Tanzania,Ask,Mwijage:tusiwapotezee lengo la miito watoto wetu!
Na Patrick P. Tibanga- Bukoba
Katika Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Siku ya 61 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa kwa mwaka 2024 uliongozwa na kauli mbiu: “Tunaitwa kupanda mbegu za matumaini na kujenga amani.” Katika ufafanuzi wake, hasa kuhusu watu walioko katika mchakato wa safari kulingana na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi wenye misingi ya utamaduni wa kusikilizana na kutambua uwepo wa Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa, lengo kuu ni kuishi kwa haki, amani na upendo. Na kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Sala kwa ajili ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025 Papa Francisko alikazia kusema kuwa sala ndiyo nguvu na ufunguo wa malengo ya matumaini.
Kwa njia hiyo Waamini ni mahujaji wa matumaini na wajenzi wa amani na kwamba, lengo kuu la safari ya maisha ni kuishi kwa haki, amani na upendo na kwamba, lengo na wito ni kuwa mashuhuda wa Injili ya matumaini kama sehemu ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu, kwa kutoa kipaumbele kwa Kristo Yesu na Kanisa lake; umoja, amani na udugu. Kila mwamini ajitahidi kugundua wito wake sahihi katika Kanisa na Ulimwengu, kwa kuwa muhujaji wa matumaini na wajenzi wa amani.
Ni katika muktadha huo wa kuombea miito ambapo Askofu Jovitus Mwijage Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba nchini Tanzania, aliongoza Ibada ya Misa Takatifu katika Seminari Ndogo ya Mtakatifu Mtakatifu Don Bosco huko Rutabo, tarehe 17 Agosti 2024 katika fursa ya kiutamaduni ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania(WAWATA) kuwategemeza iitwayo pia(kunyonyeha)wanafunzi wa Seminari ndogo hiyo. Katika mahubiri yake, aliwaomba wawaombee vijana wa Seminari ili kuweza kubaki katika njia kuu na kuufikia wito wa Upadre bila kupoteza lengo na kuwaombea Mapadre waweze kudumu daima katika viapo vyao walivyovitoa.
Askofu Mwijage alisema kuwa kumuandaa Padre inachukua muda mrefu na ndani ya muda huo kuna mengi ambayo mtu anaweza kukutana nayo ikiwemo marafiki wabaya, washauri wabaya na baadhi ni ndugu ambao wamtafanya kijana ili aachane na wito huo wa Upadre. “Wapendwa sote tuliofika hapa tumekuja kuleta ukarimu wetu ninawaomba tuwaombee watoto hawa waendelee mbele ili wasipoteze lengo na kutoka nje ya reli, sababu kumuandaa padre ili afikie wito huo ni muda mrefu na humo anaweza akakutana na mengi ikiwemo marafiki wabaya, washauri wabaya na hata wakati mwingine wakiwemo ndugu au wazazi wake.” Alisema Askofu Jovitus Mwijage katika homilia.
Askofu Mwijage katika kudadavua Injili iliyosomwa alisema kuwa Sakramenti ya Ekaristi inamshibisha mkristo roho na mwili na iwapo muumini akishiba kiroho inakua ni utajiri mkubwa na hivyo kuwasihi waseminari hao kujishikiza kwa Kristo maana yeye ndiye njia ya kweli na uzima.
“Mtu akishiba kiroho inakuwa ni utajiri mkubwa lakini watu huangalia vitu vya nje, hivyo ninawaomba wakina mama na wafadhili wote tusiwaondoe watoto wetu katika miito kwa sababu nimekwisha kuwaona wengi, huku wanamtia moyo, lakini wakiwa pembeni wanamshawishi, hata mimi niliyasikia, hivyo ninawaomba wakina mama na wote mnaotusaidia msiwaondoe watoto wetu katika miito yao,” alisisitiza Askofu Mwijage.
Mkuu wa Kanisa la Bukoba akiendelea alisema “Naomba watoto wangu mjishikize kwa Kristo na kuwa matawi yake kweli hamtopata shida lakini msipojishikiza kwake mtashindwa, na tuwaombee ili shetani asije kujigamba kuwa rafiki yao.” Askofu Mwijage katika homilia yake kadhalika aliwataka waamini kuwaombea Mapadre ili wadumu katika wito na kushika kikamilifu viapo vyao na kuendelea kulichunga taifa la Mungu na kuwaonesha waamini njia ya kwenda kwa Kristo na kuwa mfano bora katika familia, mitaa na Kanisa Katoliki.
Kwa kuhitimisha Askofu Mwijage aliwaalika watoto kujishikiza kwa Kristo maana yeye ndiye ya kweli na uzima na kuwa matawi yake na tuwaombee kubeba sura ya Kristo katika maisha yao na sura hiyo iwavute watu wengine wanaowatazama kwenda wa Kristo. “Tunaponyonyesha leo na kuombea miito tuwaombee mapadre wetu washike viapo vyao na kuendelea kuwa mifano mizuri ya kulichunga taifa la Mungu, nao watuoneshe njia ya kwenda kwa Kristo na yale yote yanayoonekana nje ndiyo yawe ndani mwetu na naomba yawe mfano mzuri katika mitaa, familia jumuiya na Kanisa lote kwa ujumla maana mapadre tumebeba dhamana kubwa katika vyombo vya udongo.”
Katika risala iliyosomwa na Katibu WAWATA Jimbo Katoliki Bukoba, Mama Fides Mwijage alibainisha mafanikio waliyoyapata kwa muda wa miaka 15 tangu kuwategemeza waseminari hao na kubainisha mafanikio yafuatayo. Katika hayo ni pamoja na “Kupanda miti miche 80 ya maparachichi Hass katika kiwanja cha WAWATA huko Kashura; kupata hati miliki ya kituo cha watoto “mtoto Semillero ya Consolatha” kilichopo Parokia ya Mtakatifu Agostino wa Hippo huko Buyango; kufundisha dini katika vigango na elimu dini shuleni; kuwa na mradi wa kununua na kuuza vitenge vya WAWATA;kukamilisha ujenzi wa jengo la kiwanda cha kukoboa, kusaga na kufungasha chakula cha mifugo; kuwalea watoto wa Semillero kwa kuwafadhili chakula, sare na baadhi ya vifaa vya darasani.”
Pamoja na hayo pia kila mwaka Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) Jimbo Katoliki Bukoba, hushiriki katika kuhamasisha miito na kuwategemeza wanafunzi wa Seminari Ndogo ya Mtakatifu Don Bosco iliyopo katika Parokia ya Mtakatifu Yosefu, Rutabo na tangu mwaka 2021 wamekuwa wakijivunia kupata mapadre waliowaandaa tangu miaka 15 iliyopita. Na Seminari hiyo kwa njia hiyo inahudumia wanafunzi kuanzia darasa la 5 mpaka darasa la 7.