杏MAP导航

Tafuta

2025.03.21 Waziri Mkuu wa Tanzania akiwa na Askofu Kilaini baada ya misa ya Jubilei ya Miaka 25 ya uaskofu wake pamoja na Kardinali Pengo. 2025.03.21 Waziri Mkuu wa Tanzania akiwa na Askofu Kilaini baada ya misa ya Jubilei ya Miaka 25 ya uaskofu wake pamoja na Kardinali Pengo. 

Ask.Rweyongeza,miaka 25 ya Uaskofu wa Askofu Kilaini:ni mtu wa watu,ni mtetezi wa wanyonge!

Kuadhimisha miaka 25 ni kubeba magumu mengi.Jubilei ni kutafakari maana ya kile kinachoadhimishwa;fursa ya kuombea miito ya Upadre na kuomba toba.Ni mahubiri ya Askofu Rweyongeza wa Jimbo la Kayanga katika Jubilei ya Uaskofu wa Askofu mstaafu wa Jimbo la Bukoba Tanzania,Askofu Kilaini iliyoadhimishwa Machi 19 katika Kanisa Kuu Bukoba.Waziri Mkuu wa Tanzania aliwasihi watanzania kujiandikisha katika daftari ya kupiga kura.Mkuu wa Mkoa wa Kagera alitoa onyo la wageni haramu.

Na Patrick Tibanga - Radio Mbiu na Angella Rwezaula – Vatican.

Mhashamu Almachius Vincenti Rweyongeza wakati mahbiri yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya miaka 25 ya Uaskofu wa Mhashamu Method Kilaini, Askofu msaidizi Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Tanzania iliyoadhimishwa katika Parokia ya Bikira Maria Mama mwenye Huruma, Kanisa Kuu Bukoba, Jimbo Katoliki Bukoba, sambamba na  Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu Mume wa Bikira Maria tarehe 19 Machi 2025,  alijikita na ufafanuzi wa mambo mengi ya Imani, maadhili, msamaha, upendo, uvumilivu, maonyo, ushauri na maono. Askofu Rweyongeza alifafanua maana ya maadhimisho ya Mtakatifu Yosefu mume wa Bikira Maria na kufafanua kwa kina sifa tatu za mtakatifu huyo: 'mvumilivu, mnyenyekevu na mwaminifu.' Kadhalika alielezea maana ya Jubilei kwa ujumla huku akifafanua awali ya yote kuwa ni kutoa shukrani.  “Kuadhimisha miaka 25 siyo haba bali inabeba magumu mengi. Jubilei ni kutafakari maana ya kile kinachoadhimishwa. Jubilei ni fursa ya kuombea miito ya Upadre, Jubilei ni wakati wa kutiana moyo. Ni fursa ya kuchota mafundisho, Jubilei ni fursa ya kuomba toba," alisema.

Jubilei ya miaka 25 ya uaskofu wa askofu Kilaini
Jubilei ya miaka 25 ya uaskofu wa askofu Kilaini

Kwa ufupi, Askofu Rweyongeza alisema kuwa: "Jubilei ya miaka 25 ya Uaskofu imebeba shangwera ya miaka 77 ya kuzaliwa. Alizaliwa Mwaka tarehe 30 Machi 1948 akiwa mtoto halali wa Ndoa Katoliki ya Ta Paulo Mutegeki na Ma Asteria Kokutona. Na kwa hiyo anawashukuru wazazi kwa malezi bora na wapumzike kwa amani. Tulisherehekea Jubilei yake ya miaka 75 ya kuzaliwa 2023. Mtunga Zaburi anasema: “Miaka ya kuishi ni 70, au tukiwa wenye afya, 80; lakini yote ni shida na taabu!” (Zab 90:10). Napenda nitumie maneno mazuri ya Mtakatifu Yohane kukutakia afya njema: “Mpenzi wangu, nakutakia mafanikio mema ya kila aina; nakutakia afya njema ya mwili kama ulivyo nayo rohoni” (3 Yoh 1:2). Pili, Jubilei ya miaka 25 ya Uaskofu imebeba shangwera ya miaka 53 ya Upadre aliopewa mnamo tarehe 18 Machi 1972, huko Roma kwa mikono ya Kardinali Rossi akiwa na pacha wake Padre Gaudios Rutakyamirwa, na ambaye apumzike kwa amani(R.I.P.) Amen. Tulisherehekea pamoja naye hapa hapa Kanisa Kuu la Bikira Maria Mama Mwenye Huruma, Bukoba tarehe 18 Machi 2022, tukaimba pamoja naye wimbo alioimba siku yake ya Upadrisho: “Nitajongea Altare yako, furaha yangu na heri yangu siku zote.” Na daima anapokuwa Sakristia akijiandaa kuadhimisha Misa anaikumbusha nafsi yake mambo matatu akisema: “Ewe Padre wa Mungu: Adhimisha Misa hii kama kwamba:

Mosi, Ni Misa yako ya kwanza, Pili, Ni Misa yako ya mwisho. Tatu, Ni Misa yako pekee. Sala hiyo anatakiwa asali kila mhudumu wa Altare na kila anayekuja kushiriki Misa, ili uone kuwa hii ni fursa ya kwanza, ya mwisho na ya pekee. Kwa nini basi, unakuwa na haraka? Lakini kwenye viwanja vya mpira huangalii saa?" Tatu, Jubilei ya miaka 25 ya kuteuliwa na Mtakatifu Papa Yohane Paulo wa Pili kuwa Askofu Msaidizi wa Dar es Salaam na kuwekwa wakfu na Kardinali Pengo Mwaka wa Jubilei Kuu 2000 mnamo tarehe 18 Machi, akisaidiwa na Askofu Nestor Timanywa wa Bukoba na Askofu Justin Tetmu Samba wa Musoma, ambao Wapumzike kwa amani. Amina!

Misa ya Jubilie ya miaka 25 ya uaskofu wa Askofu Kilaini
Misa ya Jubilie ya miaka 25 ya uaskofu wa Askofu Kilaini

Askofu wa Jimbo la Kayanga akiendelea alisema kuwa:   "Askofu Kilaini ni Askofu halisi, Askofu wa kweli, Askofu “Original”, maana yake ni Askofu Katoliki ambaye hakupiga kampeini au kuhonga, akitafuta uaskofu; au kwenda kulala usingizi fofofo, akaota ndoto, na kuamka ni Askofu akiwa amevalia mavazi ya kiaskofu na Biblia mkononi! Jubilei ya miaka 25 ya Uaskofu sio haba. Kwa ufupi, miaka hiyo imebeba majukumu yafuatayo: Tangu tarehe 18 Machi 2000 amekuwa Askofu Msaidizi, Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Tangu tarehe 5 Desemba 2009, Baba Mtakatifu Benedikto wa 16 alimuhamisha kutoka Jimbo Kuu la Dar es Salaam, na kuja kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, chini ya Askofu Nestori Timanywa, na baadaye chini ya Askofu Desderius Rwoma. Tangu tarehe 1 Oktoba 2022, Askofu Rwoma alipostaafu, kwa sababu ya umri, na afya yake kuwa mgogoro, Askofu Kilaini aliteuliwa kuwa Msimamizi wa Kitume wa Bukoba, wakati huo akatunga sala na kuhamasisha waamini kusali na kumuomba Mungu kumpata Askofu Jimbo haraka wa kuongoza Jimbo la Bukoba. Sala hiyo iligusa watu wengi sana, ikasaliwa, na hatimaye akapatikana Mhashamu Askofu Jovitus Francis Mwijage, aliyepewa Daraja la Uaskofu tarehe 27 Januari 2024. Tumshukuru Mungu."

Akofu Rweyongeza aliendelea kuelezea  maana ya kuwa kuhani kuwa: “Padre amebarikiwa ili abariki.” Ni katika mkutadha huo ambapo aligusia juu ya wanaojiita waponyaji alisema kuwa, “uponyaji unatoka kwa Mungu pekee na sio kwa wachungaji wanaowalaghai waamini kwa pesa na miujuiza,”hivyo kuwaasa Waamini Wakatoliki “waepuke imani potofu, bali wamwamini Mungu daima wakisali na kuomba kwa imani thabiti.” Askofu Rweyongeza alisema kuwa Jubilei ni shukrani, hivyo waamini waendelee “kumshukuru Mungu kwa ajili ya maisha ya Mhashamu Kilaini, wamtakie afya njema na amewaasa wazazi waelekeze familia zao juu ya kutoa shukrani kwa Mungu Aidha alisema wito wa kuwa mlinzi unamaanisha kulinda viumbe vyote, kuheshimu kila kiumbe cha Mungu na mazingira tunayoishi huku, na waamini wakizingatia kulinda uhai kwani kila binadamu ameumbwa kwa mfano na sura ya Mungu. “ Askofu Rweyongeza alisema kuwa kinachoponya ni Imani na si upako, maji, chumvi wala makelele na iwapo mtu yeyeto anajiita anaponya watu, apelekwe ICU au hospitalini waliko wagonjwa ili aponye wagonjwa wetu na watu wapate kuamini.

