Dominika II ya Kwaresima:Kupitia kung’ara Mlimani,Yesu anatayarisha wanafunzi
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika Dominika ya II ya Kwaresima, tarehe 16 Machi 2025, Mama Kanisa ametupatia fursa ya kutazama tukio la onesho la ajabu kuhusu Yesu kung’ara katika Mlima akiwa na wanafunzi wake, kama tusomavyo katika Injili ya Luka 9:28-36, na masomo mengine: Somo la kwanza: Kitabu cha Mwanzo 15:5-12,17-18; Zaburi. 27:1, 7-9, 13-14 na Somo la pili: Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi 317-4:1. Katika Kanisa la Watakatifu Urbano na Laurenti, Prima Porta Roma, Padre Janusz Brzóska wa Shirika la Mpadre wa Mtakatifu Paulo alitoa mahubiri kuhusiana na Injili ya Siku hiyo. Padre alisema kuwa: “Katika Dominika ya Pili ya Kwaresima, Kanisa linamwilisha roho zetu kwa kifungu cha Injili juu ya Kugeuzwa Sura kwa Bwana. “Wakati huo Yesu aliwachukua Petro, Yohane na Yakobo, akaenda mlimani kusali. Alipokuwa akisali, sura ya uso wake ikabadilika, mavazi yake yakawa meupe na kumeta-meta.” Wanafunzi pia waliona Musa na Eliya na kusikia sauti ya Mungu Baba, ambaye aliwaambia Yesu alikuwa nani na kwamba wanapaswa kumsikiliza. Wanafunzi waliona utukufu wa Yesu waliona kwamba hakuwa mwalimu rahisi, bali Mwana wa kweli wa Mungu, ambaye alikuwa Mungu.
Kujiandaa na mateso
Kwa nini walipata uzoefu huu? Kwa nini Yesu aliwaonesha utukufu wake? Ili kuimarisha mioyo yao katika saa ya msalaba... Ili wasije wakaingia kwenye jaribu la kukana hasa watakaposhuhudia mateso na kifo cha Yesu... Ili wasiwe na kashfa na kupoteza imani katika ukweli kwamba Yeye alikuwa Mwana wa Mungu kweli, watakapomwona, ameshindwa kibinadamu, amedhalilishwa, amehukumiwa kifo, amesulubiwa na kuuawa... Kupitia ufunuo wa utukufu wake juu ya Mlima Tabor, Yesu alitayarisha mioyo yao kwa saa ile ngumu ya msalaba wake... Kwa kutaka kuelewa kwa kina zaidi Padre huyo alisimulia historia moja: ‘Siku moja mama na baba, ijumaa ya kwanza ya mwezi, walikwenda kanisani asubuhi ili kuungama, kushiriki Ekaristi na kumpokea Yesu katika Komunyo... Waliporudi kwenye nyumba yao, hata kabla ya kuingia ndani, walisikia kilio kikubwa cha mtoto wao mkubwa ... Walihisi kuna jambo zito limetokea. Baada ya kuingia ndani ya nyumba hiyo, mtoto wao huyo aliwajulisha kuwa alipigiwa simu na taarifa za kifo cha mtoto wao wa pili aliyefariki kwa ajali ya gari...”
Padre Brzóska alisema “kaka na dada wapendwa, asubuhi hiyo Yesu alikuwa amewaalika wazazi hao kwenye maungamo na meza ya Ekaristi. Huo ndio ulikuwa Mlima wao wa Tabor. Yesu alikuwa ameimarisha mioyo yao na kuwatayarisha kuishi kwa imani mkasa wa kifo cha mtoto wao. Hata sisi hatujui nini kitatokea katika maisha yetu ... Pengine, katika muda fulani, baadhi yetu pia tutapitia msalaba wetu binafsi... Pengine Neno hili hili, Ekaristi hii, ni kwa ajili yako na kwa ajili yangu mimi kama mlima wa Kugeuzwa Sura, ambapo Yesu anaimarisha mioyo yetu kuishi kwa imani mateso yanayotungoja... Wakati mwingine katika maisha huja wakati wa giza na maumivu."
Wakati mwingine tunahisi uzito wa msalaba
Padre huyo alikaza kusema kuwa "Wakati mwingine tunahisi uzito wa msalaba kwa nguvu... Kwa kukazia juu ya imani ya Baba wa imani kuu kupitia somo lililokuwa limesomwa alisema: “Ibrahimu, ambaye tulimsikia katika somo la kwanza, pia alipitia haya. Lakini giza lile lile, hofu hiyo, mateso yale ndiyo wakati ambapo Ibrahimu alifanya agano na Mungu. Wakati mwingine kuna nyakati ngumu sana maishani mwetu, nyakati za giza na huzuni, uzoefu wa maumivu na mateso... ni nyakati tunapoingia katika agano na Mungu - wakati urafiki wetu Naye unazidi na kuimarika zaidi kuliko hapo awali. Kwa kuhitimisha Padre Brzóska alisema kuwa “Maria, Mama yetu, Tumaini letu... utuombee, ili wakati huu wa Ekaristi Bwana aitie nguvu mioyo yetu, ili tusipoteze imani kwake tunapoishi msalaba wetu binafsi,” alihitimisha.