杏MAP导航

Tafuta

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025 unanogeshwa na kauli mbiu “Tutembee kwa pamoja katika matumaini.” Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025 unanogeshwa na kauli mbiu “Tutembee kwa pamoja katika matumaini.”  

Jumatano ya Majivu, Mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima: Hija ya Imani, Matumaini na Mapendo

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025 unanogeshwa na kauli mbiu “Tutembee kwa pamoja katika matumaini.” Kwaresima ni kipindi cha imani na matumaini; toba na wongofu wa ndani, ili kukumbatia na kuambata huruma na upendo wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa mtu mmoja mmoja na kama Jumuiya ya waamini. Majivu ni ishara ya unyenyekevu, ukumbusho kwamba binadamu ni mavumbi na ni ishara ya mwanzo mpya.

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Jumatano ya Majivu. Kila mwaka, kabla ya maadhimisho ya fumbo la Pasaka, Mama Kanisa anatupatia nafasi ya kutafakari juu ya mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Hivyo kwa kuadhimisha Jumatano ya Majivu, tunaingia katika kipindi kingine cha mwaka wa Kanisa, kipindi cha Kwaresima. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025 unanogeshwa na kauli mbiu “Tutembee kwa pamoja katika matumaini.” Kwaresima ni kipindi cha imani na matumaini; toba na wongofu wa ndani, ili kukumbatia na kuambata huruma na upendo wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa mtu mmoja mmoja na kama Jumuiya ya waamini. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya hija ya imani na matumaini, kama ilivyokuwa kwa Waisraeli, waliotembea Jangwani kwa muda wa miaka arobaini, wakapata fursa ya toba na wongofu wa ndani. Hii ni safari ya pamoja kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, kwa kutoka katika ubinafsi wao na hivyo kujielekeza katika ujenzi wa umoja kwa kujitambua kwamba, wao wote wamekuwa ni wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Rej. Gal 3:26-28, mwaliko wa kuweka nia ya kuweza kufikia lengo kwa kusikilizana katika upendo na uvumilivu. Liturujia ya Neno la Mungu katika siku hii inatualika, “kufanya toba na kuanza maisha mapya.” Tuombe neema ya kupokea mwaliko wa Kristo Yesu anayetuambia, “Tubuni na kuiamini Injili” (Mk 1:15) ili sote tuweze kuupata uzima wa milele baada ya maisha haya ya hapa duniani. Kwa nini tunapakwa Majivu katika paji la Uso? Katika siku ya Jumatano ya majivu (kwa Kilatini dies cinerum), waamini wanapakwa majivu yaliyobarikiwa katika paji la uso.

Maana ya majivu: Unyenyekevu, mwanadamu ni mavumbi, ishara ya upya
Maana ya majivu: Unyenyekevu, mwanadamu ni mavumbi, ishara ya upya   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Majivu haya yanatokana na matawi yaliyotumika katika Dominika ya Matawi katika mwaka uliopita. Kupakwa majivu katika paji la uso kuna maana kuu tatu. Kwanza, kama ishara ya unyenyekevu na utayari wa kufanya toba ya kweli, yaani metanoia. Pili, majivu yanatukumbusha kuwa maisha yetu ya hapa duniani yana mwisho, kwa kuwa mwili huu upo katika hali ya uharibifu, hivyo twapaswa kuwekeza katika uzima wa roho zetu. Tatu, majivu ni ishara ya mwanzo mpya, upya wa maisha yetu ya kiroho, upya katika mahusiano yetu sisi kwa sisi, upya katika mitazamo na fikra zetu, lakini zaidi sana, upya katika Imani. Siku hii yatukumbusha kuwa huruma ya Mungu ni kubwa kuliko dhambi na udhaifu wetu. Mwenyezi Mungu yu tayari kumpokea yeyote aliye na nia ya dhati ya kuanza maisha mapya. Maana ya Kipindi cha Kwaresima. Kipindi cha Kwaresima (Lenten season) ni kipindi katika mwaka wa Kanisa kinachotangulia maadhimisho ya Fumbo la Pasaka yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni muda wa siku 40, kuanzia Jumatano ya majivu mpaka jioni ya Alhamisi kuu, katika adhimisho la Karamu ya Bwana. Kisha huanza siku kuu tatu za Pasaka yaani Alhamisi kuu, Ijumaa kuu na Jumamosi kuu. Hata hivyo, mfungo huendelea mpaka Jumamosi kuu na kuhitimishwa na Kesha la Pasaka.Kwa nini siku Arobaini (Quadragesima)? Siku arobaini zatukumbusha; kwanza, Ni muda wa maandalizi na mwanzo mpya (Preparation and a new beginning). Tunajifunza kutoka kwa Bwana wetu Yesu Kristo aliyefunga na kusali kwa siku arobaini usiku na mchana jangwani kabla ya kuanza rasmi utume wake (Mt. 4:1-11, Lk 4:1-13). Kumbe, kila mmoja wetu anapata muda wa kufanya maandalizi kabla ya jambo lolote katika maisha yetu, kukusanya nguvu za kiroho ili tufanikiwe katika yale tunayoyafanya kila siku. Pili, ni muda wa mabadiliko na kujaribiwa (Testing and transformation).

