杏MAP导航

Tafuta

Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Tanzania kwa ajili ya Kwaresima:Kwaresima ni safari ya imani na tunasafiri pamoja. Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Tanzania kwa ajili ya Kwaresima:Kwaresima ni safari ya imani na tunasafiri pamoja. 

Maaskofu Tanzania(TEC),Ujumbe wa Kwaresima 2025:Simameni Imara Katika Imani

Ujumbe wa Kwaresima 2025 wa TEC unanoongozwa na Kauli mbiu:“Simaneni Imara katika Imani(1Kor 16:13).Maaskofu wanafafanua maana ya imani kupitia Maandiko Matakatifu na Mafundisho ya Kanisa kwamba:imani ni zawadi ya kimungu,imani ni kiini cha maisha ya kila siku ya mwanadamu.Kweresima ni kipindi cha kusafiri kiroho na Kristo Mwokozi wetu,kupitia njia ya imani,ambayo mwanadamu anashiriki kuujenga Ufalme wa Mungu.Kwa upande wa Jubilei Kuu 2025 ni ya matumaini.

Na ngella Rwezaula – Vatican.

Katika Ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Tanzania (TEC) kwa ajili ya Kwaresima 2025 ambayo imeanza Jumatano ya Majivu, tarehe 5 Machi 2025, unaongozwa na kauli mbiu: “Simameni Imara katika Imani” (1Kor 16,13). Ujumbe huo umegawanyika katika sura nne ambazo nazo zimegawanyika katika sehemu kadhaa za ufafanuzi. Katika sura ya kwanza ya ujumbe huo inazungumzia uelewa wa jumla wa imani. Sura ya pili inafafanua juu ya safari ya imani, sura ya tatu inazungumzia juu ya Imani na Jubilei kuu ya Mwaka 2025 na hatimaye sura ya nne ni kuuhusu mwaliko wa Maaskofu kwa ujumla wa kusimama kidete katika imani. Vatican News inachapisha ujumbe kamili:

SURA YA KWANZA UELEWA WA JUMLA JUU YA IMANI:

Maana ya Imani

1. Imani ni hali ya kuamini au kuwa na hakika juu ya kitu, bila kuwa na uthibitisho wa moja kwa moja. Inahusiana na kuamini katika Mungu, nguvu, au dhana fulani, hata kama huwezi kuona au kuthibitisha wazi. Kadiri ya Maandiko Matakatifu, hususan Waraka kwa Waebrania, imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana” (rej. Ebr 11:1). Katekisimu ya Kanisa Katoliki inaeleza imani kuwa: ni mwambatano wa nafsi ya mtu kwa Mungu: wakati huo huo na bila kutengana ni kukubali kwa hiari ukweli wote ambao Mungu ameufunua (KKK 150).

2. Hivyo, kuamini ni kujikabidhi kikamilifu, kwa uhuru kamili na kwa furaha kwa mpango wa Mungu katika historia. Mfano mzuri tunaupata kwa babu yetu wa imani Abraham (rej. Mwa 12-22) na mama yetu Bikira Maria kwa NDIYO yake (Lk 1:38), tukitaja kwa uchache tu. Kwa msingi huo, imani ni mwitikio ambao kwao akili na mioyo yetu inasema NDIYO kwa Mungu Baba na kwa kukiri kuwa Yesu Kristo ni Bwana. Ndiyo hii inabadilisha kabisa maisha ya mtu, inafungua njia kuelekea utimilifu wa maisha na kuyafanya mapya yaliyojaa furaha na matumaini ya kweli.

Imani ni zawadi ya kimungu

3. Kwanza kabisa, imani ni zawadi ya kimungu, yaani, zawadi kutoka kwa Mungu. Imani si tu ni mwitikio wa kiakili wa mwanadamu kwa kweli fulani kuhusu Mungu bali pia ni tendo ambalo kwalo mtu anajikabidhi kwa uhuru kamili kwa Mungu ambaye ni Baba anayetupenda upeo. Mwanadamu anaweza tu kumwamini Mungu kwa sababu yeye (Mungu) anakuja karibu nasi na kugusa maisha yetu kwa njia ya Kristo kwa fumbo la umwilisho (rej. Yn 1:14), wakati huo huo Roho Mtakatifu akituwezesha kumpokea Mungu katika nafsi zake tatu.

4. Imani ni jambo la ndani kabisa (kiini) la maisha ya kila siku ya mwanadamu. Kwa asili kila mwanadamu anabeba ndani yake kiu/hamu iliyofumbika (ya ajabu) ya Mungu. “Tamaa ya kuwa na Mungu imeandikwa katika moyo wa mtu kwa sababu ameumbwa na Mungu, na kwa ajili ya Mungu” (KKK 27). Tena, hadhi ya mwanadamu kwanza kabisa iko ndani ya wito wake wa kuungana na Mungu (rej. GS 19 #1). Imani kwa Mungu ambaye ni upendo, anayejiweka karibu na mwanadamu kwa umwilisho wake na kwa kujitoa kwake msalabani, na ambaye anatuokoa na kutufungulia tena milango ya mbinguni, yaonesha dhahiri kuwa utimilifu wa mwanadamu unatokana tu na upendo wake kwa Mungu. Hakika, imani lazima iwe ndio nguvu yenye kuleta mabadiliko katika maisha yetu(rej. Papa Benedicto XVI: Utangulizi Juu ya Mwaka wa Imani, 17 Oktoba 2012).

Imani ni fadhila ya kimungu

5. Tunafundishwa kuwa “Imani ni fadhila ya kimungu ambayo kwayo tunamsadiki Mungu na kila kitu alikichosema na alichotufunulia, na ambacho Kanisa takatifu latutaka tukisadiki, kwa sababu Yeye ndiye Ukweli wenyewe“(KKK 1814). Kwa imani ‘mwanadamu hujitoa nafsi yake yote kwa Mungu”. Ni kwa sababu hiyo mwamini hutafuta kujua na kufanya mapenzi ya Mungu. “Mwenye haki ataishi kwa imani”. Imani hai “hutenda kazi kwa upendo” (Rum.1:17; Gal.5:6).

Nyanja ya imani

6. Kadiri ya Mafundisho ya Kanisa Katoliki, imani ya kweli inajidhihirisha katika namna kuu tatu: yaani katika kuiungama (Lex Credendi), kuiadhimisha (Lex Orandi) na kuishuhudia (Lex Vivendi). Tafsiri yake ni kwamba: jinsi tunavyosali (lex orandi), ndivyo tunavyoamini (lex credendi) na ndivyo tunavyoishi (lex vivendi) – (rej. Benedikto XVI, Sakramenti ya Upendo n. 34).

Imani tunaiungama

7. Kwa vile imani inahusu kukubali kwa hiari ukweli wote ambao Mungu anaufunua (KKK 150), ukweli huu hauwezi tu kubaki moyoni mwa mtu, bali lazima kuwa tayari kuukiri wazi kwa maneno yetu mbele ya wengine. Vinginevyo, itakuwa vigumu kutambua fika kama mmoja anaamini katika nini na hata kweli za imani zitabakia zikiwa mfu katika maandishi. Ni katika kukiri kwa midomo yetu hadharani kile tunachokiamini ndipo tutaweza kujipambanua kati ya wengi na kudhihirisha utambulisho wetu.

8. Kwa upande wa Mkristo Mkatoliki, ipo Kanuni ya Imani ambayo ni ufupisho wa mafundisho msingi ya Kanisa ambayo kila mwamini binafsi anapaswa kuyakiri na kuyaishi. Hivyo, mmoja atatambulika kuwa ni muamini kweli kama yuko tayari kuikiri imani yake kwa uthabiti.

