杏MAP导航

Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Sita ya Kipindi cha Pasaka Mwaka A: Kuzishika amri za Yesu ni alama ya kumpenda; upendo unaomwilishwa katika Injili ya huduma! Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Sita ya Kipindi cha Pasaka Mwaka A: Kuzishika amri za Yesu ni alama ya kumpenda; upendo unaomwilishwa katika Injili ya huduma! 

Tafakari Dominika VI ya Kipindi cha Pasaka: Upendo Ni Utambulisho wa Kikristo!

Dhamira ya masomo ya dominika hii imebebwa na ahadi ya Yesu aliyowapa Mitume; “Mkinipenda mtazishika amri zangu, nami nitamwomba Baba naye atawapa msaidizi mwingine ili akaye nanyi milele; ndiye roho wa ukweli atakayewaongoza katika kweli yote.” Wimbo wa mwanzo ni mwaliko wa kuhubiri kwa sauti ya kuimba, kutangaza kuwa Bwana amelikomboa taifa lake, na haya tuyatamke mpaka mwisho wa dunia, tukisema, aleluya – yaani msifuni Bwana!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 6 ya Kipindi cha Pasaka Mwaka A. Kipindi cha Pasaka kipo ukingoni. Dominika tarehe 21 Mei 2023 tutaadhimisha Sherehe ya kupaa Bwana mbinguni na Dominika itakayofuata yaani tarehe 28 Mei 2023 ni sherehe ya Pentekoste inayofunga wiki saba za Kipindi cha Pasaka. Ndiyo maana dhamira ya masomo ya dominika hii imebebwa na ahadi ya Yesu aliyowapa Mitume; “Mkinipenda mtazishika amri zangu, nami nitamwomba Baba naye atawapa msaidizi mwingine ili akaye nanyi milele; ndiye roho wa ukweli atakayewaongoza katika kweli yote.” Wimbo wa mwanzo ni mwaliko wa kuhubiri kwa sauti ya kuimba, kutangaza kuwa Bwana amelikomboa taifa lake, na haya tuyatamke mpaka mwisho wa dunia, tukisema, aleluya – yaani msifuni Bwana (Isa. 48:20). Sala ya mwanzo inakazia na kusema; “Ee Mungu Mwenyezi, utuwezeshe kuadhimisha kwa bidii siku hizi za furaha, tunazozitumaini kwa heshima ya Bwana aliyefufuka. Na hayo tunayoyakumbuka sasa, tuyazingatie daima kwa matendo”. Somo la kwanza ni la kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 8: 5-8, 14-17). Somo hili limegawanyika katika sehemu kuu mbili zinazotueleza jinsi Imani ya kikristo ilivyoanza Yerusalemu, kisha ikaenezwa ulimwenguni kote. Mungu alithibitisha imani hiyo kwa miujiza. Wakristo wote wameunganika katika Kristo, sababu wote wamepata zawadi moja ile ile, yaani Roho Mtakatifu. Zaidi sana linawaonesha mitume wakihubiri injili kwa nguvu ya Roho Mtakatifu na kuwashushia wale waliobatizwa Roho huyu.

Injili ya Upendo inayomwilishwa katika huduma na unyenyekevu
Injili ya Upendo inayomwilishwa katika huduma na unyenyekevu

Sehemu ya kwanza inatukumbukwa kuwa baada ya kifo cha Stephano kilichoshuhudiwa na Paulo, kulikuwa na madhulumu makali Yerusalemu dhidi ya Kanisa hasa kwa Wakristo Wayunani. Madhulumu haya yaliwafanya wakristo wayunani kwenda maeneo ya mbali hasa Siria na Antiokia na huko wakaunda jumuiya hai ya wakristo. Antiokia ndipo kwa mara ya kwanza waliitwa wakristo (Mdo 11:26). Shemasi Filipo, alichaguliwa kusimamia ugawaji wa mahitaji ya jumuiya ya Yerusalemu lakini roho wa Bwana alikuwa na mipango tofauti naye; alikimbilia Samaria akawa mhubiri na akaeneza injili kati ya wasamaria nao wakaipokea imani licha ya kuwa walionekana kama wazushi na walichukiana na wayahudi wa Yerusalemu. Mbele ya Yesu mfufuka chuki ni mwiko. Kwa hiyo tunaona kuwa Yesu akifanya kazi kwa njia ya roho wake; kati ya wakristo waliokuwa wametawanyika kwa sababu ya madhulumu. Sehemu ya pili ya somo hili inahusu kutumwa kwa Petro na Yohane kwa wasamaria walioipokea imani. Paulo katika barua yake kwa wagalatia anawaita nguzo mbili za kanisa; “Basi, Yakobo, Kefa na Yohane, walionekana kama nguzo za kanisa, walitupa mkono wa shirika, mimi na Barnaba walipotambua ile neema niliyopewa. Wakakubali kwamba sisi tuende kwa watu Mataifa na wao waende kwa Wayahudi” (Gal. 2:9). Kumbe Petro na Yohane walitumwa kwenda kukamilisha kazi iliyofanywa na Filipo yaani kuwawekea mikono wabatizwa ili wampokee Roho Mtakatifu – kama ilivyo kwa Sakramenti ya Kipaimara inapotolewa na Askofu. Ndiyo maana Luka anasema; “Roho Mtakatifu alikuwa bado hajawashukia, walikuwa wamebatizwa kwa jina la Bwana Yesu. Kisha wakawawekea mikono, wakampokea Roho Mtakatifu” (Mdo 8:16-17).

Roho wa kweli atawaongoza katika ukweli wote.
Roho wa kweli atawaongoza katika ukweli wote.