Kwaresima ni kipindi cha siku 40 za kufunga, kusali, sadaka na Neno la Mungu
Kwaresima ni kipindi cha siku 40 za kufunga, kusali, sadaka na Neno la Mungu

Musa alikaa mlimani Sinai kwa muda wa siku 40 na baada ya hapo akapokea sheria ya Mungu (Kut 24:18), wana wa Israeli walikaa Jangwani kwa muda wa miaka 40 kabla ya kuingia katika nchi ya ahadi (Kut 16:35) na Eliya alitembea muda wa siku 40 jangwani kabla ya kukutana na Mungu katika mlima Horeb (1 Fal 19:8). Tunapata siku arobaini za kufunga, ni siku za toba na wongofu wa ndani. Ni siku za kujaribiwa lakini pia ni siku za kusubiri kwa matumaini kukutana na Kristo mfufuka. Tatu, arobaini ni namba kamilifu, ni muda wa kutosha. Kwaresma inatupatia muda wa kutosha, kutathmini mahusiano yetu na Mungu na kuanza tena upya. Mwenyezi Mungu daima anatupa bado nafasi ya pili. Anatupa muda wa kutosha ili tuendelee kunufaika na ahadi alizotuahidia. Kwaresma hii itusaidie kuwa tayari kutumia vyema muda na nafasi anazotupatia Mungu, ili tunufaike na ahadi zake kwetu. Mwisho, katika siku hizi zote, tunaalikwa kusali, kufunga na kufanya matendo ya huruma. Somo la 1: Ni kitabu cha Nabii Yoel 2:12-18. Somo la kwanza tulilolisikia, ni kutoka katika kitabu cha Nabii Yoeli. Kitabu hiki ni utabiri wa Nabii Yoeli katika taifa la Yuda, lilokua linapitia katika wakati mgumu sana baada ya taifa hili kupata majanga mbalimbali ya asili. Kulikua na janga la Nzige pamoja na ukame ambavyo hivi vyote vilipelekea hofu na mashaka makubwa kwa watu. Kutokana na majanga haya, watu wakafikiri kuwa hukumu ya Bwana ilikua karibu, lakini hawakujua wafanye nini hasa. Nabii anawasisitiza kutubu na kumrudia Mungu. Anawasisitiza kukumbuka agano walilofanya na Mungu na zaidi ya yote anawakumbusha kuwa Mungu ni mwenye huruma nyingi, watakapotubu na kumrudia atawabariki tena.

Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu na utakatifu wa maisha
Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu na utakatifu wa maisha

Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mambo manne ya kujifunza. Kwanza: Toba ya kweli (True repentance). Katika somo hili la kwanza Nabii Yoeli anasisitiza juu ya toba ya kweli, akiwaalika watu kufunga na kulia na kuomboleza. Zaidi sana anawataka “kurarua mioyo” tendo linalomaanisha kwenda mbali zaidi ya mfungo wa kawaida wa kuonekana kwa nje. Kumbe kufunga tu kwa kulia, kwa kusali na kwa kuomboleza kwapaswa kuguse kabisa mioyo yetu. Ndugu mpendwa, mimi na wewe kila mwaka tunapata wasaa huu wa kufunga kwa siku arobaini kabla ya kusherekea mafumbo makuu ya ukombozi wetu. Ninapaswa kujiuliza mimi, mfungo wangu ni wa namna gani? Je, ninafunga tu kwa kutimiza wajibu kwa kuwa ni mwaliko wa kanisa kufanya hivyo au nina kitu cha ziada zaidi ninachotarajia kunufaika nacho mimi binafsi katika mustakabali wa maisha yangu ya kiroho? Haya ni maswali msingi kila mmoja wetu apaswa kujiuliza. Ninaweza kufunga lakini bado nikawa mtu wa chuki, mtu wa visasi, vinyongo, wivu, anasa nk. Nikaonesha tu kwa nje kwamba nimefunga ila katika hazina ya moyo wangu bado maisha yangu ni yale yale ya zamani. Tumwombe Mungu atusaidie ili mfungo wetu utuletee manufaa ndani kabisa ya mioyo yetu, kisha mambo ya nje nayo yatakua safi kabisa. Pili: Mungu yu tayari kutusamehe makosa yetu (God’s redness to forgive). Ni maneno ya Mungu mwenyewe anayewaalika watu wake kwa kinywa cha Nabii Yoeli, “Nirudieni mimi asema Bwana…kwa maana yeye ni mwenye rehema, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema” Mwenyezi Mungu hataki mtu yeyote apotee, bali anatutaka sote kumrudia, kwa toba ya kweli ili tupate kuokoka. Ndugu mpendwa sana, Mwenyezi Mungu anatupenda sana, anatupenda kwa mapendo makuu. Upendo wake kamwe hausemi inatosha. Mungu aliye tayari kuwaacha kondoo tisini na tisa na kumtafuta mmoja aliyepotea, ndiye mimi na wewe. Kwa njia ya mama kanisa Mtakatifu, tunapata nafasi ya kujipatanisha na Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Kitubio kila mara tunapoanguka dhambini na kushindwa kuishi kiaminifu amri za Mungu. Kwaresima hii itukumbushe ndugu zangu kuwa, Mwenyezi Mungu mwingi wa mapendo anatutazama kwa jicho moja tu, ni jicho la upendo. Hatazami udhaifu wetu, wala ukubwa na wingi wa dhambi zetu, bali anatazama nia yetu ya dhati ya kuanza maisha mapya. Mwana mpotevu alifikiri moyoni mwake, akaamua kurudi kwa Baba. Kwaresima hii itusaidie kila mmoja afikiri moyoni mwake, na aweke nia ya dhati ya kurudi kwa Mungu, kwa kuwa anatupenda na anatutafuta.

Kwaresima ni hija ya imani, matumaini na mapendo
Kwaresima ni hija ya imani, matumaini na mapendo

