Tafakari Dominika ya Saba Mwaka C wa Kanisa: Kanuni ya Dhahabu: Upendo, Haki na Msamaha
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., - Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi.Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 7 ya Mwaka C wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii inatualika, “kuchagua na kuiishi amri kuu ya mapendo.” Katika somo la kwanza, Daudi, licha ya kutendewa ubaya na Mfalme Sauli, anachagua kutenda wema na kutolipa mabaya kwa mteule wa Bwana. Katika somo la pili, mtume Paulo amtambulisha Yesu kama Adamu mpya, aliyechagua kumtii Baba, tofauti na Adamu wa kwanza aliyechagua kutotii. Kwa utii wa Kristo sisi sote tunashirikishwa uzima mpya. Shangilio (Yn 13:34), Yesu anatupa amri mpya, amri ya mapendo, kama vile alivyotupenda sisi, anatualika nasi pia kupendana. Katika somo la Injili, Yesu anatupa amri ya dhahabu (Golden Rule), yaani, kuwa tayari kuchagua kuwatendea wengine yale ambayo ningependa kufanyiwa. Anatoa ahadi ya baraka za mbinguni kwa anayeishi amri ya mapendo. Katika Dominika ya leo, ndugu yangu mpendwa, chagua kupenda, chagua kutenda mema na kutorudisha ubaya kwa ubaya. Mungu aliye mwingi wa huruma na Neema anatupenda sote kama watoto wake wateule, anatusamehe kila mara tunapopungukiwa mapendo (Zab 103:1-4, 8,10,12-13). Anatuahidi wingi wa baraka za mbinguni ikiwa tutaishi kweli amri hii ya mapendo. Somo la 1: Ni Kitabu cha 1 Sam 26:2, 7-9, 12-13, 22-23. Somo la kwanza tulilolisikia, ni kutoka katika kitabu cha kwanza cha Samweli. Ni kisa cha Mfalme Sauli ambaye alikua akimtafuta Daudi ili amwue. Mfalme Sauli, aliyepakwa mafuta na Bwana kuwa Mfalme wa kwanza wa Israeli, aliposhindwa kuongoza taifa la Mungu, Mungu alitangaza kumkataa (1 Sam 13-15). Kisha mwenyezi Mungu taratibu akaanza kumwinua na kumwandaa Daudi kuwa Mfalme, kuwa kiongozi wa watu wake. Baada ya ushindi dhidi ya Goliath na Wafilisti, Daudi alipata umaarufu mkubwa (1 Sam 17).
Kitendo hiki kinamfanya Sauli aone wivu na anamtafuta Daudi ili amwangamize (1 Sam 18, 24). Lakini Daudi anachagua kutenda wema. Hataki kumwangamiza mteule wa Bwana, hataki kunyoosha mkono wake aangamize licha ya kuwa alikuwa na nafasi ya kumtendea ubaya Mfalme Sauli. Daudi aliamua kutenda wema, kulipa ubaya kwa wema.Ndugu zangu katika somo hili la kwanza na Zaburi tuna mambo manne ya kujifunza. Kwanza: Tunaposhindwa kuchagua upendo tunaleta maumivu katika maisha yetu na ya wengine. Mfalme Sauli alipoona Daudi anakuwa, anaanza kuinuliwa na Mungu, anakubaliwa na watu baada ya kushinda vita, anaamua kumtafuta ili amuue. Moyo wake unajawa na wivu na anawaza kumtendea mabaya Daudi. Mara kadhaa na mimi na wewe tunapungukiwa upendo ndani mwetu, na matokeo yake yanaleta maumivu ndani mwetu na ndani ya wengine. Tunaposhindwa kuchagua kupenda madhara yake ni mengi. Kwanza: Chuki na Wivu. Tunapokosa upendo ndani mwetu ni chanzo cha kuwa na chuki wivu kwa wengine. Huenda maendeleo, vipaji, karama ambazo Mungu amewajalia wengine vinatuumiza rohoni. Tunaona uchungu kwa baraka ambazo Mungu ameshusha kwa wengine, katika kazi zao, katika familia zao, katika wito wao, kwa watoto wao, katika masomo na biashara zao nk. Wivu unatuondolea furaha ndani mwetu, unatuondolea amani yetu ya ndani, unatufanya kushindwa kushirikiana na wale ambao pengine wamepiga hatua moja mbele zaidi kuliko mimi na wewe. Tumwombe Mungu atusaidie ili tutambue kuwa Mungu anamwinua kila mmoja kwa wakati wake na kwamba mimi siwi bora kwa kutamani, kukusudia, na kupanga kumwua au kumwangamiza mwingine. Kuna msemo unasema, “Fimbo iliyoua nyoka haiwekwi sebuleni” ukimaanisha kuwa, yeyote anayekusudia na kudhamiria kumchafua, na kumwua kwa maneno au matendo mtu mwingine ili yeye awe bora basi huyo hafai kwa lolote. Siwezi kusimama kwa kuwaangusha wengine, wala siwezi kubarikiwa kwa kuwaombea wengine mabaya.