Imani tunaiadhimisha

9. Imani ya kweli huadhimishwa, na kadiri inavyoadhimishwa vyema ndivyo inavyodhihirisha jinsi ambavyo mtu anaamini. Ungamo la Imani linapata nafasi yake katika adhimisho la ibada kwa Mungu, yaani katika liturujia. “Liturujia ni kilele ambacho kwacho shughuli za Kanisa zinaelekezwa; na ni chemchemi ambamo nguvu yake yote hububujika” (SC n.10). Kama vile ili kuweza kushiriki vizuri liturujia ya Kanisa kunahitaji imani, vivyo hivyo, ili kuweza kuishi vizuri maisha ya kikristo tunahitaji neema za Mungu zitokanazo na liturujia.

Imani tunaishuhudia

10. Mtakatifu Yakobo Mtume, katika barua yake anahimiza kuwa “Imani bila matendo imekufa” (rej. Yak. 2:14-26) na haiwezi kuzaa matunda ya uzima wa milele (KKK uk. 27-28). Matendo hunena Zaidi kuliko maneno. Matendo huonesha umaana na ulazima wa maneno yaliyotamkwa. Kwa mfano, mtu anaposema kuwa “Yesu Kristo ni Bwana” basi anapaswa kudhihirisha jambo hilo katika maisha yake ya kila siku.

11. Imani ya kweli inabidi tuitazame kama mwanga, kwani mara tu mwanga wa imani unapozima basi mianga mingine nayo hufifia. Mwanga wa imani ni wa pekee, kwani una uwezo wa kuangazia kila kipengee cha maisha ya mwanadamu. Mwanga huu hutoka kwa Mungu mwenyewe. Imani tunayoipokea kama zawadi toka kwa Mungu, huwa ni nuru katika njia yetu maisha yetu yote (Papa Francis, Lumen Fidei n. 4). Ndio maana hata Maandiko Matakatifu yanatuhimiza kuwa nuru (Mt 5:14), yaani tuishuhudie imani kwa maisha yetu ya kila siku. Ushuhuda wa kweli unatudai kuwa kuifahamu vema imani yetu na kuwa tayari kuitetea mbele ya watu wote.

Umoja na Mfungamano wa Imani - na wito wa kuirithisha kwa wengine

12. Kadiri ya mafundisho ya Kanisa Katoliki, imani ni “moja”, kwa nafasi ya kwanza, kwa vile Mungu naye ni mmoja ambaye anajulikana na kuungamwa (rej. Efe 4:5-6). Imani ni moja kwa sababu inaelekezwa kwa Bwana mmoja, katika maisha ya Kristo, kwa historia kamili anayoshiriki pamoja nasi. Hatimaye, imani ni moja kwa vile inaungamwa na Kanisa zima, ambalo ni mwili mmoja na roho moja. Kwa vile imani ni moja, sharti iungamwe katika uhalisia na ufungamanifu wake; yaani, hakuna kipengee cha imani ambacho chastahili kupuuzwa kwani ni sawa na kupuuza imani kamili. Kwa ajili ya kulinda umoja wa imani na uenezaji wake ulio kamili, Bwana alilipatia Kanisa lake zawadi ya uhalifa wa mitume (rej. Lumen Fidei n. 47-49).

Uhusiano kati ya kuamini na kufikiri

13. Kwa kutambua upendo wa Mungu unaodhihirika kupitia kazi ya uumbaji, imani inamsaidia mwanadamu kuheshimu uumbaji zaidi na zaidi. Kuhusu ukweli huu, baba Mtakatifu Fransisko, katika hati yake kuhusu Uumbaji (Laudato Si) anasema: “Ulimwengu wote unanena juu ya upendo wa Mungu, upendo wake usio na mipaka kwetu” (n. 84). Tena, Imani inamsaidia mwanadamu kubuni mbinu mbalimbali za maendeleo ambazo hazijajikita tu katika utumiaji na faida, lakini katika kutazama uumbaji kama zawadi ambayo kila mmoja wetu ana deni la kuitunza; inatuwezesha kutengeneza mifumo mizuri ya utawala, katika kutambua kuwa madaraka yanatoka kwa Mungu na ni kwa ajili ya faida ya wote. (Lumen Fidei n.55). Hivyo, kwa imani mwanadamu anarejeshwa katika wajibu wake wa kuufanya ulimwengu mahali pazuri pa kuishi na kuujenga ufalme wa Mungu tangu hapa duniani.

14. Kwa kusoma alama za nyakati na kwa kuutazama ulimwengu wetu wa leo ambapo mwanadamu anaelekea kujiaminisha kuwa anaweza kufanya mambo yote kwa kutegemea uwezo wake tu na kudhania kuwa imani inakinzana na fikira; ni vema kuweka mkazo wa pekee katika kuonesha uhusiano uliopo kati ya imani na fikira. Wakati imani ni hali ya kuamini au kuwa na hakika juu ya kitu, bila kuwa na uthibitisho wa moja kwa moja; fikira ni mkusanyiko na mtiririko wa mawazo unaotengeneza msimamo wa kiutekelezaji ndani ya mtu. Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, anafanya majumuisho ya uhusiano kati ya imani na fikira kwa maneno haya: “uwezo wa mwanadamu wa kufikiri haubatilishwi au kupungua thamani katika kukubali kweli za imani, ambazo kwa namna yoyote ile zinafikiwa kwa uchaguzi uliojaa uhuru na uelewa” (rej. Fides et Ratio n. 43).

15. Hivyo, imani ambayo mmoja anaiishi kwa uaminifu, haikinzani na sayansi, bali inashirikiana nayo. Imani hutoa kigezo msingi katika kustawisha maslahi ya watu wote na kuiomba sayansi kubandukana na zile jitihada ambazo ni kinyume na mpango asili wa Mungu na ambazo huleta athari hasi kwa uumbaji. Katika muktadha huu, tafiti ambazo huleta athari chanya, kwa mfano, kwa ajili ya kulinda na kutetea maisha na zile zinalenga kuondoa magonjwa, yafaa kuungwa mkono.

Ubatizo – mwanzo wa safari ya imani ya mkristo

16. Imani Katoliki tunaiishi kwa pamoja na katika ushirikano huo imani ya kila mmoja huweza kukua na kustawi (rej. KKK 166). Safari yetu ya imani inaanza rasmi katika Ubatizo, Sakramenti ambayo kwayo tunampokea Roho Mtakatifu anayetufanya watoto wa Mungu katika Kristo, na hivyo kuingizwa katika jumuiya ya waamini, yaani Kanisa. Kutokana na Ubatizo, mtu anaitwa katika maisha mapya, na kufanya ungamo hili la imani yake pamoja na ndugu zake. Hakika, ni kwa njia ya Kanisa ndipo imani ya mtu binafsi hukua na kukomaa. Familia inatarajiwa kuwa ni shule ya kwanza ambamo mtoto anafundishwa juu ya imani.

SURA YA PILI

KWARESIMA NI SAFARI YA IMANI: Utangulizi

17. Kipindi cha Kwaresima ni kipindi cha siku arobaini za toba, kufunga, kusali, kutafakari na matendo ya huruma. Aidha ni kipindi cha kusafiri kiroho na Kristo Mwokozi wetu, kupitia njia ya imani, ambayo kwayo mwanadamu anashiriki kuujenga Ufalme wa Mungu, ufalme wa upendo, wa haki na amani. Katika safari ya Kwaresima, Kanisa linatuongoza kwa tafakari na mazoezi yatakayotusaidia kukutana na Bwana Mfufuka aliye jiwe kuu la msingi la Ufalme wa Mungu. Kristo ndiye msingi wa imani yetu, imani ambayo “ni mwaliko wa uongofu wa dhati na ulio mpya kwa Bwana, na Mwokozi pekee wa ulimwengu” (rej. Benedikto XVI, Barua ya Kitume Motu Proprio Porta Fidei, 6).