Tatu: Mwaliko wa pamoja wa kuanza maisha mapya (Collective renewal). Nabii Yoeli anawaalika watu wote kutubu na kumrudia Mwenyezi Mungu, anaposema, “Kusanyeni wazee, kusanyeni Watoto na hao wanyonyao maziwa, bwana arusi, na bibi arusi watoke vyumbani mwao, makuhani na wahudumu wa Bwana…” Kumbe huu ni mwaliko wa watu wote. Haachwi hata mmoja kwenye mwaliko huu wa kufanya toba. Ndugu mpendwa, kwaresma inatualika sote kutubu na kuiamini Injili, ambayo kwayo tunaanza maisha mapya na Kristo mfufuka. Licha ya kwamba kila mmoja anapokea mwaliko kwa namna yake, tukumbuke kuwa ni mwaliko kwa watu wote. Tunapofunga na kusali, tuwakumbuke pia na wengine. Huenda wapo wengi ambao bado hawajakubali mwaliko huu wa Kristo, wapo wasiomwamini bado Mungu. Wapo pia walio katika mahangaiko mbalimbali ambao hawajui hata kama kwaresma inaanza kesho. Tuwakumbuke na wengine katika mfungo wetu. Tusali kwa nia maalumu, kwa ajili ya kuombea wongofu wa katika familia zetu, kuombea amani na mapatano kati ya mataifa, kuombea haki na usawa kati ya watu, kuombea wagonjwa, maskini, na wenye shida mbalimbali za roho na za mwili. Tusimwache hata mmoja wetu nyuma katika imani, tutembee pamoja, tusimame imara kama familia moja kwa kuwa sisi tu watoto wa Baba mmoja. Nne: Toba ya kweli ni chanzo cha baraka (true repentance leads to blessings). Sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji ilikua ni ishara ya kurudishiwa tena baraka za Mungu. Nabii Yoel anawakumbusha watu na anatukumbusha sisi sote kuwa, toba ya kweli iantupelekea sio tu katika upyaisho kiroho bali pia Mungu anatubariki hata kwa maisha ya nje, sisi na familia zetu na jumuiya zetu. Ndugu zangu Wapendwa sana, toba ya kweli inatusaidia kupokea neema na baraka za Mungu zitokanazo na maadhimisho mbalimbali tunayoadhimisha kila siku. Tunapokuwa katika hali ya neema, sala zetu zinaleta matunda, sakramenti mbalimbali tunazopokea zinatuleta neema rohoni. Kumbe baraka hizi zinategemea hali ya kiroho ya anaeyzipokea. Zinakuja kwetu bure kabisa kutoka kwa Mungu ila hali yangu ya kiroho ndiyo itaamua au zininufaishe au zisininufaishe. Tuombe neema ya Mungu ili daima tujiandae kiroho ili tunufaike na neema na baraka mbalimbali tunazopewa bure na Mungu wetu.

Majivu ni yale yanayotokana na matawi ya mwaka uliotangulia
Majivu ni yale yanayotokana na matawi ya mwaka uliotangulia   (AFP or licensors)

Somo la Injili: Ni Injili ya Mt 6:1-6, 16-18. Somo la Injili Takatifu ni sehemu ya hotuba ya Yesu mlimani, inayoanzia sura ya 5 hadi sura ya 7. Ni mafundisho ya Yesu juu ya kuishi maisha maadilifu. Yesu anatutaadharisha juu ya unafiki, yaani kufanya mambo ili kuonekana kwa nje kuliko kuwa na uadilifu na utakatifu wa ndani. Katika kipindi cha Yesu, kufunga, kusali na Matendo ya huruma ilikua ni mambo ya muhimu kabisa katika dini ya Wayahudi (Rej. Tob 12:8). Matendo haya yalifanyika kama ishara ya nje ya uchaji kwa Mungu. Lakini baadhi ya watu hasa mafarisayo na waandishi walifanya Matendo hayo ili kuonekana na watu. Kumbe Yesu anatoa mafundisho hayo kutukumbusha kuwa ibada ya kweli na uchaji kwa Mungu vyapaswa kubadili utu wetu wa ndani wala sio kwa ajili ya kujionesha kwa watu. Katika somo hili la Injili ya Jumatano ya Majivu tuna mafundisho matatu ya kujifunza. Kwanza: Yesu anatufundisha namna ya kufanya matendo ya huruma (Alms giving) Mt 6:2-4. Yesu anatusisitiza “kuwa macho”, kwamba tusifanye mema ili tuonekane na watu. Tunapotoa sadaka, tusipige panda mbele yetu ili kutukuzwa na wao. Sadaka yapaswa kuwa jambo langu mimi na moyo wangu. Ndugu wapendwa, kufanya matendo ya huruma kwetu sisi pia ni moja katika ya mambo makuu tunayoalikwa kufanya. Kila mmoja anaalikwa kujitoa sadaka, kufunga kwa ajili ya kuwasaidia wenye shida na wahitaji kuliko sisi. Wapo watu wengi wasio na chakula, wasio na mavazi, wasio na malazi. Wanahitaji tone la upendo kutoka kwangu mimi na wewe. Yesu anatuonya kuwa tufanyapo matendo ya huruma, hatupaswi kujikweza sisi bali twapaswa kufanya kwa nia njema na dhamiri safi. Pili: Yesu anatufundisha namna ya kusali (Prayer) Mt. 6:5-6. Jambo la pili Yesu natufundisha juu ya kusali, kwamba, “Msalipo msiwe kama wanafiki.. Wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani na ukiisha kufunga mlango wako usali mbele za baba yako aliye sirini.” Katika kipindi hiki cha kwaresma tunaalikwa kujibidiisha katika kusali.

