JRS inasimama na wakimbizi licha ya kupunguzwa kwa USAID!
Na Linda Bordoni – Vatican.
Katika tafakari ya Padre Michael Schöpf, katika mahojiano na vyombo vya habari vya Vatican. Mkurugenzi wa kimataifa wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Jesuit (JRS) alitoa maoni yake kuhusu kusitishwa kwa ghafla na mara moja kwa ufadhili wa misaada ya kigeni na serikali ya Marekani, baada ya utawala mpya kuchukua madaraka, akisisitiza kuwa uamuzi huu unaonesha mabadiliko makubwa kutoka katika ushirikiano wa kimataifa, na kuibua wasiwasi juu ya mmomonyoko wa utaratibu wa ulimwengu unaozingatia maadili. Kwa mujibu wa Padre huyo alisema kuwa “Kuondoa hadhi kwa kundi leo hii kunaweza kusababisha jambo lile lile kwetu sote kwa kesho.”
Wakimbizi 100,000 walioathirika
Akielezea uamuzi wa serikali ya Marekani wa kusitisha ufadhili wote wa misaada ya kigeni "kusitishwa kwa ghafla," alisema iliathiri mara moja mipango inayolenga watu walio hatarini katika nchi tisa, ikiwa ni pamoja na Chad, Ethiopia, Iraq na Sudan Kusini. Alifafanua zaidi kwamba mipango hiyo, yenye jumla ya bajeti ya mwaka ya dola milioni 18, ilisaidia zaidi ya wakimbizi 100,000, hasa katika maeneo ya elimu, afya ya akili na usaidizi wa dharura. "Tulipokea barua kutoka katika serikali ya Marekani mnamo tarehe 24 Januari 2025, ikisema kwamba mipango yetu yote ilisimamishwa mara moja," Padre Schöpf alifichua. "Haraka ya uamuzi huu ilituacha bila kuwa na fursa ya kuandaa au kuandaa kipindi cha mpito, ambacho ni vigumu sana kuwaeleza wakimbizi tunaowasindikiza."
Shule pia iko hatarini
Mojawapo ya programu zilizoathirika zaidi ni mpango mkubwa wa elimu mashariki mwa Chad, "eneo lenye hali tete," ambapo Huduma ya Wajesuit (JRS) inatoa elimu kwa zaidi ya wanafunzi 10,000 na kuajiri walimu 450. Bila ufadhili, wanafunzi hawa wanakabiliwa na mustakabali usio na uhakika. Kilicho hakika, hata hivyo - alisisitiza - ni kwamba idadi kubwa itaacha shule, na kujiweka katika hatari ya kuwa mawindo rahisi kwa wasafirishaji haramu wa kibinadamu. Upungufu huo pia huathiri usaidizi wa programu za afya ya akili zinazohudumia wanafunzi wapatao 500 na shughuli za kuzalisha mapato kwa familia.
Kuzuia ufadhili
Mbali na JRS, kusitishwa kwa ufadhili kunatishia mtandao mzima wa misaada ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na UNHCR na mashirika mengine washirika ambayo yanategemea michango ya Marekani. Huku Marekani ikitoa zaidi ya asilimia 40 ya misaada ya kimaendeleo ya kimataifa, athari zinaenea zaidi ya JRS. "Hili ni wimbi la kwanza tu," alisisitiza Padre Schöpf. Mara tu mashirika mengine yakapoamua jinsi ya kukabiliana na kusitishwa kwa ufadhili, wimbi la pili la usumbufu litafuata. Mtandao wote unateseka."
Kuachwa kwa maadili
Suala jingine la kuzingatia ni motisha na uwezo wa kuzuia misaada, ambayo Schöpf alionya inawakilisha kuondoka kwa ushirikiano wa kimataifa ambao kwa muda mrefu umekuwa msingi wa juhudi za kibinadamu duniani. Mabadiliko kama haya sio tu kwa ufadhili uliopunguzwa, lakini ishara ya mabadiliko ya kina ya utaratibu wa kimataifa, alielezea. "Ikiwa tunasema kwaheri kwa umoja wa pande nyingi na utaratibu wa ulimwengu wenye msingi wa thamani, hakuna kitu ambacho kinaweza kuchukua nafasi yao. Hii ina maana ya kuingia katika mpangilio mpya wa dunia, ambapo mahusiano ya miamala yanatawala juu ya hadhi ya binadamu,” alionya Mkurugenzi wa Kimataifa wa JRS. Papa Francisko ameonya mara kwa mara dhidi ya mabadiliko hayo, Schöpf lisisitiza. Katika barua ya hivi majuzi kwa maaskofu wa Marekani, Papa aliandika hivi: “Yale yanayojengwa kwa nguvu na si juu ya ukweli wa hadhi sawa ya kila mwanadamu, huanza vibaya na mwisho wake utakuwa mbaya.”
Daima pamoja na wakimbizi
Kwa vyovyote vile hali halisi, JRS inasalia kujitolea kuwasindikiza wakimbizi na kutoa usaidizi popote inapowezekana. "Sisi sio watoa huduma tu, sisi ni shirika linalotembea na wakimbizi," Padre Schöpf alisema. "Wakati wa shida, tunasimama katika mshikamano usio na masharti na wale wanaolazimika kukimbia." Hali ambayo inatusukuma kutafakari kuhusu kushirikishana matatizo ambayo wakimbizi wanapitia kila siku kwa kiasi kikubwa zaidi. "Kwetu sisi, ni muhimu kukubali udhaifu wetu pamoja nao,"huku akibainisha kuwa, hatimaye, ni uzoefu wa Noeli. “Historia ya Noeli inatufundisha kwamba Mungu huchagua kimakusudi kuwa mwanadamu, kujitambulisha na wanaume na wanawake katika hali hatari zaidi. Nadhani hili ndilo tunaloitwa kufanya kama Huduma ya Wakimbizi ya Kijesuit,” alihitimisha. Shirika la Kijesuit (JRS) la Huduma kwa wakimbizi limezindua ombi la dharura kwa wafadhili wake, likitarajia kukusanya kati ya dola milioni 1.5 na milioni 2 ili kukidhi mahitaji ya haraka ya kifedha katika kipindi cha miezi miwili ijayo.