杏MAP导航

Tafuta

Watanzania diaspora jengeni na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa Watanzania diaspora jengeni na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa 

Askofu Lazarus Msimbe: Watanzania Dumisheni Upendo, Umoja na Mshikamano wa Kitaifa

Askofu Lazarus Vitalis Msimbe SDS., wa Jimbo Katoliki Morogoro, amewataka Watanzania waishio nchini Uingereza (Diaspora) kutambua na kuendeleza umoja, mshikamano na upendo baina ya waamini mahali walipo. Askofu Msimbe ametoa wito huo wakati akitoa mahubiri kwenye Adhimisho la Ibada yaMisa Takatifu aliyoiadhimisha tarehe 1 Machi 2025, katika Parokia ya Mtakatifu Petro, Dagenham, London. Umoja, Uhuru, upendo na mshikamano ni tunu za Kitaifa.

Na Mwandishi Wetu, London,

Hekima, umoja na amani ni ngao muhimu za watanzania mahali popote pale walipo ili kuweza kudumisha uhuru na umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa, licha ya tofauti msingi zinazoweza kujitokeza. Haki, umoja, amani, uadilifu; ukweli na uwazi pamoja na uwajibikaji ni nyenzo msingi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Kinzani, migogoro, vita na mipasuko ya kijamii inayojionesha sehemu mbalimbali za dunia ni changamoto kwa watanzania kusimama kidete kulinda na kudumisha umoja wa kitaifa na amani ambayo kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Watanzania watakiwa kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano
Watanzania watakiwa kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano

Askofu Lazarus Vitalis Msimbe SDS., wa Jimbo Katoliki Morogoro, amewataka Watanzania waishio nchini Uingereza (Diaspora) kutambua na kuendeleza umoja, mshikamano na upendo baina ya waamini mahali walipo. Askofu Msimbe ametoa wito huo wakati akitoa mahubiri kwenye Adhimisho la Ibada yaMisa Takatifu aliyoiadhimisha tarehe 1 Machi 2025, katika Parokia ya Mtakatifu Petro, Dagenham, London. Katika mahubiri yake, Askofu Msimbe alisisitiza umuhimu wa kuwa kama watoto wa kweliwenye uwazi, upendo, na mshikamano, akihimiza waumini kuendelea kushirikiana na kusaidiana.

Askofu Lazarus Vitalis Msimbe wa Jimbo la Morogoro
Askofu Lazarus Vitalis Msimbe wa Jimbo la Morogoro

Miongoni mwa wageni waliohudhuria Ibada hiyo ya Misa Takatifu ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Ndugu Mbelwa Kairuki, Maafisa Waandamizi wa Ubalozi wa Tanzania na Dada Prudencia Kimiti, MBE, Mtanzania aliyewahi kutunukiwa tuzo na Malkia. Katika salamu zake, Balozi Kairuki amewapongeza wanadiaspora wakatoliki kwa kuendeleza umoja miongoni mwao. Aidha Balozi ametumia fursa hiyo kuwatakia Waislamu mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kuwaombea Wakristo wanapojiandaa na Kipindi cha Kwaresima, akisisitiza mshikamano wa kidini miongoni mwa Watanzania.

Watanzania dumisheni haki, umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa
Watanzania dumisheni haki, umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania Wakatoliki wanaoishi London, Dr Christian Henjewele, amemshukuru Askofu Msimbe kwa kuungana na jumuiya hiyo na kumhakikishia kuwa umoja wa Watanzania Wakatoliki unaendelea kuimarika. Amemshukuru pia Balozi Kairuki kwa uwepo wake na kwa kuendelea kuunga mkono Watanzania waishio Uingereza. Adhimisho hilo pia limewakutanisha waamini kutoka London, Coventry, Cardiff, Birmingham, Milton Keynes, na miji mingine, wakishiriki pamoja katika mshikamano wa kiimani, udugu na upendo.

Askofu Msimbe
03 Machi 2025, 15:57