Pili: Vinyongo na Visasi. Mfalme Sauli anapanga kulipa kisasi, anapanga kuondoa uhai wa Daudi. Mfalme Sauli alipanga kumwua Daudi kwa kuwa alikua na roho ya kisasi ndani mwake. Wivu ulimpelekea kuwa na kisasi, anataka kumwua Daudi kwa kuwa alisifiwa kufanya mambo makubwa kuliko yeye. Ndugu wapendwa, mara kadhaa tunajenga roho ya visasi ndani mwetu. Huenda kuna watu walishatuumiza katika maisha yetu, au kwa makusudi au kwa kutokudhamiria. Matokeo yake, tunakuwa wakati fulani na roho ya kutaka kulipa kisasi, ili tushirikishane maumivu. Kwamba ninakuumiza kama wewe ulivyonisababishia maumivu mimi. Roho hii ya visasi si nzuri, wala Mungu hataki tulipe kisasi bali anatutaka kulipa daima kwa wema. Ndugu zangu sio jambo rahisi sana ndio maana tunapaswa kumwomba Mungu atusaidie kuachilia na kusamehe hasa wale watu ambao walitusababishia mioyo yetu kuvuja damu kwa sababu mbalimbali. Daudi anatufundisha kutolipa kisasi hata kwa wale waliotuumiza, wanatouwazia mabaya, wanatotuudhi na kutuwazia mabaya. Yesu ninakuomba leo nisaidie kusamehe, na uondoe ndani mwangu roho ya visasi na vinyongo. Tatu: Kudhaniana vibaya: Mfalme Sauli alifikiri pengine Daudi alitaka kumpindua katika ufalme wake. Na hivyo anapanga kumwangamiza. Daudi hakuwa wala na wazo la kumpindua Mfalme Sauli bali ni Mungu alishaanza kumkataa Sauli kwa kuwa hakufuata maelekezo yake (1 Sam 15). Ndugu mpendwa, tunapokosa upendo wa kweli ni chanzo cha kudhaniana vibaya. Mara kadhaa tunanyoosheana vidole kwa kuwa kila mmoja anataka kuonekana mwenye haki mbele za Mungu na mbele za watu. Katika familia zetu, jumuiya zetu, makazini kwetu, katika ndoa, katika mahusiano nk. Jambo hili limekua chanzo cha maanguko ya familia, ndoa, na mahusiano kati ya watu katika biashara na makazini. Tunapokua na upendo wa kweli hatuwezi kudhaniana vibaya kwa kuwa upendo huvumilia yote.