18. Kwaresima ni mwaliko tuupatao kila mwaka ili kila mmoja wetu aione fursa hii ya kiroho. Ni kipindi cha unyamavu, toba na kuzama ndani ya maisha yetu. Kipindi hiki ni cha neema ambapo kila mmoja wetu anaalikwa kufanya jitihada ya kujiinua na kujichotea neema. Bwana wetu Yesu Kristo anatuambia, “Wakati umetimia, na Ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni ni kuiamini Habari Njema” (Mk 1:15).

19. Safari ya imani yetu ni ndefu. Katika Agano la Kale, ililichukua Taifa la Israeli miaka arobaini kuingia katika Nchi ya Ahadi. Kipindi kirefu ambacho, pamoja na kutawaliwa na matendo makuu ya Mungu, kilitawaliwa pia na vishawishi vingi hata kuwafanya Waisraeli wafikirie mara kadhaa kuiacha safari iliyowaelekeza mbele kwenye Nchi ya Ahadi, na kutamani kurudi nyuma, utumwani Misri.

20. Katika Agano Jipya, ilimchukua Yesu siku arobaini za kufunga ambamo ndani yake aliishiriki hali yetu ya udhaifu, akitufundisha na kutuonesha njia ya kuvishinda vishawishi na dhambi. Safari hii ya Yesu ya siku arobaini ilikuwa ni kielelezo cha kipindi cha maisha yetu; maisha yanayoonja raha na karaha, yakidai kupokea yote hayo kuwa jicho la uradhi wa moyo unaoongozwa na imani. Ni kwa jicho tu la imani ndipo tunapoweza kung’amua uzuri na mpango wa Mungu hata katika hali zile zisizofurahisha na kupendeza, kwani kwa njia hiyo tunaweza kukaa chini na kutafakari juu ya umaana wa mateso yetu. Mtume Yakobo anatukumbusha kuwa, “kujaribiwa kwa imani yetu huleta saburi” (Yak. 1:3; 1 Pet. 1:7).

Tusafiri pamoja na Mungu

21. Safari ya kiroho ya kwenda kwa Baba mbinguni ni ya kudumu. Na safari hii inakabiliwa na mashaka mengi. Ni hatua zenye mabonde na milima. Tukiwa safarini kuna kukata tamaa, kutokuona mbele ya macho yetu kile mazuri yanayokuja. Daima tunatiwa nguvu na Imani, ambayo ni hakika ya mambo yatarajiwayo (rej. Ebr 11:1-3).

22. Kipindi cha Kwaresima tunaalikwa kuiga safari ya baba yetu wa imani; Abraham. Yeye kama mfano mwema anasifiwa kwa kuamini bila ya kuiona kesho yake ikoje. Anajitupa katika mikono ya Mungu bila shaka yo yote. Kwa Abraham, mapito magumu yapo, shida zipo, magonjwa yapo; ila Mungu ni mwaminifu daima. Abraham. Tunasoma “Kwa imani Abraham alimtii Mungu alipoitwa aende kwenye nchi ambayo Mungu angempa kama urithi. Naye aliondoka akaenda ingawa hakujua aendako. Kwa imani aliishi kama mgeni katika nchi ya ahadi. Aliishi nchi ya ugenini katika hema pamoja na Isaka na Yakobo ambao pia walikuwa warithi pamoja naye wa ahadi ile ile. Maana alikuwa akitazamia mji wenye misingi ya kudumu ambao umebuniwa na kujengwa na Mungu mwenyewe” (Ebr 11:8-10).

Safari ya imani ianzie katika familia

23. Kama vile mtoto anavyozaliwa ndani ya familia, na kukua na hadi kuwa mtu mzima; hali kadhalika nayo imani huzaliwa na kukua hadi kufikia ukomavu katika utu uzima ndani ya familia. Familia ni kanisa la nyumbani. Ni kitovu cha imani. Ndani ya familia wazazi wamepewa wajibu wa kuwafundisha watoto wao imani ili wapate kushika amri za Mungu na kuwapenda binadamu wenzao.

Hivyo wazazi wanaelekezwa kama Waisraeli walivyosisitiziwa: “Sikiliza, Ee Israeli; Bwana Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana Mungu wako, kwa moyo wako wote; na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo na uondokapo” (Kumb. 6:4-7).

24. Kipindi hiki cha Kwaresima ni kipindi cha kujiuliza; ni kwa kiasi gani kila mzazi kwa hatua ya kwanza, anaiishi imani ya kanisa. Yaani, ni kwa kiasi mzazi mwenyewe amefanya jitihada ya kuijua vyema imani yake? Je, baada ya mafundisho ya Komunio ya Kwanza na Kipaimara; amefanya jitihada ya kujifunza tena na tena imani yake ya kanisa? Sehemu hii ya kitabu cha Kumbukumbu la Torati inataka kuwaambia wazazi ya kuwa; wao wenyewe waijue imani yao kwanza vizuri kabla ya kuirithisha kwa watoto wao. Wazazi wafanye kila jitihada ya kuijua imani kwa kujisomea, kufanya mazoezi ya kwenda kanisani mara kwa mara na kujua vizuri na kwa bidii vipengele vyote vya dini. Haitoshi tu kumaliza mafundisho ya Komunio ya kwanza na Kipaimara; bali ni kurudia tena na tena mafundisho kwa kujisomea Neno la Mungu na vitabu mbalimbali vya maisha ya watakatifu.

25. Baada ya kujua mafundisho haya ya imani, kinachofuata kwa wazazi ni kuwafundisha watoto wao kwa bidii. Wazazi wajue kwamba, imani inazaliwa nyumbani kwao kwa sababu familia ni Kanisa la Nyumbani, yaani mahali ambapo watoto wanasaidiwa kukua katika Imani (rej. Amoris Laetitia, nn.15-16; Lumen Fidei n.53). Hivyo kila kinachofanyika nyumbani kitafsiriwe katika misingi ya Imani ili mtoto anapokua akue vilevile katika Imani. Kwaresima hii iwe kipindi cha kuwakumbusha wazazi kuwapeleka watoto kanisani kwa ibada za njia ya Msalaba, mafundisho ya dini na mazoezi mengine ya kiroho. Watoto wanawaangalia wazazi kwa asilimia kubwa ya majifunzo yao ya imani.

Hali Halisi ya Imani

26. Hali halisi ya maisha yetu imetawaliwa na ubaridi wa imani, kutopendelea mambo ya kiroho kabisa, na watu wana mtazamo kuwa maoni yao binafsi ni muhimu zaidi. Tumeacha kumsikiliza mwalimu Kanisa ila zaidi na zaidi kuyakumbatia malimwengu. Siku hizi imekuwa ni vigumu kumtofautisha mwamini na mtu asiye mwamini, kwa vile wote wanaishi maisha sawa na wanatenda uovu uleule. Mkristo mwamini anapokea au anatoa rushwa waziwazi. Katika masengenyo na kudhulumiana, waamini wanatenda yayo hayo. Udhaifu huu wa kushindwa kuiishi imani yetu kikamilifu unawafanya wakristo kushindwa kumpa Mungu utukufu na sifa kwa njia ya matendo yao. Tunapingana na kile alichosema Mtakatifu Ireneo kuwa, “Utukufu wa Mungu ni mwanadamu aliye hai kabisa” (rej. Irenaeus, Adversus Haereses 4, 20).

