杏MAP导航

Tafuta

Walimtambua Kristo Mfufuka wakati wa kuumega mkate! Walimtambua Kristo Mfufuka wakati wa kuumega mkate! 

Tafakari Neno la Mungu Dominika ya III Pasaka Mwaka A: Kuumega Mkate: Ekaristi

Dominika ya tatu ya Pasaka inatupa Injili juu wafuasi wa Emau. Baada ya Yesu kufa na kuzikwa, wafuasi hawa wawili wanaachana na kundi la wenzao na wanaamua kurudi nyumbani. Wakiwa njiani Yesu mfufuka anawatokea, anaongozana nao na katika mazungumzo kama msafiri mwenzao anakuwa anawafafanulia Maandiko lakini wao hawamtambui. Wanafika nyumbani, wanamkaribisha na walipokuwa wanakula, katika kuumega mkate ndipo wanatambua kuwa ni Yesu.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News dominika ya tatu ya Pasaka inatupa Injili juu wafuasi wa Emau (Lk 24:13-35). Baada ya Yesu kufa na kuzikwa, wafuasi hawa wawili wanaachana na kundi la wafuasi wenzao na wanaamua kurudi nyumbani. Wakiwa njiani Yesu mfufuka anawatokea, anaongozana nao na katika mazungumzo kama msafiri mwenzao anakuwa anawafafanulia Maandiko lakini wao hawamtambui. Wanafika nyumbani, wanamkaribisha na walipokuwa wanakula, katika kuumega mkate ndipo wanatambua kuwa ni Yesu. Hili ndilo somo tutakalokwenda kulitafakari katika kipindi chetu cha leo, lakini kwanza tutayapitia masomo mawili yanayotangulia somo hili la Injili, yaani somo la kwanza kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 2:14, 22-33) na somo la pili kutoka Waraka wa kwanza wa Mtume Petro kwa Watu Wote (1Pet 1:17-21). Ufafanuzi wa Masomo kwa Ufupi: Somo la kwanza ni sehemu ya hotuba ambayo mtume Petro aliyatoa siku ya Pentekoste. Halitupatii hotuba yote bali linaweka msisitizo pale Mtume Petro anapoonesha kuwa kifo cha Yesu kilikuwa ni mpango wa Mungu wa kumkomboa mwanadamu. Hakikuwa kifo cha ajali au kama cha mtu aliyekuwa bado na mipango ya kutekeleza halafu kifo kikamkuta na kukatisha mipango yake. Yeye alipaswa kufa namna hiyo ili akamilishe ukombozi wa mwanadamu na ulimwengu mzima. Petro analithibitisha hilo kwa kuonesha kuwa Maandiko Matakatifu yalikuwa tayari yamekwishazungumzia habari za kifo na ufufuko wa Yesu miaka mingi sana kabla hata Yesu mwenyewe hajaja duniani.

Mitume walitangaza na kushuhudia: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu
Mitume walitangaza na kushuhudia: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu

Ananukuu Zaburi ya 16 inayosema “nimemweka Bwana mbele yangu daima, kwa hiyo moyo wangu utafurahi na mwili wangu utakaa katika matumaini kwa maana hutaiacha nafsi yangu katika kuzimu wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu”. Zaburi hii ambayo kwa miaka mingi waliitumia Walawi kama sala ya kujikabidhi kwa Mungu, Petro leo anayafafanua maneno yake akionesha kuwa ni Zaburi inayomlenga Kristo. Ni Kristo aliyetabiriwa katika Zaburi hii kuwa ndiye atakayemweka Mungu mbele daima na Mungu huyo hataiacha nafsi yake kuzimuni, mahala pa wafu bali atamtoa yeye aliye matakatifu wake ili mwili wake usione uharibifu, yaani atamfufua. Anachokifanya Petro kimebaki katika Kanisa Katoliki kama mojawapo ya msingi wa usomaji na ufafanuzi wa Maandiko Matakatifu, kwamba Biblia inapata maana yake halisi inaposomwa na kutafsiriwa ikimlenga Kristo. Agano la Kale katika vitabu vyake vyote haliwezi kuelezeka wala kufafanuliwa katika undani wake bila kumwona Kristo kama kilele cha ufufunuo linaoubeba. Somo la pili, ambalo ni waraka wa huyo huyo mtume Petro, fundisho alaloliandika ni lile lile alilolihubiri siku ya Pentekoste. Hapa anafafanua mambo mawili makubwa. Jambo la kwanza anasema kifo cha Yesu ni sadaka, na ni sadaka ya ukombozi. Anawahubiria watu ambao sadaka pekee ya ukombozi waliyokuwa wanaifahamu ni ile ya mwanakondoo aliyechinjwa wakati wakiwa Misri na wakapaka damu yake kwenye mihimili ya milango yao. Petro anasisitiza kusema kuwa kitendo cha Kristo kufa msalabani, ni Yeye amekuwa mwanakondoo mpya aliyemwaga damu yake tena yenye thamani kuliko vitu viharibikavyo kama fedha na dhahabu na zaidi hata ya damu ya mwanakondoo iliyomwagwa zamani za utumwa wa Misri. Jambo la pili analolikazia Petro katika somo hili ni lile lile tulilosikia katika somo la kwanza, anarudia kusema kuwa yote haya yaliyomtokea Kristo yalikuwa yametabiriwa, kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu.

Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ni Utimilifu wa Maandiko.
Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu ni Utimilifu wa Maandiko.

Tafakari ya somo la Injili: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tunapenda kuichota tafakari ya dominika hii ya tatu ya Pasaka kukoka katika somo la Injili ambayo tulikwisha dokeza hapo mwanzo kuwa inahusu habari ya wafuasi wa Emau. Hawa hawakuwa miongoni wa mitume wa Yesu bali walikuwa ni miongoni mwa wafuasi. Mtakatifu Sirilo wa Aleksandria aliyeishi karne ya 4 anaeleza kuwa walikuwa ni miongoni mwa wale 70 ambao Yesu aliwatuma wawili wawili wakahubiri. Ni nini kiini cha habari hii? Kiini cha habari hii ni kuwa baada ya kifo cha Yesu, wafuasi hawa walikata tamaa. Matumaini yote waliyokuwa wameyaweka kwa Yesu yaliyeyuka. Hawakukipata kile walichokuwa wanakitegemea. Kwa sababu hiyo wanaamua kurudi nyumbani, wanaamua kurudi katika ile hali ya maisha waliyokuwa nayo mwanzo kama watu wanaoona kuwa ule muda walioutumia kumfuasa Yesu ni muda waliouoteza. Kwa nafsi ya wafuasi hawa, Injili inazungumza nasi ambao si mara chache tunauona namna hii ukristo wetu na hata utumishi wetu. Ukristo unapoonekana haujibu mategemeo yetu, wengi wetu tunarudi nyuma tulikotoka. Kinachotokea ni kwamba Yesu mfufuka anawatokea. Wao walikwisha sikia habari kuwa amefufuka lakini kwa sababu ya uchungu au hata na hasira waliokuwa nayo kuona mambo yameenda kombo, hawakuamini. Wanaanza kuzungumza pamoja na tena wanamshangaa kwamba hajui kilichotokea.

Mitume ni mashuhuda wa Ufufuko wa Kristo Yesu
Mitume ni mashuhuda wa Ufufuko wa Kristo Yesu

Yesu hawaachi kamwe wale aliowachagua akawatia alama yake ya ubatizo. Hata pale wanapoamua kurudi nyuma, wanapomkana, wanapomweka pembeni, Yeye huwatafuta huwafikia na huendelea kuongozana nao katika njia ya maisha kama alivyofanya kwa hawa wafuasi wa Emau. Na inatokea mara nyingi mtu wa namna hii anazidi kupiga kelele na kulalama “Mungu ameniacha, Mungu hanikumbuki tena” wakati Mungu yuko pembeni yake akimsindikiza katika njia ya maisha. Uchungu unapokuwa mkubwa kuliko maumivu yenyewe anayenyoosha mkono kusaidia anaweza kuonekana adui. Yesu hawakujitambulisha kwa wafuasi wa Emau kuwa ni nani. Yeye aliendelea kuwafafanulia Maandiko. Na ndivyo anavyofanya hadi leo. Ni wapi hali inabadilika? Hali ya wafuasi inaanza kubadilika pale wanapomkaribisha Yesu nyumbani. Wanambwambia “kaa nasi maana usiku umeingia”. Maneno hayo ambayo ni ya kawaida kabisa kwa kumkirimu mgeni, kwao lakini yanakuwa ni kama ufunguo wa kufungua mioyo yao iliyojikunja wa kukata tamaa na usiku wanaoonekana kuuongelea sio wa nje bali ni wa ndani ya mioyo hiyo. Tunaliona hili kwa sababu walipomtambua tu Yesu hawakujali tena kuwa ni usiku, bali waliondoka muda huo huo na kurudi kwa wafuasi wenzao kuwasimulia kilichotokea. Yesu anapokaribishwa hakatai. Aliingia ndani, akaketi chakulani na walipokuwa wakila akajifunua kwao katika kuumega mkate. Neno hili “kuumega mkate”limebaki katika Kanisa liliashiria adhimisho la Misa Takatifu, adhimisho la Ekaristi Takatifu. Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, somo hili la Injili ya leo liwe msaada kwetu katika kuiimarisha imani yetu. Hata leo, Yesu anaambatana nasi katika mabonde na milima ya maisha yetu ya imani. Tuichote faraja ya uwepo wake katika Neno lake na katika maisha ya Sakramenti. Humo ndimo anapoendelea kutuonesha kuwa yuko nasi daima.

Liturujia D3
21 Aprili 2023, 16:14