Pili: Upendo wa kweli ni tiba katika mahusiano na mafungamano yetu na Mungu na mahusiano kati yetu sisi kwa sisi. Daudi, tofauti na Mfalme Sauli, alichagua kupenda na kutokulipa kisasi. Matokeo yake alimfanya Sauli kujutia kitendo chake cha kutaka kumwangamiza Daudi pasi na sababu yoyote. Ndugu zangu wapendwa, upendo unatibu majeraha yaliyosababishwa na dhambi. Dhambi inaharibu mahusiano mema yaliyopo kati yetu sisi na Mungu na kati yetu sisi na kwa sisi. Tunapojibu ubaya kwa wema, tunatoa fundisho kubwa sana kwa wale ambao nyakati fulani walituumiza, walitutesa, walitudharau, walitusema vibaya, walituua kwa maneno mabaya, walitupaka matope na mambo mengine mengi kama hayo. Upendo ni tiba dhidi ya familia zilizo na machafuko, ndoa zilizo na migogoro, ni tiba dhidi ya nchi zilizo na vita na migogoro, upendo ni tiba dhidi ya nafsi zilizokata tamaa, nafsi zilizojeruhiwa, upendo ni tiba dhidi ya ukosefu wa uaminifu. Mfalme Daudi aliachilia, alikua tayari kusema, “I let it go” Mimi na wewe tuwe na ujasiri wa kutupa mzigo mzito wa maumivu moyoni mwetu kwa kuamua kupenda. Anayependa anasamehe, anahurumia, anavumilia, anaachilia, anawapokea wote, waliotutendea mema na waliotuumiza pia. Tatu: Mwenyezi Mungu anawainua wale wanaowatakia wengine Mema. Daudi katika mambo yote alimuwazia mema Mfalme Sauli. Hakuwaza kumtendea ubaya kwa kuwa alikua ni mteule wa Bwana. Bwana akamwinua Daudi kuwa Mfalme kwa wakati wake. Ndugu wapendwa, tunapochangua kupenda, tunapochagua kuwatendea wengine mema, Mungu anatubariki, Mungu anatuinua. Kila mmoja wetu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, ni mteule wa Mungu, ni mwana mpendwa wa Mungu. Tunapotenda lolote kwa mmoja wa wana wa Mungu walio wadogo, tumemtendea Yesu mwenyewe (Mt. 25:34-35). Ni mara ngapi tunawachukulia wenzetu kama wateule wa Mungu? Mara ngapi tunafikiri kabla ya kuwaza kuwatendea uovu wenzetu? Tunapowawazia na kuwatendea wenzetu mema ndugu zangu, Mungu atatubariki, Mungu atatuinua kila mmoja kwa wakati wake kwa kuwa anatupenda sote, anatuwazia mema sote.
Nne: Mwenyezi Mungu anatuhurumia na kutusamehe kila tunaposhindwa kuishi vyema amri ya mapendo. Katika zaburi ya 103:1-4, 8,10,12-13, mzaburi anatuambia, Bwana amejaa huruma na Neema. Anatusamehe kila wakati, kwa sababu ya upendo wake mkubwa, upendo ambao kamwe hausemi inatosha. Ametuweka mbali kabisa na dhambi zetu, kwa kuwa yeye ni Baba yetu mwema anayetupenda sana. Ndugu mpendwa, Dominika ya leo inatupa nafasi ya kuanza upya tena katika mahusiano yetu sisi na Mungu na mahusiano kati yetu sisi kwa sisi. Huenda nimekua chanzo cha maumivu na vilio kwa wengine, ni muda wa kukaza moyo na kuomba msamaha. Huenda nimeumizwa pia mara nyingi na wengine, au katika ndoa, au katika familia, au katika mahusiano, ni muda wa kumwambia Mungu, nifundishe kupenda. Mungu anatupokea, anatakasa Mawazo na fikra zetu, anatusamehe na anaahidi kututia tena taji ya utukufu na heshima.