27. Tukiangalia parokia na makanisa yetu yanajengwa makubwa na kwa gharama kubwa. Ukiangalia nyumba zetu ibada siku za Dominika zinajaa. Lakini, baada ya maadhimisho ya ibada hizi, wengi wetu hurudi nyumbani kama watu wasiomjua Mungu. Yaani, maisha tunayoishi ni tofauti na ile ibada tuliyoadhimisha. Ibada na imani zetu hazikolezi maisha yetu.

28. Katika maisha ya kawaida, waamini wengi wanakabiliwa na tatizo kubwa la imani za kishirikina na michanganyo. Ni kama kuishi maisha mseto; asubuhi katika ibada wanaonekana kuwa ni waamini wazuri lakini usiku wanaenda katika altare za kishirikina. Kuna sababu nyingi zinazowasukuma waamini wengi kuingia katika ushirikina, zikiwemo umaskini, kutafuta cheo, sababu za kiafya, kutafuta maisha ya mkato, nk. Mazingira kama haya hufanya ushirikina kushamiri sana.

29. Wakati mwingine kuna hali ya kujipongeza au kujikinai kwa mafanikio ya nje nje tu. Hata jambo jema tufanyalo katika makanisa laweza kutupumbaza na kuona kuwa tumempata Mungu tayari. Utakuta watu wanaenda katika ibada na kusema, tumejenga kanisa kubwa, au kwaya yetu inaimba vizuri. Nabii Amosi anatuambia ibada zisizokuwa na maisha ya Kimungu, au maisha ya kiadilifu zinachukiza: “Mimi nazichukia Sikukuu zenu, nazidharau, nami sitopendezwa na makutano yenu ya dini. Naam, ijapokuwa mnanitolea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za unga, sitazikubali; wala kuziangalia sadaka zenu za amani, na za wanyama walionona. Niondoleeni kelele za nyimbo zenu; kwa maana sitaki kuzisikia sauti za vinanda vyenu” (Amo 5:21 – 23).

Tusimame Imara katika Imani

30. Kipindi hiki cha Kwaresima tunaalikwa kwa namna ya pekee kusimama imara katika imani yetu. Hiki ni kipindi cha neema ambacho matunda yake hutarajiwa kuwa ni uadilifu, uongofu na utu wema. Ni kipindi cha kusali zaidi, kufunga zaidi na kutenda matendo mema zaidi. Tuendelee kumwomba Mungu atuzidishie imani. Tujibidishe kufanya matendo ya huruma ya kiroho, ambayo ni kuelimisha wajinga, kushauri wenye shaka, kuonya wakosefu, kuvumilia wasumbufu, kusamehe kwa moyo, kufariji wenye huzuni na kuwaombea wazima na wafu; na yale ya kimwili ambayo ni kulisha wenye njaa, kunywesha wenye kiu, kuvika walio uchi, kukaribisha wageni, kuhudumia wagonjwa, kutembelea wafungwa na kuzika wafu. Haya yote yatatuwezesha kusimama imara katika imani kwani ni dira na mwongozo wa maisha yetu ya kikristo.

SURA YA TATU

IMANI NA JUBILEI YA MWAKA 2025: 

31. Baba Mtakatifu ametangaza kwamba mwaka wa 2025 utakuwa ni Mwaka wa Jubilei, ambao hutokea kila baada ya miaka 25. Kauli mbiu ya Jubilei hiyo ni “Mahujaji wa Matumaini.” Ni wazo la Baba Mtakatifu kuwa mwaka huu wa jubilei utakuwa mwaka wa matumaini kwa ulimwengu unaoteseka kutokana na athari za vita, athari zinazoendelea za janga la UVIKO-19, na mabadiliko ya tabia nchi.

32. Kiti Kitakatifu kilitoa nembo rasmi ya Mwaka wa Jubilei 2025 ambayo tafsiri yake, inaonyesha ubinadamu kutoka Pembe Nne za Dunia (Tazama juu ya kijitabu hiki utaziona hizo pembe nne zimeshikilia msalaba) katika kitendo cha kushikamana na Msalaba. Msalaba uko katika umbo la tanga, mojawapo ya ishara za Tumaini la Kikristo linalobeba uhakika wa ushindi wa wema dhidi ya uovu. Matanga ambayo yanajizamisha baharini yakisukumwa na matukio ya maisha. Msalaba unaishia kwa umbo la nanga, ishara nyingine ya matumaini ambayo huleta imani na usalama maishani.

Jubilei maana yake nini

33. Maana halisi ya jubilei tunaipata katika kitabu cha Mambo ya Walawi (rej. Wal 25:10f) ambapo Waisraeli wanaambiwa kuwa mwaka wa hamsini ni wa jubilei. Ni mwaka Mtakatifu si tu kwa sababu unaanza, unaadhimishwa na unahitimishwa kwa madhehebu matakatifu, bali pia kwa sababu unachochea utakatifu wa maisha. Huu ni mwaka wa undoleo la dhambi, upatanisho, uongofu na toba ya kisakramenti. Ni kipindi cha kumtafuta Kristo anayetutangazia Habari Njema. “Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka uliokubaliwa na Bwana (rej. Isa 61:1-12, Mk 1:15, Lk 4:18-19).

Matunda tarajiwa ya mwaka wa jubilei

34. Jubilei ni wakati ambao utakatifu wa Mungu hudhihirika zaidi nao hutubadilisha. Katika Mwaka mtakatifu tunaalikwa kusimama imara katika imani juu ya uwepo wa Mungu. Tusimame imara kwani imani huzaa tumaini lisilo tahayarisha (Spes non confundit - Rum 5:5).

Imani itufanye kuwa watumishi

35. Imani ndicho chombo pekee cha kuhesabiwa haki tunapo mwamini Bwana Yesu Kristo (Mdo 16:31). Na ni kwa imani katika Kristo na Neno lake tunaweza kumtumikia Mungu kwa ufanisi na “kumpendeza, kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba Yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao” (Ebr 11:6). Hakuna njia nyingine ya kuwahudumia watu wa Mungu kwa utukufu isipokuwa kwa kuliamini Neno la Mungu.

Imani itupatie majibu ya maswali yanayojitokeza

36. Ninatoka wapi? Ninaenda wapi? Kwa nini nilizaliwa? Je, nafsi yangu haiwezi kufa? Nini kinatokea baada ya mimi kufa? Je, Mungu ananipenda? Kuna furaha kubwa na amani kuu katika kujua kwa uhakika majibu ya maswali haya. Imani itokanayo na Maandiko matakatifu hutusaidia kujua maana halisi na lengo halisi la maisha yetu (Mwa 1:1–2:9, 2:15–17, 3:1–24).

Imani itupatia tumaini tunalohitaji ili kustahimili magumu

37. Mungu anatuhakikishia kwamba yuko pamoja nasi daima katika magumu yetu yote, na kwamba anatembea nasi na kuteseka pamoja nasi. Hivyo, mbele ya Mungu, mateso, ukosefu wa haki, magonjwa na kifo havikosi majibu. Kama vile mateso ya Kristo aliyoyapokea kwa ajili ya mapenzi ya Baba wa milele yalivyoleta ukombozi kwetu sisi, mateso yetu leo tunayoyapokea kwa imani, yanakuwa nguvu ya mabadiliko katika maisha yetu, katika maisha ya wapendwa wetu na kwa ulimwengu mzima. Mateso huwa njia ya kufungua mioyo yetu kumpenda Mungu na watu. Kumwamini Mungu wakati wa mateso hutulinda dhidi ya kuvunjika moyo na kukata tamaa (Mt 24:13, Rum 5:5).

