Sherehe ya Mwili na Damu ya Kristo:Ekaristi inalinda na kuongeza neema ya utakaso
Padre Paschal Ighondo - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, katika Sherehe ya Ekaristi Takatifu Mwaka C wa kiliturujia. Sherehe hii kimsingi inapaswa kuadhimishwa siku ya Alhamisi Kuu, siku ambayo Yesu aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu kwa kuwaambia wanafunzi wake; “Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu” (Lk. 22:19). Kwa kuamuru hivyo Yesu alitaka fumbo la mwili na Damu yake liadhimishwe nyakati zote. Katika sikukuu hii tunaadhimisha tena ukumbusho wa Karamu ya Mwisho. Tulipoadhimisha karamu yake siku Alhamisi kuu jioni, hatukuweza kufanya hivyo kwa shangwe. Kwa hiyo kwa sababu za kichungaji Kanisa hurudia adhimisho hili ili kuwapa waamini nafasi ya kumshangilia na kumshukuru Kristo kwa ajili ya zawadi hii kubwa ya kubaki na kukaa nasi nyakati zote katika Ekaristi Takatifu kwa kufanya maandamo. Zawadi hii ni mwili na damu yake mwenyewe inayotukumbusha kufa na kufufuka kwake na pia ni chakula chetu cha kiroho. Hivyo sherehe hii huamishiwa Alhamisi baada ya Sherehe ya Utatu Mtakatifu. Lakini kwa sababu za kichungaji, inahamishiwa domenika baada ya Utatu Mtakatifu ili kuwapa nafasi waamini wengi zaidi washiriki.
Somo la kwanza la kitabu cha Mwanzo (Mwa. 14: 18-20), linatueleza juu ya tukio lililokea miaka 1800 kabla ya kuzaliwa Yesu Kristo, mara tu baada ya Ibrahimu kufika nchi ya Kaanani akitii amri ya Mungu. Ilitokea vita kati ya wafalme 4, dhidi ya wafalme 5 kama wanavyotaja katika Mwanzo 14:9. Habari za hii vita inasimuliwa Mwanzo 14:1-17. Katika vita hii walioshindwa na kuchukuliwa mateka/watumwa alikuwepo Lutu, mpwa wa Abrahamu (Mwa 14:12). Habari hizi zilipomfikia, Abrahamu alitayarisha jeshi la watu 318 kutoka kati ya watu wa kabila lake akaenda kupigana vita akashinda na kuwaokoa wote waliochukuliwa mateka pamoja na vitu vyao (Mwa. 14:13-16). Walipokuwa njiani kurudi nyumbani, Abrahamu na jeshi lake walipita karibu na Salemu, mji ambao baadaye ulijulikana kama Yerusalemu. Melkisedeki Kuhani na mfalme wa Salemu alipopata habari za Abrahamu, alitoka kuja kukutana naye kwa kuwa yeye naye alimwabudu Mungu wa kweli (Ebr 7:1). Melkisedeki alimpatia Abrahamu Mkate na Divai, chakula na kinywaji cha kawaida katika eneo lile kwa wakati ule, na kumbariki akisema; “Mungu mkuu na mwenyezi akubariki wewe Abrahamu, ahimidiwe Bwana Mungu muumba wa mbingu na dunia kwa kuwaweka maadui zako mikononi mwako (Mwa 14:20). Akimshukuru kwa ukarimu wake, Abrahamu alimzawadia Melkisedeki sehemu ya kumi ya mali aliyokuwa ameiteka kutoka kwa maadui zake.
Baadae sana Roho wa Mungu aliwaangazia waandishi wa Maandiko Matakatifu na kumwona Melkisedeki katika tukio hili kuwa ni ishara ya Yesu Kristo aliye Kuhani Mkuu. Mzaburi katika zaburi ya 110 anaeleza kwamba, kama Melkisedeki, Masiha atakuwa Kuhani Mkuu. “Mwenyezi Mungu ameapa wala hataghairi kwamba wewe ni kuhani mkuu kwa mfano wa Melkisedeki kuhani mkuu wa milele” (Zab. 110, 4). Miaka 1900 baadae, Roho alimwongoza mwandishi wa Barua kwa Waebrania kuona katika Melkisedeki ishara ya Yesu Kristo, Mfalme na Kuhani. Jina Melkisedeki humaanisha “Mfalme wa Haki,” na jina Salemu humaanisha “Amani” na mwandishi anatusaidia kuona kuwa katika majina haya mawili kuwa Melkisedeki mfalme wa Salemu ni Mfalme wa Haki na amani (Ebr 7:2). Lakini ukuhani wa Kristo ni wa juu zaidi kuliko ule wa makuhani wa Kiyahudi. Anasema makuhani wote wa Kiyahudi walikuwa wadhambi, kama ilivyokuwa kwa wanadamu wote, na kwamba makuhani wote wa dunia hii wana ukomo, yaani wanakufa. Lakini Ukuhani wa Kristo ni ukuhani wa pekee kwa kuwa hakuwa na dhambi na ukuhani wake ni wa milele kwa kuwa hafi.
