杏MAP导航

Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Saba ya Mwaka C wa Kanisa: Kanuni ya Dhahabu, Amri kuu ya Upendo kwa Mungu na Jirani ni msingi wa maisha ya Kikristo. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Saba ya Mwaka C wa Kanisa: Kanuni ya Dhahabu, Amri kuu ya Upendo kwa Mungu na Jirani ni msingi wa maisha ya Kikristo.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Saba ya Mwaka C: Kanuni ya Dhahabu na Amri Kuu ya Upendo

Kanuni ya Dhahabu na Upendo kwa Mungu na jirani: Huu ni mwendelezo wa tafakari kuhusu "Heri na Ole" Yesu anafundisha kuhusu upendo kwa adui. Mwinjili Luka anaanza kwa kutoa fundisho la Yesu: wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wanawachukia ninyi, wabarikieni wale ambao wanawalaani ninyi na waombeeni wale ambao wanawaonea ninyi. Baada ya fundisho hilo anatoa baadhi ya mifano halisi ya kuonesha namna ya kuwapenda adui zetu.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

Na kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni vivyo hivyo” (Lk 6:31) Huu ni muhtasari wa mafundisho yote Dominika ya Saba ya Mwaka C wa Kanisa; mafundisho yaliyo magumu na kuyashangaza, mepesi kuyazungumza na kuyafundisha lakini magumu kutendwa na mwanadamu huyu dhaifu mwenye damu na nyama…  “Bwana nifanye nini?” ni swali la yeyote anayemuendea Kristo akijitafutia uosho na utakaso wa roho moyoni mwake akitambua na kukiri huruma na upendo vinavyotiririka katika Mnazareti huyu mtukufu… Kristo jibu lake ni hilo tu, “... kama unavyotaka watu wakutendee wewe, watendee vivyo hivyo” (Lk 6:31). Hii ni kanuni ya dhahabu, sheria itokayo katika mtima wa Mungu, na kina, na marefu, na mapana ya huruma na bahari ya mapendo yake kwa lengo la kukuza, kuthamini, kujali na kuheshimu hadhi na utu wa mwanadamu aliyemjalia sura na mfano wake. Kanuni hii kuu inajitwika vyote, inaamini yote, inavumilia vyote, inapenda wote. Kwa njia ya kanuni hii upendo wa Mungu unamiminwa ndani mwetu kutoka mbingu za juu.

Kanuni ya Dhahabu, Amri ya Upendo na Auni ni msingi wa maisha ya amani
Kanuni ya Dhahabu, Amri ya Upendo na Auni ni msingi wa maisha ya amani

UFAFANUZI: Kanuni ya dhahabu inalenga kurekebisha ili kuboresha herufi za sheria yoyote kwa kuidadavua vema, kuondoa mushkeli wa kutoeleweka kabisa, kueleweka kidogo au kueleweka vibaya. Inasafisha ugumu, inatoa mwongozo kwenye ubabaifu na mazingira yasiyo haki… Inamdai mwanadamu, hata asiyeamini kwa njia ya dhamiri yake safi, amuheshimu na kumthamini jirani kwa vile yeye mwenyewe anatamani kuthaminiwa utu wake. Ukiitazama jamii iliyochanganyikiwa na vingi, tena vingine wala sio vya muhimu kabisa, jamii ambamo upendo umeganda kwa ubaridi wa jokofu, utaona hitaji kubwa la kanuni hii njema ya dhahabu… kwa kutambua umuhimu huu liturjia leo inatuelekeza kwenye tafakari maridhawa Mwinjili Luka akiripoti maagizo kadha wa kadha kutoka kwa Kristo mwenyewe akiyafunga yote ndani ya neno hili “…na kama mnavyotaka watu wawatendee ninyi, watendeeni vivyo hivyo.”

Wapendeni adui zenu na kuwaombea
Wapendeni adui zenu na kuwaombea   (AFP or licensors)

Maagizo hayo ni fadhila zenye kutuongoza vema katika safari ya imani: huruma na msamaha, upendo kwa Mungu na kwa jirani, kutafsiri vema na kuzuia kuendeshwa na hisia, wajibu wa kimaadili, kujitambua hasa katika udhaifu na kuukiri na kuungama uwepo wa Mungu katika kila sekunde ya uhai wetu. Maagizo haya yanadai ujasiri wa makusudi na sadaka kubwa sababu asili ya mwanadamu haimuelekezi kumpenda adui bali kumuangamiza, kusamehe madeni, kugeuza shavu la pili unapopigwa la kwanza (hmm! sijui kama yupo anayeweza), kutokuhukumu, kumwachia anayekunyang’anya kitu chako na zaidi sana kusamehe na kuachilia majeraha… Kumbe kumpenda Mungu kunathibitika katika kupenda na kusamehe na kuombea na kwa hili Daudi katika somo I (1Sam 26:2, 7-9, 12-13, 22-23) ni mfano bora wa kuigwa. Alikuwa na kibali kutoka kwa Bwana cha kumtenda apendavyo adui yake Mfalme Sauli akachagua kumsamehe na kumfundisha maana ya utu na hekima.

Upatanisho wa kweli ni mwanzo wa amani ya kudumu
Upatanisho wa kweli ni mwanzo wa amani ya kudumu   (Vatican Media)

Msamaha una nguvu kuliko tufani ukimfaidia zaidi anayesamehe kuliko hata anayesamehewa. Kusamehe ni kupenda, Mungu ni upendo, kwa hiyo kusamehe ni tabia ya kimungu, basi na tusameheane kila mmoja na mwenzake, turudishe mioyo, tushushe panga zetu, tukumbatiane tena kwa amani, furaha na busu takatifu. Maagizo ya Neno la Mungu leo yanatuongoza polepole, wala sio haraka kwani hatutastahimili, ni safari ya kukua na kukomaa hatua kwa hatua kuelekea kwenye ukamilifu kama mbegu, mche, mmea na baadaye mti uzaao, huku tukigeuzwa taratibu kutoka ndani anavyofundisha Mt. Paulo katika somo II (1Kor 15:45-49) ili kuwa watu wa kiroho kama Kristo alivyo wa kiroho tukiichukua sura yake Yeye aliye wa mbinguni. Wimbo huu “…Huu ndio ni mwanzo wa ufalme wa Mungu // umtendee mwenzako vile upendavyo kutendewa naye…”… unatutafakarisha kuwa kanuni ya dhahabu ni ishara ya kuzinduliwa ufalme wa mbinguni, tuombe neema ya kuishika vema ili tuufikie ufalme huo… hata hivyo bila bahati huenda hatujafaulu kuwatendea wenzetu yale tungependa sisi tutendewe… tazama sipendi kabisa kunyamaza...

Liturujia D7 Mwaka C
22 Februari 2025, 13:48