杏MAP导航

Tafuta

Siku kuu ya Bikira Maria Kumtembelea Elizabeti, Tuombe mapendo ya jirani! Siku kuu ya Bikira Maria Kumtembelea Elizabeti, Tuombe mapendo ya jirani! 

Papa Francisko: Hija ya Kitume Romania: Umoja wa Maaskofu

Baraza la Maaskofu Katoliki Hungaria, limekubali mwaliko wa Baraza la Maaskofu Katoliki Romania, kushiriki na Baba Mtakatifu Francisko, anapofanya hija yake ya kitume nchini Romania. Maaskofu watakuwepo kwenye Madhabahu ya “?umuleu Ciuc” yaani Bikira Maria Mfariji wa wanaoteseka, hapo tarehe 1 Juni 2019, ili kusali pamoja na kuzungumza na Baba Mtakatifu! Umoja wa Maaskofu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 31 Mei, Siku kuu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeti hadi tarehe 2 Juni 2019, Kanisa, sehemu mbali mbali za dunia, litakapokuwa linaadhimisha Siku kuu ya Kupaa Bwana Mbinguni anafanya hija ya kitume ya 30 Kimataifa nchini Romania. Baba Mtakatifu atafanya hija katika mji mkuu wa Bucharest, mji wa Ias, ulioko Kaskazini wa Romania pamoja na mji wa Blaj, Kituo kikuu cha utamaduni nchini Romania. Baba Mtakatifu akiwa nchini Romania, atatembelea Madhabahu ya “?umuleu Ciuc” yaani Bikira Maria Mfariji wa wanaoteseka.

Hija hii ya kitume inaongozwa na kauli mbiu “Twende pamoja”, mwaliko kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kutembea kwa pamoja chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kwa kukataa kishawishi cha uchoyo na ubinafsi, ili kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anatembelea Romania ili kuimarisha imani miongoni mwa ndugu zake katika Kristo sanjari na kukazia umoja na mshikamano wa familia ya Mungu nchini Romania. Baraza la Maaskofu Katoliki Hungaria, limekubali mwaliko wa Baraza la Maaskofu Katoliki Romania, kushiriki na Baba Mtakatifu Francisko, anapofanya hija yake ya kitume nchini Romania.

Maaskofu watakuwepo kwenye Madhabahu ya “?umuleu Ciuc” yaani Bikira Maria Mfariji wa wanaoteseka, hapo tarehe 1 Juni 2019, ili kusali pamoja na kuzungumza na Baba Mtakatifu. Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Baba Mtakatifu kutembelea Madhabahu haya, ambayo pia yana umuhimu wa pekee katika maisha na utume wao! Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 31 Mei anasherehekea Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu kumtembelea binamu yake Elizabeti. Ni siku ya kufunga pia Mwezi wa Rozari takatifu, kwa changamoto ya kuendelea kusali Rozari kwani huu ni muhtasari wa Injili na matendo makuu ya Mungu katika historia ya mwanadamu.

Kumbu kumbu ya Bikira Maria kumtembelea Elizabeti ni mwendelezo wa utenzi wa sifa, shukrani na furaha ya ujio wa Masiha unaotambuliwa na Yohane Mbatizaji. Hapa Bikira Maria anaoneshwa kama Tabernakulo na Sanduku la Agano Jipya na la Milele. Katika hija hii ya kitume, Baba Mtakatifu atatembelea mji mkuu wa Bucharest, mji wa Ias ulioko Kaskazini wa Romania pamoja na mji wa Blaj, Kituo kikuu cha utamaduni nchini Romania kati ya karne ya 18-19 na hapa pia ni mwanzo wa tafsiri ya Biblia ya Blaj. Itakumbukwa kwamba, mara ya mwisho, Romania ilitembelewa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1999 na watu wengi wanaifananisha Romania na “Bustani ya Mama wa Mungu”.

Hili lilikuwa ni tukio la kihistoria tangu Kanisa lilipotengana kunako mwaka 1054 na huo ukawa ni mwanzo wa kuibuka kwa Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo! Baba Mtakatifu Francisko atafanya hija ya kitume nchini Romania wakati wa Siku kuu ya Bikira Maria Kumtembelea Elizabeti yaani Mama wa Mungu ndiye anayetoka kwa haraka kwenda kumtembelea Elizabeti. Hapa wanawake wawili wanaohifadhi ndani mwao zawadi ya maisha wanakutana Bikira Maria ni mtumishi wa Bwana na Elizabeti ni kielelezo cha matumaini mapya kwa Waisraeli na huduma ya Injili ya upendo kwa jirani na mfano wa kuigwa hasa katika ulimwengu mamboleo uliogubikwa na ubinafsi na uchoyo.

Yohane Mbatizaji anaruka kwa shangwe tumboni mwa mama yake Elizabeti, ushuhuda makini wa kufunguliwa kwa ukurasa mpya naye ndiye atakayekuwa Nabii na daraja kati ya Agano la Kale na Agano Jipya. Ni mtangulizi wa Masiha na Mkombozi wa ulimwengu, changamoto na mwaliko wa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo na ukarimu kwa jirani!

Papa: Bikira Maria
30 Mei 2019, 16:24