Askofu Rweyongeza wakati wa mahubiri
Askofu Rweyongeza wakati wa mahubiri

Askofu alitoa onyo kali kwa baadhi ya viongozi wa dini wanaochezea “Imani za watu wakijifanya wanakemea mashetani kwa mgonjwa bila kumpeleka hospitali, huo ni uongo mtupu huku wengine wakiishia kuhubiri utajiri na miujiza wakiwalaghai waamini na siyo kuhubiri Yesu wa Msalaba: “ Wachungaji wanaochezea imani za watu wanaohubiri Yesu ambaye sio halisi Yesu wa utajiri na miujiza na sio Yesu anayealika watu watubu na kuacha dhambi tunatakiwa kuwapima kwa kuwapeleka ICU au chumba cha wagonjwa mahututi ili  kufanya miujiza na kuponya wagonjwa, kuwapeleka mochwari au makaburini ili awafufue waliokufa na kufanya miujiza inayoonekana na kwa watu tunaowafahamu sio kuongopea waamini.”Alisema Askofu Rweyongeza.  Askofu Rweyongeza aliendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumlinda na kumuepusha na majaribu mbali mbali ya maisha na Mungu kumtwika jukumu la Uaskofu bila mastahili yake na kuwasihi waamini kumuombea kwa wakati uliobaki na kutoa shukrani kwa Mungu zawadi ya Jubilei kwa kusaidia na kuwezesha kiasi cha Shillingi Millioni 40 kusaidia kiwanda cha Useremala kilichopo Kashozi Jimbo la  Bukoba, ambacho kimekuwa kiwanda cha Kwanza mkoani Kagera. Askofu wa Kayanga vile vile hakukosa kutaja alama zilizo kwenye mioyo ya watu kuhusu mshangwera huyo Askofu Kilaini zikiwa kama vile:  “huruma, kujitoa, kuwa na hekima na busara, kuchangamana na watu, kuwa na Imani kuu, nidhamu kuhabarisha, ujasiri na uvumilivu"… haya ni miongoni tu  mwa yale 25, na machache aliyotaja.

Waamini katika misa ya Jubilei ya miaka 25 ya uaskofu wa askofu Kilaini
Waamini katika misa ya Jubilei ya miaka 25 ya uaskofu wa askofu Kilaini

Kifungu kingine cha neno Jubilei alisema  kuwa Jubilei ya Uaskofu ni fursa ya kuishauri Serikali Sikivu (Ebr 13:17).  Hapa Askofu alielezea kuwa:Tulipopata uhuru wa bendera 1961, Baba wa Taifa alikuwa na mtihani bado wa kupiga vita maadui watatu: Ujinga, Umaskini na maradhi. Je, tumefanikiwa kwa kiwango gani kupiga vita maadui hao?  Hili lilikuwa swali muhimu ambalo linapaswa kutafakariwa. Na alitoa mfano akisema kuwa “Kuna bango katika lango la Chuo Kikuu fulani huko Afrika ya Kusini linasomeka hivi: “Ukitaka kuangamiza taifa lolote bila kumwaga damu, huhitaji kutumia silaha za nyukilia. Njia nzuri ya kuangamiza taifa ni kuharibu mfumo wa elimu na maadili. Ruhusu mbumbumbu waonekane ‘wamefaulu’ na wasonge mbele hadi Vyuo Vikuu. “Matokeo yake yatajidhihirisha baada ya muda: mbumbumbu hao wakishafaulishwa kwa kupata vyeti feki, wagonjwa watafia mikononi mwa madaktari na manesi; majengo yataporomoka mikononi mwa wahandisi; pesa zitapotelea mikononi mwa wachumi, utu utapotea mikononi mwa viongozi wa dini na serikali, na haki itapotea mikononi mwa mahakimu na wanasheria.”

Misa iliudhuriwa pia na Kardinali Pengo,Askofu Mstaafu wa Jimbo kuu Dar es Salaam
Misa iliudhuriwa pia na Kardinali Pengo,Askofu Mstaafu wa Jimbo kuu Dar es Salaam

Katika Misa hiyo ya Jubilei ilihudhuriwa na Balozi wa Papa nchini Tanzania Askofu Mkuu Angelo Acattino, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa jimbo Kuu la Dar es salaam, Maaskofu Wakuu wa majimbo makuu mbali mbali nchini Tanzania, maaskofu, Viongozi mbali mbali wa dini nyingine na serikali, Mapadre na Watawa wa mashirika mbali mbali ya Kitawa kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki Bukoba.

