Gambera Kanuti Mkwe Shirima AJ: Nidhamu, Uwajibikaji, Sadaka na Rasilimali Muda
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Kanisa wanasema, maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo Yesu huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Waamini wanahamasishwa kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba, hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu ameliangazia Fumbo la Mateso na Kifo cha binadamu, kwa njia ya ushuhuda wa maisha na matendo yake, hasa pale, watu wanapoondokewa na wapendwa wao! Hata Kristo Yesu, mbele ya kaburi la rafiki yake Lazaro alitoa machozi, ushuhuda kwamba, Yesu yuko karibu sana na waja wake kama ndugu! Kwa uchungu mkubwa alimwombea Lazaro kwa Baba yake wa mbinguni, chemchemi ya uhai na hatimaye, akamwamuru Lazaro aliyekufa kutoka nje ya kaburi!
Huu ndio mwelekeo wa matumaini ya Kikristo katika kukabiliana na Fumbo la Kifo! Kristo Yesu “anasimama dede” kupambana na kifo ambacho kimejitokeza katika kazi ya uumbaji kinyume kabisa cha upendo wa Mungu na Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu ambaye ameganga na kuponya Fumbo la Kifo katika maisha ya mwanadamu.Mzaburi anasema, “Basi, utujulishe kuzihesababu siku zetu, tujipatie moyo wa hekima.” Haya ni maneno yanayowatia waamini matumaini badala ya kujisikia kuwa wanyonge wanapoyaona maisha yao yana yoyoma na kutoweka mara kama ndoto ya mchana. Kifo kinayaanika maisha ya binadamu na kumwondolea kiburi na kuwahimiza watu kujenga na kudumisha upendo, kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha, ili sadaka na majitoleo yao yaweze kuwapatia amani na utulivu wa ndani wanapokabiliana na Fumbo la Kifo! Kristo Yesu anapenda kuimarisha matumaini ya waja wake kwamba, Yeye ndiye ufufuo na uzima! Jambo la msingi ni wao kumwamini. Mbele ya Fumbo la Kifo binadamu ni mnyonge na ni “mdogo sana kama kidonge cha piliton.” Lakini, neema katika hali na mazingira kama haya, inaweza tena kuamsha imani na Yesu mwenyewe kuwashika mkono watu wake na kuwaambia “Talitha kum” tafsiri yake “Msichana, nakuambia, inuka.” Haya ni maneno ambayo Yesu anapenda kumwambia kila mtu, simama na fufuka tena! Baba Mtakatifu Francisko anasema, haya ndiyo matumaini ya Kikristo mbele ya Fumbo la Kifo. Kwa mwamini hili ni lango ambalo liko wazi; lakini kwa mwenye mashaka, ni giza linalomwandama na kumtumbukiza mtu katika majonzi na msiba mkuu. Kwa kila mwamini, hii itakuwa ni neema siku ile mwanga huu utakapoangaza.
Baba Mtakatifu anasema, kifo ni sehemu ya matukio ya maisha ya mwanadamu, ni urithi na kumbukumbu. Tangu pale mwanadamu anapozaliwa, anaanza safari ya kuelekea katika Fumbo la kifo, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwajalia kufa kifo chema badala ya kujifungia katika muda na ubinafsi wao! Mama Kanisa anawataka watoto wake kujiandaa vyema ili kukabiliana na Fumbo la kifo katika maisha yao. Kifo ni urithi unaofumbatwa katika ushuhuda ambao unapaswa kutolewa kwa wale wanaobaki. Baba Mtakatifu anawataka Wakristo kujiuliza swali la msingi, Je, wewe leo ukifa utaacha ushuhuda gani nyuma yako? Swali hili liwasaidie waamini kujiandaa kufa vyema. Lakini, kabla ya kuitupa mkono duniani Je, kuna jambo gani ambalo ningependa kulifanya leo hii? Fumbo la kifo liwasaidie waamini kufikiri na kutenda kila siku wakitambua kwamba, daima wako safarini kuelekea kufani! Maswali haya ni muhimu kwa waamini wote, ili kuweza kujiandaa vyema ili kukabiliana na Fumbo la kifo! Ni katika muktadha huu, Shirika la Mitume wa Yesu, AJ., linaomboleza kifo cha Padre Kanuti Mkwe Shirima, AJ., kilichotokea ghafla tarehe 7 Machi 2025 huko Afrika ya Kusini, alikokuwa anafanya utume wake na kuzikwa Uru Seminari, Jimbo Katoliki la Moshi, Tanzania tarehe 20 Machi 2025, Ibada iliyoongozwa na Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki la Moshi.
