杏MAP导航

Tafuta

2024.07.01 Korea Kusini 2024.07.01 Korea Kusini 

Korea,WCC:Tuombee upatanisho wa Korea Kaskazini na Kusini na kamwe tusikubali migawanyiko

Baraza la Kiekumene la Makanisa Ulimwenguni (WCC)linaomba kusali kwa ajili ya upatanisho kati ya Korea Kaskazini na Kusini tarehe 11 Agosti.Sala hiyo kiutamaduni ni kila mwaka kabla ya tarehe 15 Agosti.Uchaguzi wa tarehe hiyo inakumbusha hafla ya kusherehekea ukombozi wa Korea kutoka utawala wa Kijapani 1945.Hata hivyo ulipelekea mgawanyiko wa Nchi mbili.

Na Angella Rwezala -Vatican

Hatutakata tamaa ndiyo  kauli mbiu  ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni ikiaalika udugu wa kimataifa na watu wote wenye mapenzi mema kuungana pamoja, Dominika tarehe 11 Agosti 2024  ili kusali kwa ajili ya amani na upatanisho wa Nchi Mbili za Korea. Kwa kuhimizwa na Baraza la Kitaifa la Makanisa nchini Korea na Shirikisho la Kikristo la Korea, sala hiyo hufanyika kila mwaka,  ifikapo Dominika kabla ya Agosti 15. Uchaguzi wa tarehe hiyo sio kwa  bahati nasibu,  bali inaangukia kwenye hafla ya kusherehekea ukombozi wa Korea kutoka  utawala wa Kijapani mnamo 1945, ambayo hata hivyo iliashiria mgawanyiko wa eneo katika maeneo mawili tofauti na kugeuka kuwa nchi mbili.

Kwa nini sala ya upatanisho wa Korea Mbili?

Mgawanyiko ulioidhinishwa na sheria ya kusitisha mapigano ambayo ilikomesha Vita vya umwagaji damu vya Korea mnamo 27 Julai 1953 na ambayo bado ni jeraha wazi. Katika sala yao inasomeka kuwa: “Inaonekana kama jana tuliposhikana mikono na kupita kwenye ukuta huu ambao umesimama hapa kwa muda mrefu, na sasa tunaitana maadui badala ya watoto wa Mungu. Tulishiriki uhusiano wetu sisi kwa sisi tulipokuwa tumejawa  na tumaini,  sasa yamevunjika,na kashfa tu na woga unakuja  na kuondoka katika mawimbi ya upepo juu yetu.” Katika sala hiyo aidha inakumbusha machungu ya Wakorea kwa “jeraha la mgawanyiko” lililosababishwa na itikadi zilizopanda chuki na ambazo bado leo zimechochewa na nguvu, zikiwemo za nje, “zinazozuia hatua za kuelekea amani.

Mungu awasaidie wote kushinda mizozo ya kiitikadi

Kwa njia hiyo basi ombi kwa Mwenyezi Mungu awasaidie Wakorea wote kushinda mizozo ya kiitikadi “kwa upendo wa Kristo, kushinda nguvu za uovu zinazozuia njia ya amani na kuyapa Makanisa ya Korea nguvu na ujasiri wa kuongoza njia ya kuelekea amani na upatanisho. Sala hiyo inaishia kwa kuzungumza juu ya amani na kuunganishwa kwa peninsula “sio kama chaguo” lakini kama lengo ambalo Wakorea wameitwa kutimiza. “Tukumbuke kwamba roho zetu na mioyo yetu imeunganishwa katika Bwana,” Inahitimishwa.

Pillay:WCC inasalia na nia ya dhati ya kuunga mkono viongozi

Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, Mchungaji Jerry Pillay, alisisitiza dhamira ya chombo cha kiekumene kwa Makanisa yanayofanya kazi kwa ajili ya amani katika Peninsula ya Korea: “WCC inasalia na nia ya dhati ya kuunga mkono uongozi baina ya Korea kwa ajili ya amani na kuunganishwa tena kwa watu waliogawanyika. Pillay aliomba “Makanisa duniani kote na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kuyasindikiza Makanisa ya Korea kwa kusali na kutenda kwa ajili ya amani na kuungana tena”. Upatanisho wa taifa pia ni mada kuu ya Kanisa Katoliki nchini Korea Kusini ambalo mwaka 1995 lilianzisha Tume maalum ya Maaskofu kwa ajili hiyo.

Mipango iliyoandaliwa awali kwa miaka mingi

Miongoni mwa mipango mingi iliyoandaliwa kwa miaka mingi, misa ya maombi na novena (pamoja na mambo mengine, tunakumbuka Jubilei ya upatanisho wa kitaifa huko Chunchon iliyoadhimishwa Juni 2000), misaada iliyotolewa kwa wakazi wa Korea Kaskazini walioathiriwa na njaa kali katika miaka ya 1990 na kazi ya ufahamu na habari inayowalenga waamini juu ya mada ya kuungana tena. Zaidi ya hayo, Maaskofu daima wamekuwa wakitetea sababu ya upatanisho na serikali mbili, hasa wakati wa mvutano mkubwa kati ya Seoul na Pyongyang. Sala ya upatanisho na amani pia ilikuwa moja ya mambo muhimu ya Ziara ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka 2014 katika Jamhuri ya Korea na Maadhimisho ya Siku ya VI ya Vijana wa Asia.

06 Agosti 2024, 16:39