Imani itupatie furaha isiyo na mwisho

38. Imani ya kweli kwa Mungu huwasha moto wa mapendo moyoni mwetu. Uhusiano huo wa upendo na Mungu ndio pekee unaoweza kutufanya tuwe na furaha kamili. Mioyo yetu ina kiu ya furaha isiyotoshelezwa na mambo ya dunia hii ila ni Mungu pekee anayeweza kuitosheleza. Bila Mungu, tunaanguka katika hali ya kutoridhika na kukata tamaa.Mtakatifu Augustino alisema: “Umetuumba kwa ajili yako, ee Bwana, na mioyo yetu haina utulivu mpaka itakapotulia ndani yako”(Maungamo ya Mtakatifu  Agostino(Lib 1, 1-2,2.5,5: CSEL 33, 1-5).

Imani itupatie nguvu ya kupenda na kusamehe

39. Kwa nguvu ya imani tunaweza kufanikiwa kuwapenda hata adui zetu. Ni mtu mwenye imani tu ndiye anayeweza kuwapenda na kuwasamehe wanaomuudhi na hata kumdhulumu (rej. Mt 5:43-48). Kusamehe ni sharti msingi kwetu sisi kupokea msamaha wa Mungu (Mt 6: 14-15). Mtu asiyesamehe anabaki kuwa mfungwa wa kinyongo chake. Kusamehe hutuweka huru, hutuwezesha kupenda na kupokea msamaha wa Mungu.

Rehema za Jubilei Kuu

40. Baba Mtakatifu anawataka Wakristo wote kuwa ni mahujaji wa matumaini. Fadhila hii ya matumaini inapaswa kuibuliwa zaidi ya yote katika neema ya Mungu na katika ukamilifu wa huruma yake. Inapaswa kugunduliwa katika alama za nyakati, ambazo, zikijumlisha ?shauku ya mioyo ya wanadamu inayohitaji uwepo wa Mungu wa kuokoa, inapaswa kuwa ishara ya matumaini (Spes non confundit, 7).

41. Baba Mtakatifu anatuasa kwamba, Waamini wote, ambao wametubu kiukweli na kujiweka huru kutoka mivuto yoyote ya dhambi (taz. Enchiridion Indulgentiarum, IV ed., norm. 20, § 1), ambao wanasukumwa na roho ya upendo na ambao, wakati wa Mwaka Mtakatifu, watajitakasa kwa njia ya Sakramenti ya kitubio na kuburudishwa na Komunyo takatifu, kusali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu, wataweza kupata msamaha wa jumla kutoka hazina ya Kanisa, pamoja na ondoleo na msamaha wa dhambi zao zote (Sehemu ya Maswali Msingi kuhusu Uinjilishaji Ulimwenguni, Jubilei 2025, 68). Rehema za jubilei zinapatikana kwa njia zifuatazo:

Hija

42. Waamini, mahujaji wa matumaini, wataweza kupata Rehema ya Jubilei inayotolewa na Baba Mtakatifu iwapo watafanya hija ya uchaji: Kwenye sehemu yoyote takatifu ya Jubilei, huko Roma, katika Nchi Takatifu na katika maeneo mengine ya kikanisa hasa Kanisa Kuu la Jimbo. Hija tuifanyayo katika mwaka huu wa Jubilei Kuu ituimarishe na kutufanya tusimame imara katika imani.

Ziara za uchaji katika maeneo matakatifu

43. Vivyo hivyo, waamini wanaweza kupata Rehema za Jubilei Kuu ikiwa mmoja mmoja au katika kikundi: huku wamesimama imara katika imani, watatembelea kwa moyo sehemu yoyote ya Jubilei na huko, kwa muda unaofaa, kuabudu Ekaristi na tafakari, wakimalizia na Baba Yetu, Kanuni ya Imani kwa namna yoyote halali, na maombi kwa Maria, Mama wa Mungu, ili katika Mwaka huu Mtakatifu kila mtu “apate kujua ukaribu wa Maria, mama mwenye upendo zaidi kuliko mama wote, asiyewaacha watoto wake kamwe”(Spes non confundit, 24).

44. Kuhusu makundi maalum: Waamini ambao wametubu dhambi kweli, lakini hawawezi kushiriki katika maadhimisho matakatifu, hija na ziara za uchaji kwa sababu kubwa (hasa watawa wa klausura na wamonaki, lakini pia wazee, wagonjwa, wafungwa, na wale ambao, kwa kazi yao hospitalini au vituo vingine vya matunzo, hutoa huduma endelevu kwa wagonjwa), wanaweza kupata Rehema za Jubilei ikiwa kwa kuunganishwa kiroho na waamini wanaoshiriki kibinafsi,(hasa wakati maneno ya Baba Mtakatifu au Askofu wa Jimbo hupitishwa kupitia njia mbalimbali za mawasiliano), wanasali sala ya Baba Yetu, wanakiri Imani kwa namna yoyote iliyoidhinishwa, na sala nyingine kulingana na malengo ya Mwaka Mtakatifu, majumbani mwao au popote pale walipojikusanya wakitolea mateso  yao au magumu ya maisha yao (Sehemu ya Maswali Msingi kuhusu Uinjilishaji Ulimwenguni, Jubilei 2025, 69).

Matendo ya huruma na toba

45. Zaidi ya hayo, waamini wataweza kupata Rehema za Jubilei iwapo, kwa moyo wa kujitolea, watashiriki katika utume wa jumla, mazoezi ya kiroho, au shughuli za majiundo kwenye nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano na Katekisimu ya Kanisa Katoliki, inayofanyika katika kanisa au mahali pengine panapofaa, kulingana na mawazo ya Baba Mtakatifu.

46. Licha ya kanuni kwamba rehema kamili yaweza kupatikana mara moja tu kwa siku(taz. Enchiridion Indulgentiarum, IV ed., norm. 18, § 1), waamini ambao wamefanya tendo la upendo kwa niaba ya roho za Toharani, ikiwa wanapokea Komunyo Takatifu mara ya pili siku hiyo, wanaweza kupata rehema kamili mara mbili kwa siku ile ile, inayotumika tu kwa marehemu(hili lazima lifanyike ndani ya adhimisho la Ekaristi; tazama kanuni namba 917 na Tume ya Kipapa kwa ajili ya tafsiri halisi ya Sheria ya Kanisa - CIC, Responsa ad dubia, 1, 11 Julai 1984). Kwa kupitia tendo hili maradufu, tendo tukuka la ukarimu wa ziada linatekelezwa, kwa njia ya kifungo hicho ambacho kwacho waamini wanaosafiri katika dunia hii wanaunganishwa katika Mwili wa fumbo wa Kristo, pamoja na wale ambao tayari wamemaliza safari yao, kwa mastahili ya ukweli kwamba “Rehema za Jubilei, shukrani kwa nguvu ya sala, imekusudiwa kwa njia mahususi kwa wale ambao wametutangulia, ili wapate “huruma kamili”(Spes non confundit, 22).

47. Kwa namna mahususi “wakati wa Mwaka Mtakatifu, tumeitwa kuwa ishara zinazoonekana za matumaini kwa wale kaka na dada zetu ambao wanapata shida za aina yoyote”(Spes non confundit, 10). Kwa hiyo, Rehema pia inahusishwa na matendo fulani ya huruma na toba, ambayo yanashuhudia uongofu unaofanywa. Waamini, wakifuata kielelezo na agizo la Kristo, wanahimizwa kufanya kazi za upendo au huruma mara nyingi zaidi, hasa katika huduma ya ndugu waliolemewa na mahitaji mbalimbali. Hasa zaidi, wanapaswa kugundua tena” matendo haya ya kimwili ya huruma: kulisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu, kuwavisha walio uchi, kuwakaribisha wageni, kuponya wagonjwa, kutembelea wafungwa, na kuwazika wafu”(Misericordiae vultus, 15) na kugundua pia ?matendo ya kiroho ya huruma: kuwashauri walio na mashaka, kuwaelimisha wajinga, kuwaonya wadhambi, kuwafariji wanyonge, kusamehe wakosaji, kuwavumilia watutendeao mabaya, na kuwaombea walio hai na wafu (KKK 2447).