Somo la Injili: Ni Injili ya Luka 6:17, 20-26. Somo la Injili Takatifu ni kutoka katika Injili ya Luka, Bwana wetu Yesu Kristo anatoa fundisho muhimu sana juu ya Upendo. Ni sehemu ya hotuba yake akiwa bado nyikani, baada ya kufundisha juu ya heri na ole, leo anafundisha fundisho kubwa juu ya Upendo. Anafanya mapinduzi (revolutionary moral teaching) juu ya chaguzi sahihi katika mahusiano yetu sisi wanadamu, akitufundisha juu ya amri kuu ya mapendo. Anatufundisha sheria ya dhahabu (Golden rule) inayotutaka kuwapenda wengine na kuwatendea wengine vile sisi tungependa kuwanyiwa. Hii ni kwa sababu, sisi sote tu wana wa Mungu, Baba yetu ni mmoja anayetupenda sisi sote. Hivyo Yesu anatutaka kuchagua daima kupenda, hata kiasi cha kuwasamehe kuwasaidia adui zetu kwani ndicho kipimo cha thawabu yetu. Katika somo hili la Injili dominika ya leo tuna mafundisho manne ya kujifunza: Kwanza: Yesu anatualika sisi sote tunaomfuata na kumsikiliza, kuwapenda adui zetu (Love your enemies). Yesu anasema na wale waliomfuata na kusmikiliza, “Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale wanaowachukia ninyi, wabarikini wanaowalaani na waombeeni wanaowaonea” Neno “wapendeni” yaani agapate linalotumika hapa ni upendo wa Kimungu, tofauti na “eros” yaani upendo wa mume na mke au “filia” yaani upendo wa kirafiki. Hii ilikua kinyume na sheria za kiyahudi na wakati huu wa Yesu ilijulikana sheria ya jicho kwa jicho (lex talionis) ambayo msingi wake ni Torah au Sheria ya Musa (Kutoka 21:24, Walawi 24:20). Kumbe anatukumbusha kuwa na huruma dhidi ya kulipiza kisasi. Pia tunaalikwa kuwa tofauti na kuonesha kweli thamani ya ukristo wetu kwa matendo kwa kuwa kama ni kutendeana wema, hata watu wa mataifa hufanya vivyo hivyo.
Ndugu wapendwa, Yesu anasema nami, anasema nawe ambaye unamsikiliza kila siku katika Neno lake, ambaye umeamua kuwa mfuasi wake kweli. Anakuagiza mimi na wewe kuwapenda adui zetu. Anatuonya juu ya kutolipiza kabisa kisasi. Katika tamaduni za wayahudi, kumpiga mtu shavu ilikua ni kosa kubwa sana. Kugeuza na shavu la pili, Yesu anatukumbusha kutolipa kabisa kisasi. Katika tamaduni za Wayahudia pia, joho iliweza kutumika kuweka dhamani na kuchukuliwa iwapo mtu alishindwa kulipa deni. Lakini kanzu haikupaswa kuwekewa dhamana hata kama mtu alishindwa kulipa deni yake. Yesua anasema, akunyang’anyaye joho, mpe na kanzu pia. Yesu anatukumbusha hapa kuwa tayari kutoa vyote yaani, ukarimu hadi mwisho hata kwa adui zetu. Mimi ninayemsikia Yesu leo nipo tayari kufanya hivyo? Pili: Yesu anatufundisha Sheria ya dhahabu yaani, kuwatendea wengine vile sisi tungependa kutendewa pia (Golden Rule). Yesu anawafundisha wafuasi wake na anatufundisha sisi sote kwamba, “Kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi watendeeni vivyo hivyo.” Ndugu mpendwa, sheria hii ya dhahabu ni msingi wa maisha yetu sisi wanadamu kwa kuwa ndiyo kiini cha amri zote. Kumpenda Mungu na kuwapenda wengine kama ninavyojipenda mimi. Kama nampenda Mungu kweli, kamwe siwezi kutenda jambo lolote baya kwa wengine kwa kuwa ndani mwangu nitajazwa na fadhila za Kimungu. Anayependa anasamehe, anayependa anahurumia, anayependa anavumilia na kuwachukulia wengine kwa upole, anayependa ana Fadhili, anayependa habagui, anayependa haangalii na kutafuta makosa, anayependa hatafuti faida yake binafsi. Tumwombe Mungu atukumbushe kila mara juu ya mapendo yake makubwa kabisa kwetu sisi wanadamu na wajibu wetu wa kuwapenda wengine kwa kipmo hicho hicho.
