杏MAP导航

Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 4 ya Pasaka. Dominika hii imepewa jina la “Dominika ya Mchungaji Mwema” Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 4 ya Pasaka. Dominika hii imepewa jina la “Dominika ya Mchungaji Mwema”  

Dominika ya Kristo Mchungaji Mwema: Siku ya Kuombea Miito Mitakatifu Ndani ya Kanisa

Dominika hii imepewa jina la “Dominika ya Mchungaji Mwema” kama anavyosali Padre katika sala mwanzo; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, utuelekeze kwenye furaha za mbinguni, kusudi sisi kondoo wako wanyonge tufike huko alikotoka mchungaji wetu shujaa.” Hii ni siku maalum kwa ajili ya kuombea miito, wito wa kwanza ni Ukristo na Utakatifu wa maisha; Ndoa, Upadre na Utawa.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 4 ya Pasaka. Dominika hii imepewa jina la “Dominika ya Mchungaji Mwema” kama anavyosali Padre katika sala mwanzo; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, utuelekeze kwenye furaha za mbinguni, kusudi sisi kondoo wako wanyonge tufike huko alikotoka mchungaji wetu shujaa.” Na katika sala baada ya komunio anahitimisha akisali; “Ee Mchungaji mwema, ututazame kwa mapendo sisi kundi lako. Upende kutuweka katika malisho ya milele sisi kondoo wako uliotukomboa kwa damu takatifu ya Mwanao.” Yesu ndiye Machungaji Mwema: “Mimi ndimi mchungaji mwema, kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele kwa kuutoa uhai wangu”. Ni siku ya kuombea Miito mitakatifu ndani ya Kanisa: “Mwombeni Bwana wa mavuno apeleke wafanyakazi katika shamba lake” (Mt 9:37, Lk 10: 2). Somo la kwanza la Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 13:14, 43-52); ni simulizi ya sehemu ya safari ya kwanza ya Mtume Paulo kueneza Injili wakiwa na Barnaba (13:1-14:28). Somo hili linatusimulia jinsi Paulo na Barnaba walivyoanza kuhubiri Injili kwa Wayahudi.

Familia imara na thabiti ni msingi imara wa miito mbali mbali ndani ya Kanisa
Familia imara na thabiti ni msingi imara wa miito mbali mbali ndani ya Kanisa

Lakini Wayahudi walipoikataa Injili kwa sababu ya wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana, mitume hawa waliwaendea wapagani ambao waliipokea kwa furaha: Ndipo Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakisema; Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa. Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na Bwana; Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia. Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini. Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote. Lakini Wayahudi wakawafitinisha wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao. Nao wakawakung’utia mavumbi ya miguu yao, wakaenda Ikonio. Na wanafunzi walijaa furaha na Roho Mtakatifu”.

Somo la pili kutoka Kitabu cha Ufunuo (Uf. 7:9,14b-17); linatupa picha ya hali yetu itakavyokuwa huko mbinguni, pale tutakuwa chini ya ulinzi na uangalizi wa mchungaji aitwaye “Mwanakondoo – Yesu. Tutakuwa wenye furaha na amani daima. Yohane katika somo la pili kutoka kitabu cha ufunuo aliona watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao, wametoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwan-kondoo, yeye aketiye katika kiti cha enzi ametanda hema yake juu yao. Hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena, wala jua halitawapiga, wala hari ile yoyote. Kwa maana huyo Mwana-kondoo, aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchem za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao. Hawa ndio walioisikia sauti ya Mchungaji mwema, wakamfuata, wakapata uzima tele.

Ni Siku ya kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa
Ni Siku ya kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa

Injili ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 10: 27-30); inamwonesha Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu na mchungaji mwenye nguvu ya kuwalinda kondoo wake. Kondoo wanamjua Yesu, kwa hiyo wanamwamini na kumfuata: Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe”. Wanaompinga Yesu hawawezi kuwapokonya kondoo katika mkono wake, sababu Yeye ana nguvu kama Baba, na Baba ana nguvu kupita wote: Wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu. Mimi na Baba tu umoja”. Tuisikilize sauti ya Kristo mchungaji wetu mwema katika nafsi za wachungaji aliotuachia kupitia kwa mtume Petro akisema; “Wewe ndiwe Petro na juu mwamba huu nitalijenga kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda” ili nasi tusishindwe katika maisha yetu ya hapa duniani.

Wajibu wa wachungaji wetu – Mapadre na watawa ni kuwahudumie waamini kwa upendo bila kutafuta maslahi binafsi. Mtume Petro anawaasa akisema: “Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshiriki wa utukufu utakaofunuliwa baadaye, lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo, si kwa kutaka fedha ya aibu bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. Mchungaji mkuu atakapojitokeza mtavikwa taji ya utukufu, ile isiyokauka” (1Pet 5:1-4), na hivyo tutaweza kusema kwa ujasiri mbele zake; “Nilipokuwapo pamoja nao, mimi niliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza: wala hapana mmoja wao aliyepotea ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie” (Yn 17:12).