48. Kwa njia hii, waamini wataweza kupata Rehema za Jubilei Kuu ikiwa watawatembelea, kwa muda ufaao, ndugu zao walio na uhitaji au shida (wagonjwa, wafungwa, wazee wapweke, walemavu), kwa maana ya kufanya safari ya kwenda kwa Kristo akiwa ndani yao (Mt 25, 34-36) kulingana na hali ya kawaida ya kiroho, kisakramenti na sala. Waamini wanaweza kurudia ziara hizi katika Mwaka Mtakatifu wote, hata kila siku, wakipata rehema kila mara.

49. Rehema Kamili za Jubilei Kuu pia zinaweza kupatikana kupitia mipango inayowekwa katika vitendo vya ukarimu, roho ya toba, na pia kwa kutoa kiasi cha pesa kwa maskini; kwa kuunga mkono kazi za kidini au kijamii, haswa katika kuunga mkono ulinzi wa uhai katika hatua zake zote, lakini pia kwa kusaidia ubora wa maisha ya watoto waliotelekezwa, vijana walio katika shida, masikini au wazee wapweke, au wahamiaji kutoka nchi mbalimbali ?wanaohama nchi zao ili kutafuta maisha bora kwa ajili yao na familia zao“ (Spes non confundit, 13).

50. Ili kuwezesha upatikanaji wa Sakramenti ya Kitubio Maaskofu wa Majimbo wanawapa Mapadri wasikilize maungamo ya waamini, kwa kuzingatia kanuni (CIC 727, 508, § 1). Mapadri wakumbuke, kwa mujibu wa Motu proprio Misericordia Dei, fursa ya kichungaji inayopatikana pia katika kusikiliza Maungamo wakati wa adhimisho la Misa Takatifu.

Changamoto za sasa dhidi ya Imani

51. Kanisa linamshukuru Mungu kwa kuadhimisha miaka 2025 ya Imani. Changamoto za Imani na migawanyiko zimekuwepo tangu Kanisa la mitume. Licha ya changamoto hizo, Kanisa la Kristo limedumu hadi leo (rej. Mt 16:18). Katika Mwaka huu Mtakatifu tutafakari pamoja baadhi ya changamoto zinazokabili imani ya Kikristo lakini kwa namna ya pekee kanisa la Tanzania.

Kupungua kwa Washiriki

52. Mambo mbalimbali yanasababisha kupungua kwa ushiriki katika masuala ya kikanisa. Hapa tutataja tu machache: Kanisa taratibu linakuwa la wazee. Vizazi vichanga mara nyingi hutanguliza uhuru binafsi, ubinafsi, na imani mchanganyiko. Kuenea kwa propaganda za upotoshaji imani na mitazamo tofauti kupitia mitandao ya kijamii huwaweka vijana kwenye safu nyingi za mitazamo ya ulimwengu, na kuwafanya kuvutwa na njia mbadala za kiroho. Mabadiliko ya kiuchumi na maisha yanachangia kupungua kwa washiriki. Mahitaji ya maisha ya kisasa hufanya iwe changamoto kwa watu binafsi kujitolea kwa shughuli za kawaida za kanisa. Kuenea kwa uchumba sugu na ndoa za dini tofauti husababisha umoja na muunganiko wa kikanisa kupungua.

Upungufu wa Mapadri/makasisi

53. Upungufu wa mapadri/makasisi ni tatizo kubwa kwa Kanisa Katoliki duniani kote. Upungufu wa mapadri una athari kubwa kwa Kanisa kutimiza kazi zake kuu za kikuhani. Mahitaji ya maisha ya kikasisi, ambayo ni pamoja na useja, kujitolea kwa huduma ya jamii, na matarajio ya kujitolea maisha yote, yanaonekana kuwa ya kutisha na yasiyopendeza kwa baadhi ya watu. Changamoto hizi hukatisha tamaa vijana kujitoa kwani huogopa uzito wa upadri kama njia ya maisha ifaayo.

Kashfa za Unyanyasaji wa kijinsia na dhidi ya watoto

54. Kashfa za unyanyasaji wa kijinsia na dhidi ya watoto zimekuwa na athari kubwa na za kudumu kwa taasisi nyingi za kidini na familia. Kashfa za unyanyasaji wa kijinsia husababisha kupoteza uaminifu, na kutathmini upya jukumu la mamlaka za kidini katika jamii. Athari za muda mrefu za kashfa za unyanyasaji wa kijinsia zinaonekana sio tu ndani ya jumuiya ya kikanisa lakini pia ndani ya jamii kwa ujumla. Kashfa za unyanyasaji wa kijinsia zinahitaji uwajibikaji, na mageuzi katika jumuia za kikanisa na familia.

Mdororo wa Kiuchumi

55. Mdororo wa kiuchumi ni changamoto kubwa ambayo makanisa na mashirika ya kidini yamekuwa yakipambana nayo katika miaka ya hivi karibuni. Mdororo wa kiuchumi ni matokeo mchanganyiko wa mambo yanayoathiri uwezo wao wa kuendeleza shughuli, kudumisha miundombinu, na kutimiza dhamira yao. Kupungua kwa usaidizi wa kifedha kunachangiwa na ukweli kwamba vizazi vizee ambavyo vina mwelekeo wa kuchangia mara kwa mara vinapungua kwa idadi.

56. Mdororo wa kiuchumi au kutokuwa na uhakika na kipato cha kiuchumi husababisha kupungua kwa mapato yanayoweza kutumika, na kusababisha watu binafsi kupunguza utoaji wa misaada, ikiwa ni pamoja na taasisi za kidini. Taasisi za kidini zinakabiliwa na ushindani wa usaidizi wa hisani na mashirika mengine yasio ya kidini. Wafadhili wengine huja na shinikizo la kufuata mrengo usio wa kiimani.

Utandawazi na Vikundi vya Unabii Mamboleo

57. Watu na vikundi vya unabii mamboleo vimekuja na mafundisho yao kuvutia watu kwa kuahidi mafanikio. Hii ni changamoto kwa imani ya kweli. Mafundisho ya Kanisa Katoliki kuhusu masuala ya kimaadili na kijamii yanatofautiana sana na yale ya imani nyingine.

58. Utandawazi huleta maoni tofauti kuhusu Kanisa, teolojia na huduma ya kichungaji. Kanisa halinakili tu mbinu na njia za mifumo mingine ya kijamii na kifalsafa, bali lina maisha ambayo ni zaidi ya hayo. Kanisa linakuwa la kidunia linaposhushwa hadhi na kuwa shirika la kijamii kama mashirika mengine mengi ambayo yapo katika jamii. Kanisa ni taasisi takatifu iliyoanzishwa na Roho Mtakatifu. Kwa bahati mbaya, baadhi ya watu leo wanalichukulia Kanisa kama shirika la lazima lenye manufaa kwa jamii tu, na jukumu lake linathaminiwa kulingana na manufaa yake ya kijamii pekee. Kuna wengine pia ambao hawaoni jukumu la kinabii na utakaso la Kanisa, ambalo linajumuisha utakaso wa mwanadamu na ulimwengu wote. Badala yake, wanakubali Kanisa tu kama nyenzo ya mapato na mapambo. Wanahitaji kwa ajili ya kupamba sherehe mbalimbali na kuangaza kwa uwepo wake.