Tatu: Yesu anatofautisha upendo wa Kimungu na upendo wa wanadamu (God’s love vs Human love). Yesu anasema, “Maana mkiwapenda wale wawapendao ninyi, mwaonesha fadhili gani? Hata wenye dhambi hufanya hivyo hivyo. Yesu anatoa tofauti kati ya upendo kwa kibinadamu, yaani upendo wa nipe nikupe (transactional love) na upendo wa Kimungu ambao hauna mipaka (unconditional love). Ndugu wapendwa, Mungu anatupenda sote bila mipaka, bila kikomo. Huruma yake haina mipaka, kwa wema hali kadhalika kwa wenye dhambi. Mungu anatupenda sote kama watoto wake wapendwa, anataka sote tuupate uzima wa milele na ndio sababu alimtuma mwanaye ili sisi sote tuwe hai tena. Upendo huu wa kimungu ndio Yesua anataka tuuishi na kuunesha kila mmoja kwa mwenzake. Kuwa tayari kupenda bila kutegemea faida, kupenda bila kutegema shukrani. Yeye anaonesha mfano wa kutupenda hata kutoa uhai wake, anawasaheme waliomtesa na kumuua. Je, ni mara ngapi tupo tayari kupenda hata kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine? Katika familia, ninapenda kiasi gani? Ninajali, ninathamini? Ninasamehe na kuhurumia? Je, nipo tayari kujishusha na kuomba msamaha pale ninapokosea, nipo tayari kusamehe pale ninapokosewa? Yesu atusaidie tuwe na mapendo ya kimungu. Yesua anatuonya kutohukumu. Mara ngapi nimewanyooshea watu vidole na kuwatuhumu na kusahau kuwa hata mimi pia sijakamilika? Yesu atusaidie tuwe na mapendo ya Kimungu. Nne: Yesu anaahidi baraka kwa wale wanaoishi na kuchagua amri ya mapendo (God’s abundant blessings). Yesu mwishoni mwa Injili hii anatuahidi sisi wafuasi wake wingi wa baraka za mbinguni. Kipimo cha kujaa na kusukwasukwa na kushindiliwa na kumwagika ni ishara ya wingi wa baraka na neema za mbinguni.
Ndugu mpendwa sana, Dominika ya leo Yesu anatuahidi wingi wa baraka za mbinguni vifuani mwetu. Lakini wingi huu wa baraka ni kwa wale ambao hawahukumu, wale ambao hawalaumu, wale ambao wapo tayari kuachilia, huenda kuna watu tumewafungia moyoni na hatuko tayari kuwasamehe, tunakua watumwa ndani mwetu sisi wenyewe, lakini pia kwa wale walio wakarimu kwa wenye shida. Yesu anaahidi kipimo cha kujaa na kusukwa sukwa na kushindiliwa hata kumwagika. Ndugu mpendwa, ruhusu baraka za Mungu zishuke juu yako kwa kuchagua na kuiishi amri kuu ya mapendo. Achilia, samehe, jali, hurumia, saidia, penda, kisha Yesu anaahidi wingi wa neema na baraka kwa ajili yako leo. Tusikubali kupoteza neema na baraka za Mungu kwa kung’ang’ania mambo yatutengayo na upendo wa Mungu wetu.Somo la pili: Ni Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo 1 Kor 15:12, 16-20. Katika somo la pili, Mtume Paulo amekuwa akiwafundisha Jumuiya ya Korintho kwa kirefu katika sura hii ya kumi na tano juu ya fumbo la Pasaka yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo kama kiini na msingi wa imani yetu. Katika sehemu tuliyosikia leo, anatufundisha kuwa, sisi sote tunarithi dhambi ya asili iliyotokana na kosa la kutotii kwa Adam. Mtume Paulo anamtambulisha Yesu kama Adamu mpya, aliyechagua kumtii Baba, ambaye kwa mapendo makubwa alikubali kufa msalabani kwa ajili yetu sisi. Tunapoumizwa, tunapoteseka, tunapodharauliwa, tunaposingiziwa, tutakua tayari kusamehe kama Bwana wetu Yesu Kristo alivyotuachia mfano. Kwa kufanya hivyo tutashiriki maisha ya Kristo tuwapo hai na kupata tuzo mbinguni baada ya maish haya ya hapa duniani. Hitimisho: Katika Dominika ya Saba ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa, ndugu yangu mpendwa, chagua kupenda, chagua kutenda mema na kutorudisha ubaya kwa ubaya. Tambua upendo na huruma kubwa ya Mungu ndani mwako, Mungu aliyekubali kufa kwa ajili yangu mimi na wewe na tuone hitaji la kuwa tayari kuwapenda wengine kama tunavyojipenda sisi. Sio jambo rahisi, tunaomba neema ya Mungu ili daima tujawe na mapendo ya kimungu ndani mwetu.