Katika somo la Pili la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorinto (1Kor. 11: 23-26), Mtume Paulo anatueleza juu ya kuwekwa Ekaristi Takatifu ambayo itadumu mpaka milele. Sadaka hii ni ukumbusho wa mateso na kifo cha Kristo. Paulo Mtume analezea upendo wa Yesu Kristo kwa kujitoa kwake kwa njia ya mateso na kifo cha aibu msalabani. Mateso, kifo na ufufuko vyote vimetafsiriwa katika Ekaristi Takatifu, ni namna moja ambayo yeye anaweza kuwa nasi daima na milele. Mwanadamu anatakiwa kuitika kwa kutambua ukuu wa mapendo hayo katika maisha ya kila siku.
Somo la Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk. 9:11-17), ni simulizi la mwujiza wa Yesu kuongeza mikate. Muujiza huu hutukumbusha jinsi Mungu alivyowalisha Waisraeli jangwani kwa chakula cha mana na papo hapo hudokeza namna Mungu anavyolilisha taifa lake la Agano Jipya kwa Ekaristi Takatifu iliyowekwa na Yesu Kristo. Hivyo tunaona bayana juu ya upendo wa Mungu kwa watu wake. Hilo linajidhihirisha wazi siku ile Bwana wetu Yesu Kristo alipowalisha watu elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili tu. Muujiza huu wa kuwalisha watu maelfu kwa mikate mitano na samaki wawili ni mwendelezo wa ukweli kwamba yeye mwenyewe amejitoa kwetu kama chakula cha kiroho yaani Ekaristi Takatifu ndiyo inayotuunganisha na Kristo kwakuwa yeye amejifanya kuwa chakula chetu cha kiroho. Ekaristi Takatifu inatuunganisha pia sisi sote kwa kushirika chakula kimoja na meza moja, na hii inatufanya tuwe mwili mmoja na roho mmoja katika Kristo. Ndiyo maana Mtume Paulo anasema:” Na sasa naishi si mimi tena, bali Kristo anaishi ndani yangu” (Gal 2:20). Ekaristi Takatifu inatuunganisha sisi kwa sisi tunaposhiriki kwa pamoja chakula na meza ileile kwa kuwa mkate huo ni mmoja, sisi ingawa ni wengi, tu mwili mmoja. Maana sote twashiriki mkate huohuo” (1Kor 10:17).
Ekaristi Takatifu inatuangazia akili na kuimarisha utashi wetu. Yesu wa Ekaristi ni mwanga wa ulimwengu anapokuja tunaangaziwa kama wafuasi wa Emaus pale walipo mtambua katika kuumega mkate. Kwa namna hiyohiyo Ekaristi Takatifu hutupatia nguvu za kushindana na vishawishi na majaribu. Vilele Ekaristi Takatifu inalinda na kuongeza neema ya utakaso. Kama vile chakula cha kawaida kinavyofanya katika uzima wa mwili, ndivyo Ekaristi Takatifu hutekeleza kwa namna ya ajabu katika uzima wetu wa kiroho. Tunapokuwa na neema ya utakaso ndivyo tunapokuwa na utukufu mkubwa zaidi Mbinguni tulioahidiwa na Mungu. Ekaristi Takatifu hututenganisha na dhambi katika maana kwamba mwili na damu ya Yesu Kristo hutolewa kwa ajili yetu kwa maondoleo ya dhambi. Kwasababu hiyo Ekaristi Takatifu haiwezi kutuunganisha na Kristo bila wakati huohuo kutuosha na dhambi za zamani na kutukinga na dhambi zijazo. Ekaristi Takatifu inaunda Kanisa maana tunapoipokea tunaunganishwa kwa ndani na Kristo. Yaani tunaunganishwa kuwa katika mwili mmoja, yaani kanisa.
Katika sherehe hii mama kanisa anatukumbusha kuwa; Ekaristi Takatifu, mwili na damu ya Kristo ni chakula chetu cha kiroho kwa uzima wa milele. Hivyo tunakumbushwa kuwa tunapoijongea meza ya Bwana, tuijongee tukiwa katika hali ya neema ya utakaso. Tukumbuke kuwa kupokea Ekaristi Takatifu kwa mazoea, hali tukiwa katika hali ya dhambi ya mauti moyoni ni kufuru kubwa mno. Ni kuila hukumu yetu wenyewe kama asemavyo Paulo: “Aulaye mwili huu na kunywa damu hii isivyopasa, ana hatia ya mwili na damu ya Kristo.” Basi tuiheshimu na kuipokea Ekaristi Takatifu katika hali ya neema ndio maana katika sala ya koleta Padre anasali kwa niaba ya jamii ya waamini akisema; “Ee Mungu, umetuachia ukumbusho wa mateso yako katika sakramenti ya ajabu. Tunakuomba utujalie kuyaheshimu mafumbo matakatifu ya mwili na damu yako, tupate daima neema ya ukombozi wako ndani yetu. Na katika sala baada ya komunyo anasali na kuomba; “Ee Bwana, tunakuomba utujaze na furaha isiyo na mwisho ya kuutazama umungu wako. Tunaona ishara ya furaha hiyo hapa duniani katika kupokea Mwili na Damu yako takatifu.