59. Leo kuna mwelekeo wa jumla kwetu kulichukulia Kanisa la kilimwengu kama lenye manufaa zaidi kwa mahitaji ya kijamii ya kisasa. Pia kuna mwelekeo unaokua kwetu wa kuzoea mahubiri na mafundisho ya Kanisa kwa mahitaji haya ya kijamii, haswa kwa mahitaji ya jamii ambayo inafanya kazi kwa njia ya kibinadamu, kwa sababu tunaogopa kukataliwa. Manabii mamboleo wameangukia katika jaribu hili, na ndiyo maana wamejikita kwa wale wanaotafuta tiba, mali na fahari za kilimwengu.

Kupoteza dhana ya dhambi

60. Kupoteza dhana ya dhambi kunaleta kutojali ukweli kwamba matendo ya uovu humchukiza Mungu, huharibu uhusiano wetu pamoja naye, na kuwa na matokeo yenye uharibifu kwa jamii. Udhihirisho wa upotevu huu wa maana ya dhambi unaonekana katika kukataa ukweli wa maadili. Wakati maswali ya maadili mema na mabaya yanapoonekana kwa uthabiti kama masuala ya maoni ya kibinafsi, ufahamu wa dhambi ya mtu na matokeo yake hupungua. Kutupiliwa mbali huku kwa sheria ya maadili hatimaye kunaweka wokovu wa mtu hatarini (taz. KKK 37, 1994-1955). “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo, wala neno lake halimo mwetu” (1Yoh 1: 8-10)

61. Ni lazima tutambue uzito wa dhambi ikiwa kweli tunathamini zawadi ya Kristo ya msamaha na upatanisho. Kuweka maisha yetu kwa Yesu Kristo huleta utambuzi mzuri wa athari mbaya za dhambi na kutia tumaini thabiti kwamba itashindwa (taz. KKK 1848).

Kutokutii Dhamiri

62. Je, tunapaswa kufuata dhamiri zetu kwa kiasi gani katika kufanya maamuzi ya kimaadili? Papa Fransisko anatuasa kwamba “kuna dhambi hata kwa wale ambao hawana imani wakati dhamiri haifuatwi. Kuisikiliza na kutii dhamiri kunamaanisha kuamua mbele ya mambo yanayoeleweka kuwa mema au mabaya”(rej. Papa Francisko:Tafakari ya Asubuhi katika Kikanisa cha Nyumba ya Mtakatifu Marta: Kuchunguza dhamiri, Jumanne tarehe 4 Septemba 2018). Kanisa linatusihi sisi sote kamwe tusiache kuunda dhamiri yetu kwa usahihi zaidi katika kuwasilisha kweli za ufunuo na sababu ambayo ni mwalimu anayeongozwa na Mungu. Kisha tunaweza kuwa na uhakika kwamba sauti ya ndani ya dhamiri pia ni sauti ya Mungu (rej. Phil 3:7-14), 17.06.2020 Katekesi, 17.03.2023 Maadhimisho ya Ibada ya Upatanisho katika Parokia ya Mtakatifu Maria huko Trionfale,Roma).

Hitimisho

63. Tukiwa Mahujaji wa Matumaini, tutumie vizuri fursa za kiroho zitakazotupatia rehema kwa mwaka huu wa Jubilei. Wakati huo huo tusimame imara katika imani ili kukabiliana na changamoto zinazogusa imani yetu tukiongozwa na kauli mbiu ya Mwaka Mtakatifu “Tumaini lisilotaharisha,” (Spes non confundit Rum 5:5).

SURA YA NNE MWALIKO WA UJUMLA WA KUSIMAMA IMARA KATIKA IMANI

Ili tuweze kusimama imara katika Imani, tunaalikwa kutimiza mambo muhimu yafuatayo:

Sala

64. Ikumbukwe kwamba haiwezekani kusimama imara katika imani pasipo maisha thabiti ya sala. Sala ni wajibu wa lazima siku zote kwa sababu kwa njia ya sala tunamtegemea Mwenyezi Mungu katika maisha yetu yote. Kusali ni wajibu unaotakiwa katika dini zote zenye ukweli kimungu. Kwetu sisi wakristo, kusali ni mapokeo ya tangu Agano la Kale. Katika Agano Jipya Kristo alikuja kukamilisha jadi hiyo kwa Yeye mwenyewe kusali mara kwa mara. Vivyo hivyo anatuasa sisi wafuasi wake kusali mara kwa mara ili tusiingie majaribuni (rej. Mt 26:41).

Utii kwa Neno la Mungu

65. Safari yetu ya kiimani katika Kwaresima tuifanyao kila mwaka haina budi kuimarishwa na Neno la Mungu kama ile ya baba yetu Abrahamu iliyoongozwa na sauti ya Mungu (rej. Mwa 12:1- 4). Utii kwa Mungu huimarisha imani yetu. Nasi kwa kumtii Mungu katika Maisha yetu ya kiimani tutaweza kufika mbinguni.

66. Abraham ni mfano bora wa kusimama imara kiimani kwa familia zetu zote. Nyakati hizi za leo familia zimesongwa na kila aina ya madhila, hususani yatokanayo na maendeleo ya sayansi na teknolojia, ambayo kama matokeo hasi vimeleta changamoto nyingi za kiimani, kimaadili, kijamii na hata kiuchumi. Yote hayo kwa pamoja yamezalisha kizazi ambacho kadiri siku zinavyosonga mbele, mwanadamu huiacha imani na kuifanya sayansi na teknolojia kama ndio msingi mkuu wa maisha yake. Matokeo yake ni kwamba familia zetu zinazidi kuwa legelege kiimani kwa sababu hazichukuliwi tena kuwa eneo la malezi muhimu ya kiimani na kiutu. Malezi ya familia ‘yamebinafsishwa’ katika tendo la kuamini kwamba kila mtu katika familia ana wajibu wa kujilea mwenyewe bila ya msaada wa mwingine kati ya wale wanaounda familia. Katika mazingira ya namna hii, dhana nzima ya familia inapotea na familia inapoteza fursa ya kuwa ‘shule ya imani’, ambamo wazazi na watoto wangetarajiwa kuwa imara katika Imani na utu wema. Ni kwa sababu hiyo, waraka huu unatuhimiza sote katika familia zetu kuiishi imani yetu licha ya changamoto ziletwazo kwetu na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Familia zinaalikwa kuzingatia kusimama imara katika imani kwa sababu “Imani ni nguzo ya maisha ya mtu hapa duniani, kwani imani inamwezesha mtu kuyapokea magumu na majaribu ya maisha kwa ujasiri na saburi (Ebr 12:1-4).

Kuishuhudia Imani

67. Kuna uhusiano mkubwa kati ya fadhila tatu kuu za kimungu: Imani, matumaini na mapendo. Katika kuziishi fadhila hizi hatuna budi kutambua kwamba fadhila hizi haziachani (Rej. 1Kor 13:13). “Imani inakua pale inapotiwa katika maisha kama uzoefu wa upendo uliopokelewa na pale inaposhirikishwa kwa wengine kama uzoefu wa neema na furaha. Inatufanya kuzaa matunda, kwa sababu inapanua ndani ya mioyo yetu matumaini na kutuwezesha kuwa na ushuhuda ulio hai; hakika, inafungua mioyo na akili za wale wanaosikiliza na kuuitikia mwaliko wa Bwana wa kushikilia neno lake na wa kuwa wafuasi wake.” Imani pia inajenga matumaini na matumaini ni dhihirisho la kile tunachokiamini. Kwa hiyo Mwaka huu wa Jubilei unatualika katika kukua na kuziishi fadhila hizi za kimungu kama wahujaji walio na matumaini.

