Dominika ya 8,Mwaka C:Maisha ni kufa na kuishi!
Na Padre Paschal Ighondo – Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 8 ya mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Dominika hii inatuandaa kuingia katika kipindi cha Kwaresima, kipindi cha kutafakari upendo, wema na huruma ya Mungu kwetu sisi wanae. Ni kipindi cha kuongeza nguvu katika sala, kufunga, kufanya toba, kuungama na kufanya mabadiliko ya maisha ya kiroho kwa ajili ya maandilizi ya sikukuu ya Pasaka. Ni kipindi cha kufa kuhusu dhambi na kuishi kitakatifu ili mwisho wa maisha ya hapa duniani kwa njia ya kifo tukaishi milele yote mbinguni na Mungu Baba pamoja na watakatifu wote. Hili linawezekana kama tukiweka tumaini letu kwa Mungu kama maneno ya wimbo wa mwanzo yanavyosisitiza yakisema: “Bwana alikuwa tegemeo langu, akanitoa akanipeleka panapo nafasi, akaniponya kwa kuwa alipendezwa nami” (Zab. 18:18-19). Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi, tunakuomba uyaongoze mambo ya ulimwengu huu yafuate utaratibu wako ili tuwe na amani; nalo Kanisa lako lipate furaha ya kukutumikia kwa utulivu”.
Somo la kwanza ni la kitabu cha Hekima ya Yoshua Bin Sira (YbS 27: 4-7). Kitabu hiki kimesheheni ushauri unaohusu nyanja mbalimbali za maisha. Sehemu tunayoisoma Domenika ya 8 ya mwaka C, inasisitiza juu ya umuhimu wa majadiliano katika maisha: kuleta muafaka, kutatua matatizo au migogoro kati ya pande mbili zinazolumbana kwa njia ya amani. Ni katika majadiliano mtu hutoa ya moyoni na kuyaweka wazi na bayana na hivyo kuwapa wengine nafasi ya kufahamu tabia yake. Ndiyo maana Yesu anasema kuwa mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu. Kwa kuwa kinywa cha mtu hunena yale yaujazayo moyo wake. Kwa hiyo ili tufahamu yaliyo ndani ya nafsi ya mtu, Yoshua bin Sira anatuasa kumpa kwanza nafasi ya kuongea na kujieleza, tumsikilize ndipo tumhukumu kwa haki kwa yaliyotoka kinywani mwake. Hali kadhalika kabla ya kupokea au kuunga mkono jambo, hoja au mtu, lazima tusikilize kwanza anayosema ili tuweze kutambua uzuri na ubaya wake, hapo ndipo tutakuwa sawa kuliongelea na kulipigania inapobidi. Haya yote yanawezekana kama kuna majadiliano na masikilizano. Msingi wa haya yote ni kumtumainia Mungu katika yote. Ndiyo maana mzaburi katika wimbo wa katikati anasema hivi: “Ni neno jema kumshukuru Bwana, na kuliimbia jina lako, Ee Uliye juu. Kuzitangaza rehema zako asubuhi, na uaminifu wako wakati wa usiku. Mwenye haki atasitawi kama mtende, atakua kama mwerezi wa Lebanoni. Waliopandwa katika nyumba ya Bwana, watasitawi katika nyua za Mungu wetu, watazaa matunda hadi wakati wa uzee, watajaa utomvu, watakuwa na ubichi, ili watangaze ya kuwa Bwana ni mwenye adili, Mwamba wangu, ndani yake hamna udhalimu (Zab. 91:1-2, 12-15).
Somo la pili ni la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa wakorinto (1Kor 15: 54-58). Katika somo hili Mtume Paulo anatueleza kuwa hali ya mwili wetu wa sasa ni ya kufa na kuoza. Mungu anataka tuwe katika hali hii kwa muda, ikiwa ni mapito kuiendea hali ya kutokufa, hali ya uzima wa milele. Kwa kifo na ufufuko wake, Yesu ametutayarishia hali hiyo ya kutokufa. Kwa hiyo maisha ni suala la kufa na kuishi. Tunaishi ili tufe na tunakufa ili tukaishi milele. Huu ni ukweli na uhalisia wa maisha yetu kwamba tunaishi na tutakufa na baada ya kufa tutaendelea kuishi. Lakini ili tuweze kuendelea kuishi katika hali ya utakatifu ni lazima tuwe tayari kufa kuhusu dhambi na kuishi maisha ya kitakatifu, ili tuwe na muungano na Mungu wetu aliye Mtakatifu. Kimsingi kifo ni ukweli ulio mgumu kuupokea na kuukubali. Licha ya kuwa kila siku watu wanakufa nasi tunashuhudia, lakini kifo kinabaki kuwa tishio na hofu kubwa kwa mwanadamu, maana hakizoeleki. Watu wengi hawapendi kujua wala kusikia habari za kifo, kwa kuwa hawana matumaini na imani juu ya ukweli wa maisha yajayo, maisha ya ufufuko. Mtume Paulo anasema hivi; “Ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini” (1Thes. 4:13). Ni wazi mtu akikosa tumaini la uwepo wa Mungu, anakosa thamani ya maisha ya sasa na yajayo. Lakini hata tunaoamini juu ya uwepo wa Mungu na maisha yajayo, tunakiogopa kifo. Hii ni kwa sababu ya kushindwa kuishi mausia ya kiinjili ya kukesha na kujiandaa kumpokea mjumbe wa Mungu – kifo – wakati wowote atakapokuja kutuchukua, ambaye hatujui siku wala saa ya kuja kwake. Zaidi sana hali ya kuishi katika dhambi, kuwa mbali Mungu, kukosa muunganiko na Yeye aliye mtakatifu, nayo inatufanya tuwe na hofu, mashaka na woga wa kufa.
