杏MAP导航

Tafuta

Sherehe za Utatu Mtakatifu, Baba Mwana na Roho Mtakatifu. Sherehe za Utatu Mtakatifu, Baba Mwana na Roho Mtakatifu. 

Sherehe ya Utatu Mtakatifu 2022:Usifiwe Utatu Mtakatifu na Umoja usiogawanyika

Katekisimu ya Kanisa Katoliki (255)inasema"Ingawa tunaweza kuona kazi ya Baba,Mwana,au Roho Mtakatifu kwa uwazi zaidi katika hali fulani yaani hivyo hatuwezi kuachanisha na nafsi nyingine,kwa sababu umoja huo wa kimungu haugawanyi,tofauti halisi ya Nafsi kutoka nafsi moja na nyingine inakaa tu katika mahusiano ambayo yanawahusu wao kwa wao”.

Na Padre Efrem Msigala, OSA, Shirika la Mt. Augustino Roma.

Karibu mpendwa Msikilizaji wa Radio Vatican na msomaji wa Vatican News katika tafakari ya Liturgia ya Neno la Mungu sherehe ya Utatu Mtakatifu. Ni moja ya sherehe zinazoadhimishwa katika kipindi cha kawaida cha liturgia ya mwaka wa Kanisa. Kila tunapoanza maadhimisho ya ibada zetu za kikatoliki tunaanza kwa ishara ya Msalaba tukitaja "Kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu." Pia tunahitimisha kwa maneno hayo, hata tunapopata baraka ya Padri, Askofu au Papa anatubariki kwa maneno hayo. Wakati wa ubatizo ni hivyo hivyo. Hata Yesu alipowatuma mitume wake alisema mkiwabatiza “kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu” (Mt.28:19). Pamoja na hayo maneno ya mwanzo mwa Misa ya sherehe ya Utatu Mtakatifu yanasema: “Usifiwe Utatu Mtakatifu na Umoja usiogawanyika.” Mungu mmoja katika nafsi tatu. Fumbo la Utatu Mtakatifu ambalo linagusa mambo yafuatayo: Baba ni Mungu, Mwana ni Mungu, na Roho Mtakatifu ni Mungu; hata hivyo, hakuna miungu watatu ila mmoja, ambaye kwa wakati mmoja ni Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu.

Hili ndilo Fumbo la Utatu wa Nafsi katika Mungu mmojaTunapoadhimisha Sherehe ya Utatu Mtakatifu ninamkumbuka Mtakatifu Augustino wa Hippo ambaye alitumia zaidi ya miaka 30 kufanyia kazi [kuhusu Utatu Mtakatifu] na kutoa kitabu cha De Trinitate, akijitahidi kupata maelezo yenye kueleweka kwa ajili ya fumbo la Utatu Mtakatifu. Anasimulia kuwa alikuwa akitembea kando ya ufuo wa bahari. Siku moja akitafakari na kujaribu kuelewa fumbo la Utatu Mtakatifu, alimwona mtoto mdogo wa kiume akikimbia na kurudi kutoka majini hadi mahali fulani kwenye ufuo wa bahari. Mvulana huyo alikuwa akitumia kopo dogo kubeba maji kutoka baharini na kuyaweka kwenye shimo dogo kwenye mchanga. Askofu wa Hippo yaani Augustino alimtazama sana yule mtoto na akamsogelea na kumuuliza, “Mwanangu, unafanya nini?” "Ninajaribu kuleta bahari yote kwenye shimo hili," alijibu yule mtoto kwa tabasamu. Augustino akasema: “Lakini hilo haliwezekani, mtoto wangu mpendwa, shimo hilo haliwezi kubeba maji hayo yote”. Yule mtoto alitulia, akasimama, akatazama machoni pa Augustino, na akajibu: “Haiwezekani zaidi ya kile unachojaribu kufanya – kufahamu ukuu wa fumbo la Utatu Mtakatifu kwa akili yako ndogo.” Augustino alivutiwa na jibu hilo kutoka kwa yule mtoto na akawa katika tafakari kubwa. Mara Augustino alipotaka kumuuliza swali jingine, yule mtoto alikuwa tayari ametoweka haonekani. Augustino akabaki katika tafakari zaidi. Hivyo akatambua kuwa Utatu Mtakatifu ni Fumbo haliwezi elezeka kwa mantiki ya kimahesabu. Ndivyo ilivyovigumu kujaza maji yote ya bahari katika shimo dogo.

Wengine husema kwamba yule mtoto alikuwa Malaika aliyetumwa na Mungu kufundisha Augustino somo la kiburi katika kujifunza. Wengine wanathibitisha kuwa ni Mtoto Kristo mwenyewe aliyemtokea Mtakatifu Augustino ili kumkumbusha juu ya mipaka ya ufahamu wa kibinadamu mbele ya mafumbo makuu ya Imani yetu. Mtakatifu Augustino akahusisha: Kumbukumbu, Uelewa na Utashi, na fundisho la Utatu Mtakatifu ambalo ni fumbo. Augustino pia katika kutafakari juu ya utatu Mtakatifu ilimfikirisha juu ya Ubatizo wa Yesu. Alipoona uwepo wa nafsi tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Lakini pia akaona kazi zao zimetenganishwa.  Mtakatifu Augustino alitafuta mlinganisho kwa kutumia analogia ili kuwasaidia wasikilizaji wake kufahamu umoja wa Utatu lakini kazi tofauti za kila mmoja. Anazungumza kuhusu uwezo wa akili ya kukumbuka, kuelewa, na kutaka. Akasema unapokumbuka hadithi, inabidi uwe umeelewa maneno yaliyokuwa yakisemwa na unahitaji nia ya kukumbuka hadithi hiyo. Unapotafuta kuelewa dhana, lazima ukumbuke dhana hiyo ni nini na utapenda wewe mwenyewe kuielewa. Unapotaka au kutamani kitu, lazima uelewe na ukumbuke kile ulicho nacho tayari.

