Jubilei:Masista wa Kikatoliki wapinga hukumu ya kifo na kukaribisha neema ya msamaha
Na Krisanne Vaillancourt Murphy,Catholic Mobilizing Network
Kila baada ya miaka 25, Papa hutangaza Jubilei ya kawaida, yaani mwaka maalum wa kuomba upatanisho, uongofu na ukombozi. Kupitia mada ya Jubilei ya mwaka huu 2025, Baba Mtakatifu Francisko alitukumbusha kwamba katika ulimwengu ambamo mizozo, wasiwasi na chuki zimesalia kuwa za kawaida sana “tumaini halikatishi tamaa.” Kama Baba Mtakatifu alivyoeleza, kwamba “Tunahitaji kutambua wema mkubwa uliopo katika ulimwengu wetu, ili tusije tukajaribiwa kujifikiria kuwa tumezidiwa na uovu na vurugu. Hivi karibuni nilipata fursa ya kufanya kazi na kundi la wanawake ambao wameonesha ushuhuda huo wa ajabu, ambao wanaweza kutupatia sisi sote msukumo na matumaini katika mwaka huu wa Jubilei. Hawa ni Masista wa Ursuline huko Cleveland, Ohio nchìini Marekani. Mkasa mmoja uliikumba Jumuiya yao ya kitawa mnamo mwaka 1995 wakati Sr. Joanne Marie Mascha wa shirika hilo, alipobakwa na kuuawa na mwanamume anayeitwa Daniel Pitcher nyuma ya nyumba Mama ya Shirika.
Sr. Joanne Marie alikuwa mwanashirika mpendwa wa Jumuiya yao, aliyejulikana na roho ya upole na ambaye alifanya kazi ya kuendeleza amani na haki duniani. Baada ya kuuawa kwake, Masisita wa Ursuline walitangaza upinzani wao kwa Pitcher kuhukumiwa kifo. Waendesha-mashtaka walipopuuza matakwa hayo, walijazwa na ujumbe na simu kutoka kwa watawa ulimwenguni pote, wakiwasihi waache kufuatilia hukumu ya kifo. Pia waliomba kwamba vurugu zake zisikabiliwe na vurugu za adhabu ya kifo. Hatimaye, Pitcher alihukumiwa, lakini Hakimu alikataa kuchagua hukumu ya kifo kama adhabu yake. Hivi karibuni, makumi ya miaka baadaye, Watawa hao walipokea barua kutoka kwa Pitcher. Alionesha majuto na huzuni yake, na akawaomba watawa hao msamaha. Baada ya mchakato wa kuhakikisha kwamba wengine walioathiriwa na mauaji ya Sr. Joanne Marie, wakiwemo wanafamilia wake, walikubaliana na uamuzi wao, na walijibu kwa barua yao wenyewe. Walikubali msamaha wake. Hawakuepuka maumivu na mateso yaliyosababishwa na uhalifu wake, wakimweleza Pitcher, “Ulipomuua, uliinyima jamii yetu, familia yake na ulimwengu wa Mungu, mtu mpole ambaye alitaka kueneza upendo wa Mungu tu.” Lakini huku wakimtia moyo awe “mtu wa wema, amani na fadhili,” walikubali msamaha huo na kusamehewa.
Ubadilishanaji huu wa barua na uzoefu mkubwa ambao wamekuwa nao kwenye jumuiya yao umewatia moyo masisita hao kupyaisha juhudi zao za kukomesha hukumu ya kifo katika jimbo la Ohio. Ikiwa Pitcher angenyongwa, mabadilishano haya yasingefanyika kamwe na masista walitaka kuhakikisha kwamba milango ya msamaha na upatanisho haifungwi kwa wengine. Historia hii yenye nguvu ya watawa wa Ursuline inaonesha umuhimu wa kuondoa baadhi ya historia kuhusu msamaha, ili wengine wawe wazi kwa mabadiliko hayo na uponyaji. Kwanza, kusamehe hakumaanishi kusahau yaliyotokea au madhara ambayo yametokea. Katika Hati ya “Fratelli tutti” (252), yaani “Wote ni Ndugu, ”Papa Francisko anasema kuwa: "Msamaha ndiyo unaotuwezesha hasa kufuata haki bila kutumbukia katika msururu wa kulipiza kisasi au kusahau ukosefu wa haki."
