Kenya:Tunapaswa kuwa na wasiwasi wa fedha nyingi zitolewazo Kanisani na Wanasiasa
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kwaresima ni kipindi cha imani na matumaini, toba na uwongofu wa ndani ili kukumbatia na kusindikizwa na huruma na upendo wa Mungu. Huo ndiyo mwaliko binafsi na kama Jumuiya ya waamini wote wenye mapenzi mema. Ni kipindi katika mwaka wa Kanisa kinachotangulia maadhimisho ya Fumbo Kuu la Pasaka yaani Mateso, Kifo na Ufufuko wa Bwana Wetu Yesu Kristo. Ni muda wa siku 40, kuanzia Jumatano ya majivu mpaka jioni ya Alhamisi kuu, katika adhimisho la Karamu ya Bwana. Baada ya hapo waamini wote wanaanza siku kuu tatu za Pasaka yaani: Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu na Jumamosi Kuu. Na mfungo huo huendelea mpaka Jumamosi Kuu na kuhitimishwa na Mkesha wa Pasaka.
Kipindi cha Kwaresima tujiulize maswali msingi
Katika kipindi hiki kwa kila mmoja anapaswa kujiuliza maswali msingi: mfungo wangu ni wa namna gani? Je, ninafunga kwa kutimiza wajibu kwa kuwa ni mwaliko wa Kanisa kufanya hivyo tu au nina kitu cha ziada zaidi ninachotarajia kunufaika nacho mimi binafsi katika mustakabali wa maisha yangu ya kiroho? Pili, tunapofunga na kusali, tunapaswa kuwakumbuka pia na wengine. Na zaidi ya hayo wale walio katika mahangaiko mbalimbali. Tusali kwa nia maalumu, kwa ajili ya kuombea uwongofu katika familia zetu, kuombea amani na mapatano kati ya mataifa, kuombea haki na usawa kati ya watu, kuombea wagonjwa, maskini, na wenye shida. “Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, funga mlango na umwombe Baba yako aliye sirini. Naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako.”
Kanisa lisionekane mnufaika wakati hakuna shule hazina vitabu,hospitali hazina dawa
Jambo la tatu ni kutoa Sadaka lakini si katika mengi tuliyo nayo au kujifanya tuonekane na tujulikane kwa watu, maana Yesu mwenyewe alisema tayari wana thawabu yao. Ni katika muktadha huo wa kufanya ujulikane, katika kipindi cha kwaresima, Viongozi mbali mbali wa kisiasa, hutumia fursa hiyo za majivuno na majigambo. Hivi karibuni wakati wa kuanza kipindi hiki, Askofu Cleophas Oseso wa Jimbo Katoliki la Nakuru, nchini Kenya katika mahubiri yake Jumatano ya Majivu, tarehe 5 Machi 2025, akirejea juu ya michango inayotolewa na wanasiasa katika Makanisa mbalimbali nchini humo alisema: “Kanisa lisijeonekane kama mnufaika wakati shule hazina vitabu, hospitali hazina dawa na madaktari na walimu hawalipwi mshahara.” Kwa mujibu wa Askofu huyo alisisisitizakuwa: “Hatujui fedha nyingi zinazotolewa katika makanisa na wanasiasa zinatoka wapi na kwa ajili hiyo tunapaswa kuwa na wasiwasi,” huku akikumbusha juu ya mafundisho ya Injili kwamba: “Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujaza. (rej. Mt. 6:3).
Kwa njia hiyo Askofu Oseso aliwaalika wanasiasa kuacha kutangaza au kuweka wazi kiasi cha michango wanayotoa katika Makanisa mbalimbali. Kwa mujibu wa Askofu Osseso alisema: “Michango itolewe kwa siri ili kuhakikisha kuwa ni ya kweli na siyo njia ya kampeni au kujionesha.”Hata hivyo mtazamo wa Askofu wa Nakuru ulikuja wakati ambapo nchini Kenya inapitia mgogoro mkubwa wa kiuchumi. Hivi karibuni tarehe 7 Machi 2025 Chama cha Hospitali binafsi kiliamuru kusitishwa kwa huduma katika vituo vyake vinavyoshirikiana nacho kupinga ukosefu wa malipo kutoka Serikalini.