Somo la pili ni la waraka wa Mtume Petro kwa Watu Wote (1Pet. 3:15-18). Somo hili laeleza kwamba kuna ugumu mwingi katika kumfuata Yesu. Lakini Yeye ametuonyesha wazi ya kuwa mateso na masumbufu ya maisha ni njia ya kupata utukufu. Basi yatupasa kuvumilia magumu yote kwa ajili ya imani katika Yesu aliyefufuka. Mtume Petro anasisitiza kuwa waliompokea Roho Mtakatifu wapo tayari kuteseka kwa ajili ya Kristo maana roho huyu anawaimarisha. Hapa Mtume Petro anawatia moyo wakristo waliokuwa wanapatwa na madhulumu kwa sababu ya imani yao akiwaasa watambue kuwa Kristo yupo pamoja nao, yupo ndani yao kwa njia ya roho wake akiwaimarisha. Hivyo madhulumu haya hayaelekezwi kwao tu bali pia kwa Kristo. Hivyo wanapaswa kufurahi kwamba wanapatwa na madhulumu hayo kwa niaba ya Kristo na wakiyapokea kwa Imani yanakuwa kama njia ya kupata utukufu. Hivyo wasilipe ovu kwa ovu bali wawatendee watesi wao kwa upole na upendo (1Pet 3:13). Somo hili linatuasa nasi kutoa ushuhuda wa imani na wa matumaini kwanza kwa njia ya maisha mema na ukarimu kwa watu wote hata kwa adui zetu. Kuwa wapole na wakarimu kwa wale wanaotudhulumu. Hii itawasaidia wao taratibu wautambue ukweli wa injili ili nao waweze kumpokea Kristo na kuongoka. Zaidi sana kuchukulia mateso ya Yesu kama baraka; kukubali kuteseka kwa ajili ya haki kama alivyoteseka Yesu kwa ajili yetu. Maana tukishiriki mateso yake tutashiriki pia utukufu wake.

Njia ya Msalaba ni kushiriki pia mateso hadi kifo cha Msalaba.
Njia ya Msalaba ni kushiriki pia mateso hadi kifo cha Msalaba.

Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 14:15-21). Sehemu hii ya Injili ni sehemu ya mazungumzo kati ya Yesu na wanafunzi wake baada ya karamu ya mwisho nayo inatueleza kuwa  kuzishika amri za Yesu ni alama ya kumpenda. Katika mazungumzo haya Yesu anaendelea kuwaimarisha mitume wake kiimani akisema; “Mioyo yenu isifadhaike” (Yn 14:1) kwa sababu ni kitambo kidogo hatakuwa pamoja nao lakini yupo pamoja nao kwani yeye sasa hafungwi na sheria za kimaumbile ndiyo maana anasema; sitawaacha yatima, naja kwenu (Yn 14:18). Hivyo wanapaswa kujifunza na kuzoea kutomwona, lakini wajisikie na kuamini kuwa yupo pamoja nao kwa njia ya roho mtakatifu, roho wake atakayemtuma kuwaangazia, kuwaimarisha na kuwalinda kwa jina lake. Katika maisha ya kawaida mtu akiona amekaribia kufa anatoa waosia. Kama ni mzazi atawaita watoto wake na kuwapa wosia. Anaweza kuwaambia: ukitaka kufanikiwa katika maisha ishi vizuri na watu, usiwe mwepesi wa kugombana na watu, ishi kwa amani na uelewano na watu. Isitoshe fanya kazi kwa bidii, tumia nguvu, akili na vipaji alivyokujalia Mungu na katika kufanya kazi na zaidi ya hayo usimsahau Mungu wako. Mtangulize katika shughuli zako zote ili abariki mipango yako na kufanikisha kazi zako. Yesu pia kabla ya kupaa mbinguni aliwapa wanafunzi wake wosia. Aliwaambia pendaneni kama mimi nilivyowapenda ninyi. Hakuna upendo ulio mkuu zaidi ya ule wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo zake. Mkipendana mtakuwa kweli wanafunzi wangu. Kumbe upendo ndiyo utambulisho wetu kama wakristo na ni kipimo cha kuurithi ufalme wa mbinguni.

Upendo wa Kristo Yesu unatubidiisha kushiriki matendo ya huruma
Upendo wa Kristo Yesu unatubidiisha kushiriki matendo ya huruma

Tukumbuke kuwa ujumbe wa Yesu katika Injili sio simulizi la yaliyokwisha kupitwa na wakati. Yesu anaendelea kurudia mawaidha yake kwetu kila mara linaposomwa Neno lake, zinapoadhimishwa Sakramenti zake maana kila inapoadhimishwa Sakramenti yoyote ni Kristo Yesu mwenyewe yupo katika nafsi ya mwadhimishaji akitujalia neema na baraka zake. Kumbe yeyote mwenye kupokea na kusadiki ukweli huu atapendwa na Mungu Baba, na kwa njia ya kifo na ufufuko wa Yesu, atapewa uzima wa milele. Sehemu hii ya Injili inatupa masharti ya kumpokea Roho Mtakatifu; Kumpenda Yesu na kuzishika amri zake hivyo tunajazwa nguvu za kumshuhudia Kristo katika maisha yetu ili baadae tukafurahi naye milele yote mbinguni kama inavyoashiria sala baada ya komunyo ikisema; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, wewe watuponya kwa kufufuka kwake Kristo ili tupate uzima wa milele. Utuzidishie neema za fumbo la Pasaka, na kutujaza mioyoni mwetu nguvu ya chakula hiki cha wokovu." Tumsifu Yesu Kristo!

Dominika ya Sita
11 Mei 2023, 11:22