Masista hao hawakusahau madhara yaliyosababishwa na kuuawa kwa Sr. Joanne Marie na kutokuwepo kwake katika Jumuiya yao. Kiukweli, baadhi ya masista bado walihisi uchungu wa kumpoteza rafiki yao mpendwa, na barua hiyo iliwazamisha tena wote kuchunguza pengo hilo kubwa. Sr. Laura Bregar alisema kwamba alipofungua barua hiyo, “ilinipiga kama tani ya matofali.” Hawakusahau na hawatasahau. Hata hivyo walichagua kusamehe na kuzuia mzunguko wa chuki na vurugu kutokea. Hii inaungana na fundisho la pili: msamaha na haki haviachani. Kiukweli, upendo wa huruma ambao uliwachochea masista, kwanza kupinga hukumu ya kifo na miongo kadhaa baadaye kusamehe Pitcher, uliendeleza maono ya kweli ya haki, kujenga ulimwengu bora, badala ya kupotosha haki kwa kuigeuza kuwa tamaa rahisi ya kulipiza kisasi. Tunaweza na tunapaswa kushughulikia madhara bila kuleta mashambulizi zaidi kwa hadhi ya binadamu.
Hatimaye, masisita hawa wenye ujasiri wanatuonesha kwamba msamaha si udhaifu. Ujasiri wao unaonekana. Ni ushuhuda wa nguvu ya imani yao na nguvu ya jumuiya yao.Kanuni zao zilipojaribiwa, hawakusimama nazo tu, walionesha uwezo wa kweli wa kanuni hizo kuugeuza ulimwengu. Watawa wa Ursuline walipokataa hukumu ya kifo, walisema ndiyo kwa matumaini. Na miongo kadhaa baadaye, Pitcher alijibu kwa kutafuta uponyaji na msamaha. Sr Susan Durkin, katika mkutano kuhusu kubadilishana barua, alisema, “binafsi, nilihisi aina fulani ya uchangamfu ndani yangu, au uzito ambao ulikuwa umeinuliwa ambao ulikuwa pale na sikuweza kutambua.” Matumaini na huruma hufungua njia mpya za uponyaji, kwa wote wanaohusika na jumuiya pana. Tukiongozwa na Historia za matumaini, kama hivi, tunaweza kushuhudia neema isiyotarajiwa ambayo msamaha unaweza kutoa. Tunapotafakari jinsi tunavyoweza kutafuta uponyaji na urejesho kupitia huruma na matumaini katika mwaka huu wa Jubilei, watawa wa Ursuline wametuonesha njia kweli. Tuache tuitikie ushuhuda wao kwa kuungana nao na kujitahidi kujenga leo hii Ufalme wa Mungu ulimwenguni.
Wata wa Ursuline wa Cleverland, huko Ohio
Chimbuko la Shirika hilo lilianzia kwenye nyumba iliyoanzishwa mnamo tarehe 18 Septemba 1874 huko Youngstown na Watawa wa Ursulines wa Cleveland. Konventi hiyo ya watawa ilipata maendeleo ya haraka na mapema ikaweza kufungua matawi mengine. Mnamo 1943, pamoja na kugawanywa kwa eneo la Youngstown kutoka katika jimbo la Cleveland, Waursuline walijitegemea kutoka nyumba mama. Taasisi hiyo iliendelea kutawaliwa kwa mujibu wa kanuni za kimonaki hadi tarehe 15 Januari 1948, ilipopitisha aina ya huduma wa mtindo wa Watawa wanaojitolea kwa ajili ya elimu ya vijana na utengenezaji wa mavazi matakatifu. Makao yao makuu yao yako Canfield, Ohio nchini Marekani.