杏MAP导航

Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 25 ya Mwaka C wa Kanisa: Mali, madaraka na uaminifu kwa Mungu na jirani. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya 25 ya Mwaka C wa Kanisa: Mali, madaraka na uaminifu kwa Mungu na jirani. 

Tafakari Dominika 25 Mwaka C wa Kanisa: Mali, Madaraka Na Uaminifu Kwa Mungu na Jirani

Leo tunayatafakari masomo ya dominika ya 25 ya mwaka C wa Kanisa. Tunaupokea mwaliko wa Kristo anayetuambia “hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili ... Mungu na mali.” Tukiongozwa na maneno haya tunakwenda kuyapitia masomo yote ili kuona kile ambacho Neno la Mungu linatufundisha katika dominika hii yaani: Mali, Madaraka na Uaminifu kwa Mungu.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu ambapo kwa siku ya leo tunayatafakari masomo ya dominika ya 25 ya mwaka C wa Kanisa. Tunaupokea mwaliko wa Kristo anayetuambia “hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili ... Mungu na mali.” Tukiongozwa na maneno haya tunakwenda kuyapitia masomo yote matatu ili kuona kile ambacho Neno la Mungu linatufundisha katika dominika hii ya 25. ufafanuzi wa masomo: Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha Nabii Amos (Amo 8:4-7). Katika kipindi cha nabii Amos, taifa la Israeli lilikuwa limestawi sana kiuchumi. Kwa bahati mbaya ustawi huu wa kiuchumi haukwenda sambamba na ustawi wa imani na ibada. Kitu pekee wengi walichokuwa wakiwaza ni biashara na namna ya kujiongezea faida na matokeo yake ni kuwa maisha yalistawi lakini thamani au ubora wa maisha yenyewe ukashuka. Kuliongezeka unyonyaji na unyanyasaji hasa kwa watu wa tabaka la chini na katika imani, zile ibada na mambo waliyokuwa wamezoea kuyafanya kwa furaha kwa ajili ya kumtukuza Mungu zilianza kuonekana ni mzigo kwao. Kulikuwa na sikukuu ya kidini ya mwezi mpya pamoja na siku ya sabato ambapo hawakuruhusiwa kufanya kazi ili waweze kushiriki vema maadhimisho yake. Hizi walitamani ziishe upesi ili warudi kwenye biashara zao. Katika somo tunasikia wanasema “hivi mwezi mpya utaisha lini tupate kuuza nafaka, na sabato nayo tupate kuanika ngano.”

Maendeleo ya vitu yasimikwe katika kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu
Maendeleo ya vitu yasimikwe katika kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu

Katika somo hili, Nabii Amos anachofanya ni kuwapa watu angalisho. Ni kama anawaambia “angalieni njia hii inawapeleka wapi”! Bila kubeza umuhimu wa utafutaji wa mali, nabii Amos anawatahadharisha waisraeli na kututahadharisha sisi pia leo kuwa unaweza kuwa kikwazo  katika maisha ya imani na pale unapopitiliza unaweza kudhoofisha hadhi ya utu badala ya kuuboresha. Tukiingia katika somo la pili (1 Tim 2:1-8), tunaupokea mwaliko wa mtume Paulo, mwaliko wa kusali kwa ajili ya kuwaombea watu wote. Paulo anaweka msitizo wa pekee katika kuwaombea viongozi na wenye mamlaka. Katika mazingira ya kihistoria ambapo ukristo ulionekana kuwa adui wa watawala hasa kwa dola ya Kirumi, Mtume Paulo anakuja kutuonesha kuwa kuwa ukristo si adui wa viongozi na watawala. Ukristo ni adui wa uovu  na huo ndio inaoupinga bila kujishikamanisha na upande wowote wa kiitikadi. Katika dominika hii ambapo tunapewa tahadhari juu ya hatari ya kutumikia mali, ombi hili la Paulo linabeba maana nyingine zaidi. Linatuonesha kuwa viongozi na watawala wapo pia katika hatari hiyo ya kujikuta wanamtumikia “bwana” mwingine ambaye si wananchi au si kwa mafaa ya wale waliokabidhiwa. Tunahitaji kuwaombea ili Mungu aziweke hai daima dhamiri zao na awaangazie ili kama anavyosema mtume Paulo “tuishi maisha ya utulivu na amani katika utauwa na ustahivu.”