Kwa hivyo, ingawa kitendo fulani kama kukumbuka kinaweza kuonekana au kushikika zaidi, kinategemea kuelewa na mapenzi ya mtu aliyonayo. Kwa vile matendo haya hayawezi kutenganishwa kikamilifu, vivyo hivyo na Mungu:  Nafsi za Kimungu pia hazitenganishwi katika yale wanayofanya. Lakini ndani ya utendaji mmoja wa kimungu kila mmoja anaonyesha kile kinachofaa kwake katika Utatu, hasa katika utume wa kiungu wa Umwilisho wa Mwana na kipawa cha Roho Mtakatifu. Katekisimu ya Kanisa katoliki inasema: Ingawa tunaweza kuona kazi ya Baba, Mwana, au Roho Mtakatifu kwa uwazi zaidi katika hali fulani yaani (Baba katika Uumbaji, Mwana ukombozi pale Msalabani, Roho Mtakatifu mwenye kutakasa aliyejitokeza siku ya Pentekoste), hivyo hatuwezi kuachanisha na nafsi nyingine: “Kwa sababu umoja huo wa kimungu haugawanyi, tofauti halisi ya Nafsi kutoka nafsi moja na nyingine inakaa tu katika mahusiano ambayo yanawahusu wao kwa wao” (KKK, 255). Baba anamfunua Mwana, Mwana anamfunua Baba, na Baba na Mwana wanafunuliwa na Roho Mtakatifu.

Katekismu ya kanisa Katoliki (232 -233) zinaelezea kuwa Wakristo wanabatizwa “katika jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu” na Kabla ya kupokea sakramenti, wazazi kwa niaba ya watoto au kama wanabatizwa wakubwa wanakiri imani juu ya utatu mtakatifu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu: hivyo tunabatizwa katika jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu: si kwa majina yetu ingawa mbatizaji anaanza kutaja jina la mbatizwa anasema: John nakubatiza “kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.”  Pia katekismu Katoliki namba 234 na 237 zinaeleza kuwa Fumbo la Utatu Mtakatifu ndilo fumbo kuu la imani na maisha ya Kikristo. Ni siri ya Mungu ndani yake. Kwa hiyo ni chanzo cha mafumbo mengine yote ya imani, nuru inayowaangazia.

Pia Katekismu ya Kanisa Katoliki (236) imejaribu kuelezea jinsi mababa wa kanisa walivyojaribu kutofautisha kati ya theologia na uchumi (ikonomia) ya wokovu. "Teolojia" inarejelea fumbo la maisha ya ndani kabisa ya Mungu ndani ya Utatu Mtakatifu na "uchumi au ikonomia" kwa kazi zote ambazo kwazo Mungu hujifunua na kuwasilisha maisha yake. Kupitia ikonomia theologia inafunuliwa kwetu; lakini kinyume chake, theologia inaangazia ikonomia nzima. Matendo ya Mungu yanadhihirisha yeye ni nani ndani yake; siri ya utu wake wa ndani hutuangazia ufahamu wetu wa kazi zake zote. Ndivyo ilivyo, kwa mfano, kati ya wanadamu. Mtu hujidhihirisha katika matendo yake, na kadiri tunavyomjua mtu vizuri zaidi, ndivyo tunavyoelewa matendo yake. Kwa hiyo tunapoadhimisha sherehe ya Utatu Mtakatifu tunagusa Fumbo asili la Mungu. Asili ambayo ni ya kijumuiya, umoja. Ndiyo maana hata katika uumbaji wa Mwanadamu alisema: “Natuumbe mtu kwa sura na mfano wetu...” Hapa alimaanisha umoja katika utatu, ushirikiano katika uumbaji.

Kwa njia hiyo sisi tulioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu pia tunashiriki hali hii ya kijumuiya, kijamii. Je katika jumuiya zetu ndogo ndogo tunapanga mipango kwa pamoja?, je tunashirikiana katika utekelezaji wake kwa pamoja?. Leo tunakumbushwa ushirikiano na mshikamano katika jumuiya zetu, vyama vya kitume katika parokia zetu lakini pia katika mipango mbalimbali kwenye vigango na parokia. Pamoja na hayo maisha yetu yaongozwe na maneno ya Yesu katika amri Kuu: kumpenda Mungu na kumpenda jirani. Tunapoadhimisha sherehe ya Utatu Mtakatifu tukumbuke mfano wa Utatu wa ushirika, umoja na upendo. Tukumbuke pia kama waamini wa Mungu wa Utatu, tumeitwa kuwa wa ushirika na Mungu na binadamu wengine. Halafu kufanywa au kuumbwa kwa mfano wa Mungu wetu wa Utatu ina maana kwamba tumeitwa kushiriki, kuakisi maisha ya Mungu mwenyewe ya upendo, uhusiano na wenzetu katika jumuiya na katika jamii.

SHEREHE YA UTATU MTAKATIFU MUNGU MMOJA
11 Juni 2022, 19:35