Katika mahubiri yake, Askofu Ludovick Joseph Minde, alimshukuru Mungu kwa zawadi ya Padre Kanuti Mkwe Shirima, AJ; amewashukuru wazazi waliompatia malezi na makuzi bora aliyowashirikisha watu wa Mungu katika maisha na utume wake kama Padre. Kwa hakika umati mkubwa uliohudhuria mazishi yake ni ushuhuda wa malezi yake makini yaliyojikita katika: nidhamu, uwajibikaji, sadaka na kujituma katika maisha; mambo yaliyomwilishwa katika uongozi bora, uliyoiwezesha Seminari ya Uru, inayomilikuwa na kuongozwa na Shirika la Mitume wa Yesu, AJ., kupata mafanikio makubwa katika taaluma.Leo Uru Seminari inajivunia kuwa na mabalozi wema waliofundwa wakapikika kitaluni hapo na leo hii ni mfano bora wa kuigwa katika jamii. Kati ya wanafunzi waliosoma Uru Seminari ni Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi. Wamo pia aliyewahi kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Simon Nyakoro Sirro. Hayati Cyril Chami, aliyewahi kuwa Waziri na kuna umati mkubwa wa wanafunzi kutoka Uru Seminari wanaoshikilia nafasi mbalimbali za uongozi katika jamii na wameendelea kuwa ni mifano bora ya kuigwa katika maisha ya ndoa na familia. Hii yote ni kutokana na nidhamu ambayo Padre Kanuti Mkwe Shirima, AJ., enzi ya uhai wake kama Gambera aliipatia kipaumbele cha kwanza bila kusahau rasilimali muda. Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi ameshiriki Ibada ya Misa Takatifu ya mazishi ya Gambera mstaafu Padre Kanuti Mkwe Shirima, AJ., na kuwasilisha mchango wa shilingi milioni 50 kutoka kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi, CCM, kama mchango wake wa kumuenzi Padre Kanuti Mkwe Shirima.
HISTORIA FUPI YA MAREHEMU PADRI KANUTI MKWE SHIRIMA, AJ. Kuzaliwa: Marehemu Padri Kanuti Shirima alizaliwa tarehe 31/05/1949, Marangu-Olele, Mkoani Kilimanjaro, kwa familia ya Baba Athanasi Makundi na Mama Yulitha Mashirima, akiwa mtoto wa pili kati ya watoto kumi. Ubatizo, Komunio ya Kwanza na Kipaimara: Marehemu Padri Kanute Shirima alibatizwa tarehe 26/12/1949, na kupewa Komunio ya Kwanza mwaka 1962, na Kipaimara mwaka 1964, katika Parokia ya Mtakatifu Yosefu, Mashati, Rombo. Elimu ya Msingi na Sekondari: 1961 – 1965: Shule ya Msingi Olele, Rombo. 1966 – 1967: Shule ya Kati (Middle School) Olele, Rombo. 1968 – 1971: Seminari ya St. Mary’s, Nadiket, Moroto, Uganda. Malezi na Majiundo ya Kitawa na Upadre: 1972 – 1973: Uaspiranti – Shirika la Mitume wa Yesu, Moroto, Uganda. 1974 – 1975: Unovisi – Shirika la Mitume wa Yesu, Moroto, Uganda. 12/12/1975: Nadhiri za Kwanza, Shirika la Mitume wa Yesu, Moroto, Uganda. 1975 – 1976: Masomo ya Falsafa, Seminari Kuu Alokulum, Gulu, Uganda. 1977 – 1981: Masomo ya Taalimungu, Seminari Kuu ya Mtakatifu Thoma wa Aquino, Nairobi, Kenya.15/08/1980: Nadhiri za Daima, Shirika la Mitume wa Yesu, Nairobi, Kenya. 23/11/1980: Daraja Takatifu la Ushemasi, Seminari Kuu ya Mitume wa Yesu, Nairobi, Kenya na Mhashamu Askofu Sisto Mazzoldi, MCCJ mmojawapo wa wanzilishi wa Shirika letu. 07/06/1981: Daraja la Upadri, Kanisa Kuu, Kristo Mfalme, Jimbo Katoliki la Moshi, Tanzania na Mhashamu Askofu Joseph Spendi aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Moshi.