Tunafika sasa katika Injili (Lk 16:1-13) Yesu anatoa mfano wa wakili mjanja. Tungeweza kumuita meneja au msimamizi wa mradi. Mtu huyu alishindwa kusimamia vema mradi aliokabidhiwa na matokeo yake mwenye mradi akamfukuza kazi. Yeye kabla watu hawajajua kama amefukuzwa kazi, akaenda kuwatafuta waliokuwa wateja wa ule mradi ule, akawapunguzia madeni yao. Alifanya hivyo ili ajenge nao urafiki ili baadaye wao nao waweza kuja kumsaidia kama kulipa fadhila. Mfano huu wa Yesu unashangaza kidogo. Yesu anaonekana kutupa fundisho kutoka kwa mfano mbaya wa mtu anayejitafutia urafiki kwa mali ya udhalimu. Na unazidi kushangaza hasa pale ambapo tunasikia msimamizi huyu anasifiwa kwa ujanja wake. Mojawapo ya namna ya kuutafsiri mfano huu ni kuuangalia katika wigo mpana wa Injili ya Luka. Mfano huu ni mmoja kati ya mifano mitatu ambayo Yesu anaitoa kwa mfululizo katika injili ya Luka. Wa kwanza ni ule wa mwana mpotevu tulioutafakari dominika ya 24 ya Mwaka C wa Kanisa, wa pili ni huu na wa tatu ni wa tajiri na Lazaro tutakaoutafakari dominika ya ishirini na sita.

Mali itumike kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi
Mali itumike kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Mifano hii yote mitatu inahusu mali ikionesha namna ambayo mfuasi wa Kristo anapaswa kuishi kuhusiana na mali. Mwana mpotevu alichukua urithi wake akaenda kuutapanya mbali na nyumbani, tajiri wa kwenye mfano wa Lazaro alizitumia mali zake bila kujali jirani yake mwenye shida. Katika muktadha wa mifano hiyo na wa liturujia ya dominika hii mfano wa wakili unakuja kutupa tahadhari juu ya matumizi ya mali na madaraka. Wakili tunayemsikia ni mfano wa yule anayeamua kufuata njia ya ulimwengu katika utafutaji wa mali na katika matumizi ya madaraka. Hii ni njia ya ubinafsi, ya kutumia vibaya madaraka na ya kutafuta mwanya wa kujiokoa mwenyewe hata kama utawaingiza wengine hasara au kukwamisha miradi. Mwisho wa mfano huo Yesu anasema aliye mwaminifu katika liliko dogo, huwa mwaminifu katika lililo kubwa.” Anatualika tuifuate njia ya waana wa nuru katika utafutaji wa mali na katika matumizi ya madaraka. Njia hii ni njia ya uaminifu. Kilele cha fundisho la somo hili la injili ni mwaliko huo wa Yesu wa kutambua kuwa njia hizi mbili haziendi pamoja: uaminifu na ubinafsi haviendi pamoja kwa maana hakuna awezaye kutumikia mabwana wawili.

Madaraka ni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu
Madaraka ni kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, baada ya kuyasoma na kuyafafanua masomo yote matatu ya dominika hii, dominika inayotutahadharisha juu ya hatari ya utafutaji uliopitiliza wa mali na hatari ya matumizi mabaya ya mali na madaraka ninaguswa kutafakari nanyi kipengele kidogo tulichokisikia katika injili, kipengele cha tajiri kumsifia wakili mjanja aliyetafuta kujinufaisha kwa udhalimu. Ni kipande kinachoonesha ni wapi njia isiyo ya Mungu inaweza kutufikisha. Ni njia isiyotosheka kuuona uovu au mwenendo mbaya bali inakwenda mbele zaidi hata kuusifia na wakati mwingine kuupendekeza kama ndio mwenendo sahihi. Vipo vitu ambavyo huko nyuma hukuweza hata kuvisikia kwa sababu ilikuwa ni aibu kuvitaja, vitu vilivyoenda kinyume na mila, tamaduni na desturi zetu njema; sasa vinasikika kila kona na hata kupigiwa debe kama ni vitu vinavyofaa. Maandiko Matakatifu yanatukumbusha daima “usiwaonee wivu waovu, usiwahusudu watu waovu” (rej. Mithali 24:1). Kuupokea basi mwaliko wa Neno la Mungu leo na ili kujikita katika njia ya kumtumikia Mungu bila kuyumba yumba ni muhimu kutokuyapa thamani yale yanayopingana na njia ya imani ilhali tukiyapa thamani yale yanayotusaidia kujikita katika njia yetu.

Liturujia D25
17 Septemba 2022, 16:45