Kifo ni matokeo ya dhambi ya asili, dhambi ya wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva ya kutotii amri na maagizo ya Mungu (Mw. 3:19). Ni ukweli kuwa kila nafsi itaonja mauti. Mtakatifu Fransisko wa Asisi anasema; “Usifiwe, ee Bwana wangu, kwa ajili ya dada yangu kifo cha mwili, ambacho hakuna mtu aishie awezaye kukikwepa. Ole wao wanaokufa katika dhambi ya mauti! Heri yao watakaokutwa ndani ya mapenzi yako matakatifu sana, kwani kifo cha pili hakitawafanyia ubaya” (KKK 1014). Baba Mtakatifu, Mtakatifu Yahane Paulo II, alisema; “Ninapata amani tele ninapofikiria kuhusu wakati, ambapo Bwana ataniita kutoka maisha kwenda maisha.” Maana yake, anapata furaha na amani tele anapofikiria siku yake ya kufa, ambapo Mungu atamwita kutoka maisha haya ya duniani kuelekea mbinguni kwenye maisha ya umilele. Mtakatifu Thereza wa Avila alisema; “Nataka kumwona Mungu, na kumwona Mungu, lazima nife.” Kumbe kifo ni sehemu ya mpangilio wa maisha yetu. Hatuwezi kikiepa. Hata hivyo hatupaswi kuwa na mashaka, tujiandae kufa vyema kwa kutambua, kujutia, kukiri na kutubu dhambi zetu, tujipatanishe na Mungu, tukubali kufa kuhusu dhambi ili tuishi katika Kristo na hivyo tutakuwa na ujasiri wa kutamka maneno ya mtume Paulo akisema; “Mimi kuishi kwangu ni Kristo na kufa ni faida” hana mashaka kabisa juu ya ujio wa kifo. Nasi pia hatupaswi kuogopa, kwani kwa kifo cha Kristo Msalabani, kifo chetu kimepata maana mpya, ambapo kwayo maisha mapya yanazaliwa, maisha ya milele mbinguni.
Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk 6: 39-45). Sehemu hii ya Injili imesheheni misemo ya hekima na busara za Yesu juu ya viongozi au walimu wanavyopaswa kuwa. Katika hali ya kawaida mwalimu anapaswa kuwa na uwezo wa kuona, kutambua, kuhukumu na kutenda vyema ili awe mfano mwema kwa wanafunzi wake. Kama mwalimu ni kipofu, yaani hawezi kuona, kusoma na kutambua alama za nyakati ili atoe maelekezo yanayostahili, ni hatari sana kwa kuwa anaweza kuwapoteza wanafunzi wake. Yesu anasisitiza umuhimu wa kuona, kusikiliza, kutambua na kuongoza kuliko kwema na sahihi. Pia anatuonya tusiwe wepesi katika kuwahumu wengine, maana hata sisi nasi tuna maboriti katika macho yetu, yaani tuna makosa, hatuko wakamilifu, tu wadhaifu, tu wadhambi mbele za Mungu na tunahitaji msamaha. Kilicho cha maana ni kuonyana na kusaidiana katika kuepuka nafasi za dhambi. Hivyo tuepuke maisha ya unafiki, tuwe wakweli na wema mbele za watu na mbele za Mungu.
Tunapojiandaa kuanza kipindi kitakatifu cha Kwaresima tukumbuke kuwa hapa duniani tu wapitaji. “Sisi ni raia wa mbinguni” (Fil. 3:20). Huko ndiko tulikotoka, kwa maana tulitoka kwa Mungu na “Mungu wetu yuko mbinguni” (Zab.115:3a), kama tulitoka kwa Mungu aliye mbinguni, basi tunapaswa kurudi mbinguni. Huku duniani tuliko ni ugenini, kama tunavyosali katika sala ya salamu Malkia, “Mama mwenye huruma, uzima tulizo na matumaini yetu salamu, tunakusihi ugenini hapa sisi wana wa Eva.” Maandiko Matakatifu yanasema: “wao walikuwa wageni na wakimbizi duniani, kama wangalikuwa wanaifikiria nchi waliyotoka zamani, wangalipata nafasi ya kurudi huko” (Ebr. 11:15). Tukumbuke daima kuwa maisha ni kufa na kuishi, tumwombe Mungu atufundishe kuzihesabu siku za maisha yetu hapa duniani na kujua kuwa ni chache ili zinapoisha tuwe tayari tumejiandaa kurudi kwetu Mbinguni. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Mungu, wewe unatupatia vitu hivi vya kutoa kwa heshima ya jina lako, na kuvihesabia kuwa sadaka ya ibada yetu ya kukutumikia. Tunakuomba hayo kwa rehema yako, ili hayo unayotujalia yatuletee mastahili, yatuletee pia tuzo”. Na katika sala baada ya Komunio anahitimisha maadhimisho ya Dominika hii akisali hivi: “Ee Bwana, baada ya kushiba sadaka iletayo wokovu, tunakuomba huruma yako; na kama unavyotulisha sakramenti hii hapa duniani, utushirikishe uzima wa milele kwa hisani yako”.
Tumsifu Yesu Kristo.