Waziri Mkuu wa Tanzania: kujiandikisha daftari ya kupiga kura

Akihutubia waamini waliofika katika Jubilei hiyo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bwana Kassim Majaliwa alisema kuwa mwaka 2025 ni mwaka wa uchaguzi hivyo kuwataka wananchi kujiandikisha na kujitokeza kupiga kura ili kuwa na haki ya kuchagua viongozi wanaowahitaji na kuwasihi wananchi kujitokeza kuhakiki daftari la kudumu la wapiga kura ili kuboresha taarifa zao pamoja na kutoa wito kwa Watanzania kulinda Amani na utulivu ndani ya nchi na kufanya uchaguzi wa huru, haki na Amani ili kuwa na taifa la mfano.

Mkuu wa Mkoa Kagera

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajat Bi Fatma Abubakari Mwasa, kupitia hotuba yake mbele ya viongozi wa Kanisa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  aliwashauri wakazi wa mkoa wa Kagera kuwa walinzi wa kwanza wa amani ya nchi na kukemea  wahamiaji haramu wanaoingia nchini kwa kujifanya vibarua katika mashamba yaliyopo mpakani na kuwahimiza wakazi wa mkoa huo wa Kagera kufanya kazi kwa bidii na kuacha tabia ya kuwadekeza watoto na wanafunzi wa Shule kutofanya kazi, na  kutengeneza taifa la wavivu na wazembe badala yake watumie fursa zinazotolewa na Serikali kujiinua kiuchumi. Akitoa hotuba yake katika Maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa alisema kuna mambo aliyokuwa anasita kuyasema lakini amepata ujasiri kuyaongea kwa kuwa Baba Askofu Kilaini alimpatia ujasiri wa kuyasema, na alisisitiza kuwa watu wote waheshimu ndoa na kuwaombea wanandoa ili waishi kwa uaminifu na upendo kama alivyokuwa Mtakatifu Yoseph aliyeishi kwa uaminifu na kuitunza familia Takatifu.

Waseminari katika misa ya Jubilei
Waseminari katika misa ya Jubilei

"Kuna mambo matatu nilisita kuyasema kwa kuwa Wahaya mna msemo: “Kakitandugwaho” yaani lisianzie kwangu, lianzie kwao hao hao,"  lakini leo hii  Baba Askofu Kilaini amenipa nguvu. "Nimezunguka kule Karagwe, kuna Kijiji kinaitwa Nyakakika, Kagondo n.k nimekuta, watu wamekodisha zaidi ya Ekari 16,000 kwa watu kutoka Nchi za Nje wanafuga ng'ombe, nadhani haya ni mambo ya kukemea kuliko kuzuia wawekezaji wa ndani." Alisema Bi Fatma Mwassa katika hotuba yake. Mkuu wa Mkoa alisema watu wanaingia katika mkoa huo kimkakati na wanapowapokea kama vibarua wajue kuwa hawana nia njema, na kueleza kuwa serikali inamshikilia kijana mmoja ambaye ni kibarua wa kulima waliyemgundua kuwa na Passport za nchi mbili tofauti.

Picha ya pamoja baada ya misa
Picha ya pamoja baada ya misa

 “Tumekubaliana kuanzisha mashamba ya Vijana ya Kilimo, na kwa kuwa baadhi ya wakazi wa mkoa wa Kagera hawajazoea kufanya kazi nimeenda kwa makontrakta wa Kagera na kiwanda cha sukari Mtibwa na Wizara ya Elimu wakaleta maburdoza na matrekta tukawalimia bure ili kurahisisha na kuwagawia vijana walime Kahawa na mazao mengine, vijana wakasema hatuwezi kulima mpaka mtupatie chakula cha mchana na usiku, kwa sababu tuna shughuli zetu nyingi,” alieleza kwa masikitiko, kiongozi wa Mkoa wa Kagera.  Bi Fatma Mwassa alisema, tabia mbaya zaidi inayoendelea ni watanzania wa makabila ya mkoani Kagera kuanza kukubali kuolewa na wahamiaji hao, na kuwaoa mabinti wanaokuja nao na kuanza kuzaa watoto ambao baadae watachaguliwa kuwa viongozi wa Kijiji, vitongoji na baadae watakuwa wabunge na mwisho watachukua hata uongozi wa Juu katika Nchi mwisho kusababisha machafuko kama yanayoendelea kutoka mataifa jirani.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera akiwa katikati ya waamini
Mkuu wa Mkoa wa Kagera akiwa katikati ya waamini
Mahubiri ya Askofu Rweyongeza kwa miaka 25 ya uaskofu wa Kilaini
21 Machi 2025, 16:14