68. Nuru ya imani imewekwa kwa uthabiti katika huduma ya haki, sheria na amani. Imani inatokana na upendo wa Mungu ambapo maana na thamani ya maisha yetu huwa dhahiri. Maisha yetu yanaangazwa kiasi kwamba yanaingia katika nafsi tatu za Mungu zilizo fumbuliwa kwetu na upendo huo. Nuru ya Imani ina uwezo wa kuimarisha utajiri wa mahusiano ya kibinadamu na kuboresha Maisha ya pamoja.

Imani na siasa za kilimwengu (secular)

69. Katika Kwaresima ya mwaka huu tunaalikwa kusimama imara katika imani, imani tunayoweza kuikiri hadharani na kuiishi kwa uadilifu. Kwa kufuata mwaliko huu tunatafuta mapenzi ya Mungu kwa ulimwengu ambapo si tu hadhi ya mwanadamu inatakiwa kulindwa bali pia kuheshimu na kuutunza uumbaji ambao ni zawadi tulizopewa na Mungu kwa manufaa ya wote.

70. Waamini wanaalikwa kushiriki katika kila jambo jema kama raia. Wanaalikwa pia kutii sheria zilizowekwa kihalali na mamlaka na kuishi maisha ya uadilifu kadiri ya sheria hizo. Ushiriki wa Waamini katika shughuli za jamii na siasa ni sehemu ya wajibu wao wa kiimani. Lengo la ushiriki huu ni kusaidia kujenga jamii iliyo bora zaidi kwa sababu ili kuunda maisha ya kisiasa yaliyo kweli ya kibinadamu, hakuna lililo bora zaidi kuliko kustawisha ndani ya watu hisia za haki, upendo na huduma kwa manufaa ya wote. Kwa kutekeleza wajibu huu wakristo wanapata fursa ya kuwa “mwanga na nuru” kwa ulimwengu (Mt 5:14) na kuwa wahudumu wa hekima ya kikristo katika jamii inayowazunguka (rej. Dikrii ya utume wa walei – Apostolicam Actuositatem, 14.)

71. Mwaka huu 2025 taifa letu litakuwa katika kipindi mahsusi cha uchaguzi wa viongozi ambao watapewa dhamana ya kulinda, kutetea na kusimamia ustawi wa haki katika taifa letu. Tunapenda kuwaalika wakristo wote na watu wenye mapenzi mema kutekeleza zoezi hili kwa umakini na uadilifu mkubwa, tukitambua kuwa kila mwananchi mwenye haki ya kupiga kura anatakiwa kufanya hivyo kadiri ya Katiba kama wajibu mkubwa ambao raia anatakiwa kuushiriki.

72. Katika mazingira ya uchaguzi wa kisiasa, mara nyingi watu wengi hujikuta wapo katika changamoto hata za kupoteza msimamo wao wa imani. Hupenda kutumia njia za mkato kupata nafasi za uongozi kama vile ushirikina, uongo na rushwa. Wanasahau kwamba kila uongozi hutoka kwa Mungu maana sauti ya watu ni sauti ya Mungu. Hivyo wanatakiwa kutegemea nguvu za Mungu na kuwa tayari kuwasikiliza wananchi wote kwa manufaa ya nchi nzima. Tunatoa ushauri kwa viongozi wa kisiasa tukisisitiza utoaji wa fursa ya kusikilizwa hata wale wachache wenye mawazo tofauti. Hii itatusaidia kukuza na kuheshimu utofauti wa kufikiri kwa manufaa ya nchi, kupinga chuki na kujenga umoja

73. Katika demokrasia, ushiriki wa umma katika siasa huleta maendeleo, hujenga na kustawisha umoja na mshikamano kwa njia ya mgawanyo sawa wa rasilimali za taifa. Ujenzi wa maisha bora na ustawi wa jamii zetu ni jukumu la sisi sote. Tunaalikwa kujenga utamaduni wa uadilifu katika kuheshimu Katiba na sheria zinazotuongoza.

HITIMISHO

74. Sisi Maaskofu tunawaalika waamini wote na taifa zima la Mungu kusimama imara katika imani. Mtumie vema kipindi hiki cha Kwaresima kwa kujitafakari kiundani ili kujichotea neema na baraka. Aidha zingatieni mafundisho ya Kanisa juu ya Mwaka wa Jubilei, ili kupata rehema kamili za mwaka huu Mtakatifu 2025.

Ni sisi Maaskofu wenu,

1. Wolfgang Pisa, OFMCap, Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania, na Askofu wa Lindi. 2. Mhashamu Eusebius Nzigilwa, Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Tanzania na Askofu wa Mpanda. 3. Mwadhama Protase Kard. Rugambwa, Askofu Mkuu wa Tabora 4. Mhashamu Askofu Mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa`ichi, OFMCap, Dar es Salaam. 5. Mhashamu Askofu Mkuu Damian Dallu, Songea 6. Mhashamu Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya, OFMCap Dodoma 7. Mhashamu Askofu Mkuu Isaac Amani, Arusha 8. Mhashamu Askofu Mkuu Renatus Nkwande, Mwanza, 9. Mhashamu Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga, Mbeya 10. Mhashamu Askofu Agapiti Ndorobo, Mahenge 11. Mhashamu Askofu Augustino Shao, Zanzibar 12. Mhashamu Askofu Severine NiweMugizi, Rulenge-Ngara 13. Mhashamu Askofu Ludovick Minde, ALCP/ OSS, Moshi 14. Mhashamu Askofu Michael Msonganzila, Musoma 15. Mhashamu Almachius Rweyongeza, Kayanga 16. Mhashamu Askofu Salutaris Libena, Ifakara 17. Mhashamu Askofu Eusebius Nzigilwa, Mpanda 18. Mhashamu Askofu Rogath Kimaryo, CSSp Same 19. Mhashamu Askofu Bernadine Mfumbusa, Kondoa 20. Mhashamu Askofu John Ndimbo, Mbinga 21. Mhashamu Askofu Titus Mdoe, Mtwara 22. Mhashamu Askofu Joseph Mlola, ALCP/ OSS, Kigoma, 23. Mhashamu Askofu Prosper Lyimo, (Askofu Msaidizi, Arusha) 24. Mhashamu Askofu Liberatus Sangu, Shinyanga,

25. Mhashamu Askofu Edward Mapunda, Singida 26. Mhashamu Askofu Flavian Kassala, Geita. 27. Mhashamu Askofu Beatus Urassa, Sumbawanga 28. Mhashamu Askofu Antony Lagwen, Mbulu 29. Mhashamu Askofu Filbert Mhasi, TunduruMasasi 30. Mhashamu Askofu Simon Masondole, Bunda 31. Mhashamu Askofu Lazarus Msimbe, S.D.S., Morogoro 32. Mhashamu Askofu Henry Mchamungu, (Askofu Msaidizi Dar es Salaam) 33. Mhashamu Askofu Stefano Musomba, (Askofu Msaidizi Dar es Salaam) 34. Mhashamu Askofu Christopher Ndizeye, Kahama 35. Mhashamu Askofu Thomas Kiangio, Tanga 36. Mhashamu Askofu Eusebio Kyando, Njombe 37. Mhashamu Askofu Jovitus Mwijage, Bukoba 38. Mhashamu Askofu Vincent Mwagala, Mafinga 39. Mhashamu Askofu Wilbroad Kibozi, (Askofu Msaidizi Dodoma) 40. Mhashamu Askofu Godfrey Mwasekaga, (Askofu Msaidizi Mbeya);

Ujumbe wa kwaresima wa Maaskofu wa TEC
05 Machi 2025, 12:43