Mapadre na watawa wamewekwa wakfu ili wawaongoze watu katika imani, kuhuisha maisha ya Kiroho na kuikuza ile mbegu iliyosiwa ndani ya mioyo yao wakati wa ubatizo wakiwalisha kwa Neno la Mungu na Sakramenti ya Ekaristi, wakiwaponya kwa sakramenti ya Upatanisho, na kuwaimarisha kwa sakramenti ya Kipaimara. Ili watu wasibaki na njaa na kiu kubwa ya Neno la Mungu na masakramenti kwa mapadre kujihusisha na shughuli zingine za maendeleo ni vizuri kufuata ushauri wa mitume kwa Kanisa la mwanzo: “Haipendezi sisi kuliacha Neno la Mungu na kuhudumu Mezani…chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho na Hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili, na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno” (Mdo 6:2, 4). Mahusiano ya kibinadamu si kamilifu, hata katika familia bora, kutokuelewana kwaweza kutokea hata katika jumuiya za Kikristo. Hata hivyo, umoja na mshikamano ni lazima kwa kondoo na mchungaji wakati wote. Mgawanyiko ndani ya jumuiya huleta majeraha na maumivu makubwa. Ni lazima turuhusu kuongozwa na wachungaji wetu. Wajibu wetu katika jumuiya ni lazima uwe ule wa utendaji siyo wa kutazama na kuwaachia wengine. Ushirikiano utawapa mapadre wetu ujasiri na kuwatia moyo katika roho ya huduma na kutangaza habari za Ufalme wa Mungu ndani ya mioyo yetu na katika Jumuiya zetu.

Ni Siku ya kuwakumbuka na kuwaombea Mapadre.
Ni Siku ya kuwakumbuka na kuwaombea Mapadre.

Wajibu wa waamini kwa Wachungaji wao ni kuwa kwanza wanapaswa kutambua kuwa wachungaji wao ni binadamu wenye madhaifu na mapungufu kama binadamu wengine. Pale wanapokosea nao wakayaona madhaifu na mapungufu yao wanapaswa kuwasahihisha kidugu na katika roho ya upendo na heshima kubwa. Wapendwa waanimi, fahamuni kuwa kuwaumbua wachungaji wenu kwa makossa yao ya kibinadamu hamuwasaidii bali mnawajeruhi na kuwafanya washindwe kuwahudumia na hivyo wa kwanza kuteseka zaidi ni ninyi mnaopaswa kuhudumiwa. Tambueni kuwa wachungaji wenu wamezungukwa na maadui wengi maana daima kazi yao inawadai kuogelea kinyume na mawimbi ya maji, hivyo waombeeni na zaidi sana kuwatia moyo ili wawahudumie kwa upendo zaidi na wale walio wazee na wagonjwa wahudumieni ili wasikate tamaa; “Mimi siombi uwatoe ulimwenguni, bali uwalinde na yule mwovu” (Yn 17:15); waombeeni ili watakatifuzwe katika ukweli; Uwatakase katika ile kweli, Neno lako ndiyo kweli” (Yn 17:17), ili wajitoe, wawe tayari kutumikia ndani ya Kanisa, wakihubiri Neno la Mungu na kuadhimisha Sakramenti za wokovu, silaha makini dhidi ya shetani na hila zake.

Waombeeni ili wakue katika utakatifu kila siku ya maisha yao, wakitoa huduma zao kwa moyo mkunjufu na utayari; wawe waaminifu, wakweli na wanyofu kwa Mungu, kwa Kanisa na kwa nafsi zao wenyewe, wenye dhamiri safi na isiyo na makunyanzi wasiwe na hila ndani mwao (Yn 1:47); waombeeni ili watambue kuwa wao pamoja nanyi ni mali ya Kristo; “Jina lako limewadhihirisha watu wale ulionipa katika ulimwengu, walikuwa wako, ukanipa mimi, na Neno lako wamelishika” (Yn 17:6); waombeeni ili watambue kuwa udanganyifu hauwezi kuwaleta watu kwa Kristo bali ukweli unaohubiriwa, uliosimikwa katika ushuhuda wa maisha yao. Waamini, waombeeni Waseminaristi na watakaji wa maisha ya utawa na upadre, ili wawe daima wasikivu kwa Roho wa Mungu anayewaita kwa wito maalumu wa upadre, waongezeke na kukua katika uchaji, waongezeke na kukua katika ufahamu wa kile anachowaitia Mungu wakue katika Upendo kwa Mungu na Kanisa. Hivi tutapata wachungaji wema watakaotuongoza vyema kwenye malisho mema na kutufikisha salama katika ufalme wa Mungu mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo!

Dominika 4 Pasaka
04 Mei 2022, 15:34