Dominika III ya Mwaka C:Wote waliokuwamo katika Sinagogi wakamkazia macho Yesu!
Na Padre Joseph Herman Luwela - Vatican.
Ni kama hawaamini wanachokiona, wanakaza macho yao wasikie atasema nini kwa andiko hilo walilojua linamuhusu Masiha peke yake… kwamba mtu waliyedhani wanamfahamu, mtoto wa Seremala masikini, hana elimu wala hela, wamemuona tangu anazaliwa na kukua, wanawafahamu hata ndugu zake, leo amejivika ukamilifu wa nabii mkubwa kama Isaya (Isa 61:1kk), kwamba Roho wa Bwana aweza kuwa juu ya kijana wa kawaida kama huyu, yaani mtoto huyu wa Maria ndiye wa kuwahubiria masikini habari njema, kutangaza uhuru wa wafungwa na uoni wa vipofu… mmh! hapana kwa kweli, ‘wote waliokuwamo katika Sinagogi, wakubwa kwa wadogo, wakamkazia macho’...
Lakini ndio ukweli, njia za Mungu sio zetu, Seremala huyu wa Nazareti ndiye Mwana wa Aliye juu, Masihi aliyetabiriwa na kungojewa kwa karne nyingi, sasa amefika tayari kutusikia na kutusikiliza, ahimidiwe Mungu milele. Nasi tunaweza kumkazia macho, sio macho makavu na mekundu, macho ya hasira na kutoamini, macho ya kiburi na dharau, tumkazie Kristo macho mema tukistaajabu makuu yanayotufikia kwa njia yake ili kujipatia furaha takatifu. Macho yetu yamuelekee Yeye katika hali zote, tumpende, tumtukuze, tumuabudu na tumsifu milele ili naye atukazie macho yake ya kibuluu yenye upole na unyofu ili macho yetu yanapogongana na macho yake tujipatie kupona. Tunapomtazama Kristo tuwakazie pia macho jirani zetu walio katika dhiki ya mwili na roho, ni wengi wanaohitaji huruma na msaada wetu. Ni jambo jema kuwapa maneno ya faraja na kutia moyo lakini ni jambo jema zaidi kuwanyoshea mkono wa kusaidia na kuwainua ili nao walisikie neno hili pamoja nasi “Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu” (Lk 4:21)
UFAFANUZI
Katika Dominika hii ya Neno la Mungu,neno linalotuunganisha,linalotukomboa na kutujenga, Mwinjili Luka anazungumza nawe “Theofilo” mtukufu (Lk 1:3, Mdo 1:1)… (Mwandishi wa Injili ya Luka na Matendo ya Mitume ni mmoja akiangazia zaidi mafundisho ya Mtakatifu Paulo kama Mtakatifu Marko anavyoangazia zaidi mafundisho ya Mtakatifu Petro, huenda pia kilikuwa kitabu kimoja kikagawanywa baadaye)… huyu Theofilo ni nani? Theos ni Mungu na Filos ni mpendwa hivi ‘Theofilo ni Mpendwa wa Mungu’, ndiye wewe unayesoma au kusikiliza tafakari hii, Mungu anakupenda sana... ulipokee neno hilo kwa uchaji, furaha. Imani kuu na matumaini zaidi shukrani ya kupendwa.
Theofilo wangu ambalo Mtakatifu Luka anakuletea, umkazie Kristo macho yako mema na umsikilize kwa makini Ezra Kuhani akikusomea madini ya Torati kutoka mimbari ya mti katika somo I (Neh 1-4a, 5-6, 8-10)… kadiri ya somo hilo mkristo yakupasa umuhimidi Bwana Mungu Mkuu ukiitikia ‘amina, amina’ pamoja na kuinua mikono yako na kuipokea faraja itokayo kwa Mungu, nanyi mkiisha kulisikia neno lake na kuliishi, msiomboleze wala msilie, mle kilichonona na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu maana siku hii ni takatifu kwa Bwana.
Furaha hii ya somo I kutoka kwa Nehemia na Ezra ipo katika kumkazia macho mema Kristo aliyepakwa mafuta kwa Roho kutuhubiria habari njema sisi masikini na katika kuushika wosia wa Mtakatifu Paulo katika somo II (1Kor 12:12-30). Paulo anatukumbusha hitaji la usawa, ushirikiano na mapendo ya kweli. Kila mmoja athaminiwe kwa mchango wake anaoutoa kwa nafasi yake kwa sababu kidogokidogo hujenga kikubwa. Kila mmoja wetu atumie karama aliyojaliwa kwa ajili ya manufaa ya familia nzima ya mwanadamu, talanta hizo zitujenge na kutuimarisha ili sote tumtumikie Mungu kwa furaha. Iondoke kwetu roho ya uchoyo, ubinafsi na mikono mifupi kusaidia.
Kama vile kiungo kimoja cha mwili kikipata shida viungo vyote huumia pamoja nacho nasi tuonje shida za wenzetu na furaha zao. Ni katika jina la huduma ya utumishi wa kimapendo ndipo tunaweza kudhihirisha ufuasi wetu kwa Kristo mbele ya dunia yote… Mkristo Kristo yupo nyumbani kwako Nazareti leo, ndani ya mtima wako, umkazie macho na kumkaribisha sababu wewe ni Theofilo, Mpendwa wake, naye anakuja kwako.