Utume na Masomo ya Uzamifu: 1981: Utume, Uru Seminari, mlezi na Makamu Gambera. 1982 – 1989: Gambera, Uru Seminari. 1989 – 1992: Masomo ya Uzamifu Chuo Kikuu cha Kikatoliki, Leuven, Ubelgiji. 1993 - 1995: Mkufunzi, Seminari Kuu ya Mitume wa Yesu, Nairobi, Kenya. 1996 – 1998: Gambera, Seminari Kuu ya Mitume wa Yesu, Nairobi, Kenya. 1999 – 2008: Paroko, Parokia ya Mwili na Damu Takatifu, Naibili, Moshi, Tanzania. Tangu Mwaka 2009 – 2010: Wakili Paroko, Parokia ya Masakta, Jimbo Katoliki la Mbulu, Tanzania. 2011 – 2021: Paroko, Parokia ya Rozari Takatifu, Glen Cowie, Witbank, Afrika Kusini. 2022- 2025: Paroko, Parokia ya Watakatifu Mashahidi wa Uganda, Schoonoord, Witbank, Afrika Kusini. Ugonjwa hadi mauti: Padri Kanuti Shirima hakuwa na historia ya kuugua na kulazwa hospitalini. Alifariki ghafla asubuhi ya tarehe 7/3/2025, akiwa anajiandaa kwenda kumwona daktari, baada ya kujisikia vibaya kwa siku chache. Padri Kanute Shirima alifariki akiwa na miaka 76 ya kuzaliwa, 50 ya Maisha ya Kitawa na 44 ya Upadri. Tutamkumbuka Padre Kanuti Shirima, AJ alivyojitoa kuhudumu na kutumika bila kujibakiza kuwatumikia watu na Mungu kwa msimamo thabiti bila kuyumbishwa na chochote katika kusimamia yale aliyoamini ni sahihi kwa kadiri ya Sheria na kanuni. Padre Kanuti anakumbukwa kwa ujasiri wa uchapa kazi bila kujibakiza, Moyo wa ukarimu mfano wanafunzi wasiokuwa na uwezo wa kifedha na waliotamani kusoma aliwasaidia kufikia ndoto zao na hamasa zake za kutaka kila mtu kutumia vyema muda na kusisitiza kila mtu afanye jambo kwa wakati sahihi mahali sahihi na kwa nia sahihi. Kweli katika ufundishaji alikuwa mbobezi wa historia ya Kanisa, aliipenda na alifundisha kwa makini na wanafunzi kuelewa.
Shukrani: Awali ya yote, tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya maisha na wito aliomjalia. Kisha, tunawashukuru wazazi wake (na kwa namna ya pekee, mama yake mpendwa aliye kati yetu hapa), kwa kumpokea kama zawadi ya Mungu kwao, kumlea na kumpa makuzi mazuri yaliyomsaidia kuitikia wito wake mpaka mwisho. Pia, tunawashukuru ndugu zake, jamaa, marafiki, waalimu na walezi wake wote, wa ngazi zote; na watu wote wa Mungu, aliojaliwa kukutana nao katika safari yake ya maisha na wito wake, kwa ushirikiano na misaada yao ya hali na mali, iliyomwezesha kudumu katika wito wake mpaka mwisho. Shukrani zetu za dhati ziwafikie Baba Askofu Xolelo Thaddaeus Kumalo wa Jimbo Katoliki la Witbank, Afrika Kusini, Jumuiya za Kitawa na za Wakleri zinazohudumu Jimboni kwake, wakiwemo Mitume wa Yesu; na Wanaparokia wa Parokia za Glen Cowie na Schoonnoord, alizohudumia Padri Kanuti Shirima, kwanza kwa sala zao, na kisha kwa msaada wao wa hali na mali uliowezesha mwili wake kuwa hapa leo kwa mazishi. Kwa njia ya pekee sana, tunamshukuru Baba Askofu wetu wa Jimbo Katoliki Moshi, Mhashamu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS, kwa upendo wake mkuu wa kukubali kupangua ratiba yake ya siku ya leo, na kufika kushiriki pamoja nasi kumwombea na kumlaza mpendwa wetu, Marehemu Padri Kanuti Shirima, katika amani ya Kristo Yesu. Aidha tunawashukuru wote mliofika kushiriki Ibada hii ya mazishi ya mpendwa wetu, marehemu Padri Kanuti Shirima, na sasa kwa heshima na unyenyekevu wote namwomba Baba Askofu atuongoze. Karibu Baba Askofu. (Imesomwa na Pd. Albert Mugisha, AJ.)