杏MAP导航

Tafuta

Watoto nchini Burkina Faso Watoto nchini Burkina Faso 

Burkina Faso na Eritrea,Mapadre wa Pavoni wanasaidia Wanafunzi Vijana Viziwi

Katika nchi hizo mbili za Afrika,katika shule zilizoanzishwa na Shirika la Wana wa Maria,kazi inafanywa ili kuongeza uwezo wa watoto viziwi,waliotengwa na maisha ya kijamii na kiuchumi.Mkuu wa Kanda ya Italia,Padre Dall'Era:"wanafunzi wote,hata wale wasio na ulemavu wanashirikiana kupitia lugha ya ishara.Hakuna ubaguzi,kuna ushirikiano mzuri,bali lazima tukubali,unyanyapaa ni vigumu kutokomeza."

Na Enrico Casale na Angella Rwezaula – Vatican.

Ukimya hauwezi kuwa kikwazo. Kutosikia hakupaswi kuwa kizuizi kinachowatenga watoto viziwi kutoka katika maisha ya kijamii na kiuchumi. Ujumuishi ni kanuni iliyo nyuma ya shule ya Saaba, iliyoundwa nchini Burkina Faso, na ile ya Asmara, nchini Eritrea, iliyoanzishwa na Watawa wa Pavoniani, Shirika lililoanzishwa na Padre Lodovico Pavoni wa Brescia nchini Italia. Alieleza hayo Padre Dario Dall'Era, mkuu wa Kanda ya Italia wa Shirika hilo kwamba,  pia ni kitu kingine zaidi: nyuma yake kuna nia ya kuimarisha uwezo wa vijana hawa na kuwapa fursa ya ukombozi. "Tunabaki kwenye mstari wa mwanzilishi wetu, Mtakatifu Lodovico Pavoni. Tunawapa vijana ambao hawakuwa na maisha mazuri, mafunzo ya kitaaluma ambayo yanawatayarisha kwa ajili ya maisha ya baadaye ya kufanya kazi na, wakati huo huo, inawaruhusu kupokea aina ya mshahara, ili kujitegemea kutoka kwa familia zao." Padre Dario alikumbusha kuwa: “Ni mfano ambao tayari umejaribiwa sana nchini Italia na Ulaya. "Kwa sehemu kubwa ya karne ya ishirini, watoto wa familia maskini hawakuweza kwenda shuleni: walipaswa kuchunga mifugo, kufanya kazi mashambani, kuingia kwenye warsha. Kuhudhuria shule kulionekana kuwa ni kupoteza muda. Shule za Pavonia zilitoa kazi na mafunzo ya ufundi stadi, na kufanya elimu ikubalike zaidi kwa familia."

Burkina Faso, ushirikiano


Nchini Italia, pamoja na mageuzi ya shule ya miaka ya 1970, mtindo huu uliingia katika mgogoro. "Katika Afrika, hata hivyo, bado ni halali. Nchini Burkina Faso tunatoa kozi za mbinu za kilimo na ufundi hasa uchomeleaji." Shule hii ina kitu cha ziada: watoto wenye uwezo na viziwi wanasoma hapo. “Wanafunzi huingiliana kupitia lugha ya ishara ambayo kila mtu anahitajika kujifunza. Hakuna ubaguzi shuleni, kinyume chake, muunganiko mzuri unatokeza. Tunafanya kazi ili kuhakikisha kuwa viziwi wanakubalika katika jamii, ingawa, kiukweli, unyanyapaa ni vigumu kutokomeza."

Mpango nchini Eritrea

Mpango kama huo pia unaendelea nchini Eritrea. Wapavoni wamekuwepo katika nchi hiyo ndogo katika Pembe ya Afrika tangu mwaka 1969, wakati vita vikali vya uhuru vilipokuwa vikiendelea kati ya Waeritrea na serikali kuu ya Ethiopia. Mapadre wa Shirika la Pavonia walianzisha programu za usaidizi kwa watoto yatima, wakiwapa mavazi, chakula na matibabu. Kisha, katika miaka ya 1980, mipango ya kwanza ya kuasili ya masafa marefu ilizaliwa ili kusaidia familia zilizowakaribisha wavulana na wasichana hawa walioachwa bila wazazi. Kwa upande wa Laura Arici, wa Kikundi cha Misheni za Afrika, (NGO) iliyoundwa kusaidia watawa wa Pavoni alisema:"Katika miaka ya 1990, Shule ya Ufundi ya Pavoni huko Asmara na shule ya kilimo ya Hagaz ilipata uhai, iliyoundwa kwa ushirikiano na Shirika la Ndugu wa Shule za Kikristo (Lasallian).

Walitoa mafunzo ya hali ya juu ya kiufundi na kilimo, ambayo yaliwahakikishia wanafunzi uwezekano wa kupata chuo kikuu baada ya kuhitimu." Taasisi zote mbili baadaye zilichukuliwa na mamlaka huko Asmara kama sehemu ya kampeni ya kutaifisha vituo vya huduma za kijamii na afya vinavyoendeshwa na mashirika ya kitawa. Pamoja na hayo, Wapavoni hawakuacha shughuli zao. Kituo cha Kijamii cha Pavoni huko Asmara kiliendelea kufanya kazi. Kwa mujibu wa Arici aliarifu kuwa: “Katikati watoto viziwi na wenye uwezo wanakaribishwa. Wanapewa kozi za kimsingi za sayansi ya kompyuta, kuweka vitabu, kukata na kushona. Masomo hufanywa kwa lugha ya ishara. Hizi ndizo fursa pekee ambazo viziwi wanazo kufuata njia ya elimu katika mji mkuu wa Eritrea."

Mafunzo ya wazazi


Baada ya muda, wavulana walijiunga na familia zao. "Baba na mama wamehisi uhitaji wa kujifunza lugha ya ishara pia," meneja anaendelea kusema: "Wanazoezwa kwa njia hii kuboresha mawasiliano na watoto wao. Ni lazima kusema kwamba njia za masomo huambatana na shughuli za burudani: kituo ni aina ya hotuba ambapo watoto pia hujifunza maadili ya kibinadamu na ya kidini." Mafunzo haya ya kibinadamu yamekuwa sehemu muhimu ya shughuli za Wapavoni tangu wakati wa mwanzilishi wao, aliyeishi kati ya karne ya 18 na 19. “Katika shule zetu tumekuwa tukitoa kiwango cha juu cha elimu. Tumekuwa tukitaka watoto wetu wawe walimu wa sanaa, wasikivu wa kufanya kazi vizuri, ubora, na ubunifu wa hali ya juu. Kwa sababu hii sisi daima tunajaribu kuchochea mawazo na tamaa ya kuunda kitu kipya. Yote hii, hata hivyo, haijawahi kutengwa na mafunzo ya kibinafsi. Walimu wetu walifanya kazi kila siku ili kuhakikisha kwamba watoto wanakuwa sio tu mafundi bora bali pia watu wanaowajibika na raia, wanaoheshimu maadili." anahitimisha Padre Dario.
 

06 Machi 2025, 10:23