wa Nchi Takatifu katika Kanisa lililojaa watu. Washiriki wote walivaa stole nyeupe, ambazo ziliandikwa kwa Kiarabu “Al Rajaa” (Hope). Maombi hayo yaliongozwa na Mwaka Mtakatifu na nia ya maombi ya Baba Mtakatifu Francisko.
Katika neno lake la mwisho katika Kanisa la Mtakatifu Salvatore, Padre Ibrahim alitoa shukrani kwa ushiriki mpana wa watu wa Mungu katika Njia ya Msalaba. “Tunajikuta katika nyakati ngumu, lakini ni wakati wa sala na msamaha, bila ambayo kusingekuwa na mwanzo mpya,” alisisitiza Msimamizi wa Nchi Takatifu. Kama kila mwaka, Njia ya Msalaba ya kawaida ilikuwa onyesho la mshikamano wa kina na Wakristo kutoka ulimwenguni kote na ishara ya matumaini kwa wanafunzi wa shule za Kikristo za Yerusalemu.
Shule ya Kikatoliki ya Schmidt huko Yerusalemu itaonesha ukaribu wake wa pekee na Roma na Vatican kwa hija ya Jubilei ambayo italeta wanafunzi, walimu na wafanyakazi kwenye Jiji la Milele kuanzia tarehe 23 hadi 30 Novemba 2025. Wanafunzi wamefurahishwa na mikutano ijayo huko Roma na pamoja na Papa Francisko wanapomwombea apone.