Kwaresima ni hija ya imani, matumaini na mapendo thabiti
Kwaresima ni hija ya imani, matumaini na mapendo thabiti   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Na tusalipo,Yesu anatualika kuingia katika chumba chetu cha ndani, yaani kuwa karibu kabisa na Mungu, kusogeza moyo wetu karibu kabisa na Mungu wetu. Tunaalikwa kuwa na mawasiliano ya karibu kabisa ya Yesu, Baba yetu anayetupenda na anayeona undani kabisa wa  moyo wa kila mmoja wetu, yeye mwenyewe anatujibu sala zetu, tunapomwendea kwa moyo mnyofu. Tusisali ili tu tuonekane na watu. Ukristo wetu na usiwe tu wa mambo ya nje nje ambayo hayana madhara yoyote katika utu wetu wa ndani. Tatu: Yesu anatufundisha namna ya kufunga (Fasting) Mt. 6:16-18. Katika sehemu ya mwisho ya Injili, Yesu anatufundisha namna tunapaswa kufunga. Baadhi ya watu katika kipindi hiki cha Yesu walifunga kwa namna ambayo kila mtu alitambua kuwa wamefunga. Yesu anawaita hawa ni wanafki. Anatuasa tufungapo, mtu yeyote wala asijue kuwa tumefunga kwa kuwa mfungo wapaswa kuwa jambo lako binafsi na Mungu. Katika Kipindi cha Kwaresima hii, kila mmoja anaalikwa kufunga. Mara nyingi tunafunga pengine vile vitu tunavyovipenda sana, tunajikatalia ili kutoa sadaka na kujifanya mazoezi yetu ya kiroho. Tufanye jambo hilo kweli katika muktadha wa kiroho. Sio lazima kila mtu ajue kwamba mimi nimefunga. Mfungo haupaswi kuonekana kama ni mzigo kwetu bali njia yetu ya kujiweka karibu zaidi na Mungu. Tukizingatia mambo haya matatu anayotundisha Yesu basi mfungo wetu utatuletea faida na matunda mengi katika maisha yetu ya kiroho na maisha yetu ya nje pia. Somo la pili: Ni Waraka wa Pili wa Mtume Paulo 2 Kor 5:20-6:2. Katika somo la pili, 2 Kor 5:20-6:2, Mtume Paulo anawaasa Wakorintho na anatuasa sisi sote; kwanza, kujipatanisha na Mungu, kwa njia ya sakramenti ya kitubio. Pili, anatukumbusha thamani ya sadaka ya Kristo, yeye ambaye hakujua dhambi alikubali kujitoa kwa ajili yetu sisi wenye dhambi, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu. Anatualika nasi kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine. Tatu, anatuasa, tuipokee neema hii kutoka kwa Kristo, ili ifanye kazi ndani mwetu. Pasaka iwe na maana katika maisha yetu ya kila siku, kila siku ni siku ya wokovu, ni wakati uliokubalika. Hitimisho: Tunapoanza kipindi cha Kwaresima, tuombe neema ya kupokea mwaliko wa Kristo Yesu anayetuambia, “Tubuni na kuiamini Injili” (Mk 1:15) ili sote tuweze kuupata uzima wa milele baada ya maisha haya ya hapa duniani.

05 Machi 2025, 16:36